Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
ACTS
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 16
Acts Swahili 16:1  Paulo alifika Derbe na Lustra, ambako aliishi mfuasi mmoja aitwaye Timotheo. Mama yake ambaye pia alikuwa mfuasi, alikuwa Myahudi; lakini baba yake alikuwa Mgiriki.
Acts Swahili 16:2  Timotheo alikuwa na sifa kubwa kati ya wale ndugu wa Lustra na Ikonio.
Acts Swahili 16:3  Paulo alitaka Timotheo aandamane naye safarini, kwa hiyo alimtahiri. Alifanya hivyo kwa sababu Wayahudi wote walioishi sehemu hizo walijua kwamba baba yake Timotheo alikuwa Mgiriki.
Acts Swahili 16:4  Walipokuwa wanapita katika ile miji waliwapa watu yale maagizo yaliyotolewa na mitume na wazee kule Yerusalemu, wakawaambia wayazingatie.
Acts Swahili 16:5  Hivyo, yale makanisa yalizidi kuwa imara katika imani, na idadi ya waumini ikaongezeka kila siku.
Acts Swahili 16:6  Walipitia sehemu za Frugia na Galatia kwani Roho Mtakatifu hakuwaruhusu kuhubiri huo ujumbe mkoani Asia.
Acts Swahili 16:7  Walipofika kwenye mipaka ya Musia, walijaribu kuingia mkoani Bithunia, lakini Roho wa Yesu hakuwaruhusu.
Acts Swahili 16:8  Basi, walipitia Musia, wakaenda moja kwa moja mpaka Troa.
Acts Swahili 16:9  Usiku huo, Paulo aliona ono ambalo alimwona mtu mmoja wa Makedonia amesimama pale na kumwomba: "Vuka, uje Makedonia ukatusaidie."
Acts Swahili 16:10  Mara baada ya Paulo kuona ono hilo, tulijitayarisha kwenda Makedonia bila kukawia, tukiwa na hakika kwamba Mungu ametuita tuwapelekee Habari Njema.
Acts Swahili 16:11  Kutoka Troa, tulisafiri kwa meli moja kwa moja mpaka Samothrake, na kesho yake tukatia nanga Neapoli.
Acts Swahili 16:12  Kutoka huko, tulikwenda mpaka Filipi, mji wa wilaya ya kwanza ya Makedonia, na ambao pia ni koloni la Waroma. Tulikaa katika mji huo siku kadhaa.
Acts Swahili 16:13  Siku ya Sabato tulitoka nje ya mji, tukaenda kando ya mto ambapo tulidhani ya kuwa ni mahali pa kusali. Tuliketi, tukaongea na wanawake waliokusanyika mahali hapo.
Acts Swahili 16:14  Miongoni mwa wale waliotusikiliza alikuwa mwanamke mmoja mcha Mungu aitwaye Ludia mwenyeji wa Thuatira, ambaye alikuwa mfanyabiashara ya nguo za kitani za rangi ya zambarau. Bwana aliufungua moyo wake hata akayapokea yale maneno Paulo aliyokuwa anasema.
Acts Swahili 16:15  Baada ya huyo mama pamoja na jamaa yake kubatizwa, alitualika akisema, "Kama kweli mmeona kwamba mimi namwamini Bwana, karibuni nyumbani kwangu mkakae." Akatuhimiza twende.
Acts Swahili 16:16  Siku moja, tulipokuwa tunakwenda mahali pa kusali, msichana mmoja aliyekuwa na pepo mwenye uwezo wa kuagua alikutana nasi. Msichana huyo alikuwa anawapatia matajiri wake fedha nyingi kwa uaguzi wake.
Acts Swahili 16:17  Basi, huyo msichana alimfuata Paulo na sisi, akipiga kelele na kusema, "Hawa watu ni watumishi wa Mungu Mkuu. Wanawatangazieni njia ya wokovu."
Acts Swahili 16:18  Akawa anafanya hivyo kwa siku nyingi hata siku moja Paulo alikasirika, akamgeukia na kumwambia huyo pepo, "Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu!" Mara huyo pepo akamtoka.
Acts Swahili 16:19  Matajiri wa yule msichana walipoona kwamba tumaini lao la kupata mali limekwisha, waliwakamata Paulo na Sila, wakawaburuta mpaka hadharani, mbele ya wakuu.
Acts Swahili 16:20  Wakawashtaki kwa mahakimu wakisema, "Watu hawa ni Wayahudi na wanafanya fujo katika mji wetu.
Acts Swahili 16:21  Wanafundisha desturi ambazo sisi raia wa Roma haturuhusiwi kuzikubali wala kuzifuata."
Acts Swahili 16:22  Kundi la watu likajiunga nao, likawashambulia. Wale mahakimu wakawatatulia Paulo na Sila mavazi yao, wakaamuru wapigwe viboko.
Acts Swahili 16:23  Baada ya kupigwa sana wakatiwa ndani, na askari wa gereza akaamriwa kuwaweka chini ya ulinzi mkali.
Acts Swahili 16:24  Kutokana na maagizo hayo, huyo askari aliwaweka katika chumba cha ndani kabisa cha gereza na kuifunga miguu yao kwenye nguzo.
Acts Swahili 16:25  Karibu na usiku wa manane Paulo na Sila walikuwa wakisali na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, huku wafungwa wengine wakiwa wanasikiliza.
Acts Swahili 16:26  Ghafla, kulitokea mtetemeko mkuu wa ardhi ambao uliitikisa misingi ya gereza. Mara, milango yote ikafunguka na minyororo iliyowafunga hao wafungwa ikaachana.
Acts Swahili 16:27  Askari wa gereza alipoamka na kuiona milango ya gereza imefunguliwa, alidhani kwamba wafungwa wote walikuwa wametoroka na hivyo akauchomoa upanga wake, akataka kujiua.
Acts Swahili 16:28  Lakini Paulo akaita kwa sauti kubwa: "Usijidhuru mwenyewe kwa maana sisi sote tuko hapa."
Acts Swahili 16:29  Baada ya kumwita mtu alete taa, huyo askari wa gereza alikimbilia ndani, akajitupa mbele ya miguu ya Paulo na Sila huku akitetemeka kwa hofu.
Acts Swahili 16:30  Halafu aliwaongoza nje, akawauliza, "Waheshimiwa, nifanye nini nipate kuokoka?"
Acts Swahili 16:31  Wao wakamjibu, "Mwamini Bwana Yesu nawe utaokolewa pamoja na jamaa yako yote."
Acts Swahili 16:32  Basi, wakamhubiria neno la Bwana yeye pamoja na jamaa yake.
Acts Swahili 16:33  Yule askari aliwachukua saa ileile ya usiku akawasafisha majeraha yao, kisha yeye na jamaa yake wakabatizwa papo hapo.
Acts Swahili 16:34  Halafu akawachukua Paulo na Sila nyumbani kwake, akawapa chakula. Yeye na jamaa yake yote wakafanya sherehe kwa vile sasa walikuwa wanamwamini Mungu.
Acts Swahili 16:35  Kesho yake asubuhi, mahakimu waliwatuma maofisa wao wakisema, "Wafungueni wale watu."
Acts Swahili 16:36  Yule askari wa gereza alimpasha habari Paulo: "Mahakimu wametuma ujumbe ili mfunguliwe. Sasa mnaweza kutoka na kwenda zenu kwa amani."
Acts Swahili 16:37  Lakini Paulo alimjibu, "Ati nini? Ingawa hatukuwa na kosa, walitupiga viboko hadharani hali sisi ni raia wa Roma. Tena, walitutia ndani na sasa wanataka kutufungulia kwa siri! Hata kidogo! Ni lazima wao wenyewe waje hapa watufungulie."
Acts Swahili 16:38  Hao maofisa waliwapasha habari mahakimu juu ya jambo hilo, nao waliposikia kwamba Paulo na Sila walikuwa raia wa Roma, waliogopa.
Acts Swahili 16:39  Hivyo, walikwenda kuwataka radhi na baada ya kuwatoa ndani waliwaomba watoke katika mji ule.
Acts Swahili 16:40  Paulo na Sila walitoka gerezani, wakaenda nyumbani kwa Ludia. Huko walionana na ndugu waumini na baada ya kuwatia moyo wakaondoka.