Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
ACTS
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 22
Acts Swahili 22:1  "Ndugu zangu na akina baba, nisikilizeni sasa nikijitetea mbele yenu!"
Acts Swahili 22:2  Waliposikia akiongea nao kwa Kiebrania wakazidi kukaa kimya zaidi kuliko hapo awali. Naye Paulo akaendelea kusema,
Acts Swahili 22:3  "Mimi ni Myahudi, mzaliwa wa Tarso katika Kilikia. Lakini nililelewa papa hapa mjini Yerusalemu chini ya mkufunzi Gamalieli. Nilifundishwa kufuata kwa uthabiti Sheria ya wazee wetu. Nilijitolea kwa moyo wote kwa Mungu kama ninyi wenyewe mlivyo hivi leo.
Acts Swahili 22:4  Niliwatesa hata kuwaua wale watu waliofuata Njia hii. Niliwatia nguvuni wanaume kwa wanawake na kuwafunga gerezani.
Acts Swahili 22:5  Kuhani Mkuu na baraza lote la wazee wanaweza kushuhudia jambo hilo. Kutoka kwao nilipokea barua walioandikiwa wale ndugu Wayahudi waliokuwa huko Damasko. Nilikwenda Damasko ili niwatie nguvuni watu hao na kuwaleta wamefungwa mpaka Yerusalemu ili waadhibiwe.
Acts Swahili 22:6  "Basi, nilipokuwa njiani karibu kufika Damasko, yapata saa sita mchana, mwangu mkubwa kutoka mbinguni ulitokea ghafla ukaniangazia pande zote.
Acts Swahili 22:7  Hapo nilianguka chini, nikasikia sauti ikiniambia: Saulo, Saulo! Kwa nini unanitesa?
Acts Swahili 22:8  Nami nikauliza: Nani wewe, Bwana? Naye akaniambia: Mimi ni Yesu wa Nazareti ambaye wewe unamtesa.
Acts Swahili 22:9  Wale wenzangu waliuona ule mwanga lakini hawakusikia sauti ya yule aliyeongea nami.
Acts Swahili 22:10  Basi, mimi nikauliza: Nifanye nini Bwana? Naye Bwana akaniambia: Simama, nenda Damasko na huko utaambiwa yote ambayo umepangiwa kufanya.
Acts Swahili 22:11  Kutokana na ule mwanga mkali sikuweza kuona na hivyo iliwabidi wale wenzangu kuniongoza kwa kunishika mkono mpaka nikafika Damasko.
Acts Swahili 22:12  "Huko kulikuwa na mtu mmoja aitwaye Anania, mtu mcha Mungu, mwenye kuitii Sheria yetu na aliyeheshimika sana mbele ya Wayahudi waliokuwa wanaishi Damasko.
Acts Swahili 22:13  Yeye alikuja kuniona, akasimama karibu nami, akasema: Ndugu Saulo! Ona tena. Papo hapo nikaona tena, nikamwangalia.
Acts Swahili 22:14  Halafu Anania akasema: Mungu wa babu zetu amekuchagua upate kujua matakwa yake na kumwona yule mtumishi wake mwadilifu na kumsikia yeye mwenyewe akiongea.
Acts Swahili 22:15  Kwa maana utamshuhudia kwa watu wote ukiwaambia yale uliyoyaona na kuyasikia.
Acts Swahili 22:16  Sasa basi, ya nini kukawia zaidi? Simama ubatizwe na uondolewe dhambi zako kwa kuliungama jina lake.
Acts Swahili 22:17  "Basi, nilirudi Yerusalemu, na nilipokuwa nikisali Hekaluni, niliona maono.
Acts Swahili 22:18  Nilimwona Bwana akiniambia: Haraka! Ondoka Yerusalemu upesi kwa maana watu wa hapa binadamu hawataukubali ushuhuda wako juu yangu.
Acts Swahili 22:19  Nami nikamjibu: Bwana, wao wanajua wazi kwamba mimi ni yule aliyekuwa anapitapita katika masunagogi na kuwatia nguvuni na kuwapiga wale waliokuwa wanakuamini.
Acts Swahili 22:20  Na kwamba wakati shahidi wako Stefano alipouawa, mimi binafsi nilikuwako pale nikakubaliana na kitendo hicho na kuyalinda makoti ya wale waliokuwa wanamuua.
Acts Swahili 22:21  Naye Bwana akaniambia: Nenda; ninakutuma mbali kwa mataifa mengine."
Acts Swahili 22:22  Mpaka hapa, wale watu walikuwa wanamsikiza, lakini aliposema maneno haya, walianza kusema kwa sauti kubwa, "Mwondoe duniani! Mtu wa namna hiyo hastahili kuishi."
Acts Swahili 22:23  Waliendelea kupayukapayuka huku wakitikisa makoti yao na kurusha vumbi angani.
Acts Swahili 22:24  Mkuu wa jeshi aliwaamuru watu wake wampeleke Paulo ndani ya ngome, akawaambia wamchape viboko ili wapate kujua kisa cha Wayahudi kumpigia kelele.
Acts Swahili 22:25  Lakini walipokwisha mfunga ili wamchape viboko, Paulo alimwuliza jemadari mmoja aliyesimama hapo, "Je, ni halali kwenu kumpiga viboko raia wa Roma kabla hajahukumiwa?"
Acts Swahili 22:26  Yule jemadari aliposikia hayo, alimpasha habari mkuu wa jeshi akisema, "Unataka kufanya nini? Mtu huyu ni raia wa Roma!"
Acts Swahili 22:27  Basi, mkuu wa jeshi alimwendea Paulo, akamwambia, "Niambie; je, wewe ni raia wa Roma?" Paulo akamjibu, "Naam."
Acts Swahili 22:28  Mkuu wa jeshi akasema, "Mimi nami nimekuwa raia wa Roma kwa kulipa gharama kubwa." Paulo akasema, "Lakini mimi ni raia wa Roma kwa kuzaliwa."
Acts Swahili 22:29  Wale watu ambao walikuwa tayari kumchunguza Paulo walitoweka mara. Hata yule mkuu wa jeshi aliogopa alipojua kwamba Paulo ni raia wa Roma na kwamba alikuwa amekwisha mfunga minyororo.
Acts Swahili 22:30  Kesho yake, mkuu wa jeshi alitaka kujua mashtaka kamili ambayo Wayahudi walikuwa wamemwekea Paulo. Hivyo, alimfungua Paulo minyororo, akaamuru makuhani wakuu na Baraza lote wafanye kikao. Kisha alimleta Paulo, akamsimamisha mbele ya Baraza.