Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
LUKE
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 16
Luke Swahili 16:1  Yesu aliwaambia wanafunzi wake: "Tajiri mmoja alikuwa na karani wake. Huyu karani alichongewa kwamba alitumia ovyo mali ya tajiri wake.
Luke Swahili 16:2  Yule tajiri akamwita akamwambia: Ni mambo gani haya ninayosikia juu yako? Toa hesabu ya mapato na matumizi ya mali yangu, kwa maana huwezi kuwa karani tena.
Luke Swahili 16:3  Yule karani akafikiri: Bwana wangu amenifukuza kazi ya ukarani; nitafanya nini? Kwenda kulima siwezi; kwenda kuombaomba kama maskini ni aibu.
Luke Swahili 16:4  Naam, najua la kufanya, ili nitakapofukuzwa kazi, watu waweze kunikaribisha nyumbani kwao.
Luke Swahili 16:5  Basi, akawaita wadeni wa bwana wake, mmoja mmoja, akamwambia yule wa kwanza: Unadaiwa kiasi gani na bwana wangu?
Luke Swahili 16:6  Yeye akamjibu: Mapipa mia ya mafuta ya zeituni. Yule karani akamwambia: Chukua hati yako ya deni, keti haraka, andika hamsini.
Luke Swahili 16:7  Kisha akamwuliza mdeni mwingine: Wewe unadaiwa kiasi gani? Yeye akamjibu: Magunia mia ya ngano. Yule karani akamwambia: Chukua hati yako ya deni, andika themanini.
Luke Swahili 16:8  "Basi, yule bwana akamsifu huyo karani asiye mwaminifu, kwa kuwa alitumia busara. Kwa maana watu wa dunia hii wana busara zaidi na mambo yao kuliko watu wa mwanga."
Luke Swahili 16:9  Naye Yesu akaendelea kusema, "Nami nawaambieni, jifanyieni marafiki kutokana na mali ya dunia, ili zitakapowaishieni, mweze kupokewa nao katika makao ya milele.
Luke Swahili 16:10  Yeyote aliye mwaminifu katika mambo madogo, atakuwa mwaminifu katika mambo makubwa; na yeyote asiye mwaminifu katika mambo madogo, hatakuwa mwaminifu katika mambo makubwa.
Luke Swahili 16:11  Kama basi, ninyi si hamjawa waaminifu mali mbaya za dunia, ni nani atakayewakabidhi zile mali za kweli?
Luke Swahili 16:12  Na kama hamjakuwa waaminifu katika mali ya mtu mwingine, ni nani atakayewakabidhi mali yenu wenyewe?
Luke Swahili 16:13  "Hakuna mtumishi awezaye kuwatumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia mmoja na kumpenda mwingine, au ataambatana na mmoja na kumdharau mwingine. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali."
Luke Swahili 16:14  Lakini Mafarisayo waliposikia hayo, kwa vile wao walikuwa wanapenda sana fedha, wakamdharau Yesu.
Luke Swahili 16:15  Hapo akawaambia, "Ninyi mnajifanya wema mbele ya watu, lakini Mungu anaijua mioyo yenu. Kwa maana kile kinachoonekana kuwa kitukufu mbele ya watu, Mungu anakiona kuwa takataka.
Luke Swahili 16:16  "Sheria na maandishi ya manabii vilikuweko mpaka wakati wa Yohane mbatizaji. Tangu hapo, Ufalme wa Mungu unahubiriwa, na kila mmoja anauingia kwa nguvu.
Luke Swahili 16:17  Lakini ni rahisi zaidi mbingu na dunia kupita, kuliko hata herufi moja ya Sheria kufutwa.
Luke Swahili 16:18  "Yeyote anayemwacha mke wake na kuoa mwingine, anazini; na yeyote anayemwoa mwanamke aliyepewa talaka, anazini.
Luke Swahili 16:19  "Palikuwa na mtu mmoja tajiri, ambaye alikuwa anavaa mavazi ya bei kubwa sana ya rangi ya zambarau, na ya kitani safi, na kufanya sherehe kila siku.
Luke Swahili 16:20  Kulikuwa pia na maskini mmoja jina lake Lazaro, aliyekuwa amejaa vidonda na alikuwa analazwa mlangoni pa nyumba ya huyo tajiri.
Luke Swahili 16:21  Lazaro alitamani kula makombo yaliyoanguka kutoka meza ya tajiri; na zaidi ya hayo, mbwa walikuwa wanakuja na kulamba vidonda vyake!
Luke Swahili 16:22  "Ikatokea kwamba huyo maskini akafa, malaika wakamchukua, wakamweka karibu na Abrahamu. Na yule tajiri pia akafa, akazikwa.
Luke Swahili 16:23  Huyo tajiri, alikuwa na mateso makali huko kuzimu, akainua macho yake, akamwona Abrahamu kwa mbali na Lazaro karibu naye.
Luke Swahili 16:24  Basi, akaita kwa sauti: Baba Abrahamu, nionee huruma; umtume Lazaro angalau achovye ncha ya kidole chake katika maji, auburudishe ulimi wangu, maana ninateseka mno katika moto huu.
Luke Swahili 16:25  Lakini Abrahamu akamjibu: Kumbuka mwanangu, kwamba ulipokea mema yako katika maisha, naye Lazaro akapokea mabaya. Sasa lakini, yeye anatulizwa, nawe unateswa.
Luke Swahili 16:26  Licha ya hayo, kati yetu na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wanaotaka kuja kwenu kutoka huku wasiweze, wala wanaotaka kutoka kwenu kuja kwetu wasiweze.
Luke Swahili 16:27  Huyo aliyekuwa tajiri akasema: Basi baba, nakuomba umtume aende nyumbani kwa baba yangu,
Luke Swahili 16:28  maana ninao ndugu watano, ili awaonye wasije wakaja huku kwenye mateso.
Luke Swahili 16:29  Lakini Abrahamu akamwambia: Ndugu zako wanao Mose na manabii; waache wawasikilize hao.
Luke Swahili 16:30  Lakini yeye akasema: Sivyo baba Abrahamu, ila kama mtu atafufuka kutoka wafu na kuwaendea, watatubu.
Luke Swahili 16:31  Naye Abrahamu akasema: Kama hawawasikilizi Mose na manabii, hawatajali hata kama mtu angefufuka kutoka wafu."