Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
LUKE
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 5
Luke Swahili 5:1  Siku moja Yesu alikuwa amesimama kando ya ziwa Genesareti, na watu wengi walikuwa wamemzunguka wakisongana wanalisikiliza neno la Mungu.
Luke Swahili 5:2  Akaona mashua mbili ukingoni mwa ziwa; wavuvi wenyewe walikuwa wametoka, wanaosha nyavu zao.
Luke Swahili 5:3  Baada ya Yesu kuingia katika mashua moja, iliyokuwa ya Simoni, alimtaka Simoni aisogeze majini, mbali kidogo na ukingo wa ziwa. Akaketi, akafundisha umati wa watu akiwa ndani ya mashua.
Luke Swahili 5:4  Alipomaliza kufundisha, akamwambia Simoni, "Peleka mashua mpaka kilindini, mkatupe nyavu zenu mpate kuvua samaki."
Luke Swahili 5:5  Simoni akamjibu, "Bwana, tumejitahidi kuvua samaki usiku kucha bila kupata kitu, lakini kwa kuwa umesema, nitatupa nyavu."
Luke Swahili 5:6  Baada ya kufanya hivyo, wakavua samaki wengi, hata nyavu zao zikaanza kukatika.
Luke Swahili 5:7  Wakawaita wenzao waliokuwa katika mashua nyingine waje kuwasaidia. Wakaja, wakazijaza mashua zote mbili samaki, hata karibu zingezama.
Luke Swahili 5:8  Simoni Petro alipoona hayo, akapiga magoti mbele ya Yesu akisema, "Ondoka mbele yangu, ee Bwana, kwa kuwa mimi ni mwenye dhambi!"
Luke Swahili 5:9  Simoni pamoja na wenzake wote walishangaa kwa kupata samaki wengi vile.
Luke Swahili 5:10  Hali kadhalika Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, waliokuwa wavuvi wenzake Simoni. Yesu akamwambia Simoni, "Usiogope; tangu sasa utakuwa ukivua watu."
Luke Swahili 5:11  Basi, baada ya kuzileta zile mashua ukingoni mwa ziwa, wakaacha yote, wakamfuata.
Luke Swahili 5:12  Ikawa, Yesu alipokuwa katika mmojawapo wa miji ya huko, mtu mmoja mwenye ukoma mwili mzima akamwona. Basi, mtu huyo akaanguka kifudifudi akamwomba Yesu: "Mheshimiwa, ukitaka, waweza kunitakasa."
Luke Swahili 5:13  Yesu akaunyosha mkono wake, akamgusa na kusema, "Nataka, takasika!" Mara ule ukoma ukamwacha.
Luke Swahili 5:14  Yesu akamwamuru: "Usimwambie mtu yeyote; bali nenda ukajionyeshe kwa kuhani, ukatoe sadaka kwa ajili ya kutakasika kwako kama inavyotakiwa na Sheria ya Mose, iwe uthibitisho kwao kwamba umepona."
Luke Swahili 5:15  Lakini habari za Yesu zilizidi kuenea kila mahali. Watu makundi mengi wakakusanyika ili kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao.
Luke Swahili 5:16  Lakini yeye alikwenda zake mahali pasipo na watu, akawa anasali huko.
Luke Swahili 5:17  Siku moja Yesu alikuwa akifundisha. Mafarisayo na walimu wa Sheria kutoka katika kila kijiji cha Galilaya, Yudea na Yerusalemu, walikuwa wameketi hapo. Nguvu ya Bwana ilikuwa pamoja naye kwa ajili ya kuponyea wagonjwa.
Luke Swahili 5:18  Mara watu wakaja wamemchukua mtu mmoja aliyepooza maungo, amelala kitandani; wakajaribu kumwingiza ndani wamweke mbele ya Yesu.
Luke Swahili 5:19  Lakini kwa sababu ya wingi wa watu, hawakuweza kuingia ndani. Basi, wakapanda juu ya dari, wakaondoa vigae, wakamshusha huyo aliyepooza pamoja na kitanda chake, wakamweka mbele ya Yesu.
Luke Swahili 5:20  Yesu alipoona jinsi walivyokuwa na imani kubwa, akamwambia huyo mtu, "Rafiki, umesamehewa dhambi zako."
Luke Swahili 5:21  Walimu wa Sheria na Mafarisayo wakaanza kujiuliza: "Nani huyu anayemkufuru Mungu kwa maneno yake? Hakuna mtu awezaye kusamehe dhambi ila Mungu peke yake!"
Luke Swahili 5:22  Yesu alitambua mawazo yao, akawauliza, "Mnawaza nini mioyoni mwenu?
Luke Swahili 5:23  Ni lipi lililo rahisi zaidi: kusema, Umesamehewa dhambi, au kusema, Simama utembee?
Luke Swahili 5:24  Basi, nataka mjue kwamba Mwana wa Mtu anao uwezo wa kusamehe dhambi duniani." Hapo akamwambia huyo mtu aliyepooza, "Simama, chukua kitanda chako uende zako nyumbani."
Luke Swahili 5:25  Mara, huyo mtu aliyepooza akasimama mbele yao wote, akachukua kitanda chake akaenda zake nyumbani huku akimtukuza Mungu.
Luke Swahili 5:26  Wote wakashangaa na kushikwa na hofu; wakamtukuza Mungu wakisema: "Tumeona maajabu leo."
Luke Swahili 5:27  Baada ya hayo, Yesu akatoka nje, akamwona mtoza ushuru mmoja aitwaye Lawi, ameketi ofisini. Yesu akamwambia, "Nifuate!"
Luke Swahili 5:29  Kisha Lawi akamwandalia Yesu karamu kubwa nyumbani mwake; na kundi kubwa la watoza ushuru na watu wengine walikuwa wameketi pamoja nao.
Luke Swahili 5:30  Mafarisayo na walimu wa Sheria wakawanung'unikia wafuasi wake wakisema: "Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?"
Luke Swahili 5:31  Yesu akawajibu, "Wenye afya hawahitaji daktari, lakini wanaomhitaji ni wale walio wagonjwa.
Luke Swahili 5:32  Sikuja kuwaita watu wema, bali wenye dhambi, ili wapate kutubu."
Luke Swahili 5:33  Watu wengine wakamwambia Yesu, "Wafuasi wa Yohane mbatizaji hufunga mara nyingi na kusali; hata wafuasi wa Mafarisayo hufanya vivyo hivyo. Lakini wafuasi wako hula na kunywa."
Luke Swahili 5:34  Yesu akawajibu, "Je, mnaweza kuwataka wale walioalikwa arusini wafunge hali bwana arusi yuko pamoja nao?
Luke Swahili 5:35  Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kati yao, na wakati huo ndipo watakapofunga."
Luke Swahili 5:36  Yesu akawaambia mfano huu: "Hakuna mtu akataye kiraka cha nguo mpya na kukitia katika vazi kuukuu; kama akifanya hivyo, atakuwa amelikata hilo vazi jipya, na hicho kiraka hakitachukuana na hilo vazi kuukuu.
Luke Swahili 5:37  Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu; kwani hiyo divai mpya itavipasua hivyo viriba, divai itamwagika, na viriba vitaharibika.
Luke Swahili 5:39  Wala hakuna mtu ambaye hutamani kunywa divai mpya baada ya kunywa ya zamani, kwani husema: Ile ya zamani ni nzuri zaidi."