Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
MATTHEW
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 16
Matt Swahili 16:1  Mafarisayo na Masadukayo walimwendea Yesu, na kwa kumjaribu, wakamwomba afanye ishara itokayo mbinguni.
Matt Swahili 16:2  Lakini Yesu akawajibu, "Wakati wa jioni ukifika ninyi husema: Hali ya hewa itakuwa nzuri kwa maana anga ni jekundu!
Matt Swahili 16:3  Na alfajiri mwasema: Leo hali ya hewa itakuwa ya dhoruba, maana anga ni jekundu na tena mawingu yametanda! Basi, ninyi mnajua sana kusoma majira kwa kuangalia anga, lakini kutambua dalili za nyakati hizi hamjui.
Matt Swahili 16:4  Kizazi kiovu kisicho na uaminifu! Mnataka ishara, lakini hamtapewa ishara yoyote isipokuwa tu ile ya Yona." Basi, akawaacha, akaenda zake.
Matt Swahili 16:5  Wanafunzi wake walipokwisha vukia upande wa pili wa ziwa, walijikuta wamesahau kuchukua mikate.
Matt Swahili 16:6  Yesu akawaambia, "Muwe macho na mjihadhari na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo!"
Matt Swahili 16:7  Lakini wao wakawa wanajadiliana: "Anasema hivyo kwa kuwa hatukuchukua mikate."
Matt Swahili 16:8  Yesu alijua mawazo yao, akawaambia, "Enyi watu wenye imani haba! Mbona mnajadiliana juu ya kutokuwa na mikate?
Matt Swahili 16:9  Je, hamjaelewa bado? Je, hamkumbuki nilipoimega ile mikate mitano kwa ajili ya wale watu elfu tano? Je, mlijaza vikapu vingapi vya makombo?
Matt Swahili 16:10  Au, ile mikate saba waliyogawiwa wale watu elfu nne, je, mlikusanya vikapu vingapi vya mabaki?
Matt Swahili 16:11  Inawezekanaje hamwelewi ya kwamba sikuwa nikisema juu ya mikate? Jihadharini na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo!"
Matt Swahili 16:12  Hapo wanafunzi wakafahamu kwamba aliwaambia wajihadhari siyo na chachu ya mikate, bali na mafundisho ya Mafarisayo na Masadukayo.
Matt Swahili 16:13  Yesu alipofika pande za Kaisarea Filipi, aliwauliza wanafunzi wake, "Watu wanasema Mwana wa Mtu kuwa ni nani?"
Matt Swahili 16:14  Wakamjibu, "Wengine wanasema kuwa ni Yohane mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii."
Matt Swahili 16:15  Yesu akawauliza, "Na ninyi je, mwasema mimi ni nani?"
Matt Swahili 16:16  Simoni Petro akajibu, "Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai."
Matt Swahili 16:17  Yesu akasema, "Heri wewe Simoni mwana wa Yona, kwa maana si binadamu aliyekufunulia ukweli huu, ila Baba yangu aliye mbinguni.
Matt Swahili 16:18  Nami nakwambia: wewe ni Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala kifo chenyewe hakitaweza kulishinda.
Matt Swahili 16:19  Nitakupa funguo za Ufalme wa mbinguni; kila utakachofunga duniani, kitafungwa pia mbinguni; kila utakachofungua duniani, kitafunguliwa pia mbinguni."
Matt Swahili 16:20  Kisha akawaonya wanafunzi wasimwambie mtu yeyote kwamba yeye ndiye Kristo.
Matt Swahili 16:21  Tangu wakati huo Yesu alianza kuwajulisha waziwazi wanafunzi wake: "Ni lazima mimi niende Yerusalemu, na huko nikapate mateso mengi yatakayosababishwa na wazee, makuhani wakuu na walimu wa Sheria. Nitauawa, na siku ya tatu nitafufuliwa."
Matt Swahili 16:22  Hapo Petro akamchukua kando, akaanza kumkemea: "Isiwe hivyo Bwana! Jambo hili halitakupata!"
Matt Swahili 16:23  Lakini Yesu akageuka, akamwambia Petro, "Ondoka mbele yangu Shetani! Wewe ni kikwazo kwangu. Mawazo yako si ya mungu bali ni ya kibinadamu!"
Matt Swahili 16:24  Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Kama mtu yeyote anataka kuwa mfuasi wangu, ni lazima ajikane mwenyewe, auchukue msalaba wake, anifuate.
Matt Swahili 16:25  Maana, mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe, atayapoteza;
Matt Swahili 16:26  lakini mtu anayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu, atayapata. Je, mtu atafaidi nini akiupata utajiri wote wa ulimwengu na hali amepoteza maisha yake? Au, mtu atatoa kitu gani kiwe badala ya maisha yake?
Matt Swahili 16:27  Maana, Mwana wa Mtu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika wake, na hapo ndipo atakapomlipa kila mtu kadiri ya matendo yake.
Matt Swahili 16:28  Kweli nawaambieni, wako wengine papahapa ambao hawatakufa kabla ya kumwona Mwana wa Mtu akija katika Ufalme wake."