Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
ACTS
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 28
Acts Swahili 28:1  Tulipokwisha fika salama kwenye nchi kavu, tuligundua kwamba kile kisiwa kinaitwa Malta.
Acts Swahili 28:2  Wenyeji wa hapo walikuwa wema sana kwetu. Mvua ilikuwa inaanza kunyesha na kulikuwa na baridi, hivyo waliwasha moto, wakatukaribisha.
Acts Swahili 28:3  Paulo aliokota mzigo mdogo wa kuni akawa anazitia motoni. Hapo, kwa sababu ya lile joto la moto, nyoka akatoka katika kuni akamnasa Paulo mkononi na kujishikilia hapo.
Acts Swahili 28:4  Wenyeji wa pale walipokiona kile kiumbe kinaning'inia kwenye mkono wake waliambiana, "Bila shaka mtu huyu amekwisha ua mtu, na ingawa ameokoka kuangamia baharini, Haki haitamwacha aendelee kuishi!"
Acts Swahili 28:5  Lakini Paulo alikikung'utia kile kiumbe motoni na hakuumizwa hata kidogo.
Acts Swahili 28:6  Wale watu walikuwa wakitazamia kwamba angevimba au hapohapo angeanguka chini na kufa. Baada ya kungojea kwa muda mrefu bila kuona kwamba Paulo amepatwa na jambo lolote lisilo la kawaida, walibadilisha fikira zao juu yake, wakasema kuwa ni mungu.
Acts Swahili 28:7  Karibu na mahali pale palikuwa na mashamba ya Publio, mkuu wa kile kisiwa. Publio alitukaribisha kirafiki, tukawa wageni wake kwa siku tatu.
Acts Swahili 28:8  Basi, ikawa kwamba baba yake Publio alikuwa amelala kitandani, mgonjwa, ana homa na kuhara. Paulo alikwenda kumwona na baada ya kusali, akaweka mikono yake juu ya mgonjwa, akamponya.
Acts Swahili 28:9  Kutokana na tukio hilo, wagonjwa wote katika kile kisiwa walikuja wakaponywa.
Acts Swahili 28:10  Watu walitupatia zawadi mbalimbali na wakati tulipoanza tena safari, walitia ndani ya meli masurufu tuliyohitaji.
Acts Swahili 28:11  Baada ya miezi mitatu tulianza tena safari yetu kwa meli moja ya Aleksandria iitwayo "Miungu Pacha". Meli hiyo ilikuwa imetia nanga kisiwani wakati wote wa baridi.
Acts Swahili 28:12  Tulifika katika mji wa Sirakusa, tukakaa hapo kwa siku tatu.
Acts Swahili 28:13  Toka huko tuling'oa nanga, tukazunguka na kufika Regio. Baada ya siku moja, upepo ulianza kuvuma kutoka kusini, na baada ya siku mbili tulifika bandari ya Potioli.
Acts Swahili 28:14  Huko tuliwakuta ndugu kadhaa ambao walituomba tukae nao kwa juma moja. Hivi ndivyo tulivyopata kufika Roma.
Acts Swahili 28:15  Ndugu wa kule Roma walipopata habari zetu, wakaja kutulaki kwenye soko la Apio na Mikahawa Mitatu. Paulo alipowaona alimshukuru Mungu, akapata moyo.
Acts Swahili 28:16  Tulipofika Roma, Paulo aliruhusiwa kukaa peke yake pamoja na askari mmoja wa kumlinda.
Acts Swahili 28:17  Baada ya siku tatu, Paulo aliwaita pamoja viongozi wa Kiyahudi wa mahali hapo. Walipokusanyika, Paulo aliwaambia, "Wananchi wenzangu, mimi, ingawa sikufanya chochote kibaya wala kupinga desturi za wazee wetu, nilitiwa nguvuni kule Yerusalemu na kutiwa mikononi mwa Waroma.
Acts Swahili 28:18  Waliponihoji na kuona kwamba sikuwa na hatia yeyote, walitaka kuniacha.
Acts Swahili 28:19  Lakini Wayahudi wengine walipinga jambo hilo, nami nikalazimika kukata rufani kwa Kaisari, ingawa sikuwa na chochote cha kuwashtaki wananchi wenzangu.
Acts Swahili 28:20  Ni kwa sababu hiyo nimeomba kuonana na kuongea nanyi, maana nimefungwa minyororo hii kwa sababu ya tumaini lile la Israeli."
Acts Swahili 28:21  Wao wakamwambia, "Sisi hatujapokea barua yoyote kutoka Yudea, wala hakuna ndugu yeyote aliyefika hapa na kutoa habari rasmi au kusema chochote kibaya juu yako.
Acts Swahili 28:22  Lakini tunafikiri inafaa tusikie kutoka kwako mwenyewe mambo yaliyo kichwani mwako. Kwa maana tujualo sisi kuhusu hicho kikundi ni kwamba kinapingwa kila mahali."
Acts Swahili 28:23  Basi, walipanga naye siku kamili ya kukutana, na wengi wakafika huko alikokuwa anakaa. Tangu asubuhi mpaka jioni Paulo aliwaeleza na kuwafafanulia juu ya Ufalme wa Mungu akijaribu kuwafanya wakubali habari juu ya Yesu kwa kutumia Sheria ya Mose na maandiko ya manabii.
Acts Swahili 28:24  Baadhi yao walikubali maneno yake, lakini wengine hawakuamini.
Acts Swahili 28:25  Basi, kukawa na mtengano wa fikira kati yao. Walipokuwa wanakwenda zao, Paulo alisema jambo hili, "Kweli ni sawa yale aliyoyanena Roho Mtakatifu kwa wazee wenu kwa njia ya nabii Isaya
Acts Swahili 28:26  akisema: Nenda kwa watu hawa ukawaambie: kusikia mtasikia, lakini hamtaelewa; kutazama mtatazama, lakini hamtaona.
Acts Swahili 28:27  Maana akili za watu hawa zimepumbaa, wameziba masikio yao, wamefumba macho yao. La sivyo, wangeona kwa macho yao, wangesikia kwa masikio yao. Wangeelewa kwa akili zao, na kunigeukia, asema Bwana, nami ningewaponya."
Acts Swahili 28:28  Halafu Paulo akamaliza na kusema, "Jueni basi, kwamba ujumbe wa Mungu juu ya wokovu umepelekwa kwa watu wa mataifa. Wao watasikiliza!"
Acts Swahili 28:29  Paulo alipokwisha sema hayo, Wayahudi walijiondokea huku wakiwa wanabishana vikali wao kwa wao.
Acts Swahili 28:30  Kwa muda wa miaka miwili mizima Paulo aliishi katika nyumba aliyoipanga yeye mwenyewe; akawa anawakaribisha wote waliofika kumsalimu.
Acts Swahili 28:31  Alikuwa akihubiri Ufalme wa Mungu na kufundisha juu ya Bwana Yesu Kristo kwa uhodari, bila kizuizi.