Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
JOHN
1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 21
John Swahili 21:1  Baada ya hayo Yesu aliwatokea tena wanafunzi wake kando ya ziwa Tiberia. Aliwatokea hivi:
John Swahili 21:2  Simoni Petro, Thoma (aitwaye Pacha), na Nathanieli mwenyeji wa Kana Galilaya, wana wawili wa Zebedayo na wanafunzi wake wengine wawili, walikuwa wote pamoja.
John Swahili 21:3  Simoni Petro aliwaambia, "Nakwenda kuvua samaki." Nao wakamwambia, "Nasi tutafuatana nawe." Basi, wakaenda, wakapanda mashua, lakini usiku huo hawakupata chochote.
John Swahili 21:4  Kulipoanza kupambazuka, Yesu alisimama kando ya ziwa, lakini wanafunzi hawakujua kwamba alikuwa yeye.
John Swahili 21:5  Basi, Yesu akawauliza, "Vijana, hamjapata samaki wowote sio?" Wao wakamjibu, "La! Hatujapata kitu."
John Swahili 21:6  Yesu akawaambia, "Tupeni wavu upande wa kulia wa mashua nanyi mtapata samaki." Basi, wakatupa wavu lakini sasa hawakuweza kuuvuta tena kwa wingi wa samaki.
John Swahili 21:7  Hapo yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akamwambia Petro, "Ni Bwana!" Simoni Petro aliposikia ya kuwa ni Bwana, akajifunga vazi lake (maana hakuwa amelivaa), akarukia majini.
John Swahili 21:8  Lakini wale wanafunzi wengine walikuja pwani kwa mashua huku wanauvuta wavu uliojaa samaki; hawakuwa mbali na nchi kavu, ila walikuwa yapata mita mia moja kutoka ukingoni.
John Swahili 21:9  Walipofika nchi kavu waliona moto wa makaa umewashwa na juu yake pamewekwa samaki na mkate.
John Swahili 21:10  Yesu akawaambia, "Leteni hapa baadhi ya samaki mliovua."
John Swahili 21:11  Basi, Simoni Petro akapanda mashuani, akavuta hadi nchi kavu ule wavu uliokuwa umejaa samaki wakubwa mia moja na hamsini na watatu. Na ingawa walikuwa wengi hivyo wavu haukukatika.
John Swahili 21:12  Yesu akawaambia, "Njoni mkafungue kinywa." Hakuna hata mmoja wao aliyethubutu kumwuliza: "Wewe ni nani?" Maana walijua alikuwa Bwana.
John Swahili 21:13  Yesu akaja, akatwaa mkate akawapa; akafanya vivyo hivyo na wale samaki.
John Swahili 21:14  Hii ilikuwa mara ya tatu Yesu kuwatokea wanafunzi wake baada ya kufufuka kutoka wafu.
John Swahili 21:15  Walipokwisha kula, Yesu alimwuliza Simoni Petro, "Simoni, mwana wa Yohane! Je, wanipenda mimi zaidi kuliko hawa?" Naye akajibu, "Naam, Bwana; wajua kwamba mimi nakupenda." Yesu akamwambia, "Tunza wana kondoo wangu."
John Swahili 21:16  Kisha akamwambia mara ya pili, "Simoni mwana wa Yohane! Je, wanipenda?" Petro akamjibu, "Naam, Bwana; wajua kwamba nakupenda." Yesu akamwambia, "Tunza kondoo wangu."
John Swahili 21:17  Akamwuliza mara ya tatu, "Simoni mwana wa Yohane! Je, wanipenda?" Hapo Petro akahuzunika kwa sababu alimwuliza mara ya tatu: "Wanipenda?" akamwambia, "Bwana, wewe wajua yote; wewe wajua kwamba mimi nakupenda." Yesu akamwambia, "Tunza kondoo wangu!
John Swahili 21:18  Kweli nakwambia, ulipokuwa kijana ulizoea kujifunga mshipi na kwenda kokote ulikotaka. Lakini utakapokuwa mzee utanyosha mikono yako, na mtu mwingine atakufunga na kukupeleka usikopenda kwenda."
John Swahili 21:19  (Kwa kusema hivyo, alionyesha jinsi Petro atakavyokufa na kumtukuza Mungu.) Kisha akamwambia, "Nifuate."
John Swahili 21:20  Hapo Petro akageuka, akamwona yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda, anafuata (Huyu mwanafunzi ndiye yule ambaye wakati wa chakula cha jioni, alikaa karibu sana na Yesu na kumwuliza: "Bwana ni nani atakayekusaliti?")
John Swahili 21:21  Basi, Petro alipomwona huyo akamwuliza Yesu, "Bwana, na huyu je?"
John Swahili 21:22  Yesu akamjibu, "Kama nataka abaki mpaka nitakapokuja, yakuhusu nini? Wewe nifuate mimi."
John Swahili 21:23  Basi, habari hiyo ikaenea miongoni mwa wale ndugu kwamba mwanafunzi huyo hafi. Lakini Yesu hakumwambia kwamba mwanafunzi huyo hafi, ila, "Kama nataka abaki mpaka nitakapokuja, yakuhusu nini?"
John Swahili 21:24  Huyo ndiye yule aliyeshuhudia mambo haya na kuyaandika. Nasi twajua kwamba aliyoyasema ni kweli.
John Swahili 21:25  Kuna mambo mengine mengi aliyofanya Yesu, ambayo kama yangeandikwa yote, moja baada ya lingine, nadhani hata ulimwengu wenyewe usingetosha kuviweka vitabu ambavyo vingeandikwa.