Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
ACTS
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 4
Acts Swahili 4:1  Petro na Yohane walipokuwa bado wanawahutubia watu, makuhani na mkuu wa walinzi wa Hekalu pamoja na Masadukayo walifika.
Acts Swahili 4:2  Walikasirika sana, maana hao mitume walikuwa wanawahubiria watu kwamba Yesu alifufuka, jambo ambalo linaonyesha wazi kwamba wafu watafufuka.
Acts Swahili 4:3  Basi, waliwatia nguvuni na kwa kuwa usiku ulikuwa umekaribia, wakawaweka chini ya ulinzi mpaka kesho yake.
Acts Swahili 4:4  Lakini wengi kati ya wale waliosikia ujumbe wao waliamini, na idadi ya waumini ikawa imefika karibu elfu tano.
Acts Swahili 4:5  Kesho yake, viongozi wa Wayahudi, wazee na walimu wa Sheria, walikusanyika pamoja huko Yerusalemu.
Acts Swahili 4:6  Walikutana pamoja na Anasi, Kayafa, Yohane, Aleksanda na wengine waliokuwa wa ukoo wa Kuhani Mkuu.
Acts Swahili 4:7  Waliwasimamisha mitume mbele yao, wakawauliza, "Ninyi mmefanya jambo hili kwa nguvu gani na kwa jina la nani?"
Acts Swahili 4:8  Hapo, Petro, akiwa amejawa na Roho Mtakatifu, akawaambia, "Viongozi na wazee wa watu!
Acts Swahili 4:9  Ikiwa mnatuuliza leo juu ya kile kitendo chema alichofanyiwa yule mtu aliyekuwa kiwete na jinsi alivyopata kuwa mzima,
Acts Swahili 4:10  basi, ninyi na watu wote wa Israeli mnapaswa kujua kwamba mtu huyu anasimama mbele yenu leo, mzima kabisa, kwa nguvu ya jina lake Yesu wa Nazareti ambaye ninyi mlimsulubisha, lakini Mungu akamfufua kutoka wafu.
Acts Swahili 4:11  Huyu ndiye ambaye Maandiko Matakatifu yanasema: Jiwe mlilokataa ninyi waashi, sasa limekuwa jiwe kuu la msingi.
Acts Swahili 4:12  Wokovu haupatikani kwa mtu mwingine yeyote, kwa maana duniani pote, binadamu hawakupewa jina la mtu mwingine ambaye sisi tunaweza kuokolewa naye."
Acts Swahili 4:13  Hao wazee wa baraza, wakiwa wanajua kwamba Petro na Yohane walikuwa watu wasio na kisomo wala elimu yoyote, walishangaa juu ya jinsi walivyosema kwa uhodari. Wakatambua kwamba walikuwa wamejiunga na Yesu.
Acts Swahili 4:14  Lakini walipomwona yule mtu aliyeponywa amesimama pamoja nao, hawakuweza kusema kitu.
Acts Swahili 4:15  Hivyo, waliwaamuru watoke nje ya baraza, nao wakabaki ndani wakizungumza kwa faragha.
Acts Swahili 4:16  Wakaulizana, "Tufanye nini na watu hawa? Kila mtu anayeishi Yerusalemu anajua kwamba mwujiza huu wa ajabu umefanyika, nasi hatuwezi kukana jambo hilo.
Acts Swahili 4:17  Lakini ili tupate kuzuia jambo hili lisienee zaidi kati ya watu, tuwaonye wasiongee na mtu yeyote kwa jina la Yesu."
Acts Swahili 4:18  Kwa hiyo wakawaita tena ndani, wakawaonya wasiongee tena hadharani, wala kufundisha kwa jina la Yesu.
Acts Swahili 4:19  Lakini Petro na Yohane wakawajibu, "Amueni ninyi wenyewe kama ni haki mbele ya Mungu kuwatii ninyi kuliko kumtii yeye.
Acts Swahili 4:20  Kwa maana hatuwezi kuacha kusema juu ya mambo yale tuliyoyaona na kuyasikia."
Acts Swahili 4:21  Basi, hao wazee wa Baraza wakawaonya kwa ukali zaidi, halafu wakawaacha huru. Hawakuweza kuwapa adhabu kwa sababu watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa sababu ya tukio hilo.
Acts Swahili 4:22  Huyo mtu aliyeponywa alikuwa na umri wa miaka zaidi ya arobaini.
Acts Swahili 4:23  Mara tu walipoachwa huru, Petro na Yohane walirudi kwa wenzao, wakawaeleza yale waliyoambiwa na makuhani wakuu na wazee.
Acts Swahili 4:24  Waliposikia habari hiyo waliungana pamoja katika kumwomba Mungu wakisema, "Bwana, wewe ni Muumba wa mbingu na nchi, bahari na vyote vilivyomo!
Acts Swahili 4:25  Ndiwe uliyemfanya mtumishi wako, babu yetu Daudi, aseme kwa nguvu ya Roho Mtakatifu: Kwa nini mataifa yameghadhibika? Mbona watu wamefanya mipango ya bure?
Acts Swahili 4:26  Wafalme wa dunia walijiweka tayari, na watawala walikutana pamoja, ili kumwasi Bwana na Kristo wake.
Acts Swahili 4:27  "Maana, kwa hakika, ndivyo Herode, Pontio Pilato, watu wa Israeli na watu wa mataifa walivyokutanika papa hapa mjini, kumpinga Yesu Mtumishi wako Mtakatifu ambaye umemtia mafuta.
Acts Swahili 4:28  Naam, walikutana ili wafanye yale ambayo ulikusudia na kupanga tangu mwanzo kwa uwezo wako na mapenzi yako.
Acts Swahili 4:29  Lakini sasa, ee Bwana, angalia vitisho vyao. Utuwezeshe sisi watumishi wako kuhubiri neno lako kwa uhodari.
Acts Swahili 4:30  Nyosha mkono wako uponye watu. Fanya ishara na maajabu kwa jina la Yesu Mtumishi wako Mtakatifu."
Acts Swahili 4:31  Walipomaliza kusali, pale mahali walipokuwa wamekutanika pakatikiswa, nao wote wakajazwa Roho Mtakatifu. Wote wakaanza kuhubiri neno la Mungu bila uoga.
Acts Swahili 4:32  Jumuiya yote ya waumini ilikuwa moyo mmoja na roho moja. Hakuna hata mmoja aliyekuwa na kitu chochote akakiweka kuwa mali yake binafsi, ila waligawana vyote walivyokuwa navyo.
Acts Swahili 4:33  Mitume walishuhudia kwa nguvu nyingi kufufuka kwa Bwana Yesu, naye Mungu akawapa baraka nyingi.
Acts Swahili 4:34  Hakuna mtu yeyote aliyetindikiwa kitu, maana waliokuwa na mashamba au nyumba walikuwa wanaviuza
Acts Swahili 4:35  na kuwakabidhi mitume fedha hizo, zikagawiwa kila mmoja kadiri ya mahitaji yake.
Acts Swahili 4:36  Kulikuwa na Mlawi mmoja, mzaliwa wa Kupro, jina lake Yosefu, ambaye mitume walimwita jina Barnaba (maana yake, "Mtu mwenye kutia moyo").
Acts Swahili 4:37  Yeye pia alikuwa na shamba lake, akaliuza; akazichukua zile fedha, akawakabidhi mitume.