Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
REVELATION OF JOHN
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 12
Reve Swahili 12:1  Kisha ishara kubwa ikaonekana mbinguni. Palikuwa hapo mwanamke aliyevikwa jua, na mwezi chini ya miguu yake, na taji ya nyota kumi na mbili juu ya kichwa chake!
Reve Swahili 12:2  Alikuwa mja mzito, na akapaaza sauti kwa maumivu na uchungu wa kujifungua mtoto.
Reve Swahili 12:3  Ishara nyingine ikatokea mbinguni: joka kubwa jekundu na lenye pembe kumi na vichwa saba; na kila kichwa kilikuwa na taji.
Reve Swahili 12:4  Joka hilo liliburuta kwa mkia wake theluthi moja ya nyota za anga na kuzitupa duniani. Nalo lilisimama mbele ya huyo mama aliyekuwa karibu kujifungua mtoto, tayari kabisa kummeza mtoto, mara tu atakapozaliwa.
Reve Swahili 12:5  Kisha mama huyo akajifungua mtoto wa kiume, ambaye atayatawala mataifa yote kwa fimbo ya chuma. Lakini mtoto akanyakuliwa na kupelekwa kwa Mungu na kwenye kiti chake cha enzi.
Reve Swahili 12:6  Huyo mama akakimbilia jangwani, ambako Mungu alikuwa amemtayarishia mahali pa usalama ambapo angehifadhiwa kwa muda wa siku elfu moja mia mbili na sitini.
Reve Swahili 12:7  Kisha kukazuka vita mbinguni: Mikaeli na malaika wake walipigana na hilo joka, nalo likawashambulia pamoja na malaika wake.
Reve Swahili 12:8  Lakini joka hilo halikuweza kuwashinda, na hatimaye hapakuwa tena na nafasi mbinguni kwa ajili yake na malaika wake.
Reve Swahili 12:9  Basi, joka hilo kuu likatupwa nje. Joka hilo ndiye yule nyoka wa kale ambaye huitwa pia Ibilisi au Shetani. Ndiye anayeudanganya ulimwengu wote. Naam, alitupwa duniani, na malaika wake wote pamoja naye.
Reve Swahili 12:10  Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka mbinguni ikisema: "Sasa ukombozi utokao kwa Mungu umefika! Nguvu na Utawala wa Mungu wetu umedhihirika. Na Kristo wake ameonyesha mamlaka yake! Maana yule mdhalimu wa ndugu zetu, aliyesimama mbele ya Mungu akiwashtaki usiku na mchana, sasa ametupwa nje.
Reve Swahili 12:11  Ndugu zetu wameshinda kwa damu ya Mwanakondoo na kwa nguvu ya ukweli walioutangaza; maana hawakuyathamini maisha yao kuwa kitu sana, wakawa tayari kufa.
Reve Swahili 12:12  Kwa sababu hiyo, furahini enyi mbingu na vyote vilivyomo ndani yenu. Lakini, ole wenu nchi na bahari, maana Ibilisi amewajieni akiwa na ghadhabu kuu, kwa sababu anajua kwamba siku zake zilizobakia ni chache."
Reve Swahili 12:13  Joka lilipotambua kwamba limetupwa chini duniani, likaanza kumwinda yule mama aliyekuwa amejifungua mtoto wa kiume.
Reve Swahili 12:14  Lakini mama huyo akapewa mabawa mawili ya tai apate kuruka mbali sana na hilo joka, mpaka mahali, pake jangwani ambapo angehifadhiwa salama kwa muda wa miaka mitatu na nusu.
Reve Swahili 12:15  Basi, joka likatapika maji mengi kama mto, yakamfuata huyo mama nyuma ili yamchukue.
Reve Swahili 12:16  Lakini nchi ikamsaidia huyo mama: ikajifunua kama mdomo na kuyameza maji hayo yaliyotoka kinywani mwa hilo joka.
Reve Swahili 12:17  Basi, joka hilo likamkasirikia huyo mama, likajiondokea, likaenda kupigana na wazawa wengine wa huyo mama, yaani wote wanaotii amri za Mungu na kuuzingatia ukweli wa Yesu.