Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
LUKE
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 19
Luke Swahili 19:1  Yesu aliingia mjini Yeriko, akawa anapita katika njia za mji huo.
Luke Swahili 19:2  Kulikuwa na mtu mmoja mjini, jina lake Zakayo ambaye alikuwa mkuu wa watoza ushuru tena mtu tajiri.
Luke Swahili 19:3  Alitaka kuona Yesu alikuwa nani, lakini kwa sababu ya umati wa watu, na kwa vile alikuwa mfupi, hakufaulu.
Luke Swahili 19:4  Hivyo, alitangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu ili aweze kumwona Yesu, kwa maana alikuwa apitie hapo.
Luke Swahili 19:5  Basi, Yesu alipofika mahali pale, aliangalia juu akamwambia, "Zakayo, shuka upesi, maana leo ni lazima nishinde nyumbani mwako."
Luke Swahili 19:6  Zakayo akashuka haraka, akamkaribisha kwa furaha.
Luke Swahili 19:7  Watu wote walipoona hayo, wakaanza kunung'unika wakisema, "Amekwenda kukaa kwa mtu mwenye dhambi."
Luke Swahili 19:8  Lakini Zakayo akasimama akamwambia Yesu, "Sikiliza Bwana! Mimi nitawapa maskini nusu ya mali yangu, na kama nimenyang'anya mtu yeyote kitu, nitamrudishia mara nne."
Luke Swahili 19:9  Yesu akamwambia, "Leo wokovu umefika katika nyumba hii, kwa vile huyu pia ni wa ukoo wa Abrahamu.
Luke Swahili 19:10  Kwa maana Mwana wa Mtu amekuja kutafuta na kuokoa waliopotea."
Luke Swahili 19:11  Wakati watu walipokuwa bado wanasikiliza hayo, Yesu akawaambia mfano. (Hapo alikuwa anakaribia Yerusalemu, na watu wale walidhani kwamba muda si muda, Ufalme wa Mungu ungefika.)
Luke Swahili 19:12  Hivyo akawaambia, "Kulikuwa na mtu mmoja wa ukoo wa kifalme aliyefanya safari kwenda nchi ya mbali ili apokee madaraka ya ufalme, halafu arudi.
Luke Swahili 19:13  Basi, kabla ya kuondoka aliwaita watumishi wake kumi, akawapa kiasi cha fedha kila mmoja na kumwambia: Fanyeni nazo biashara mpaka nitakaporudi.
Luke Swahili 19:14  Lakini wananchi wenzake walimchukia na hivyo wakatuma wajumbe waende wakaseme: Hatumtaki huyu atutawale.
Luke Swahili 19:15  "Huyo mtu mashuhuri alirudi nyumbani baada ya kufanywa mfalme, na mara akaamuru wale watumishi aliowapa zile fedha waitwe ili aweze kujua kila mmoja amepata faida gani.
Luke Swahili 19:16  Mtumishi wa kwanza akatokea, akasema: Mheshimiwa, faida iliyopatikana ni mara kumi ya zile fedha ulizonipa.
Luke Swahili 19:17  Naye akamwambia: Vema; wewe ni mtumishi mwema. Kwa kuwa umekuwa mwaminifu katika jambo dogo, utakuwa na madaraka juu ya miji kumi!
Luke Swahili 19:18  Mtumishi wa pili akaja, akasema: Mheshimiwa, faida iliyopatikana ni mara tano ya zile fedha ulizonipa.
Luke Swahili 19:19  Naye akamwambia pia: Nawe utakuwa na madaraka juu ya miji mitano.
Luke Swahili 19:20  "Mtumishi mwingine akaja, akasema: Chukua fedha yako; niliificha salama katika kitambaa,
Luke Swahili 19:21  kwa maana niliogopa kwa sababu wewe ni mtu mkali. Wewe ni mtu ambaye huchukua yasiyo yako, na huchuma ambacho hukupanda.
Luke Swahili 19:22  Naye akamwambia: Nakuhukumu kutokana na msemo wako, ewe mtumishi mbaya! Ulijua kwamba mimi ni mtu mkali, ambaye huchukua yasiyo yangu na kuchuma nisichopanda.
Luke Swahili 19:23  Kwa nini basi, hukuiweka fedha yangu benki, nami ningeichukua pamoja na faida baada ya kurudi kwangu?
Luke Swahili 19:24  Hapo akawaambia wale waliokuwa pale: Mnyang'anyeni hizo fedha, mkampe yule aliyepata faida mara kumi.
Luke Swahili 19:25  Nao wakamwambia: Lakini Mheshimiwa, huyo ana faida ya kiasi hicho mara kumi!
Luke Swahili 19:26  Naye akawajibu: Kila aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa. Lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa.
Luke Swahili 19:27  Na sasa, kuhusu hao maadui wangu ambao hawapendi niwe mfalme wao, waleteni hapa, mkawaue papa hapa mbele yangu."
Luke Swahili 19:28  Yesu alisema hayo, kisha akatangulia mbele yao kuelekea Yerusalemu.
Luke Swahili 19:29  Alipokaribia kufika Bethfage na Bethania, karibu na mlima wa Mizeituni, aliwatuma wanafunzi wake wawili,
Luke Swahili 19:30  akawaambia: "Nendeni katika kijiji kilicho mbele yenu. Mtakapokuwa mnaingia kijijini, mtamkuta mwana punda amefungwa ambaye hajatumiwa na mtu. Mfungeni, mkamlete hapa.
Luke Swahili 19:31  Kama mtu akiwauliza, kwa nini mnamfungua, mwambieni, Bwana ana haja naye."
Luke Swahili 19:32  Basi, wakaenda, wakakuta sawa kama alivyowaambia.
Luke Swahili 19:33  Walipokuwa wanamfungua yule mwana punda, wenyewe wakawauliza, "Kwa nini mnamfungua mwana punda huyu?"
Luke Swahili 19:35  Basi, wakampelekea Yesu yule mwana punda. Kisha wakatandika mavazi yao juu yake wakampandisha Yesu.
Luke Swahili 19:36  Yesu akaendelea na safari, na watu wakatandaza mavazi yao barabarani.
Luke Swahili 19:37  Alipofika karibu na Yerusalemu, katika mteremko wa mlima wa Mizeituni, umati wote na wanafunzi wake, wakaanza kushangilia na kumtukuza Mungu kwa sauti kubwa, kwa sababu ya mambo makuu waliyoyaona;
Luke Swahili 19:38  wakawa wanasema: "Abarikiwe Mfalme ajaye kwa jina la Bwana. Amani mbinguni, na utukufu juu mbinguni!"
Luke Swahili 19:39  Hapo baadhi ya Mafarisayo waliokuwako katika lile kundi la watu, wakamwambia Yesu, "Mwalimu, wanyamazishe wanafunzi wako!"
Luke Swahili 19:40  Yesu akawajibu, "Nawaambieni, kama hawa wakinyamaza, hakika hayo mawe yatapaza sauti."
Luke Swahili 19:41  Alipokaribia zaidi na kuuona ule mji, Yesu aliulilia
Luke Swahili 19:42  akisema: "Laiti ungelijua leo hii yale yaletayo amani! Lakini sasa yamefichika machoni pako.
Luke Swahili 19:43  Maana siku zaja ambapo adui zako watakuzungushia maboma, watakuzingira na kukusonga pande zote.
Luke Swahili 19:44  Watakupondaponda wewe pamoja na watoto wako ndani ya kuta zako; hawatakuachia hata jiwe moja juu jingine, kwa sababu hukuutambua wakati Mungu alipokujia kukuokoa."
Luke Swahili 19:45  Kisha, Yesu aliingia Hekaluni, akaanza kuwafukuzia nje wafanyabiashara
Luke Swahili 19:46  akisema, "Imeandikwa: Nyumba yangu itakuwa nyumba ya sala; lakini ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi."
Luke Swahili 19:47  Yesu akawa anafundisha kila siku Hekaluni. Makuhani wakuu, walimu wa Sheria na viongozi wa watu walitaka kumwangamiza,
Luke Swahili 19:48  lakini hawakuwa na la kufanya, maana watu wote walikuwa wakimsikiliza kwa makini kabisa.