Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
III JOHN
1
Chapter 1
III Swahili 1:1  Mimi mzee nakuandikia wewe Gayo, rafiki yangu, ninayekupenda kweli.
III Swahili 1:2  Mpenzi wangu, nakutakia mafanikio mema ya kila aina; nakutakia afya njema ya mwili kama ulivyo nayo rohoni.
III Swahili 1:3  Nimefurahi sana ndugu kadhaa walipofika hapa, wakaiambia juu ya uaminifu wako kuhusu ukweli; naam, wewe unaishi daima katika ukweli.
III Swahili 1:4  Hakuna kitu kinachonifurahisha zaidi kuliko kusikia kwamba watoto wangu wanaishi katika ukweli.
III Swahili 1:5  Mpenzi wangu, wewe ni mwaminifu kila mara unapowahudumia ndugu, hata kama ni wageni.
III Swahili 1:6  Ndugu hao wamelieleza kanisa hapa habari za upendo wako. Tafadhali uwasaidie waendelee na safari yao kwa namna itakayompendeza Mungu,
III Swahili 1:7  Maana wanaanza safari yao katika utumishi wa Kristo bila kupokea msaada wowote kutoka kwa watu wasioamini.
III Swahili 1:8  Basi, sisi tunapaswa kuwasaidia watu hawa, ili nasi tupate kushiriki katika kazi yao kwa ajili ya ukweli.
III Swahili 1:9  Niliandika barua fupi kwa hilo kanisa; lakini Diotrefe, ambaye hupenda kuwa kiongozi wao, hataki kabisa kunisikiliza.
III Swahili 1:10  Basi, nitakapokuja nitayafichua mambo yote anayofanya, maneno mabaya anayotutolea na uongo anaosema juu yetu. Isitoshe, yeye hukataa kuwakaribisha hao ndugu walio safarini, na hata huwazuia watu wengine wanaotaka kuwakaribisha, na hujaribu kuwafukuzia nje ya kanisa.
III Swahili 1:11  Mpenzi wangu, usifuate mfano mbaya, bali mfano mwema. Kila atendaye mema ni wa Mungu; lakini anayetenda mabaya hajapata kumwona Mungu.
III Swahili 1:12  Kila mtu anamsifu Demetrio; naam, ukweli wenyewe unamsifu. Nasi pia tunatoa ushahidi wetu juu yake, nawe wajua kwamba tunachosema ni kweli.
III Swahili 1:13  Ninayo bado mengi ya kukwambia, lakini sipendi kuyaandika kwa kalamu na wino.
III Swahili 1:14  Natumaini kukuona karibuni na hapo tutazungumza ana kwa ana. Nakutakia amani. Rafiki zako wanakusalimu. Wasalimu rafiki zetu wote kila mmoja binafsi.