Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
MARK
1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 2
Mark Swahili 2:1  Baada ya siku kadhaa, Yesu alirudi Kafarnaumu, watu wakapata habari kwamba alikuwa nyumbani.
Mark Swahili 2:2  Basi, wakaja watu wengi sana hata nafasi yoyote ikakosekana mlangoni. Yesu alikuwa akiwahubiria ujumbe wake,
Mark Swahili 2:3  wakati mtu mmoja aliyepooza alipoletwa kwake akiwa amechukuliwa na watu wanne.
Mark Swahili 2:4  Kwa sababu ya huo umati wa watu, hawakuweza kumpeleka karibu na Yesu. Basi, wakatoboa sehemu ya dari iliyokuwa juu ya mahali alipokuwa Yesu. Walipokwisha pata nafasi, wakamteremsha huyo mtu akiwa amelala juu ya mkeka.
Mark Swahili 2:5  Yesu alipoona imani yao, akamwambia huyo mtu aliyepooza, "Mwanangu, umesamehewa dhambi zako."
Mark Swahili 2:6  Baadhi ya walimu wa Sheria waliokuwa wameketi hapo wakawaza mioyoni mwao,
Mark Swahili 2:7  "Anathubutuje kusema hivyo? Anamkufuru Mungu! Hakuna mtu awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake."
Mark Swahili 2:8  Yesu alitambua mara mawazo yao, akawaambia, "Mbona mnawaza hivyo mioyoni mwenu?
Mark Swahili 2:9  Ni lipi lililo rahisi zaidi: kumwambia mtu huyu aliyepooza, Umesamehewa dhambi zako, au kumwambia, Inuka! Chukua mkeka wako utembee?
Mark Swahili 2:10  Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anayo mamlaka ya kuwasamehe watu dhambi duniani." Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza,
Mark Swahili 2:11  "Nakwambia simama, chukua mkeka wako uende nyumbani!"
Mark Swahili 2:12  Mara, watu wote wakiwa wanamtazama, huyo mtu akainuka, akauchukua mkeka wake, akaenda zake. Watu wote wakashangaa na kumtukuza Mungu wakisema, "Hatujapata kamwe kuona jambo kama hili."
Mark Swahili 2:13  Yesu alikwenda tena kando ya ziwa. Umati wa watu ukamwendea, naye akaanza kuwafundisha.
Mark Swahili 2:14  Alipokuwa akipita, akamwona Lawi mwana wa Alfayo, ameketi katika ofisi ya ushuru. Yesu akamwambia, "Nifuate!" Lawi akasimama, akamfuata.
Mark Swahili 2:15  Baadaye, Yesu alikuwa amekaa mezani, nyumbani kwa Lawi, kula chakula. Watoza ushuru wengi na wenye dhambi walikuwa wamemfuata Yesu na wengi wao wakawa wamekaa mezani pamoja naye na wanafunzi wake.
Mark Swahili 2:16  Basi, baadhi ya walimu wa Sheria ambao walikuwa Mafarisayo walipomwona Yesu akila pamoja na watu wenye dhambi na watoza ushuru, wakawauliza wanafunzi wake, "Kwa nini anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?"
Mark Swahili 2:17  Yesu alipowasikia, akawaambia, "Watu wenye afya hawahitaji daktari; wanaomhitaji ni wale walio wagonjwa. Sikuja kuwaita watu wema, ila wenye dhambi."
Mark Swahili 2:18  Wakati mmoja wanafunzi wa Yohane na wanafunzi wa Mafarisayo walikuwa wanafunga. Basi, watu wakaja, wakamwuliza Yesu, "Kwa nini wanafunzi wa Yohane na wa Mafarisayo wanafunga, lakini wanafunzi wako hawafungi?"
Mark Swahili 2:19  Yesu akajibu, "Walioalikwa harusini wanawezaje kufunga kama bwana harusi yupo pamoja nao? Wakati wote wawapo pamoja na bwana harusi hawawezi kufunga.
Mark Swahili 2:20  Lakini wakati utafika ambapo bwana harusi ataondolewa kati yao; wakati huo ndipo watakapofunga.
Mark Swahili 2:21  "Hakuna mtu anayekata kiraka kutoka katika nguo mpya na kukishonea katika nguo kuukuu. Kama akifanya hivyo, hicho kiraka kipya kitararuka kutoka hilo vazi kuukuu, nalo litaharibika zaidi.
Mark Swahili 2:22  Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu. Kama akifanya hivyo, divai itavipasua hivyo viriba, nayo divai pamoja na hivyo viriba vitaharibika. Divai mpya hutiwa katika viriba vipya!"
Mark Swahili 2:23  Siku moja ya Sabato, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano. Walipokuwa wanatembea, wanafunzi wake wakaanza kukwanyua masuke ya ngano.
Mark Swahili 2:24  Mafarisayo wakawaambia, "Tazama! Kwa nini wanafanya jambo ambalo si halali kufanya wakati wa Sabato?"
Mark Swahili 2:25  Yesu akawajibu, "Je, hamjapata kusoma juu ya kile alichofanya Daudi wakati alipohitaji chakula? Yeye pamoja na wenzake waliona njaa,
Mark Swahili 2:26  naye akaingia ndani ya Nyumba ya Mungu, akala ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu. Jambo hili lilifanyika wakati Abiathari alikuwa Kuhani Mkuu. Na ni makuhani tu peke yao waliokuwa wameruhusiwa kula mikate hiyo. Lakini Daudi aliila, tena akawapa na wenzake."
Mark Swahili 2:27  Basi, Yesu akawaambia, "Sabato iliwekwa kwa ajili ya binadamu na si binadamu kwa ajili ya Sabato!
Mark Swahili 2:28  Kwa hiyo, Mwana wa Mtu ni Bwana hata wa Sabato."