Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
MATTHEW
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 27
Matt Swahili 27:1  Kulipopambazuka, makuhani wakuu wote na wazee wa watu walifanya mashauri juu ya Yesu wapate kumwua.
Matt Swahili 27:2  Wakamfunga pingu, wakamchukua, wakamkabidhi kwa Pilato, mkuu wa mkoa.
Matt Swahili 27:3  Hapo, Yuda ambaye ndiye aliyemsaliti, alipoona kwamba wamekwisha mhukumu Yesu, akajuta, akawarudishia makuhani wakuu zile sarafu thelathini za fedha.
Matt Swahili 27:4  Akawaambia, "Nimekosa kwa kumtoa mtu asiye na hatia auawe." Lakini wao wakasema, "Yatuhusu nini sisi? Hilo ni shauri lako."
Matt Swahili 27:5  Naye akazitupa zile fedha Hekaluni, akatoka nje, akaenda akajinyonga.
Matt Swahili 27:6  Makuhani wakuu wakazichukua zile fedha, wakasema, "Haifai kuziweka katika hazina ya Hekalu kwa maana ni fedha za damu."
Matt Swahili 27:7  Basi, wakashauriana, wakazitumia kununua shamba la mfinyanzi liwe mahali pa kuzika wageni.
Matt Swahili 27:8  Ndiyo maana mpaka leo shamba hilo linaitwa Shamba la Damu.
Matt Swahili 27:9  Hivyo maneno ya nabii Yeremia yakatimia: "Walizichukua sarafu thelathini za fedha, thamani ya yule ambaye watu wa Israeli walipanga bei,
Matt Swahili 27:10  wakanunua nazo shamba la mfinyanzi, kama Bwana alivyoniagiza."
Matt Swahili 27:11  Yesu alisimamishwa mbele ya mkuu wa mkoa. Basi, mkuu wa mkoa akamwuliza, "Je, wewe ndiwe Mfalme wa Wayahudi?" Yesu akamwambia, "Wewe umesema."
Matt Swahili 27:12  Lakini makuhani wakuu na wazee walipokuwa wanamshtaki, hakujibu neno.
Matt Swahili 27:13  Hivyo Pilato akamwuliza, "Je, husikii mashtaka hayo yote wanayotoa juu yako?"
Matt Swahili 27:14  Lakini Yesu hakumjibu hata neno moja; hata huyo mkuu wa mkoa akashangaa sana.
Matt Swahili 27:15  Ilikuwa kawaida wakati wa Sikukuu ya Pasaka mkuu wa mkoa kuwafungulia Wayahudi mfungwa mmoja waliyemtaka.
Matt Swahili 27:16  Wakati huo kulikuwa na mfungwa mmoja, jina lake Baraba.
Matt Swahili 27:17  Hivyo, watu walipokusanyika pamoja, Pilato akawauliza, "Mwataka nimfungue yupi kati ya wawili hawa, Baraba ama Yesu aitwae Kristo?"
Matt Swahili 27:18  Alisema hivyo maana alijua wazi kwamba walimleta kwake kwa sababu ya wivu.
Matt Swahili 27:19  Pilato alipokuwa amekaa katika kiti cha hukumu, mke wake akampelekea ujumbe: "Usijitie katika shauri la mtu huyu mwema, maana leo nimeteseka sana katika ndoto kwa sababu yake."
Matt Swahili 27:20  Lakini makuhani wakuu na wazee wakawashawishi watu waombe Baraba afunguliwe na Yesu auawe.
Matt Swahili 27:21  Mkuu wa mkoa akawauliza, "Ni yupi kati ya hawa wawili mnayetaka nimfungue?" Wakamjibu, "Baraba!"
Matt Swahili 27:22  Pilato akawauliza, "Sasa, nifanye nini na Yesu aitwaye Kristo?" Wote wakasema, "Asulubiwe!"
Matt Swahili 27:23  Pilato akauliza, "Kwa nini? Amefanya kosa gani?" Wao wakazidi kupaaza sauti: "Asulubiwe!"
Matt Swahili 27:24  Basi, Pilato alipotambua kwamba hafanikiwi chochote na kwamba maasi yalikuwa yanaanza, alichukua maji, akanawa mikono mbele ya ule umati wa watu, akasema, "Mimi sina lawama juu ya kifo cha mtu huyu; shauri lenu wenyewe."
Matt Swahili 27:25  Watu wote wakasema, "Damu yake na iwe juu yetu na juu ya watoto wetu!"
Matt Swahili 27:26  Hapo Pilato akawafungulia Baraba kutoka gerezani, lakini akamtoa Yesu asulubiwe.
Matt Swahili 27:27  Kisha askari wa mkuu wa mkoa wakamwingiza Yesu ndani ya ikulu, wakamkusanyikia kikosi kizima.
Matt Swahili 27:28  Wakamvua nguo zake, wakamvika joho la rangi nyekundu.
Matt Swahili 27:29  Kisha wakasokota taji ya miiba, wakamvika kichwani, wakamwekea pia mwanzi katika mkono wake wa kulia. Wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki wakisema, "Shikamoo mfalme wa Wayahudi!"
Matt Swahili 27:30  Wakamtemea mate, wakauchukua ule mwanzi, wakampiga nao kichwani.
Matt Swahili 27:31  Baada ya kumdhihaki, wakamvua lile joho, wakamvika nguo zake, kisha wakampeleka kumsulubisha.
Matt Swahili 27:32  Walipokuwa wakienda, wakamkuta mtu mmoja jina lake Simoni, mwenyeji wa Kurene, wakamlazimisha kuuchukua msalaba wake Yesu.
Matt Swahili 27:33  Walipofika mahali paitwapo Golgotha, maana yake, "Mahali pa Fuvu la kichwa,"
Matt Swahili 27:34  wakampa mchanganyiko wa divai na nyongo. Lakini Yesu alipoonja akakataa kunywa.
Matt Swahili 27:35  Walimsulubisha, kisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura.
Matt Swahili 27:37  Juu ya kichwa chake wakaweka shtaka dhidi yake lilioandikwa, "Huyu ni Yesu, Mfalme wa Wayahudi."
Matt Swahili 27:38  Wanyang'anyi wawili walisulubishwa pia pamoja naye, mmoja upande wa kushoto na mwingine upande wa kulia.
Matt Swahili 27:39  Watu waliokuwa wanapita mahali hapo walimtukana wakitikisa vichwa vyao na kusema,
Matt Swahili 27:40  "Wewe! Si ulijidai kulivunja Hekalu na kulijenga kwa siku tatu? Sasa jiokoe mwenyewe. Kama wewe ni Mwana wa Mungu, basi shuka msalabani!"
Matt Swahili 27:41  Hali kadhalika na makuhani wakuu pamoja na walimu wa Sheria na wazee walimdhihaki wakisema,
Matt Swahili 27:42  "Aliwaokoa wengine, lakini kujiokoa mwenyewe hawezi! Eti yeye ni mfalme wa Wayahudi! Basi, sasa na ashuke msalabani, nasi tutamwamini.
Matt Swahili 27:43  Alimtumainia Mungu na kusema eti yeye ni Mwana wa Mungu; basi, Mungu na amwokoe kama anamtaka."
Matt Swahili 27:44  Hali kadhalika na wale waliosulubiwa pamoja naye wakamtukana.
Matt Swahili 27:45  Tangu saa sita mchana mpaka saa tisa, nchi yote ikawa katika giza.
Matt Swahili 27:46  Mnamo saa tisa Yesu akalia kwa sauti kubwa, "Eli, Eli, lema sabakthani?" Maana yake, "Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?"
Matt Swahili 27:47  Lakini wale waliosimama pale waliposikia hivyo wakasema, "Anamwita Eliya."
Matt Swahili 27:48  Mmoja wao akakimbia, akachukua sifongo, akaichovya katika siki, akaiweka juu ya mwanzi, akampa anywe.
Matt Swahili 27:49  Wengine wakasema, "Acha tuone kama Eliya anakuja kumwokoa."
Matt Swahili 27:50  Basi, Yesu akalia tena kwa sauti kubwa, akakata roho.
Matt Swahili 27:51  Hapo pazia la Hekalu likapasuka vipande viwili, toka juu mpaka chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka;
Matt Swahili 27:52  makaburi yakafunguka na watu wengi wa Mungu waliokufa wakafufuliwa;
Matt Swahili 27:53  nao, baada ya kufufuka kwake, wakatoka makaburini, wakaingia katika Mji Mtakatifu, wakaonekana na watu wengi.
Matt Swahili 27:54  Basi, jemadari na wale waliokuwa wakimlinda Yesu walipoona tetemeko la ardhi na yale mambo yaliyotukia, wakaogopa sana, wakasema, "Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu."
Matt Swahili 27:55  Mahali hapo walikuwapo wanawake wengi wakitazama kwa mbali. Hao ndio wale waliomfuata Yesu kutoka Galilaya wakimtumikia.
Matt Swahili 27:56  Miongoni mwao walikuwa Maria Magdalene, Maria mama yao Yakobo na Yosefu, pamoja na mama yao wana wa Zebedayo.
Matt Swahili 27:57  Ilipokuwa jioni, akaja mtu mmoja tajiri mwenyeji wa Armathaya, jina lake Yosefu. Yeye pia alikuwa mwanafunzi wa Yesu.
Matt Swahili 27:58  Akamwendea Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu. Basi, Pilato akaamuru apewe.
Matt Swahili 27:59  Yosefu akauchukua ule mwili akauzungushia sanda safi ya kitani,
Matt Swahili 27:60  akauweka ndani ya kaburi lake jipya alilokuwa amelichonga katika mwamba. Kisha akavingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango wa kaburi, akaenda zake.
Matt Swahili 27:61  Maria Magdalene na yule Maria mwingine walikuwa wameketi kulielekea kaburi.
Matt Swahili 27:62  Kesho yake, yaani siku iliyofuata ile ya Maandalio, makuhani wakuu na Mafarisayo walimwendea Pilato,
Matt Swahili 27:63  Wakasema, "Mheshimiwa, tunakumbuka kwamba yule mdanganyifu alisema kabla ya kufa ati, Baada ya siku tatu nitafufuka.
Matt Swahili 27:64  Kwa hiyo amuru kaburi lilindwe mpaka siku ya tatu ili wanafunzi wake wasije wakamwiba na kuwaambia watu kwamba amefufuka. Uongo huu wa mwisho utakuwa mbaya kuliko ule wa awali."
Matt Swahili 27:65  Pilato akawaambia, "Haya, mnao walinzi; nendeni mkalinde kadiri mjuavyo."
Matt Swahili 27:66  Basi, wakaenda, wakalilinda kaburi, wakatia mhuri juu ya lile jiwe na kuacha hapo askari walinzi.