Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
JOHN
1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 9
John Swahili 9:1  Yesu alipokuwa akipita alimwona mtu mmoja, kipofu tangu kuzaliwa.
John Swahili 9:2  Basi, wanafunzi wakamwuliza, "Mwalimu! Ni nani aliyetenda dhambi: mtu huyu, ama wazazi wake, hata akazaliwa kipofu?"
John Swahili 9:3  Yesu akajibu, "Jambo hili halikutukia kwa sababu ya dhambi zake yeye, wala dhambi za wazazi wake; ila alizaliwa kipofu ili nguvu ya Mungu ionekane ikifanya kazi ndani yake.
John Swahili 9:4  Kukiwa bado mchana yatupasa kuendelea kufanya kazi za yule aliyenituma; maana usiku unakuja ambapo mtu hawezi kufanya kazi.
John Swahili 9:5  Wakati ningali ulimwenguni, mimi ni mwanga wa ulimwengu."
John Swahili 9:6  Baada ya kusema hayo, akatema mate chini, akafanyiza tope, akampaka yule kipofu machoni,
John Swahili 9:7  akamwambia, "Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu." (maana ya jina hili ni "aliyetumwa"). Basi, huyo kipofu akaenda, akanawa, kisha akarudi akiwa anaona.
John Swahili 9:8  Basi, jirani zake na wale waliokuwa wanajua kwamba hapo awali alikuwa maskini mwombaji, wakasema, "Je, huyu siye yule maskini aliyekuwa akiketi na kuomba?"
John Swahili 9:9  Baadhi yao wakasema, "Ndiye." Wengine wakasema, "La! Ila anafanana naye." Lakini huyo aliyekuwa kipofu akasema, "Ni mimi!"
John Swahili 9:10  Basi, wakamwuliza, "Sasa, macho yako yalipataje kufumbuliwa?"
John Swahili 9:11  Naye akawajibu, "Yule mtu aitwaye Yesu alifanya tope, akanipaka machoni na kuniambia: Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu. Basi, mimi nikaenda, nikanawa, nikapata kuona."
John Swahili 9:12  Wakamwuliza, "Yeye yuko wapi?" Naye akawajibu, "Mimi sijui!"
John Swahili 9:13  Kisha wakampeleka huyo mtu aliyekuwa kipofu kwa Mafarisayo.
John Swahili 9:14  Siku hiyo Yesu alipofanya tope na kumfumbua macho mtu huyo, ilikuwa siku ya Sabato.
John Swahili 9:15  Basi, Mafarisayo wakamwuliza mtu huyo, "Umepataje kuona?" Naye akawaambia, "Alinipaka tope machoni, nami nikanawa na sasa naona."
John Swahili 9:16  Baadhi ya Mafarisayo wakasema, "Mtu huyu hakutoka kwa Mungu, maana hashiki sheria ya Sabato." Lakini wengine wakasema, "Mtu mwenye dhambi awezaje kufanya ishara za namna hii?" Kukawa na mafarakano kati yao.
John Swahili 9:17  Wakamwuliza tena huyo mtu aliyekuwa kipofu, "Maadam yeye amekufungua macho, wasemaje juu yake?" Naye akawaambia, "Yeye ni nabii!"
John Swahili 9:18  Viongozi wa Wayahudi hawakusadiki kwamba mtu huyo alikuwa kipofu hapo awali na sasa anaona mpaka walipowaita wazazi wake.
John Swahili 9:19  Basi, wakawauliza hao wazazi, "Je, huyu ndiye mtoto wenu ambaye ninyi mwasema alizaliwa kipofu? Sasa amepataje kuona?"
John Swahili 9:20  Wazazi wake wakajibu, "Tunajua kwamba huyu ni mtoto wetu, na kwamba alizaliwa kipofu.
John Swahili 9:21  Lakini amepataje kuona, hatujui; na wala hatumjui yule aliyemfumbua macho. Mwulizeni yeye mwenyewe; yeye ni mtu mzima, anaweza kujitetea mwenyewe."
John Swahili 9:22  Wazazi wake walisema hivyo kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Wayahudi kwani viongozi hao walikuwa wamepatana ya kwamba mtu yeyote atakayekiri kwamba Yesu ni Kristo atafukuzwa nje ya sunagogi.
John Swahili 9:23  Ndiyo maana wazazi wake walisema: "Yeye ni mtu mzima, mwulizeni."
John Swahili 9:24  Basi, wakamwita tena aliyekuwa kipofu, wakamwambia, "Sema ukweli mbele ya Mungu! Sisi tunajua kwamba mtu huyu ni mwenye dhambi."
John Swahili 9:25  Yeye akajibu, "Kama ni mwenye dhambi mimi sijui. Lakini kitu kimoja najua: Nilikuwa kipofu, na sasa naona."
John Swahili 9:26  Basi, wakamwuliza, "Alikufanyia nini? Alikufumbuaje macho yako?"
John Swahili 9:27  Huyo mtu akawajibu, "Nimekwisha waambieni, nanyi hamkusikiliza; kwa nini mwataka kusikia tena? Je, ninyi pia mnataka kuwa wafuasi wake?"
John Swahili 9:28  Lakini wao wakamtukana wakisema, "Wewe ni mfuasi wake; sisi ni wafuasi wa Mose.
John Swahili 9:29  Sisi tunajua kwamba Mungu alisema na Mose, lakini mtu huyu hatujui ametoka wapi!"
John Swahili 9:30  Naye akawajibu, "Hili ni jambo la kushangaza! Ninyi hamjui ametoka wapi, lakini amenifumbua macho yangu!
John Swahili 9:31  Tunajua kwamba Mungu hawasikilizi watu wenye dhambi, ila humsikiliza yeyote mwenye kumcha na kutimiza mapenzi yake.
John Swahili 9:32  Tangu mwanzo wa ulimwengu haijasikika kwamba mtu ameyafumbua macho ya mtu aliyezaliwa kipofu.
John Swahili 9:33  Kama mtu huyu hakutoka kwa Mungu, hangeweza kufanya chochote!"
John Swahili 9:34  Wao wakamjibu, "Wewe ulizaliwa na kulelewa katika dhambi; unawezaje kutufundisha sisi?" Basi, wakamfukuzia mbali.
John Swahili 9:35  Yesu alisikia kwamba walikuwa wamemfukuzia mbali, naye alipomkuta akamwuliza, "Je, wewe unamwamini Mwana wa Mtu?"
John Swahili 9:36  Huyo mtu akajibu, "Mheshimiwa, niambie yeye ni nani, ili nipate kumwamini."
John Swahili 9:37  Yesu akamwambia, "Umekwisha mwona, naye ndiye anayesema nawe sasa."
John Swahili 9:38  Basi, huyo mtu akasema, "Ninaamini Bwana!" Akamsujudia.
John Swahili 9:39  Yesu akasema, "Mimi nimekuja ulimwenguni kutoa hukumu, kusudi wasioona wapate kuona, na wale wanaoona wawe vipofu."
John Swahili 9:40  Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa pamoja naye walisikia maneno hayo, wakamwuliza, "Je, sisi pia ni vipofu?"
John Swahili 9:41  Yesu akawajibu, "Kama mngekuwa vipofu, hamngekuwa na hatia; lakini sasa ninyi mwasema: Sisi tunaona, na hiyo yaonyesha kwamba mna hatia bado.