Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
JOHN
1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 5
John Swahili 5:1  Baada ya hayo kulikuwa na sikukuu ya Wayahudi, naye Yesu akaenda Yerusalemu.
John Swahili 5:2  Huko Yerusalemu, karibu na mlango uitwao Mlango wa Kondoo, kulikuwa na bwawa la maji liitwalo kwa Kiebrania Bethzatha, ambalo lilikuwa na baraza tano zenye matao.
John Swahili 5:3  Humo barazani mlikuwa na wagonjwa wengi wamekaa: vipofu, viwete na waliopooza. Walikuwa wakingojea maji yatibuliwe,
John Swahili 5:4  maana mara kwa mara malaika alishuka majini nyakati fulani na kuyatibua. Mtu yeyote aliyekuwa wa kwanza kuingia majini baada ya maji kutibuliwa, alipona ugonjwa wowote aliokuwa nao.
John Swahili 5:5  Basi, hapo palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa mgonjwa kwa muda wa miaka thelathini na minane.
John Swahili 5:6  Naye alipomwona huyo mtu amelala hapo, akatambua kwamba alikuwa amekaa hapo kwa muda mrefu, akamwuliza, "Je, wataka kupona?"
John Swahili 5:7  Naye akajibu, "Mheshimiwa, mimi sina mtu wa kunipeleka majini wakati yanapotibuliwa. Kila nikijaribu kuingia, mtu mwingine hunitangulia."
John Swahili 5:8  Yesu akamwambia, "Inuka, chukua mkeka wako utembee."
John Swahili 5:9  Mara huyo mtu akapona, akachukua mkeka wake, akatembea. Jambo hili lilifanyika siku ya Sabato.
John Swahili 5:10  Kwa hiyo baadhi ya Wayahudi wakamwambia huyo mtu aliyeponywa, "Leo ni Sabato, si halali kubeba mkeka wako."
John Swahili 5:11  Lakini yeye akawaambia, "Yule mtu aliyeniponya ndiye aliyeniambia: Chukua mkeka wako, tembea."
John Swahili 5:12  Nao wakamwuliza, "Huyo mtu aliyekwambia: Chukua mkeka wako, tembea, ni nani?"
John Swahili 5:13  Lakini yeye hakumjua huyo mtu aliyemponya, maana Yesu alikuwa amekwisha ondoka mahali hapo, kwani palikuwa na umati mkubwa wa watu.
John Swahili 5:14  Basi, baadaye Yesu alimkuta huyo aliyeponywa Hekaluni, akamwambia, "Sasa umepona; usitende dhambi tena, usije ukapatwa na jambo baya zaidi."
John Swahili 5:15  Huyo mtu akaenda, akawaambia viongozi wa Wayahudi kwamba Yesu ndiye aliyemponya.
John Swahili 5:16  Kwa vile Yesu alifanya jambo hilo siku ya Sabato, Wayahudi walianza kumdhulumu.
John Swahili 5:17  Basi, Yesu akawaambia, "Baba yangu anafanya kazi daima, nami pia nafanya kazi."
John Swahili 5:18  Kwa sababu ya maneno haya, viongozi wa Wayahudi walizidi kutafuta njia ya kumwua Yesu: si kwa kuwa aliivunja Sheria ya Sabato tu, bali pia kwa kuwa alisema kwamba Mungu ni Baba yake, na hivyo akajifanya sawa na Mungu.
John Swahili 5:19  Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, Mwana hawezi kufanya kitu peke yake; anaweza tu kufanya kile anachomwona Baba akikifanya. Maana kile anachofanya Baba, Mwana hukifanya vilevile.
John Swahili 5:20  Baba ampenda Mwana, na humwonyesha kila kitu anachokifanya yeye mwenyewe, tena atamwonyesha mambo makuu kuliko haya, nanyi mtastaajabu.
John Swahili 5:21  Kama vile Baba huwafufua wafu na kuwapa uzima, vivyo hivyo naye Mwana huwapa uzima wale anaopenda.
John Swahili 5:22  Baba hamhukumu mtu yeyote; shughuli yote ya hukumu amemkabidhi Mwana,
John Swahili 5:23  ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba ambaye amemtuma.
John Swahili 5:24  "Kweli nawaambieni, anayesikia neno langu, na kumwamini yule aliyenituma, anao uzima wa milele. Hatahukumiwa kamwe, bali amekwisha pita kutoka kifo na kuingia katika uzima.
John Swahili 5:25  Kweli nawaambieni, wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo wafu wataisikia sauti ya Mwana wa Mungu, nao watakaoisikia, wataishi.
John Swahili 5:26  Kama vile Baba alivyo asili ya uhai, ndivyo pia alivyomjalia Mwanawe kuwa asili ya uhai.
John Swahili 5:27  Tena amempa mamlaka ya kuhukumu kwa sababu yeye ni Mwana wa Mtu.
John Swahili 5:28  Msistaajabie jambo hili; maana wakati unakuja ambapo wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake,
John Swahili 5:29  nao watafufuka: wale waliotenda mema watafufuka na kuishi, na wale waliotenda maovu watafufuka na kuhukumiwa.
John Swahili 5:30  "Mimi siwezi kufanya kitu kwa uwezo wangu mwenyewe. Mimi nina hukumu kama ninavyosikia kutoka kwa Baba, nayo hukumu yangu ni ya haki. Nia yangu si kufanya nipendavyo mwenyewe, bali apendavyo yule aliyenituma.
John Swahili 5:31  Nikijishuhudia mimi mwenyewe, ushahidi wangu hauwezi kukubaliwa kuwa wa kweli.
John Swahili 5:32  Lakini yuko mwingine ambaye hutoa ushahidi juu yangu, nami najua kwamba yote anayosema juu yangu ni ya kweli.
John Swahili 5:33  Ninyi mlituma ujumbe kwa Yohane naye aliushuhudia ukweli.
John Swahili 5:34  Si kwamba mimi nautegemea ushahidi wa wanadamu, lakini nasema mambo haya ili mpate kuokolewa.
John Swahili 5:35  Yohane alikuwa kama taa iliyokuwa ikiwaka na kuangaza, nanyi mlikuwa tayari kufurahia mwanga huo kwa kitambo.
John Swahili 5:36  Lakini mimi nina ushahidi juu yangu ambao ni mkuu zaidi kuliko ule wa Yohane. Kwa maana kazi ninazofanya, kazi alizonipa Baba nizifanye, ndizo zinazonishuhudia kwamba Baba ndiye aliyenituma.
John Swahili 5:37  Naye Baba aliyenituma hunishuhudia. Ninyi hamjapata kamwe kusikia sauti yake, wala kuuona uso wake,
John Swahili 5:38  na ujumbe wake haukai ndani yenu maana hamkumwamini yule aliyemtuma.
John Swahili 5:39  Ninyi huyachunguza Maandiko Matakatifu mkidhani kwamba ndani yake mtapata uzima wa milele; na kumbe maandiko hayohayo yananishuhudia!
John Swahili 5:40  Hata hivyo, ninyi hamtaki kuja kwangu ili mpate uzima.
John Swahili 5:42  Lakini nawajua ninyi, najua kwamba upendo kwa Mungu haumo mioyoni mwenu.
John Swahili 5:43  Mimi nimekuja kwa mamlaka ya Baba yangu, lakini hamnipokei; bali mtu mwingine akija kwa mamlaka yake mwenyewe, mtampokea.
John Swahili 5:44  Mwawezaje kuamini, hali ninyi mnapenda kupokea sifa kutoka kwenu ninyi wenyewe, wala hamtafuti sifa kutoka kwake yeye aliye peke yake Mungu?
John Swahili 5:45  Msifikiri kwamba mimi nitawashtaki kwa Baba. Mose ambaye ninyi mmemtumainia ndiye atakayewashtaki.
John Swahili 5:46  Kama kweli mngemwamini Mose, mngeniamini na mimi pia; maana Mose aliandika juu yangu.
John Swahili 5:47  Lakini hamuyaamini yale aliyoandika, mtawezaje basi, kuamini maneno yangu?"