Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
MATTHEW
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 25
Matt Swahili 25:1  "Wakati huo, Ufalme wa mbinguni utafanana na wasichana kumi waliochukua taa zao, wakaenda kumlaki bwana arusi.
Matt Swahili 25:2  Watano miongoni mwao walikuwa wapumbavu na watano walikuwa wenye busara.
Matt Swahili 25:3  Wale wapumbavu walichukua taa zao, lakini hawakuchukua akiba ya mafuta.
Matt Swahili 25:4  Lakini wale wenye busara walichukua mafuta katika chupa pamoja na taa zao.
Matt Swahili 25:5  Kwa kuwa bwana arusi alikawia kuja, wale wanawali wote wote walisinzia, wakalala.
Matt Swahili 25:6  Usiku wa manane kukawa na kelele: Haya, haya! Bwana arusi anakuja; nendeni kumlaki.
Matt Swahili 25:7  Hapo wale wanawali wote wakaamka, wakazitayarisha taa zao.
Matt Swahili 25:8  Wale wapumbavu wakawaambia wale wenye busara: Tupeni mafuta yenu kidogo maana taa zetu zinazimika.
Matt Swahili 25:9  Lakini wale wenye busara wakawaambia, Hayatatutosha sisi na ninyi! Afadhali mwende dukani mkajinunulie wenyewe!
Matt Swahili 25:10  Basi, wale wanawali wapumbavu walipokwenda kununua mafuta, bwana arusi akafika, na wale wanawali waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye katika jumba la arusi, kisha mlango ukafungwa.
Matt Swahili 25:11  Baadaye wale wanawali wengine wakaja, wakaita: Bwana, bwana, tufungulie!
Matt Swahili 25:12  Lakini yeye akawajibu, Nawaambieni kweli, siwajui ninyi."
Matt Swahili 25:13  Kisha Yesu akasema, "Kesheni basi, kwa maana hamjui siku wala saa.
Matt Swahili 25:14  "Itakuwa kama mtu mmoja aliyetaka kusafiri ng'ambo: aliwaita watumishi wake, akawakabidhi mali yake.
Matt Swahili 25:15  Alimpa kila mmoja kadiri ya uwezo wake: mmoja sarafu tano za fedha ziitwazo talanta, mwingine talanta mbili na mwingine talanta moja, kisha akasafiri.
Matt Swahili 25:16  Mara yule aliyekabidhiwa talanta tano akafanya kazi nazo akapata faida talanta tano.
Matt Swahili 25:17  Hali kadhalika na yule aliyekabidhiwa talanta mbili akapata faida talanta mbili.
Matt Swahili 25:18  Lakini yule aliyekabidhiwa talanta moja akaenda akachimba shimo ardhini, akaificha fedha ya bwana wake.
Matt Swahili 25:19  "Baada ya muda mrefu, yule bwana alirudi, akaanza kukagua hesabu ya matumizi na mapato ya fedha yake.
Matt Swahili 25:20  Mtumishi aliyekabidhiwa talanta tano akaja amechukua zile talanta tano faida, akamwambia, Bwana, ulinikabidhi talanta tano, hapa pana talanta tano zaidi faida niliyopata.
Matt Swahili 25:21  Bwana wake akamwambia, Vema, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu katika mambo madogo nitakukabidhi makubwa. Njoo ufurahi pamoja na bwana wako.
Matt Swahili 25:22  "Mtumishi aliyekabidhiwa talanta mbili akaja, akatoa talanta mbili faida, akisema, Bwana, ulinikabidhi talanta mbili. Chukua talanta mbili zaidi faida niliyopata.
Matt Swahili 25:23  Bwana wake akamwambia, Vema, mtumishi mwema na mwaminifu. Umekuwa mwaminifu katika mambo madogo, nitakukabidhi makubwa. Njoo ufurahi pamoja na bwana wako.
Matt Swahili 25:24  "Lakini yule aliyekabidhiwa talanta moja akaja, akasema, Bwana, najua wewe ni mtu mgumu; wewe huvuna pale ambapo hukupanda, na kukusanya pale ambapo hukutawanya.
Matt Swahili 25:25  Niliogopa, nikaificha fedha yako katika ardhi. Chukua basi mali yako.
Matt Swahili 25:26  "Bwana wake akamwambia, Wewe ni mtumishi mwovu na mvivu! Unajua kuwa mimi huvuna mahali ambapo sikupanda, na hukusanya pale ambapo sikutawanya.
Matt Swahili 25:27  Ilikupasa basi, kuiweka fedha yangu katika benki, nami ningelichukua mtaji wangu na faida yake!
Matt Swahili 25:28  Basi, mnyang'anyeni hiyo fedha mkampe yule mwenye talanta kumi.
Matt Swahili 25:29  Maana, aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa.
Matt Swahili 25:30  Na kuhusu huyu mtumishi asiye na faida, mtupeni nje gizani! Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.
Matt Swahili 25:31  "Wakati Mwana wa Mtu atakapokuja katika utukufu wake na malaika wote wakiwa pamoja naye, hapo ataketi juu ya kiti chake cha enzi kitukufu,
Matt Swahili 25:32  na mataifa yote yatakusanyika mbele yake, naye atawatenganisha watu kama mchungaji anavyotenganisha kondoo na mbuzi.
Matt Swahili 25:33  Atawaweka kondoo upande wake wa kulia na mbuzi upande wake wa kushoto.
Matt Swahili 25:34  "Kisha Mfalme atawaambia wale walio upande wake wa kulia, Njoni enyi mliobarikiwa na Baba yangu; pokeeni Ufalme mliotayarishiwa tangu kuumbwa kwa ulimwengu.
Matt Swahili 25:35  Maana nilikuwa na njaa nanyi mkanipa chakula; nilikuwa na kiu nanyi mkanipa maji; nilikuwa mgeni nanyi mkanikaribisha;
Matt Swahili 25:36  nilikuwa uchi, mkanivika; nilikuwa mgonjwa nanyi mkaja kunitazama; nilikuwa gerezani nanyi mkaja kunitembelea.
Matt Swahili 25:37  Hapo, hao watu wema watamjibu mfalme Bwana, ni lini tulikuona mwenye njaa nasi tukakupa chakula, au ukiwa na kiu nasi tukakunywesha maji?
Matt Swahili 25:38  Ni lini tulikuona ukiwa mgeni nasi tukakukaribisha, au bila nguo nasi tukakuvika?
Matt Swahili 25:39  Ni lini tulikuona ukiwa mgonjwa au mfungwa nasi tukaja kukutazama?
Matt Swahili 25:40  Mfalme atawajibu, Kweli nawaambieni, kila kitu mlichomtendea mmojawapo wa hawa ndugu zangu wadogo, mlinitendea mimi.
Matt Swahili 25:41  "Kisha atawaambia wale walio upande wake wa kushoto, Ondokeni mbele yangu enyi mliolaaniwa! Nendeni katika moto wa milele aliotayarishiwa Ibilisi na malaika wake.
Matt Swahili 25:42  Maana nilikuwa na njaa nanyi hamkunipa chakula; nilikuwa na kiu nanyi hamkunipa maji.
Matt Swahili 25:43  Nilikuwa mgeni nanyi hamkunikaribisha; nilikuwa mgonjwa na mfungwa nanyi hamkuja kunitazama.
Matt Swahili 25:44  "Hapo nao watajibu, Bwana, ni lini tulikuona ukiwa na njaa au kiu, ukiwa mgeni au bila nguo, ukiwa mgonjwa au mfungwa, nasi hatukuja kukuhudumia?
Matt Swahili 25:45  Naye atawajibu, Nawaambieni kweli, kila mlipokataa kumtendea mambo haya mmojawapo wa hawa wadogo, mlikataa kunitendea mimi.
Matt Swahili 25:46  Basi, hawa watakwenda kwenye adhabu ya milele, lakini wale waadilifu watakwenda kwenye uzima wa milele."