Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
LUKE
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 1
Luke Swahili 1:1  Mheshimiwa Theofilo: Watu wengi wamejitahidi kuandika juu ya mambo yale yaliyotendeka kati yetu.
Luke Swahili 1:2  Waliandika kama tulivyoelezwa na wale walioyaona kwa macho yao tangu mwanzo, na waliotangaza ujumbe huo.
Luke Swahili 1:3  Inafaa nami pia, Mheshimiwa, baada ya kuchunguza kwa makini mambo yote tangu mwanzo, nikuandikie kwa mpango,
Luke Swahili 1:4  ili nawe uweze kujionea mwenyewe ukweli wa mambo yale uliyofundishwa.
Luke Swahili 1:5  Wakati Herode alipokuwa mfalme wa Yudea, kulikuwa na kuhani mmoja jina lake Zakaria, wa kikundi cha Abia. Mke wake alikuwa anaitwa Elisabeti, naye alikuwa wa ukoo wa kuhani Aroni.
Luke Swahili 1:6  Wote wawili walikuwa wanyofu mbele ya Mungu, wakiishi kwa kufuata amri na maagizo yote ya Bwana bila lawama.
Luke Swahili 1:7  Lakini hawakuwa wamejaliwa watoto kwa vile Elisabeti alikuwa tasa, nao wote wawili walikuwa wazee sana.
Luke Swahili 1:8  Siku moja, ilipokuwa zamu yake ya kutoa huduma ya ukuhani mbele ya Mungu,
Luke Swahili 1:9  Zakariya alichaguliwa kwa kura, kama ilivyokuwa desturi, kuingia hekaluni ili afukize ubani.
Luke Swahili 1:10  Watu, umati mkubwa, walikuwa wamekusanyika nje wanasali wakati huo wa kufukiza ubani.
Luke Swahili 1:11  Malaika wa Bwana akamtokea humo ndani, akasimama upande wa kulia wa madhabahu ya kufukizia ubani.
Luke Swahili 1:12  Zakariya alipomwona alifadhaika, hofu ikamwingia.
Luke Swahili 1:13  Lakini malaika akamwambia, "Zakariya, usiogope, kwa maana sala yako imesikilizwa, na Elisabeti mkeo atakuzalia mtoto wa kiume, nawe utampa jina Yohane.
Luke Swahili 1:14  Utakuwa na furaha kubwa na watu wengi watashangilia kwa sababu ya kuzaliwa kwake.
Luke Swahili 1:15  Atakuwa mkuu mbele ya Bwana. Hatakunywa divai wala kileo, atajazwa Roho Mtakatifu tangu tumboni mwa mama yake.
Luke Swahili 1:16  Atawaelekeza wengi wa watu wa Israeli kwa Bwana Mungu wao.
Luke Swahili 1:17  Atamtangulia Bwana akiongozwa na nguvu na roho kama Eliya. Atawapatanisha kina baba na watoto wao; atawafanya wasiotii wawe na fikira za uadilifu, na hivyo amtayarishie Bwana watu wake."
Luke Swahili 1:18  Zakariya akamwambia huyo malaika, "Ni kitu gani kitakachonihakikishia jambo hilo? Mimi ni mzee, hali kadhalika na mke wangu."
Luke Swahili 1:19  Malaika akamjibu, "Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele ya Mungu, na nimetumwa niseme nawe, nikuletee hii habari njema.
Luke Swahili 1:20  Sikiliza, utakuwa bubu kwa sababu huyasadiki haya maneno yatakayotimia kwa wakati wake. Hutaweza kusema mpaka hayo niliyokuambia yatakapotimia."
Luke Swahili 1:21  Wakati huo, wale watu walikuwa wanamngoja Zakariya huku wakishangaa juu ya kukawia kwake Hekaluni.
Luke Swahili 1:22  Alipotoka nje, hakuweza kusema nao. Ikawa dhahiri kwao kwamba alikuwa ameona maono Hekaluni. Lakini akawa anawapa ishara kwa mikono, akabaki bubu.
Luke Swahili 1:23  Zamu yake ya kuhudumu ilipokwisha, alirudi nyumbani.
Luke Swahili 1:24  Baadaye Elisabeti mkewe akapata mimba. Akajificha nyumbani kwa muda wa miezi mitano, akisema:
Luke Swahili 1:25  "Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana; ameniangalia na kuniondolea aibu niliyokuwa nayo mbele ya watu."
Luke Swahili 1:26  Mnamo mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu aende kwenye mji uitwao Nazareti huko Galilaya,
Luke Swahili 1:27  kwa msichana mmoja aitwaye Maria, mchumba wa mtu mmoja jina lake Yosefu, wa ukoo wa Daudi.
Luke Swahili 1:28  Malaika akamwendea, akamwambia, "Salamu Maria! Umejaliwa neema nyingi! Bwana yu pamoja nawe."
Luke Swahili 1:29  Maria aliposikia maneno hayo alifadhaika sana, akawaza: maneno haya yanamaanisha nini?
Luke Swahili 1:30  Malaika akamwambia, "Usiogope Maria, kwa maana Mungu amekujalia neema.
Luke Swahili 1:31  Utachukua mimba, utamzaa mtoto wa kiume na utampa jina Yesu.
Luke Swahili 1:32  Yeye atakuwa mkuu na ataitwa Mwana wa Mungu Mkuu. Bwana Mungu atampa kiti cha mfalme Daudi, babu yake.
Luke Swahili 1:33  Kwa hivyo atautawala ukoo wa Yakobo milele, na ufalme wake hautakuwa na mwisho."
Luke Swahili 1:34  Maria akamjibu, "Yatawezekanaje hayo, hali mimi ni bikira?"
Luke Swahili 1:35  Malaika akamjibu, "Roho Mtakatifu atakushukia, na uwezo wake Mungu Mkuu utakujia kama kivuli; kwa sababu hiyo, mtoto atakayezaliwa ataitwa Mtakatifu, Mwana wa Mungu.
Luke Swahili 1:36  Ujue pia kwamba hata Elisabeti, jamaa yako, naye amepata mimba ingawa ni mzee, na sasa ni mwezi wa sita kwake yeye ambaye watu walimfahamu kuwa tasa.
Luke Swahili 1:37  Kwa maana hakuna jambo lisilowezekana kwa Mungu."
Luke Swahili 1:38  Maria akasema, "Mimi ni mtumishi wa Bwana, nitendewe kama ulivyosema." Kisha yule malaika akaenda zake.
Luke Swahili 1:39  Siku kadhaa baadaye, Maria alifunga safari akaenda kwa haraka hadi mji mmoja ulioko katika milima ya Yuda.
Luke Swahili 1:40  Huko, aliingia katika nyumba ya Zakariya, akamsalimu Elisabeti.
Luke Swahili 1:41  Mara tu Elisabeti aliposikia sauti ya Maria, mtoto mchanga tumboni mwake Elisabeti akaruka. Naye Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifiu,
Luke Swahili 1:42  akasema kwa sauti kubwa, "Umebarikiwa kuliko wanawake wote, naye utakayemzaa amebarikiwa.
Luke Swahili 1:43  Mimi ni nani hata mama wa Bwana wangu afike kwangu?
Luke Swahili 1:44  Nakwambia, mara tu niliposikia sauti yako, mtoto mchanga tumboni mwangu aliruka kwa furaha.
Luke Swahili 1:45  Heri yako wewe uliyesadiki kwamba yatatimia yale Bwana aliyokwambia."
Luke Swahili 1:47  "Moyo wangu wamtukuza Bwana, roho yangu inafurahi kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
Luke Swahili 1:48  Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma mtumishi wake mnyenyekevu. Hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
Luke Swahili 1:49  Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu, jina lake ni takatifu.
Luke Swahili 1:50  Huruma yake kwa watu wanaomcha hudumu kizazi hata kizazi.
Luke Swahili 1:51  Amefanya mambo makuu kwa mkono wake: amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
Luke Swahili 1:52  amewashusha wenye nguvu kutoka vitu vyao vya enzi, akawakweza wanyenyekevu.
Luke Swahili 1:53  Wenye njaa amewashibisha mema, matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
Luke Swahili 1:54  Amemsaidia Israeli mtumishi wake, akikumbuka huruma yake.
Luke Swahili 1:55  Kama alivyowaahidia wazee wetu Abrahamu na wazawa wake hata milele."
Luke Swahili 1:56  Maria alikaa na Elisabeti kwa muda upatao miezi mitatu, halafu akarudi nyumbani kwake.
Luke Swahili 1:57  Wakati wa kujifungua kwake Elisabeti ulifika, akajifungua mtoto wa kiume.
Luke Swahili 1:58  Jirani na watu wa jamaa yake walipopata habari kwamba Bwana amemwonea huruma kubwa, walifurahi pamoja naye.
Luke Swahili 1:59  Halafu siku ya nane walifika kumtahiri mtoto, wakataka kumpa jina la baba yake, Zakariya.
Luke Swahili 1:60  Lakini mama yake akasema, "La, sivyo, bali ataitwa Yohane."
Luke Swahili 1:61  Wakamwambia, "Mbona hakuna yeyote katika ukoo wake mwenye jina hilo?"
Luke Swahili 1:62  Basi, wakamwashiria baba yake wapate kujua alitaka mtoto wake apewe jina gani.
Luke Swahili 1:63  Naye akaomba kibao cha kuandikia, akaandika hivi: "Yohane ndilo jina lake." Wote wakastaajabu.
Luke Swahili 1:64  Papo hapo midomo na ulimi wake Zakariya vikafunguliwa, akawa anaongea akimsifu Mungu.
Luke Swahili 1:65  Hofu ikawaingia jirani wote, na habari hizo zikaenea kila mahali katika milima ya Yudea.
Luke Swahili 1:66  Wote waliosikia mambo hayo waliyatafakari mioyoni mwao wakisema: "Mtoto huyu atakuwa mtu wa namna gani?" Maana, hakika nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye.
Luke Swahili 1:67  Zakariya, baba yake mtoto, akajazwa Roho Mtakatifu, akatamka ujumbe wa Mungu:
Luke Swahili 1:68  "Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli, kwani amekuja kuwasaidia na kuwakomboa watu wake.
Luke Swahili 1:69  Ametupatia Mwokozi shujaa, mzawa wa Daudi mtumishi wake.
Luke Swahili 1:70  Aliahidi hapo kale kwa njia ya manabii wake watakatifu,
Luke Swahili 1:71  kwamba atatuokoa mikononi mwa adui zetu na kutoka mikononi mwa wote wanaotuchukia.
Luke Swahili 1:72  Alisema atawahurumia wazee wetu, na kukumbuka agano lake takatifu.
Luke Swahili 1:73  Kiapo alichomwapia Abrahamu baba yetu, ni kwamba atatujalia sisi
Luke Swahili 1:74  tukombolewe kutoka adui zetu, tupate kumtumikia bila hofu,
Luke Swahili 1:75  kwa unyofu na uadilifu mbele yake, siku zote za maisha yetu.
Luke Swahili 1:76  Nawe mwanangu, utaitwa, nabii wa Mungu Mkuu, utamtangulia Bwana kumtayarishia njia yake;
Luke Swahili 1:77  kuwatangazia watu kwamba wataokolewa kwa kuondolewa dhambi zao.
Luke Swahili 1:78  Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma. Atasababisha pambazuko angavu la ukombozi litujie kutoka juu,
Luke Swahili 1:79  na kuwaangazia wote wanaokaa katika giza kuu la kifo, aongoze hatua zetu katika njia ya amani."
Luke Swahili 1:80  Mtoto akakua, akapata nguvu rohoni. Alikaa jangwani mpaka alipojionyesha rasmi kwa watu wa Israeli.