Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
MATTHEW
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 26
Matt Swahili 26:1  Yesu alipomaliza kusema hayo yote, aliwaambia wanafunzi wake,
Matt Swahili 26:2  "Mnajua kwamba baada ya siku mbili tutakuwa na sikukuu ya Pasaka, na Mwana wa Mtu atatolewa ili asulubiwe."
Matt Swahili 26:3  Wakati huo makuhani wakuu na wazee wa watu walikutana pamoja katika ukumbi wa Kayafa, Kuhani Mkuu.
Matt Swahili 26:4  Wakashauriana jinsi ya kumtia Yesu nguvuni kwa hila wamuue.
Matt Swahili 26:5  Lakini wakaamua jambo hilo lisifanyike wakati wa sikukuu, kusije kukatokea ghasia kati ya watu.
Matt Swahili 26:6  Yesu alipokuwa Bethania, nyumbani kwa Simoni, aitwaye Mkoma,
Matt Swahili 26:7  mama mmoja aliyekuwa na chupa ya alabasta yenye marashi ya thamani kubwa, alimjia pale mezani alipokuwa amekaa kula chakula, akammiminia hayo marashi kichwani.
Matt Swahili 26:8  Wanafunzi wake walipoona hayo wakakasirika, wakasema, "Ya nini hasara hii?
Matt Swahili 26:9  Marashi haya yangaliweza kuuzwa kwa bei kubwa, maskini wakapewa hizo fedha."
Matt Swahili 26:10  Yesu alitambua mawazo yao, akawaambia, "Mbona mnamsumbua huyu mama? Yeye amenitendea jambo jema.
Matt Swahili 26:11  Maskini mnao daima pamoja nanyi, lakini mimi sitakuwapo pamoja nanyi daima.
Matt Swahili 26:12  Huyu mama amenimiminia marashi ili kunitayarisha kwa maziko.
Matt Swahili 26:13  Nawaambieni kweli, popote ambapo hii Habari Njema itahubiriwa ulimwenguni, kitendo hiki alichofanya mama huyu kitatajwa kwa kumkumbuka yeye."
Matt Swahili 26:14  Kisha, Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili, akaenda kwa makuhani wakuu,
Matt Swahili 26:15  akawaambia, "Mtanipa kitu gani kama nikimkabidhi Yesu kwenu?" Wakamhesabia sarafu thelathini za fedha;
Matt Swahili 26:16  na tangu wakati huo Yuda akawa anatafuta nafasi ya kumsaliti.
Matt Swahili 26:17  Siku ya kwanza kabla ya Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, wanafunzi walimwendea Yesu wakamwuliza, "Unataka tukuandalie wapi chakula cha Pasaka?"
Matt Swahili 26:18  Yeye akawajibu, "Nendeni mjini kwa mtu fulani, mkamwambie: Mwalimu anasema, wakati wangu umefika; kwako nitakula Pasaka pamoja na wanafunzi wangu."
Matt Swahili 26:19  Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaandaa Pasaka.
Matt Swahili 26:20  Kulipokuwa jioni, Yesu akakaa mezani pamoja na wanafunzi wake kumi na wawili.
Matt Swahili 26:21  Walipokuwa wakila, Yesu akasema, "Nawaambieni kweli, mmoja wenu atanisaliti."
Matt Swahili 26:22  Wanafunzi wakahuzunika sana, wakaanza kuuliza mmojammoja, "Bwana! Je, ni mimi?"
Matt Swahili 26:23  Yesu akajibu, "Atakayechovya mkate pamoja nami katika bakuli ndiye atakayenisaliti.
Matt Swahili 26:24  Naam, Mwana wa Mtu anakwenda zake kama Maandiko Matakatifu yasemavyo, lakini ole wake mtu yule atakayemsaliti Mwana wa Mtu! Ingalikuwa afadhali kwa mtu huyo kama hangalizaliwa."
Matt Swahili 26:25  Yuda, ambaye ndiye aliyetaka kumsaliti, akamwuliza, "Mwalimu! Je, ni mimi?" Yesu akamjibu, "Wewe umesema."
Matt Swahili 26:26  Walipokuwa wanakula, Yesu akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa wanafunzi wake akisema, "Twaeni mle; huu ni mwili wangu."
Matt Swahili 26:27  Kisha akatwaa kikombe, akamshukuru Mungu, akawapa akisema, "Nyweni nyote;
Matt Swahili 26:28  maana hii ni damu yangu inayothibitisha agano, damu inayomwagwa kwa ajili ya watu wengi ili kuwaondolea dhambi.
Matt Swahili 26:29  Nawaambieni, sitakunywa tena divai ya zabibu mpaka siku ile nitakapoinywa mpya pamoja nanyi katika Ufalme wa Baba yangu."
Matt Swahili 26:30  Baada ya kuimba wimbo, wakaondoka, wakaenda katika mlima wa Mizeituni.
Matt Swahili 26:31  Kisha Yesu akawaambia, "Usiku huu wa leo, ninyi nyote mtakuwa na mashaka nami, maana Maandiko Matakatifu yasema: Nitampiga mchungaji, na kondoo wa kundi watatawanyika.
Matt Swahili 26:32  Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulieni Galilaya."
Matt Swahili 26:33  Petro akamwambia Yesu "Hata kama wote watakuwa na mashaka nawe na kukuacha, mimi sitakuacha kamwe."
Matt Swahili 26:34  Yesu akamwambia, "Kweli nakwambia, usiku huu kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu."
Matt Swahili 26:35  Petro akamwambia, "Hata kama ni lazima nife pamoja nawe, sitakukana kamwe." Wale wanafunzi wengine wote wakasema vivyo hivyo.
Matt Swahili 26:36  Kisha Yesu akaenda pamoja nao bustanini Gethsemane, akawaambia wanafunzi wake, "Kaeni hapa nami niende pale mbele kusali."
Matt Swahili 26:37  Akawachukua Petro na wana wawili wa Zebedayo, akaanza kuwa na huzuni na mahangaiko.
Matt Swahili 26:38  Hapo akawaambia, "Nina huzuni kubwa moyoni hata karibu kufa. Kaeni hapa mkeshe pamoja nami."
Matt Swahili 26:39  Basi, akaenda mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akasali: "Baba yangu, kama inawezekana, aacha kikombe hiki cha mateso kinipite; lakini isiwe nitakavyo mimi, ila utakavyo wewe."
Matt Swahili 26:40  Akawaendea wale wanafunzi, akawakuta wamelala. Akamwambia Petro, "Ndiyo kusema hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja?
Matt Swahili 26:41  Kesheni na kusali ili msije mkaingia katika majaribu. Roho i tayari lakini mwili ni dhaifu."
Matt Swahili 26:42  Akaenda tena mara ya pili akasali: "Baba yangu, kama haiwezekani kikombe hiki kinipite bila mimi kukinywa, basi, mapenzi yako yafanyike."
Matt Swahili 26:43  Akawaendea tena, akawakuta wamelala, maana macho yao yalikuwa yamebanwa na usingizi.
Matt Swahili 26:44  Basi, akawaacha, akaenda tena kusali mara ya tatu kwa maneno yaleyale.
Matt Swahili 26:45  Kisha akawaendea wale wanafunzi, akawaambia, "Je, mngali mmelala na kupumzika? Tazameni! Saa yenyewe imefika, na Mwana wa Mtu atatolewa kwa watu wenye dhambi.
Matt Swahili 26:46  Amkeni, twendeni zetu. Tazameni! Anakuja yule atakayenisaliti."
Matt Swahili 26:47  Basi, Yesu alipokuwa bado anasema nao, mara akaja Yuda, mmoja wa wale kumi na wawili. Pamoja naye walikuja watu wengi wenye mapanga na marungu ambao walitumwa na makuhani wakuu na wazee wa watu.
Matt Swahili 26:48  Huyo aliyetaka kumsaliti Yesu, alikuwa amekwisha wapa ishara akisema: "Yule nitakayembusu ndiye; mkamateni."
Matt Swahili 26:49  Basi, Yuda akamkaribia Yesu, akamwambia, "Shikamoo, Mwalimu!" Kisha akambusu.
Matt Swahili 26:50  Yesu akamwambia, "Rafiki, fanya ulichokuja kufanya." Hapo wale watu wakaja, wakamkamata Yesu, wakamtia nguvuni.
Matt Swahili 26:51  Mmoja wa wale waliokuwa pamoja na Yesu akanyosha mkono, akauchomoa upanga wake, akampiga mtumishi wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio.
Matt Swahili 26:52  Hapo Yesu akamwambia, "Rudisha upanga wako alani, maana yeyote anayeutumia upanga, atakufa kwa upanga.
Matt Swahili 26:53  Je, hamjui kwamba ningeweza kumwomba Baba yangu naye mara angeniletea zaidi ya majeshi kumi na mawili ya malaika?
Matt Swahili 26:54  Lakini yatatimiaje Maandiko Matakatifu yasemayo kwamba ndivyo inavyopaswa kuwa?"
Matt Swahili 26:55  Wakati huohuo Yesu akauambia huo umati wa watu waliokuja kumtia nguvuni, "Je, mmekuja kunikamata kwa mapanga na marungu kama kwamba mimi ni mnyang'anyi? Kila siku nilikuwa Hekaluni nikifundisha, na hamkunikamata!
Matt Swahili 26:56  Lakini haya yote yametendeka ili Maandiko ya manabii yatimie." Kisha wanafunzi wote wakamwacha, wakakimbia.
Matt Swahili 26:57  Basi, hao watu waliomkamata Yesu walimpeleka nyumbani kwa Kayafa, Kuhani Mkuu, walikokusanyika walimu wa Sheria na wazee.
Matt Swahili 26:58  Petro alimfuata kwa mbali mpaka uani kwa Kuhani Mkuu, akaingia ndani pamoja na walinzi ili apate kuona mambo yatakavyokuwa.
Matt Swahili 26:59  Basi, makuhani wakuu na Baraza lote wakatafuta ushahidi wa uongo dhidi ya Yesu wapate kumwua,
Matt Swahili 26:60  lakini hawakupata ushahidi wowote, ingawa walikuja mashahidi wengi wa uongo. Mwishowe wakaja mashahidi wawili,
Matt Swahili 26:61  wakasema, "Mtu huyu alisema: Ninaweza kuliharibu Hekalu la Mungu na kulijenga tena kwa siku tatu."
Matt Swahili 26:62  Kuhani Mkuu akasimama, akamwuliza Yesu, "Je, hujibu neno? Watu hawa wanashuhudia nini dhidi yako?"
Matt Swahili 26:63  Lakini Yesu akakaa kimya. Kuhani Mkuu akamwambia, "Nakuapisha kwa Mungu aliye hai, twambie kama wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu!"
Matt Swahili 26:64  Yesu akamwambia, "Wewe umesema! Lakini nawaambieni, tangu sasa mtamwona Mwana wa Mtu ameketi upande wa kulia wa Mwenyezi, akija juu ya mawingu ya mbinguni."
Matt Swahili 26:65  Hapo, Kuhani Mkuu akararua mavazi yake, akasema, "Amekufuru! Tuna haja gani tena ya mashahidi? Sasa mmesikia kufuru yake.
Matt Swahili 26:66  Ninyi mwaonaje?" Wao wakamjibu, "Anastahili kufa!"
Matt Swahili 26:67  Kisha wakamtemea mate usoni, wakampiga makofi. Wengine wakiwa wanampiga makofi,
Matt Swahili 26:68  wakasema, "Haya Kristo, tutabirie; ni nani amekupiga!"
Matt Swahili 26:69  Petro alikuwa ameketi nje uani. Basi, mtumishi mmoja wa kike akamwendea, akasema, "Wewe ulikuwa pamoja na Yesu wa Galilaya."
Matt Swahili 26:70  Petro akakana mbele ya wote akisema, "Sijui hata unasema nini."
Matt Swahili 26:71  Alipokuwa akitoka mlangoni, mtumishi mwingine wa kike akamwona, akawaambia wale waliokuwa pale, "Mtu huyu alikuwa pamoja na Yesu wa Nazareti."
Matt Swahili 26:73  Baadaye kidogo, watu waliokuwa pale wakamwendea Petro, wakamwambia, "Hakika, wewe pia ni mmoja wao, maana msemo wako unakutambulisha."
Matt Swahili 26:74  Hapo Petro akaanza kujilaani na kuapa akisema, "Simjui mtu huyo!" Mara jogoo akawika.
Matt Swahili 26:75  Petro akakumbuka maneno aliyoambiwa na Yesu: "Kabla jogoo hajawika, utanikana mara tatu." Basi, akatoka nje akalia sana.