Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
MATTHEW
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 19
Matt Swahili 19:1  Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, alitoka Galilaya, akaenda katika mkoa wa Yudea, ng'ambo ya mto Yordani.
Matt Swahili 19:3  Mafarisayo kadhaa walimjia, wakamwuliza kwa kumtega, "Je, ni halali mume kumpa talaka mkewe kwa kisa chochote?"
Matt Swahili 19:4  Yesu akawajibu, "Je, hamkusoma katika Maandiko Matakatifu kwamba Mungu aliyemuumba mtu tangu mwanzo alimfanya mwanamume na mwanamke,
Matt Swahili 19:5  na akasema: Kwa sababu hiyo mwanamume atamwacha baba yake na mama yake, ataungana na mke wake, nao wawili watakuwa mwili mmoja?
Matt Swahili 19:6  Kwa hiyo wao si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi, alichounganisha Mungu, binadamu asikitenganishe."
Matt Swahili 19:7  Lakini wao wakamwuliza, "Kwa nini basi, Mose alituagiza mwanamke apewe hati ya talaka na kuachwa?"
Matt Swahili 19:8  Yesu akawajibu, "Mose aliwaruhusu kuwaacha wake zenu kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu.
Matt Swahili 19:9  Lakini haikuwa hivyo tangu mwanzo. Basi nawaambieni, yeyote atakayemwacha mke wake isipokuwa kwa sababu ya uzinzi, akaoa mke mwingine, anazini."
Matt Swahili 19:10  Wanafunzi wake wakamwambia, "Ikiwa mambo ya mume na mkewe ni hivyo, ni afadhali kutooa kabisa."
Matt Swahili 19:11  Yesu akawaambia, "Si wote wanaoweza kulipokea fundisho hili, isipokuwa tu wale waliojaliwa na Mungu.
Matt Swahili 19:12  Maana kuna sababu kadhaa za kutoweza kuoa: wengine ni kwa sababu wamezaliwa hivyo, wengine kwa sababu wamefanywa hivyo na watu, na wengine wameamua kutooa kwa ajili ya Ufalme wa mbinguni. Awezaye kulipokea fundisho hili na alipokee."
Matt Swahili 19:13  Kisha watu wakamletea Yesu watoto wadogo ili awawekee mikono na kuwaombea. Lakini wanafunzi wakawakemea.
Matt Swahili 19:14  Yesu akasema, "Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie; maana Ufalme wa mbinguni ni wa watu walio kama watoto hawa."
Matt Swahili 19:15  Basi, akawawekea mikono, kisha akaondoka mahali hapo.
Matt Swahili 19:16  Mtu mmoja alimjia Yesu, akamwuliza, "Mwalimu, nifanye kitu gani chema ili niupate uzima wa milele?"
Matt Swahili 19:17  Yesu akamwambia, "Mbona unaniuliza kuhusu jambo jema? Kuna mmoja tu aliye mwema. Ukitaka kuingia katika uzima, shika amri."
Matt Swahili 19:18  Yule mtu akamwuliza, "Amri zipi?" Yesu akasema, "Usiue, usizini, usiibe, usitoe ushahidi wa uongo,
Matt Swahili 19:19  waheshimu baba yako na mama yako; na, mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe."
Matt Swahili 19:20  Huyo kijana akamwambia, "Hayo yote nimeyazingatia tangu utoto wangu; sasa nifanye nini zaidi?"
Matt Swahili 19:21  Yesu akamwambia, "Kama unapenda kuwa mkamilifu, nenda ukauze mali yako uwape maskini hiyo fedha, nawe utakuwa na hazina mbinguni, kisha njoo unifuate."
Matt Swahili 19:22  Huyo kijana aliposikia hayo, alienda zake akiwa mwenye huzuni, maana alikuwa na mali nyingi.
Matt Swahili 19:23  Hapo Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Kweli nawaambieni, itakuwa vigumu sana kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa mbinguni.
Matt Swahili 19:24  Tena nawaambieni, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano, kuliko kwa tajiri kuingia katika Ufalme wa mbinguni."
Matt Swahili 19:25  Wale wanafunzi waliposikia hivyo walishangaa, wakamwuliza, "Ni nani basi, awezaye kuokoka?"
Matt Swahili 19:26  Yesu akawatazama, akasema, "Kwa binadamu jambo hili haliwezekani, lakini kwa Mungu mambo yote huwezekana."
Matt Swahili 19:27  Kisha Petro akasema, "Na sisi je? Tumeacha yote tukakufuata; tutapata nini basi?"
Matt Swahili 19:28  Yesu akawaambia, "Nawaambieni kweli, Mwana wa Mtu atakapoketi katika kiti cha enzi cha utukufu wake katika ulimwengu mpya, ninyi mlionifuata mtaketi katika viti kumi na viwili mkiyahukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.
Matt Swahili 19:29  Na kila aliyeacha nyumba, au ndugu, au dada, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, atapokea mara mia zaidi, na kupata uzima wa milele.
Matt Swahili 19:30  Lakini walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza.