Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
ACTS
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 15
Acts Swahili 15:1  Basi, watu wengine walifika Antiokia kutoka Yudea wakaanza kuwafundisha wale ndugu wakisema, "Kama hamtatahiriwa kufuatana na mapokeo ya Sheria ya Mose, hamtaweza kuokolewa."
Acts Swahili 15:2  Jambo hili lilisababisha ubishi mkubwa, na baada ya Paulo na Barnaba kujadiliana nao, ikaamuliwa Paulo na Barnaba pamoja na waumini kadhaa wa lile kanisa la Antiokia waende Yerusalemu kuwaona wale mitume na wazee kuhusu jambo hilo.
Acts Swahili 15:3  Basi, kanisa liliwaaga, nao walipokuwa wanapitia Foinike na Samaria waliwaeleza watu jinsi mataifa mengine yalivyomgeukia Mungu. Habari hizo zikawafurahisha sana ndugu hao wote.
Acts Swahili 15:4  Walipofika Yerusalemu walikaribishwa na kanisa, mitume na wazee; nao wakawapa taarifa juu ya yote Mungu aliyoyafanya pamoja nao.
Acts Swahili 15:5  Lakini waumini wengine waliokuwa wa kikundi cha Mafarisayo walisimama, wakasema, "Ni lazima watu wa mataifa mengine watahiriwe na kufundishwa kuifuata Sheria ya Mose."
Acts Swahili 15:6  Basi, mitume na wazee walifanya mkutano maalum wa kuchunguza jambo hilo.
Acts Swahili 15:7  Baada ya majadiliano marefu, Petro alisimama, akasema, "Ndugu zangu, ninyi mnafahamu kwamba hapo awali Mungu alipenda kunichagua mimi miongoni mwenu niihubiri Habari Njema, ili watu wa mataifa wapate kusikia na kuamini.
Acts Swahili 15:8  Naye Mungu anayejua mioyo ya watu, alithibitisha kwamba amewakubali kwa kuwapa nao Roho Mtakatifu kama alivyotupa sisi.
Acts Swahili 15:9  Hakufanya ubaguzi wowote kati yetu na wao; aliitakasa mioyo yao kwa imani.
Acts Swahili 15:10  Sasa basi, kwa nini kumjaribu Mungu kwa kuwatwika hao waumini mzigo ambao wala babu zetu, wala sisi hatukuweza kuubeba?
Acts Swahili 15:11  Isiwe hivyo, ila tunaamini kwamba, sisi kama vile wao, tunaokolewa kwa njia ya neema ya Bwana Yesu."
Acts Swahili 15:12  Kikundi chote kilikaa kimya, kikawasikiliza Barnaba na Paulo wakieleza miujiza na maajabu ambayo Mungu alitenda kwa mikono yao kati ya watu wa mataifa mengine.
Acts Swahili 15:13  Walipomaliza kuongea, Yakobo alianza kusema: "Ndugu zangu, nisikilizeni!
Acts Swahili 15:14  Simoni ameeleza jinsi Mungu hapo awali alivyojishughulisha na watu wa mataifa mengine, akachagua baadhi yao wawe watu wake.
Acts Swahili 15:15  Jambo hili ni sawa kabisa na maneno ya manabii, kama Maandiko Matakatifu yasemavyo:
Acts Swahili 15:16  Baada ya mambo haya nitarudi. Nitaijenga tena ile nyumba ya Daudi iliyoanguka; nitayatengeneza magofu yake na kuijenga tena.
Acts Swahili 15:17  Hapo watu wengine wote, watu wa mataifa yote niliowaita wawe wangu, watamtafuta Bwana.
Acts Swahili 15:18  Ndivyo asemavyo Bwana, aliyefanya jambo hili lijulikane tangu kale.
Acts Swahili 15:19  "Kwa hiyo, uamuzi wangu ni huu: tusiwataabishe watu wa mataifa wanomgeukia Mungu.
Acts Swahili 15:20  Bali tuwapelekee barua kuwaambia wasile vyakula vilivyotiwa najisi kwa kutambikiwa sanamu za miungu; wajiepushe na uasherati; wasile mnyama yeyote aliyenyongwa, na wasinywe damu.
Acts Swahili 15:21  Kwa maana kwa muda mrefu maneno ya Mose yamekuwa yakihubiriwa katika kila mji na kusomwa katika masunagogi yote kila siku ya Sabato."
Acts Swahili 15:22  Mitume, wazee na kanisa lote waliamua kuwachagua watu fulani miongoni mwao na kuwatuma Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba. Basi, wakamchagua Yuda aitwaye pia Barsaba, na Sila ambao wote walikuwa wanajulikana zaidi kati ya ndugu.
Acts Swahili 15:23  Wakawapa barua hii: "Sisi mitume na wazee, ndugu zenu, tunawasalimuni ninyi ndugu wa mataifa mengine mlioko huko Antiokia, Siria na Kilikia.
Acts Swahili 15:24  Tumesikia kwamba watu wengine kutoka huku kwetu waliwavurugeni kwa maneno yao, wakaitia mioyo yenu katika wasiwasi. Lakini wamefanya hivyo bila ya idhini yoyote kutoka kwetu.
Acts Swahili 15:25  Hivyo, tumeamua kwa pamoja kuwachagua watu kadhaa na kuwatuma kwenu pamoja na wapenzi wetu Barnaba na Paulo,
Acts Swahili 15:26  ambao wamehatarisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo.
Acts Swahili 15:27  Kwa hiyo, tunawatuma Yuda na Sila kwenu; hawa watawaambieni wao wenyewe haya tuliyoandika.
Acts Swahili 15:28  Basi, Roho Mtakatifu na sisi tumekubali tusiwatwike mzigo zaidi ya mambo haya muhimu:
Acts Swahili 15:29  Msile vyakula vilivyotambikiwa sanamu; msinywe damu; msile nyama ya mnyama aliyenyongwa; na mjiepushe na uasherati. Mtakuwa mmefanya vema kama mkiepa kufanya mambo hayo. Wasalaam!"
Acts Swahili 15:30  Baada ya kuwaaga, hao wajumbe walielekea Antiokia ambako waliita mkutano wa waumini, wakawapa hiyo barua.
Acts Swahili 15:31  Walipoisoma hiyo barua, maneno yake yaliwatia moyo, wakafurahi sana.
Acts Swahili 15:32  Yuda na Sila, ambao nao walikuwa manabii, walizungumza na hao ndugu kwa muda mrefu wakiwatia moyo na kuwaimarisha.
Acts Swahili 15:33  Baada ya kukaa huko kwa muda fulani, ndugu wa Antiokia waliwaaga wakiwatakia amani, kisha wakarudi kwa wale waliokuwa wamewatuma.
Acts Swahili 15:35  Paulo na Barnaba walibaki huko Antiokia kwa muda; wakafundisha na kuhubiri neno la Bwana, pamoja na watu wengine wengi.
Acts Swahili 15:36  Baada ya siku kadhaa, Paulo alimwambia Barnaba, "Turudi tukawatembelee wale ndugu katika kila mji tulikolihubiri neno la Bwana tukajionee jinsi wanavyoendelea."
Acts Swahili 15:37  Barnaba alitaka wamchukue pia Yohane aitwaye Marko.
Acts Swahili 15:38  Lakini Paulo hakupendelea kumchukua Marko, ambaye awali aliwaacha kule Pamfulia na kukataa kushiriki katika kazi yao.
Acts Swahili 15:39  Basi kukatokea ubishi mkali kati yao, na wakaachana. Barnaba akamchukua Marko, wakapanda meli kwenda Kupro.
Acts Swahili 15:40  Naye Paulo akamchagua Sila, na baada ya ndugu wa mahali hapo kumweka chini ya ulinzi wa neema ya Bwana, akaondoka.
Acts Swahili 15:41  Katika safari hiyo alipitia Siria na Kilikia akiyaimarisha makanisa.