Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
ACTS
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 2
Acts Swahili 2:1  Siku ya Pentekoste ilipofika, waumini wote walikuwa wamekusanyika pamoja.
Acts Swahili 2:2  Ghafla, sauti ikasikika kutoka angani; sauti iliyokuwa kama ya upepo mkali, ikajaza ile nyumba yote walimokuwa wamekaa.
Acts Swahili 2:3  Kisha, vikatokea vitu vilivyoonekana kama ndimi za moto, vikagawanyika na kutua juu ya kila mmoja wao.
Acts Swahili 2:4  Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema lugha mbalimbali kadiri Roho alivyowawezesha.
Acts Swahili 2:5  Na huko Yerusalemu walikuwako Wayahudi, watu wamchao Mungu, waliotoka katika kila nchi duniani.
Acts Swahili 2:6  Waliposikia sauti hiyo, kundi kubwa la watu lilikusanyika. Wote walishtuka sana kwani kila mmoja wao aliwasikia hao waumini wakisema kwa lugha yake mwenyewe.
Acts Swahili 2:7  Walistaajabu na kushangaa, wakisema, "Je, hawa wote tunaowasikia wakisema hivi, si wenyeji wa Galilaya?
Acts Swahili 2:8  Imekuwaje, basi, kwamba kila mmoja wetu anawasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe?
Acts Swahili 2:9  Baadhi yetu ni Waparthi, Wamedi na Waelami; wengine ni wenyeji wa Mesopotamia, Yudea, Kapadokia, Ponto na Asia,
Acts Swahili 2:10  Frugia na Pamfulia, Misri na sehemu za Libya karibu na Kurene; wengine wetu ni wageni kutoka Roma,
Acts Swahili 2:11  Wayahudi na watu walioongokea dini ya Kiyahudi; wengine wametoka Krete na Arabia. Sisi sote tunasikia wakisema kwa lugha zetu wenyewe mambo makuu ya Mungu."
Acts Swahili 2:12  Wote walishangaa na kufadhaika huku wakiulizana, "Hii ina maana gani?"
Acts Swahili 2:13  Lakini wengine wakawadhihaki wakisema, "Watu hawa wamelewa divai mpya!"
Acts Swahili 2:14  Lakini Petro alisimama pamoja na wale kumi na mmoja akaanza kuwahutubia watu kwa sauti kubwa: "Ndugu Wayahudi nanyi nyote mnaokaa hapa Yerusalemu, sikilizeni kwa makini maneno yangu.
Acts Swahili 2:15  Watu hawa hawakulewa kama mnavyodhani; mbona ni saa tatu tu asubuhi?
Acts Swahili 2:16  Ukweli ni kwamba jambo hili ni lile alilosema nabii Yoeli:
Acts Swahili 2:17  Katika siku zile za mwisho, asema Bwana, nitawamiminia binadamu wote Roho wangu. Watoto wenu, wanaume kwa wanawake, watautangaza ujumbe wangu; vijana wenu wataona maono, na wazee wenu wataota ndoto.
Acts Swahili 2:18  Naam, hata watumishi wangu, wanaume kwa wanawake, nitawamiminia Roho wangu, siku zile, nao watautangaza ujumbe wangu.
Acts Swahili 2:19  Nitatenda miujiza juu angani, na ishara chini duniani; kutakuwa na damu, moto na moshi mzito;
Acts Swahili 2:20  jua litatiwa giza, na mwezi utakuwa mwekundu kama damu, kabla ya kutokea ile siku kuu na tukufu ya Bwana.
Acts Swahili 2:21  Hapo, yeyote atakayeomba kwa jina la Bwana, ataokolewa.
Acts Swahili 2:22  "Wananchi wa Israeli, sikilizeni maneno haya! Yesu wa Nazareti alikuwa mtu ambaye mamlaka yake ya kimungu yalithibitishwa kwenu kwa miujiza, maajabu na ishara Mungu alizofanya kati yenu kwa njia yake, kama mnavyojua.
Acts Swahili 2:23  Kufuatana na mpango wake mwenyewe Mungu alikwisha amua kwamba Yesu angetiwa mikononi mwenu; nanyi mkamuua kwa kuwaachia watu wabaya wamsulubishe.
Acts Swahili 2:24  Lakini Mungu alimfufua kutoka wafu akamwokoa katika maumivu ya kifo kwa maana haingewezekana kabisa kifo kimfunge.
Acts Swahili 2:25  Maana Daudi alisema juu yake hivi: Nilimwona Bwana mbele yangu daima; yuko nami upande wangu wa kulia, na hivyo sitatikisika.
Acts Swahili 2:26  Kwa hiyo, moyo wangu ulifurahi; tena nilipiga vigelegele vya furaha. Mwili wangu utakaa katika tumaini;
Acts Swahili 2:27  kwa kuwa hutaiacha roho yangu katika kuzimu, wala kumruhusu mtakatifu wako aoze.
Acts Swahili 2:28  Umenionyesha njia za kuufikia uzima, kuwako kwako kwanijaza furaha!
Acts Swahili 2:29  "Ndugu zangu, napenda kuwaambieni waziwazi juu ya mambo yaliyompata Daudi, babu yetu. Yeye alikufa, akazikwa, tena kaburi lake liko papa hapa petu mpaka leo.
Acts Swahili 2:30  Lakini kwa vile Daudi alikuwa nabii, alijua kuwa Mungu alimwapia kiapo kwamba atamtawaza mmoja wa uzawa wake kuwa mfalme mahali pake.
Acts Swahili 2:31  Daudi aliona kabla mambo yatakayofanywa na Mungu na hivyo akasema juu ya ufufuo wa Kristo wakati aliposema: Hakuachwa kuzimu, mwili wake haukuoza.
Acts Swahili 2:32  Basi, Mungu alimfufua huyo Yesu na sisi sote ni mashahidi wa tukio hilo.
Acts Swahili 2:33  Yesu aliinuliwa juu mpaka upande wa kulia wa Mungu, akapokea kutoka kwa Baba ile zawadi aliyoahidi yaani Roho Mtakatifu; na mnachoona sasa na kusikia ni mmiminiko wa huyo Roho.
Acts Swahili 2:34  Maana Daudi mwenyewe, hakupanda mpaka mbinguni; ila yeye alisema: Bwana alimwambia Bwana wangu: Keti upande wangu wa kulia,
Acts Swahili 2:35  hadi nitakapowafanya adui zako kibao cha kukanyagia miguu yako.
Acts Swahili 2:36  "Watu wote wa Israeli wanapaswa kufahamu kwa hakika kwamba huyo Yesu mliyemsulubisha ninyi, ndiye huyo ambaye Mungu amemfanya kuwa Bwana na Kristo."
Acts Swahili 2:37  Basi, watu waliposikia hayo, walichomwa moyo, wakawauliza Petro na wale mitume wenzake: "Ndugu zetu, tufanye nini?"
Acts Swahili 2:38  Petro akajibu, "Tubuni na kila mmoja wenu abatizwe kwa jina la Yesu Kristo ili mpate kuondolewa dhambi zenu na kupokea ile zawadi ya Roho Mtakatifu.
Acts Swahili 2:39  Maana, ahadi ile ilikuwa kwa ajili yenu, kwa ajili ya watoto wenu, kwa ajili ya wote wanaokaa mbali; na kwa ajili ya kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita kwake."
Acts Swahili 2:40  Kwa maneno mengine mengi, Petro alisisitiza na kuwahimiza watu akisema, "Jiokoeni katika kizazi hiki kiovu."
Acts Swahili 2:41  Wengi waliyakubali maneno yake, wakabatizwa. Watu wapatao elfu tatu wakaongezeka katika kile kikundi siku hiyo.
Acts Swahili 2:42  Hawa wote waliendelea kujifunza kutoka kwa mitume, kuishi pamoja kidugu, kumega mkate na kusali.
Acts Swahili 2:43  Miujiza na maajabu mengi yalifanyika kwa njia ya mitume hata kila mtu akajawa na hofu.
Acts Swahili 2:44  Waumini wote waliendelea kuwa kitu kimoja na mali zao waligawana pamoja.
Acts Swahili 2:45  Walikuwa wakiuza mali na vitu vyao kisha wakagawana fedha kadiri ya mahitaji ya kila mmoja.
Acts Swahili 2:46  Waliendelea kukutana pamoja kila siku Hekaluni. Lakini wakati wa kumega mkate, walikutana katika nyumba zao na wakakishiriki chakula hicho kwa furaha na moyo mkunjufu.
Acts Swahili 2:47  Walimtukuza Mungu, wakapendwa na watu wote. Kila siku Bwana aliwaongezea idadi ya watu waliokuwa wakiokolewa.