Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
ACTS
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 3
Acts Swahili 3:1  Siku moja, saa tisa alasiri, Petro na Yohane walikuwa wanakwenda Hekaluni, wakati wa sala.
Acts Swahili 3:2  Na pale karibu na mlango wa Hekalu uitwao "Mlango Mzuri", palikuwa na mtu mmoja, kiwete tangu kuzaliwa. Watu walimbeba huyo mtu kila siku na kumweka hapo ili aombe chochote kwa wale waliokuwa wakiingia Hekaluni.
Acts Swahili 3:3  Alipowaona Petro na Yohane wakiingia Hekaluni, aliwaomba wampe chochote.
Acts Swahili 3:4  Petro na Yohane walimkodolea macho, naye Petro akamwambia, "Tutazame!"
Acts Swahili 3:5  Naye akawageukia, akitazamia kupata kitu kutoka kwao.
Acts Swahili 3:6  Kisha Petro akamwambia, "Sina fedha wala dhahabu lakini kile nilicho nacho nitakupa. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, tembea!"
Acts Swahili 3:7  Halafu, akamshika mkono wa kulia, akamwinua. Papo hapo miguu na magoti yake yakapata nguvu.
Acts Swahili 3:8  Akaruka, akasimama na kuanza kutembea. Halafu akaingia pamoja nao Hekaluni, akitembea na kurukaruka huku akimtukuza Mungu.
Acts Swahili 3:9  Watu wote waliokuwa hapo walimwona akitembea na kumsifu Mungu.
Acts Swahili 3:10  Walipomtambua kuwa ndiye yule aliyekuwa anaombaomba karibu na ule "Mlango Mzuri" wa Hekalu, wakashangaa mno hata wasiweze kuelewa yaliyompata.
Acts Swahili 3:11  Watu wote, wakiwa na mshangao mkubwa wakaanza kukimbilia mahali palipoitwa "Ukumbi wa Solomoni," ambapo yule mtu alikuwa bado anaandamana na Petro na Yohane.
Acts Swahili 3:12  Basi, Petro alipowaona watu hao akawaambia, "Wananchi wa Israeli, kwa nini mnashangazwa na jambo hili? Mbona mnatukodolea macho kana kwamba ni kwa nguvu zetu au utakatifu wetu sisi wenyewe tumemfanya mtu huyu aweze kutembea?
Acts Swahili 3:13  Mungu wa Abrahamu, Isaka na Yakobo, Mungu wa baba zetu amemtukuza Yesu mtumishi wake. Yeye ndiye yuleyule mliyemtia mikononi mwa wakuu na kumkataa mbele ya Pilato hata baada ya Pilato kuamua kumwacha huru.
Acts Swahili 3:14  Alikuwa mtakatifu na mwema; lakini ninyi mlimkataa, mkataka mtu mwingine aliyekuwa muuaji afunguliwe.
Acts Swahili 3:15  Basi, mlimuua yule ambaye ni chanzo cha uzima. Lakini Mungu alimfufua, na sisi ni mashahidi wa tukio hilo.
Acts Swahili 3:16  Jina la Yesu na imani katika jina hilo ndivyo vilivyompa nguvu mtu huyu mnayemwona na kumfahamu. Imani kwa Yesu ndiyo iliyomponya kabisa mtu huyu kama mnavyoona nyote.
Acts Swahili 3:17  "Sasa ndugu zangu, nafahamu kwamba ninyi na wakuu wenu mlitenda hayo kwa sababu ya kutojua kwenu.
Acts Swahili 3:18  Lakini ndivyo Mungu alivyotimiza yale aliyotangaza zamani kwa njia ya manabii wote, kwamba ilikuwa lazima Kristo wake ateseke.
Acts Swahili 3:19  Basi, tubuni mkamrudie Mungu ili afute dhambi zenu.
Acts Swahili 3:20  Fanyeni hivyo ili Bwana awape nyakati za kuburudika rohoni na kuwaletea yule Kristo aliyemteua ambaye ndiye Yesu.
Acts Swahili 3:21  Ni lazima yeye abaki huko mbinguni mpaka utakapofika wakati wa kurekebishwa vitu vyote, kama Mungu alivyosema kwa njia ya manabii wake watakatifu wa tangu zamani.
Acts Swahili 3:22  Kwa maana Mose alisema, Bwana Mungu wenu atawapelekeeni nabii kama mimi kutoka kati yenu ninyi wenyewe.
Acts Swahili 3:23  Yeyote yule ambaye hatamsikiliza nabii huyo atatengwa mbali na watu wa Mungu na kuangamizwa.
Acts Swahili 3:24  Manabii wote, kuanzia Samweli na wale waliomfuata, walitangaza habari za mambo haya ambayo yamekuwa yakitendeka siku hizi.
Acts Swahili 3:25  Ahadi zile Mungu alizotoa kwa njia ya manabii ni kwa ajili yenu; na mnashiriki lile agano Mungu alilofanya na babu zenu, kama alivyomwambia Abrahamu: Kwa njia ya wazawa wako, jamaa zote za dunia zitabarikiwa.
Acts Swahili 3:26  Basi, ilikuwa kwa ajili yenu kwanza kwamba Mungu alimfufua mtumishi wake, alimtuma awabariki kwa kumfanya kila mmoja wenu aachane kabisa na maovu yake."