Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
ROMANS
1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 10
Roma Swahili 10:1  Ndugu zangu, ninataka na kutazamia kwa moyo wangu wote hao wananchi wenzangu wakombolewe. Tena nawaombea kwa Mungu daima.
Roma Swahili 10:2  Maana naweza kuthibitisha kwa niaba yao kwamba wanayo bidii ya kumtafuta Mungu; lakini bidii hiyo haikujengwa juu ya ujuzi wa kweli.
Roma Swahili 10:3  Maana hawakufahamu jinsi Mungu anavyowafanya watu wawe waadilifu, na wamejaribu kuanzisha mtindo wao wenyewe, na hivyo hawakuikubali njia hiyo ya Mungu ya kuwafanya wawe waadilifu.
Roma Swahili 10:4  Maana kwa kuja kwake Kristo, Sheria imefikia kikomo chake, ili kila mtu anayeamini akubaliwe kuwa mwadilifu.
Roma Swahili 10:5  Kuhusu kukubaliwa kuwa mwadilifu kwa kuitii Sheria, Mose aliandika hivi: "Mtu yeyote anayetimiza matakwa ya Sheria ataishi."
Roma Swahili 10:6  Lakini, kuhusu kukubaliwa kuwa mwadilifu kwa njia ya imani, yasemwa hivi: "Usiseme moyoni mwako: Nani atapanda mpaka mbinguni? (yaani, kumleta Kristo chini);
Roma Swahili 10:7  wala usiseme: Nani atashuka mpaka Kuzimu (yaani, kumleta Kristo kutoka kwa wafu)."
Roma Swahili 10:8  Maandiko Matakatifu yesema hivi, "Ujumbe huo wa Mungu uko karibu nawe, uko kinywani mwako na moyoni mwako" nao ndio ile imani tunayoihubiri.
Roma Swahili 10:9  Kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba Yesu ni Bwana na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka wafu, utaokoka.
Roma Swahili 10:10  Maana tunaamini kwa moyo na kukubaliwa kuwa waadilifu; na tunakiri kwa midomo yetu na kuokolewa.
Roma Swahili 10:11  Maandiko Matakatifu yasema: "Kila amwaminiye hatakuwa na sababu ya kuaibika."
Roma Swahili 10:12  Jambo hili ni kwa wote, kwani hakuna tofauti kati ya Wayahudi na wasio Wayahudi; Bwana wa wote ni mmoja, naye ni mkarimu sana kwao wote wamwombao.
Roma Swahili 10:13  Maana Maandiko Matakatifu yasema: "Kila mtu atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa."
Roma Swahili 10:14  Basi, watamwombaje yeye ambaye hawamwamini? Tena, watamwaminije kama hawajapata kusikia habari zake? Na watasikiaje habari zake kama hakuna mhubiri?
Roma Swahili 10:15  Na watu watahubirije kama hawakutumwa? Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Ni jambo la kupendeza mno kuja kwa wale wanaohubiri Habari Njema!"
Roma Swahili 10:16  Lakini wote hawakuipokea hiyo Habari Njema. Maana Isaya alisema: "Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?"
Roma Swahili 10:17  Hivyo basi, imani inatokana na kuusikiliza ujumbe, na huo ujumbe unatokana na neno la Kristo.
Roma Swahili 10:18  Lakini nauliza: je, hawakuusikia huo ujumbe? Naam, waliusikia; kama Maandiko Matakatifu yasemavyo: "Sauti yao imeenea duniani kote; maneno yao yamefika mpaka kingo za ulimwengu."
Roma Swahili 10:19  Tena nauliza: je, yawezekana kwamba watu wa Israeli hawakufahamu? Mose mwenyewe ni kwa kwanza kujibu: "Nitawafanyeni mwaonee wivu watu ambao si taifa; nitawafanyeni muwe na hasira juu ya taifa la watu wapumbavu."
Roma Swahili 10:20  Tena Isaya anathubutu hata kusema: "Wale ambao hawakunitafuta wamenipata; nimejionyesha kwao wasiouliza habari zangu."
Roma Swahili 10:21  Lakini kuhusu Israeli anasema: "Mchana kutwa niliwanyoshea mikono yangu watu waasi na wasiotii."