Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
ACTS
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 19
Acts Swahili 19:1  Wakati Apolo alipokuwa Korintho, Paulo alisafiri sehemu za bara, akafika Efeso ambako aliwakuta wanafunzi kadhaa.
Acts Swahili 19:2  Akauliza, "Je, mlipopata kuwa waumini mlipokea Roho Mtakatifu?" Nao wakamjibu, "La! Hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatujasikia."
Acts Swahili 19:3  Naye akasema, "Sasa mlipata ubatizo wa namna gani?" Wakamjibu, "Ubatizo wa Yohane."
Acts Swahili 19:4  Naye Paulo akasema, "Ubatizo wa Yohane ulikuwa wa kuonyesha kwamba watu wametubu. Yohane aliwaambia watu wamwamini yule ambaye alikuwa anakuja baada yake, yaani Yesu."
Acts Swahili 19:5  Baada ya kusikia hayo, walibatizwa kwa jina la Bwana Yesu.
Acts Swahili 19:6  Basi, Paulo akawawekea mikono, na Roho Mtakatifu akawashukia, wakaanza kusema lugha mbalimbali na kutangaza ujumbe wa Mungu.
Acts Swahili 19:7  Wote jumla, walikuwa watu wapatao kumi na wawili.
Acts Swahili 19:8  Kwa muda wa miezi mitatu Paulo alikuwa akienda katika sunagogi, akawa na majadiliano ya kuvutia sana juu ya Ufalme wa Mungu.
Acts Swahili 19:9  Lakini wengine walikuwa wakaidi, wakakataa kuamini, wakaanza kuongea vibaya hadharani juu ya Njia ya Bwana. Hapo Paulo alivunja uhusiano nao, akawachukua pembeni wale wanafunzi wake, akawa anazungumza nao kila siku katika jumba la masomo la Turano.
Acts Swahili 19:10  Aliendelea kufanya hivyo kwa muda wa miaka miwili hata wakazi wote wa Asia, Wayahudi na watu wa mataifa mengine, wakaweza kusikia neno la Bwana.
Acts Swahili 19:11  Mungu alifanya miujiza ya ajabu kwa mikono ya Paulo.
Acts Swahili 19:12  Watu walikuwa wakichukua leso na nguo nyingine za kazi ambazo Paulo alikuwa amezitumia, wakazipeleka kwa wagonjwa, nao wakaponywa magonjwa yao; na wale waliokuwa na pepo wabaya wakatokwa na pepo hao.
Acts Swahili 19:13  Wayahudi kadhaa wenye kupunga pepo wabaya, walisafiri huko na huko, wakijaribu kulitumia jina la Bwana Yesu kwa wale waliokuwa wamepagawa na pepo wabaya. Walikuwa wakisema: "Ninawaamuru kwa jina la Yesu ambaye Paulo anamhubiri."
Acts Swahili 19:14  Watoto saba wa Skewa, Kuhani Mkuu wa Kiyahudi, walikuwa miongoni mwa hao waliokuwa wanafanya hivyo.
Acts Swahili 19:15  Lakini pepo mbaya aliwajibu, "Ninamfahamu Yesu, ninamjua pia Paulo, lakini ninyi ni nani?"
Acts Swahili 19:16  Kisha yule mtu aliyepagawa aliwarukia wote kwa kishindo, akawashinda nguvu. Na hao watoto wa Skewa wakakimbia kutoka ile nyumba wakiwa uchi na wamejaa majeraha.
Acts Swahili 19:17  Kila mtu huko Efeso, Myahudi na asiye Myahudi, alisikia juu ya tukio hilo. Wote waliingiwa na hofu, wakalitukuza jina la Bwana Yesu.
Acts Swahili 19:18  Waumini wengi walijitokeza wakakiri hadharani mambo waliyokuwa wametenda.
Acts Swahili 19:19  Wengine waliokuwa wameshughulikia mambo ya uchawi hapo awali, walikusanya vitabu vyao, wakavichoma mbele ya wote. Walikisia gharama ya vitabu hivyo, wakaona yafikia vipande vya fedha elfu hamsini.
Acts Swahili 19:20  Kwa namna hiyo, neno la Bwana lilizidi kuenea na kuwa na nguvu zaidi.
Acts Swahili 19:21  Baada ya mambo hayo, Paulo aliamua kwenda Yerusalemu kwa kupitia Makedonia na Akaya. Alisema, "Baada ya kufika huko, itanilazimu kuona Roma pia."
Acts Swahili 19:22  Hivyo, aliwatuma wawili wa wasaidizi wake, Timotheo na Erasto, wamtangulie kwenda Makedonia, naye akabaki kwa muda huko Asia.
Acts Swahili 19:23  Wakati huo ndipo kulipotokea ghasia kubwa huko Efeso kwa sababu ya hiyo Njia ya Bwana.
Acts Swahili 19:24  Kulikuwa na mfua fedha mmoja aitwaye Demetrio, ambaye alikuwa na kazi ya kutengeneza sanamu za nyumba ya mungu wa kike aitwaye Artemi. Shughuli hiyo iliwapatia mafundi faida kubwa.
Acts Swahili 19:25  Demetrio aliwakusanya hao wafanyakazi pamoja na wengine waliokuwa na kazi kama hiyo, akawaambia, "Wananchi, mnafahamu kwamba kipato chetu kinatokana na biashara hii.
Acts Swahili 19:26  Sasa, mnaweza kusikia na kujionea wenyewe mambo Paulo anayofanya, si tu hapa Efeso, ila pia kote katika Asia. Yeye amewashawishi na kuwageuza watu wakakubali kwamba miungu ile iliyotengenezwa na watu si miungu hata kidogo.
Acts Swahili 19:27  Hivyo iko hatari kwamba biashara yetu itakuwa na jina baya. Si hivyo tu, bali pia jambo hilo linaweza kuifanya nyumba ya mungu Artemi kuwa si kitu cha maana. Hatimaye sifa zake huyo ambaye Asia na dunia yote inamwabudu, zitakwisha."
Acts Swahili 19:28  Waliposikia hayo, waliwaka hasira, wakaanza kupiga kelele: "Mkuu ni Artemi, wa Efeso!"
Acts Swahili 19:29  Mji wote ukajaa ghasia. Wakawavamia Gayo na Aristarko, wenyeji wa Makedonia, ambao walikuwa wasafiri wenzake Paulo, wakakimbia nao mpaka kwenye ukumbi wa michezo.
Acts Swahili 19:30  Paulo mwenyewe alitaka kuukabili huo umati wa watu, lakini wale waumini walimzuia.
Acts Swahili 19:31  Maofisa wengine wa huo mkoa wa Asia, waliokuwa rafiki zake, walimtumia Paulo ujumbe wakimsihi asijihatarishe kwa kwenda kwenye ukumbi wa michezo.
Acts Swahili 19:32  Wakati huo, kila mtu alikuwa anapayuka; wengine hili na wengine lile, mpaka hata ule mkutano ukavurugika. Wengi hawakujua hata sababu ya kukutana kwao.
Acts Swahili 19:33  Kwa vile Wayahudi walimfanya Aleksanda ajitokeze mbele, baadhi ya watu katika ule umati walidhani kuwa ndiye. Basi, Aleksanda aliwaashiria watu kwa mkono akitaka kujitetea mbele ya ule umati wa watu.
Acts Swahili 19:34  Lakini walipotambua kuwa yeye ni Myahudi, wote kwa sauti moja walipiga kelele: "Mkuu ni Artemi wa Efeso!" Wakaendelea kupayukapayuka hivyo kwa muda wa saa mbili.
Acts Swahili 19:35  Hatimaye karani wa mji alifaulu kuwanyamazisha, akawaambia, "Wananchi wa Efeso, kila mtu anajua kwamba mji huu wa Efeso ni mlinzi wa nyumba ya mungu Artemi na mlinzi wa ile sanamu iliyoanguka kutoka mbinguni.
Acts Swahili 19:36  Hakuna anayeweza kukana mambo haya. Hivyo basi, tulieni; msifanye chochote bila hadhari.
Acts Swahili 19:37  Mmewaita watu hawa hapa ingawaje hawakuikufuru nyumba ya mungu wala kumtukana mungu wetu wa kike.
Acts Swahili 19:38  Kama, basi Demetrio na wafanyakazi wake wana mashtaka yao kuhusu watu hawa, yapo mahakama na wakuu wa mikoa; wanaweza kushtakiana huko.
Acts Swahili 19:39  Kama mna matatizo mengine, yapelekeni katika kikao halali.
Acts Swahili 19:40  Kwa maana tungaliweza kushtakiwa kwa kusababisha ghasia kutokana na vituko vya leo. Ghasia hii haina msingi halali na hatungeweza kutoa sababu za kuridhisha za ghasia hiyo."