Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
ROMANS
1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 14
Roma Swahili 14:1  Mkaribisheni kwenu mtu aliye dhaifu, lakini msibishane naye juu ya mawazo yake binafsi.
Roma Swahili 14:2  Watu huhitilafiana: mmoja imani yake inamruhusu kula kila kitu; lakini mwingine ambaye imani yake ni dhaifu, hula tu mboga za majani.
Roma Swahili 14:3  Mtu ambaye hula kila kitu asimdharau yule ambaye hawezi kula kila kitu; naye ambaye hula tu mboga za majani asimhukumu anayekula kila kitu, maana Mungu amemkubali.
Roma Swahili 14:4  Wewe ni nani hata uthubutu kumhukumu mtumishi wa mwingine? Akisimama au akianguka ni shauri la Bwana wake; naam, atasimama imara, maana Bwana anaweza kumsimamisha.
Roma Swahili 14:5  Mtu anaweza kufikiria siku fulani kuwa ya maana zaidi kuliko nyingine; mtu mwingine aweza kuzifikiria siku zote kuwa sawa. Kila mmoja na afuate msimamo wa akili yake.
Roma Swahili 14:6  Anayeadhimisha siku fulani anaadhimisha siku hiyo kwa ajili ya kumtukuza Mungu; naye anayekula chakula fulani anafanya hivyo kwa kumtukuza Bwana maana anamshukuru Mungu. Kadhalika naye anayeacha kula chakula fulani anafanya hivyo kwa ajili ya kumtukuza Bwana, naye pia anamshukuru Mungu.
Roma Swahili 14:7  Maana hakuna mtu yeyote miongoni mwetu aishiye kwa ajili yake mwenyewe, wala hakuna anayekufa kwa ajili yake mwenyewe
Roma Swahili 14:8  maana tukiishi twaishi kwa ajili ya Bwana; tukifa, tunakufa kwa ajili ya Bwana. Basi, kama tukiishi au tukifa, sisi ni mali yake Bwana.
Roma Swahili 14:9  Maana Kristo alikufa, akafufuka ili wapate kuwa Bwana wa wazima na wafu.
Roma Swahili 14:10  Kwa nini, basi wewe wamhukumu ndugu yako? Nawe, kwa nini wamdharau ndugu yako? Sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Mungu.
Roma Swahili 14:11  Maana Maandiko yanasema: "Kama niishivyo, asema Bwana kila mtu atanipigia magoti, na kila mmoja atakiri kwamba mimi ni Mungu."
Roma Swahili 14:12  Kwa hiyo, kila mmoja wetu atatoa hoja yake mbele ya Mungu.
Roma Swahili 14:13  Basi, tuache kuhukumiana, bali tuazimie kutokuwa kamwe kikwazo kwa ndugu yetu au kumsababisha aanguke katika dhambi.
Roma Swahili 14:14  Katika kuungana na Bwana Yesu, nina hakika kwamba hakuna kitu chochote kilicho najisi kwa asili yake; lakini, mtu akidhani kwamba kitu fulani ni najisi, basi, kwake huwa najisi.
Roma Swahili 14:15  Kama ukimhuzunisha ndugu yako kwa sababu ya chakula unachokula, basi mwenendo wako hauongozwi na mapendo. Usikubali hata kidogo chakula chako kiwe sababu ya kupotea kwa mtu mwingine ambaye Kristo alikufa kwa ajili yake!
Roma Swahili 14:16  Basi, msikubalie kitu mnachokiona kuwa kwenu ni kitu chema kidharauliwe.
Roma Swahili 14:17  Maana Utawala wa Mungu si shauri la kula na kunywa, bali unahusika na kuwa na uadilifu, amani na furaha iletwayo na Roho Mtakatifu.
Roma Swahili 14:18  Anayemtumikia Kristo namna hiyo humpendeza Mungu, na kukubaliwa na watu.
Roma Swahili 14:19  Kwa hiyo tuyazingatie daima mambo yenye kuleta amani, na yanayotusaidia kujengana.
Roma Swahili 14:20  Basi, usiiharibu kazi ya Mungu kwa sababu ya ubishi juu ya chakula. Vyakula vyote ni halali, lakini haifai kula chakula ambacho kitamfanya mtu aanguke katika dhambi.
Roma Swahili 14:21  Afadhali kuacha kula nyama, kunywa divai, au kufanya chochote ambacho chaweza kumsababisha ndugu yako aanguke.
Roma Swahili 14:22  Basi, shikilia unachoamini kati yako na Mungu wako. Heri mtu yule ambaye, katika kujiamulia la kufanya, haipingi dhamiri yake.
Roma Swahili 14:23  Lakini mtu anayeona shaka juu ya chakula anachokula, anahukumiwa kama akila, kwa sababu msimamo wa kitendo chake haumo katika imani. Na, chochote kisicho na msingi wake katika imani ni dhambi.