Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
MARK
1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 5
Mark Swahili 5:1  Basi, wakafika katika nchi ya Wagerase, ng'ambo ya ziwa.
Mark Swahili 5:2  Mara tu Yesu aliposhuka mashuani, mtu mmoja aliyepagawa na pepo mchafu alitoka makaburini, akakutana naye.
Mark Swahili 5:3  Mtu huyo alikuwa akiishi makaburini wala hakuna mtu aliyeweza tena kumfunga kwa minyororo.
Mark Swahili 5:4  Mara nyingi walimfunga kwa pingu na minyororo lakini kila mara aliweza kuikata hiyo minyororo na kuzivunja hizo pingu, wala hakuna mtu aliyeweza kumzuia.
Mark Swahili 5:5  Mchana na usiku alikaa makaburini na milimani akipaaza sauti na kujikatakata kwa mawe.
Mark Swahili 5:6  Alipomwona Yesu kwa mbali, alimkimbilia, akamwinamia
Mark Swahili 5:7  akisema kwa sauti kubwa, "Una shauri gani nami, wewe Yesu Mwana wa Mungu aliye juu? Kwa jina la Mungu, nakusihi usinitese!"
Mark Swahili 5:8  (Alisema hivyo kwa kuwa Yesu alikuwa amemwambia, "Pepo mchafu, mtoke mtu huyu.")
Mark Swahili 5:9  Basi, Yesu akamwuliza, "Jina lako nani?" Naye akajibu, "Jina langu ni Jeshi, maana sisi tu wengi."
Mark Swahili 5:10  Kisha akamsihi Yesu asiwafukuze hao pepo katika nchi ile.
Mark Swahili 5:11  Kulikuwa na kundi kubwa la nguruwe malishoni kwenye mteremko wa mlima.
Mark Swahili 5:12  Basi, hao pepo wakamsihi, "Utupeleke kwa hao nguruwe, tuwaingie."
Mark Swahili 5:13  Naye akawaruhusu. Basi, hao pepo wachafu wakatoka, wakawaingia wale nguruwe. Kundi lote la nguruwe wapatao elfu mbili likaporomoka kwenye ule mteremko mkali mpaka ziwani, likatumbukia majini.
Mark Swahili 5:14  Wachungaji wa hao nguruwe walikimbia, wakatangaza jambo hilo mjini na mashambani. Watu wakafika kuona yaliyotukia.
Mark Swahili 5:15  Wakamwendea Yesu, wakamwona na mtu yuleyule aliyekuwa amepagawa na jeshi la pepo ameketi chini, amevaa nguo na ana akili yake sawa, wakaogopa.
Mark Swahili 5:16  Watu walishuhudia tukio hilo wakaeleza wengine mambo yaliyompata huyo mtu aliyekuwa amepagawa na pepo na juu ya wale nguruwe.
Mark Swahili 5:17  Basi, wakaanza kumwomba aondoke katika nchi yao.
Mark Swahili 5:18  Yesu alipokuwa anapanda mashuani, yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo akamwomba amruhusu kwenda naye.
Mark Swahili 5:19  Lakini Yesu akamkatalia. Badala yake akamwambia, "Nenda nyumbani kwa jamaa yako, ukawaambie mambo yote Bwana aliyokutendea na jinsi alivyokuonea huruma."
Mark Swahili 5:20  Basi, huyo mtu akaenda, akaanza kutangaza huko Dekapoli mambo yote Yesu aliyomtendea; watu wote wakashangaa.
Mark Swahili 5:21  Yesu alivukia tena upande wa pili wa ziwa kwa mashua. Umati mkubwa wa watu ukakusanyika mbele yake, naye akawa amesimama kando ya ziwa.
Mark Swahili 5:22  Hapo akaja mmojawapo wa maofisa wa sunagogi, jina lake Yairo. Alipomwona Yesu, akajitupa mbele ya miguu yake,
Mark Swahili 5:23  akamsihi akisema, "Binti yangu mdogo ni mgonjwa karibu kufa. Twende tafadhali, ukamwekee mikono yako, apate kupona na kuishi."
Mark Swahili 5:24  Basi, Yesu akaondoka pamoja naye. Watu wengi sana wakamfuata, wakawa wanamsonga kila upande.
Mark Swahili 5:25  Mmojawapo alikuwa mwanamke mwenye ugonjwa wa kutokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili.
Mark Swahili 5:26  Mwanamke huyo alikuwa amekwisha sumbuka sana kuwaendea waganga wengi. Na ingawa alikuwa amekwisha tumia mali yake yote, hakupata nafuu bali hali yake ilizidi kuwa mbaya.
Mark Swahili 5:27  Alikuwa amesikia habari za Yesu, na hivyo akaupenya msongamano wa watu kutoka nyuma, akagusa vazi lake.
Mark Swahili 5:28  Alifanya hivyo, maana alijisemea, "Nikigusa tu vazi lake, nitapona."
Mark Swahili 5:29  Mara chemchemi ya damu yake ikakauka, akajisikia mwilini mwake kwamba ameponywa ugonjwa wake.
Mark Swahili 5:30  Yesu alitambua mara kwamba nguvu imemtoka. Basi akaugeukia ule umati wa watu, akauliza, "Nani aliyegusa mavazi yangu?"
Mark Swahili 5:31  Wanafunzi wake wakamjibu, "Unaona jinsi watu wanavyokusonga; mbona wauliza nani aliyekugusa?"
Mark Swahili 5:32  Lakini Yesu akaendelea kutazama amwone huyo aliyefanya hivyo.
Mark Swahili 5:33  Hapo huyo mwanamke, akifahamu yaliyompata, akajitokeza akitetemeka kwa hofu, akajitupa chini mbele ya Yesu na kusema ukweli wote.
Mark Swahili 5:34  Yesu akamwambia, "Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako."
Mark Swahili 5:35  Yesu alipokuwa bado anaongea, watu walifika kutoka nyumbani kwa yule ofisa wa sunagogi, wakamwambia, "Binti yako amekwisha kufa. Ya nini kuendelea kumsumbua Mwalimu?"
Mark Swahili 5:36  Lakini, bila kujali walichosema, Yesu akamwambia mkuu wa sunagogi, "Usiogope, amini tu."
Mark Swahili 5:37  Wala hakumruhusu mtu yeyote kufuatana naye ila Petro, Yakobo na Yohane nduguye Yakobo.
Mark Swahili 5:38  Wakafika nyumbani kwa ofisa wa sunagogi naye Yesu akasikia makelele, kilio na maombolezo mengi.
Mark Swahili 5:39  Akaingia ndani, akawaambia, "Mbona mnapiga kelele na kulia? Msichana hakufa, amelala tu."
Mark Swahili 5:40  Lakini wao wakamcheka. Basi, akawaondoa wote nje, akawachukua baba na mama ya huyo msichana na wale wanafunzi wake, wakaingia chumbani alimokuwa huyo msichana.
Mark Swahili 5:41  Kisha akamshika mkono, akamwambia, "Talitha, kumi," maana yake, "Msichana, nakwambia, amka!"
Mark Swahili 5:42  Mara msichana akasimama, akaanza kutembea. (Alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili.) Hapo watu wakashangaa kupita kiasi.
Mark Swahili 5:43  Yesu akawakataza sana wasimjulishe mtu jambo hilo. Kisha akawaambia wampe huyo msichana chakula.