Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
ACTS
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 25
Acts Swahili 25:1  Siku tatu baada ya kufika mkoani, Festo alitoka Kaisarea, akaenda Yerusalemu.
Acts Swahili 25:2  Makuhani wakuu pamoja na viongozi wa Wayahudi walimpa habari kuhusu mashtaka yaliyokuwa yanamkabili Paulo. Walimsihi Festo
Acts Swahili 25:3  awafanyie fadhili kwa kumleta Paulo Yerusalemu; walikuwa wamekula njama wamuue akiwa njiani.
Acts Swahili 25:4  Lakini Festo alijibu, "Paulo atabaki kizuizini kule Kaisarea na mimi nitakwenda huko karibuni.
Acts Swahili 25:5  Waacheni viongozi wenu waende huko pamoja nami wakatoe mashtaka yao juu yake kama amefanya chochote kiovu."
Acts Swahili 25:6  Festo alikaa nao kwa muda wa siku nane au kumi hivi, kisha akarudi Kaisarea. Kesho yake alikwenda barazani, akaamuru Paulo aletwe ndani.
Acts Swahili 25:7  Wakati Paulo alipofika, Wayahudi waliokuwa wametoka Yerusalemu walimzunguka wakaanza kutoa mashtaka mengi mazitomazito ambayo hawakuweza kuthibitisha.
Acts Swahili 25:8  Kwa kujitetea, Paulo alisema, "Mimi sikufanya kosa lolote kuhusu Sheria ya Wayahudi, wala kuhusu Hekalu, wala kumhusu Kaisari."
Acts Swahili 25:9  Festo alitaka kujipendekeza kwa Wayahudi na hivyo akamwuliza Paulo, "Je, ungependa kwenda Yerusalemu na huko ukahukumiwe mbele yangu kuhusu mashtaka haya?"
Acts Swahili 25:10  Paulo akajibu, "Nasimama mbele ya mahakama ya Kaisari na papa hapa ndipo ninapopaswa kupewa hukumu. Kama unavyojua vizuri, sikuwatendea Wayahudi ubaya wowote.
Acts Swahili 25:11  Basi, ikiwa nimepatikana na kosa linalostahili adhabu ya kifo, siombi kusamehewa adhabu hiyo. Lakini kama hakuna ukweli katika mashtaka waliyotoa watu hawa, hakuna awezaye kunikabidhi kwao. Nakata rufani kwa Kaisari!"
Acts Swahili 25:12  Basi, baada ya Festo kuzungumza na washauri wake, akamwambia Paulo, "Umekata rufani kwa Kaisari, basi, utakwenda kwa Kaisari."
Acts Swahili 25:13  Siku chache baadaye, mfalme Agripa na Bernike walifika Kaisarea ili kutoa heshima zao kwa Festo.
Acts Swahili 25:14  Walikuwa huko siku kadhaa naye Festo akamweleza mfalme kesi ya Paulo: "Kuna mtu mmoja hapa ambaye Felisi alimwacha kizuizini.
Acts Swahili 25:15  Nilipokwenda Yerusalemu makuhani wakuu na wazee wa Wayahudi walimshtaki na kuniomba nimhukumu.
Acts Swahili 25:16  Lakini mimi niliwajibu kwamba si desturi ya Waroma kumtoa mtu aadhibiwe kabla mshtakiwa hajakutana na washtaki wake ana kwa ana na kupewa fursa ya kujitetea kuhusu hayo mashtaka.
Acts Swahili 25:17  Basi, walipofika hapa sikukawia, ila nilifanya kikao mahakamani kesho yake, nikaamuru mtu huyo aletwe.
Acts Swahili 25:18  Washtaki wake walisimama lakini hawakutoa mashtaka maovu kama nilivyokuwa ninatazamia.
Acts Swahili 25:19  Ila tu walikuwa na mabishano kadhaa pamoja naye kuhusu dini yao na kuhusu mtu mmoja aitwaye Yesu ambaye alikufa, lakini Paulo anashikilia kwamba yu hai.
Acts Swahili 25:20  Sikujua la kufanya kuhusu shauri hilo. Basi, nilimwuliza Paulo kama angependa kwenda mahakamani kule Yerusalemu kwa ajili ya mashtaka hayo.
Acts Swahili 25:21  Lakini Paulo alikata rufani, akaomba aachwe kizuizini mpaka uamuzi wa shauri hilo ufanywe na Kaisari. Kwa hiyo niliamua akae kizuizini mpaka nitakapoweza kumpeleka kwa Kaisari."
Acts Swahili 25:22  Basi Agripa akamwambia Festo, "Ningependa kumsikia mtu huyu mimi mwenyewe." Festo akamwambia, "Utamsikia kesho."
Acts Swahili 25:23  Hivyo, kesho yake, Agripa na Bernike walifika kwa shangwe katika ukumbi wa mkutano wakiwa wameandamana na wakuu wa majeshi na viongozi wa mji. Festo aliamuru Paulo aletwe ndani,
Acts Swahili 25:24  Kisha akasema, "Mfalme Agripa na wote mlioko hapa pamoja nasi! Hapa mbele yenu yuko mtu ambaye jumuiya yote ya Wayahudi hapa na kule Yerusalemu walinilalamikia wakipiga kelele kwamba hastahili kuishi tena.
Acts Swahili 25:25  Lakini mimi sikuona kuwa alikuwa ametenda chochote kibaya hata astahili kupewa adhabu ya kifo. Lakini, kwa vile Paulo mwenyewe alikata rufani kwa Kaisari, niliamua kumpeleka.
Acts Swahili 25:26  Kwa upande wangu sina habari kamili ambayo naweza kumwandikia Kaisari juu yake. Ndiyo maana nimemleta hapa mbele yenu na mbele yako mfalme Agripa, ili baada ya kumchunguza, niweze kuwa na la kuandika.
Acts Swahili 25:27  Kwa maana nadhani itakuwa kichekesho kumpeleka mfungwa bila kutaja wazi mashtaka yanayomkabili."