Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
LUKE
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 6
Luke Swahili 6:1  Siku moja ya Sabato, Yesu alikuwa anapita katika mashamba ya ngano, na wanafunzi wake wakaanza kukwanyua masuke ya ngano, wakaondoa punje zake kwa mikono, wakala.
Luke Swahili 6:2  Baadhi ya Mafarisayo wakawauliza, "Mbona mnafanya jambo ambalo si halali siku ya Sabato?"
Luke Swahili 6:3  Yesu akawajibu, "Je, hamjasoma jinsi alivyofanya Daudi pamoja na wenzake wakati walipokuwa na njaa?
Luke Swahili 6:4  Yeye aliingia ndani ya nyumba ya Mungu, akachukua ile mikate iliyowekwa mbele ya Mungu, akala na kuwapa wenzake. Kisheria, ni makuhani tu peke yao ndio walioruhusiwa kula mikate hiyo."
Luke Swahili 6:5  Hivyo akawaambia, "Mwana wa Mtu ni Bwana wa Sabato."
Luke Swahili 6:6  Siku nyingine ya Sabato, Yesu aliingia katika sunagogi, akafundisha. Mle ndani mlikuwa na mtu ambaye mkono wake wa kuume ulikuwa umepooza.
Luke Swahili 6:7  Walimu wa Sheria na Mafarisayo walitaka kupata kisingizio cha kumshtaki Yesu na hivyo wakawa wanangojea waone kama angemponya mtu siku ya Sabato.
Luke Swahili 6:8  Lakini Yesu alijua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, "Inuka, simama katikati." Yule mtu akaenda akasimama katikati.
Luke Swahili 6:9  Kisha Yesu akawaambia, "Nawaulizeni, je, ni halali siku ya Sabato kutenda jambo jema au kutenda jambo baya; kuokoa maisha au kuyaangamiza?"
Luke Swahili 6:10  Baada ya kuwatazama wote waliokuwa pale, akamwambia yule mtu, "Nyosha mkono wako." Naye akafanya hivyo, na mkono wake ukawa mzima tena.
Luke Swahili 6:11  Lakini wao wakakasirika sana, wakajadiliana jinsi ya kumtendea Yesu maovu.
Luke Swahili 6:12  Siku moja Yesu alikwenda mlimani kusali, akakesha huko usiku kucha akimwomba Mungu.
Luke Swahili 6:13  Kesho yake aliwaita wanafunzi wake, na miongoni mwao akachagua kumi na wawili ambao aliwaita mitume:
Luke Swahili 6:14  Simoni (ambaye Yesu alimpa jina Petro) na Andrea ndugu yake, Yakobo na Yohane, Filipo na Bartholomayo,
Luke Swahili 6:15  Mathayo na Thoma, Yakobo wa Alfayo na Simoni (aliyeitwa Zelote),
Luke Swahili 6:16  Yuda wa Yakobo na Yuda Iskarioti ambaye baadaye alikuwa msaliti.
Luke Swahili 6:17  Baada ya kushuka mlimani pamoja na mitume, Yesu alisimama mahali palipokuwa tambarare. Hapo palikuwa na kundi kubwa la wanafunzi wake na umati wa watu waliotoka pande zote za Yudea na Yerusalemu na pwani ya Tiro na Sidoni. Wote walifika kumsikiliza Yesu na kuponywa magonjwa yao.
Luke Swahili 6:18  Aliwaponya pia wote waliokuwa wanasumbuliwa na pepo wachafu.
Luke Swahili 6:19  Watu wote walitaka kumgusa, kwa maana nguvu ilikuwa inatoka ndani yake na kuwaponya wote.
Luke Swahili 6:20  Yesu akawageukia wanafunzi wake, akasema: "Heri ninyi mlio maskini, maana Ufalme wa Mungu ni wenu.
Luke Swahili 6:21  Heri ninyi mnaosikia njaa sasa, maana baadaye mtashiba. Heri ninyi mnaolia sasa, maana baadaye mtacheka kwa furaha.
Luke Swahili 6:22  "Heri yenu ninyi iwapo watu watawachukia, watawatenga, watawatukana na kuwaharibieni jina kwa ajili ya Mwana wa Mtu!
Luke Swahili 6:23  Wakati hayo yatakapotokea, furahini na kucheza, maana hakika tuzo lenu ni kubwa mbinguni. Kwa maana wazee wao waliwatendea manabii vivyo hivyo.
Luke Swahili 6:24  Lakini ole wenu ninyi mlio matajiri, maana mmekwisha pata faraja yenu.
Luke Swahili 6:25  Ole wenu ninyi mnaoshiba sasa, maana baadaye mtasikia njaa. Ole wenu ninyi mnaocheka kwa furaha sasa, maana baadaye mtaomboleza na kulia.
Luke Swahili 6:26  Ole wenu ninyi iwapo watu wote wanawasifu, maana wazee wao waliwafanyia manabii wa uongo vivyo hivyo.
Luke Swahili 6:27  "Lakini nawaambieni ninyi mnaonisikiliza: wapendeni adui zenu, watendeeni mema wale wanaowachukieni.
Luke Swahili 6:28  Watakieni baraka wale wanaowalaani, na waombeeni wale wanaowatendea vibaya.
Luke Swahili 6:29  Mtu akikupiga shavu moja mgeuzie na la pili. Mtu akikunyang'anya koti lako mwachie pia shati lako.
Luke Swahili 6:30  Yeyote anayekuomba mpe, na mtu akikunyang'anya mali yako usimtake akurudishie.
Luke Swahili 6:31  Watendeeni wengine kama mnavyotaka wawatendee ninyi.
Luke Swahili 6:32  "Na ikiwa mnawapenda tu wale wanaowapenda ninyi, je, mtapata tuzo gani? Hakuna! Kwa maana hata wenye dhambi huwapenda wale wanaowapenda wao.
Luke Swahili 6:33  Tena, kama mkiwatendea mema wale tu wanaowatendeeni mema, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi hufanya vivyo hivyo!
Luke Swahili 6:34  Na kama mnawakopesha wale tu mnaotumaini watawalipeni, je, mtapata tuzo gani? Hata wenye dhambi huwakopesha wenye dhambi wenzao ili warudishiwe kima kilekile!
Luke Swahili 6:35  Ila nyinyi wapendeni adui zenu, na kuwatendea mema; kopesheni bila kutazamia malipo, na tuzo lenu litakuwa kubwa, nanyi mtakuwa watoto wa Mungu aliye juu. Kwa maana yeye ni mwema kwa wale wasio na shukrani na walio wabaya.
Luke Swahili 6:37  "Msiwahukumu wengine, nanyi hamtahukumiwa; msiwalaumu wengine, nanyi hamtalaumiwa; wasameheni wengine, nanyi mtasamehewa.
Luke Swahili 6:38  Wapeni wengine wanavyohitaji, nanyi mtapewa. Naam, mtapokea mikononi mwenu kipimo kilichojaa, kikashindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika. Kwa maana kipimo kilekile mnachotumia kwa wengine ndicho ambacho Mungu atatumia kwenu."
Luke Swahili 6:39  Akawaambia mfano huu: "Je, kipofu anaweza kumwongoza kipofu mwenzake? La! Wote wataanguka shimoni.
Luke Swahili 6:40  Mwanafunzi hamshindi mwalimu wake, lakini kila mwanafunzi akisha hitimu huwa kama mwalimu wake.
Luke Swahili 6:41  Unawezaje kukiona kibanzi kilicho katika jicho la mwenzio, usione boriti iliyo katika jicho lako mwenyewe?
Luke Swahili 6:42  Au, unawezaje kumwambia mwenzako, Ndugu, ngoja nikuondoe kibanzi katika jicho lako, na huku huioni boriti iliyoko katika jicho lako mwenyewe? Mnafiki wewe! Toa kwanza boriti iliyoko jichoni mwako, na hivyo utaona sawasawa kiasi cha kuweza kuondoa kibanzi kilicho katika jicho la ndugu yako.
Luke Swahili 6:43  "Mti mwema hauzai matunda mabaya, wala mti mbaya hauzai matunda mazuri.
Luke Swahili 6:44  Watu huutambua mti kutokana na matunda yake. Ni wazi kwamba watu hawachumi tini katika michongoma, wala hawachumi zabibu katika mbigili.
Luke Swahili 6:45  Mtu mwema hutoa yaliyo mema kutoka katika hazina bora iliyo moyoni mwake; na mtu mbaya hutoa yaliyo mabaya katika hazina mbaya iliyo moyoni mwake, kwa maana mtu huongea kutokana na yale yaliyojaa moyoni mwake.
Luke Swahili 6:46  "Mbona mwaniita Bwana, Bwana, na huku hamtimizi yale ninayosema?
Luke Swahili 6:47  Nitawapeni mfano unaofaa kuonyesha alivyo yeyote yule anayekuja kwangu, akasikia maneno yangu na kuyatimiza:
Luke Swahili 6:48  Huyo anafanana na mtu ajengaye nyumba, ambaye amechimba chini na kuweka msingi wake juu ya mwamba; kukatokea mafuriko ya mto, mkondo wa maji ukaipiga nyumba ile, lakini haukuweza kuitikisa, kwa sababu ilikuwa imejengwa imara.
Luke Swahili 6:49  Lakini yeyote anayesikia maneno yangu lakini asifanye chochote, huyo anafanana na mtu aliyejenga nyumba juu ya udongo, bila msingi. Mafuriko ya mto yakatokea, mkondo wa maji ukaipiga nyumba ile, ikaanguka na kuharibika kabisa!"