Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
I CORINTHIANS
1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 12
I Co Swahili 12:1  Ndugu, kuhusu vipaji vya kiroho, napenda mfahamu vizuri mambo haya:
I Co Swahili 12:2  Mnajua kwamba, kabla ya kuongoka kwenu, mlitawaliwa na kupotoshwa na sanamu tupu.
I Co Swahili 12:3  Basi, jueni kwamba mtu yeyote anayeongozwa na Roho wa Mungu hawezi kusema: "Yesu alaaniwe!" Hali kadhalika, mtu yeyote hawezi kusema: "Yesu ni Bwana," asipoongozwa na Roho Mtakatifu.
I Co Swahili 12:4  Vipaji vya kiroho ni vya namna nyingi, lakini Roho avitoaye ni mmoja.
I Co Swahili 12:5  Kuna namna nyingi za kutumikia, lakini Bwana anayetumikiwa ni mmoja.
I Co Swahili 12:6  Kuna namna mbalimbali za kufanya kazi ya huduma, lakini Mungu ni mmoja, anayewezesha kazi zote katika wote.
I Co Swahili 12:7  Kila mtu hupewa mwangaza wa Roho kwa faida ya wote.
I Co Swahili 12:8  Roho humpa mmoja ujumbe wa hekima, na mwingine ujumbe wa elimu apendavyo Roho huyohuyo.
I Co Swahili 12:9  Roho huyohuyo humpa mmoja imani, na humpa mwingine kipaji cha kuponya;
I Co Swahili 12:10  humpa mmoja kipaji cha kufanya miujiza, mwingine kipaji cha kusema ujumbe wa Mungu, mwingine kipaji cha kubainisha vipaji vitokavyo kwa Roho na visivyo vya Roho; humpa mmoja kipaji cha kusema lugha ngeni, na mwingine kipaji cha kuzifafanua.
I Co Swahili 12:11  Hizo zote ni kazi za Roho huyohuyo mmoja, ambaye humpa kila mtu kipaji tofauti, kama apendavyo mwenyewe.
I Co Swahili 12:12  Kama vile mwili ulivyo mmoja wenye viungo vingi, na viungo hivyo vyote--ingawaje ni vingi--hufanya mwili mmoja, ndivyo ilivyo pia kwa Kristo.
I Co Swahili 12:13  Maana sisi, tukiwa Wayahudi au watu wa mataifa mengine, watumwa au watu huru, sote tumebatizwa kwa Roho mmoja katika mwili huo mmoja; na sote tukanyweshwa Roho huyo mmoja.
I Co Swahili 12:14  Mwili hauna kiungo kimoja tu, bali una viungo vingi.
I Co Swahili 12:15  Kama mguu ungejisemea: "Kwa kuwa mimi si mkono, basi mimi si mali ya mwili", je, ungekoma kuwa sehemu ya mwili? La hasha!
I Co Swahili 12:16  Kama sikio lingejisemea: "Kwa vile mimi si jicho, basi mimi si mali ya mwili", je, kwa hoja hiyo lingekoma kuwa sehemu ya mwili? La!
I Co Swahili 12:17  Kama mwili wote ungekuwa jicho, sikio lingekuwa wapi? Na kama mwili wote ungekuwa sikio, mtu angewezaje kunusa?
I Co Swahili 12:18  Lakini kama ilivyo, Mungu alizipanga sehemu hizo tofauti katika mwili kama alivyopenda.
I Co Swahili 12:19  Kama sehemu zote zingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi?
I Co Swahili 12:20  Ukweli ni kwamba, sehemu za mwili ni nyingi, lakini mwili ni mmoja.
I Co Swahili 12:21  Basi, jicho haliwezi kuuambia mkono: "Sikuhitaji wewe", wala kichwa hakiwezi kuiambia miguu: "Siwahitaji ninyi."
I Co Swahili 12:22  Zaidi ya hayo, inaonekana kwamba sehemu zile za mwili zinazoonekana kuwa ni dhaifu ndizo zilizo muhimu zaidi.
I Co Swahili 12:23  Tena, viungo vile tunavyovifikiria kuwa havistahili heshima kubwa, ndivyo tunavyovitunza kwa uangalifu zaidi; viungo vya mwili ambavyo havionekani kuwa vizuri sana, huhifadhiwa zaidi,
I Co Swahili 12:24  ambapo viungo vingine havihitaji kushughulikiwa. Mungu mwenyewe ameuweka mwili katika mpango, akakipa heshima zaidi kiungo kile kilichopungukiwa heshima,
I Co Swahili 12:25  ili kusiweko na utengano katika mwili bali viungo vyote vishughulikiane.
I Co Swahili 12:26  Kama kiungo kimoja kinaumia viungo vyote huumia pamoja nacho. Kiungo kimoja kikisifiwa viungo vingine vyote hufurahi pamoja nacho.
I Co Swahili 12:27  Basi, ninyi nyote ni mwili wa Kristo; kila mmoja wenu ni kiungo cha mwili huo.
I Co Swahili 12:28  Mungu ameweka katika kanisa: kwanza mitume, pili manabii, tatu walimu; kisha ameweka wale wenye kipaji cha kufanya miujiza, kuponya, kusaidia; viongozi na wenye kusema lugha ngeni.
I Co Swahili 12:29  Je, wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni walimu? Wote ni wenye kipaji cha kufanya miujiza?
I Co Swahili 12:30  Je, wote ni wenye kipaji cha kuponya? Wote ni wenye kipaji cha kusema lugha ngeni? Je, wote hufafanua lugha?
I Co Swahili 12:31  Muwe basi, na tamaa ya kupata vipaji muhimu zaidi. Nami sasa nitawaonyesheni njia bora zaidi kuliko hizi zote.