Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
LUKE
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 23
Luke Swahili 23:1  Kisha, wote kwa jumla, wakasimama, wakampeleka Yesu mbele ya Pilato.
Luke Swahili 23:2  Wakaanza kumshtaki wakisema: "Tulimkuta mtu huyu akiwapotosha watu wetu, akipinga kulipa kodi kwa Kaisari na kujiita ati yeye ni Kristo, Mfalme."
Luke Swahili 23:3  Pilato akamwuliza Yesu, "Wewe ni Mfalme wa Wayahudi?" Yesu akamjibu, "Wewe umesema."
Luke Swahili 23:4  Pilato akawaambia makuhani wakuu na umati wa watu, "Sioni kosa lolote katika mtu huyu."
Luke Swahili 23:5  Lakini wao wakasisitiza wakisema: "Anawachochea watu kwa mafundisho yake katika nchi yote ya Yudea; alianza Galilaya, na sasa yuko hapa."
Luke Swahili 23:6  Pilato aliposikia hayo, akauliza, "Je, mtu huyu ni mwenyeji wa Galilaya?"
Luke Swahili 23:7  Alipojua kwamba Yesu alikuwa chini ya utawala wa Herode, akampeleka kwa Herode, ambaye wakati huo alikuwa Yerusalemu.
Luke Swahili 23:8  Herode alifurahi sana alipomwona Yesu. Alikuwa amekwisha sikia habari zake, na hivyo alikuwa anatazamia kwa muda mrefu kumwona kwa macho yake mwenyewe. Zaidi ya hayo, alikuwa anatumaini kumwona Yesu akitenda mwujiza.
Luke Swahili 23:9  Basi, akamwuliza maswali mengi kwa muda mrefu, lakini Yesu hakumjibu neno.
Luke Swahili 23:10  Makuhani wakuu na walimu wa Sheria wakajitokeza mbele, wakatoa mashtaka yao kwa nguvu sana.
Luke Swahili 23:11  Basi, herode pamoja na maaskari wake, wakamwaibisha Yesu na kumfanyia mzaha; kisha wakamvika vazi la kifalme, wakamrudisha kwa Pilato.
Luke Swahili 23:12  Herode na Pilato, ambao hapo awali walikuwa maadui, tangu siku hiyo wakawa marafiki.
Luke Swahili 23:13  Basi, Pilato akaitisha mkutano wa makuhani wakuu, viongozi na watu,
Luke Swahili 23:14  akawaambia, "Mmemleta mtu huyu kwangu mkisema kwamba alikuwa anawapotosha watu. Sasa sikilizeni! Baada ya kuchunguza jambo hilo mbele yenu, sikumpata na kosa lolote kuhusu mashtaka yenu juu yake.
Luke Swahili 23:15  Wala si mimi tu, bali hata Herode hakuona kosa lolote, kwa maana amemrudisha kwangu. Ni dhahiri kwamba mtu huyu hakufanya chochote kinachostahili adhabu ya kifo.
Luke Swahili 23:16  Hivyo, nitaamuru apigwe viboko, halafu nitamwachilia."
Luke Swahili 23:17  Kila sikukuu ya Pasaka, ilimlazimu Pilato kuwafungulia mfungwa mmoja.
Luke Swahili 23:18  Lakini wote wakapiga kelele pamoja: "Mwondoe huyo, utufungulie Baraba!"
Luke Swahili 23:19  (Baraba alikuwa ametiwa ndani kwa kusababisha uasi katika mji na pia kwa sababu ya kuua.)
Luke Swahili 23:20  Pilato alitaka kumwachilia Yesu, hivyo akasema nao tena;
Luke Swahili 23:21  lakini wao wakapiga kelele: "Msulubishe, msulubishe!"
Luke Swahili 23:22  Pilato akawaambia mara ya tatu, "Amefanya kosa gani? Sioni kosa lolote kwake linalomstahili auawe; kwa hiyo nitampiga viboko, halafu nimwachilie."
Luke Swahili 23:23  Lakini wao wakazidi kupiga kelele kwa nguvu sana, kwamba Yesu ni lazima asulubiwe. Mwishowe, sauti zao zikashinda.
Luke Swahili 23:24  Basi, Pilato akaamua kwamba matakwa yao yatimizwe.
Luke Swahili 23:25  Akamfungua kutoka gerezani yule waliyemtaka, ambaye alikuwa ametiwa gerezani kwa sababu ya uasi na kuua; akamtoa Yesu kwao, wamfanyie walivyotaka.
Luke Swahili 23:26  Walipokuwa wakimpeleka, walikutana na mtu mmoja, aitwaye Simoni wa Kurene, aliyekuwa anatoka shambani. Basi, walimkamata, wakamtwika ule msalaba auchukue nyuma ya Yesu.
Luke Swahili 23:27  Watu, umati kwa umati, walimfuata; miongoni mwao wakiwemo wanawake waliokuwa wanaomboleza na kumlilia.
Luke Swahili 23:28  Yesu akawageukia, akasema, "Enyi kina mama wa Yerusalemu! Msinililie mimi, ila lieni kwa ajili yenu wenyewe na kwa ajili ya watoto wenu.
Luke Swahili 23:29  Maana, hakika siku zitakuja ambapo watasema: Heri yao wale walio tasa, ambao hawakupata kuzaa wala kunyonyesha watoto!
Luke Swahili 23:30  Wakati huo, ndipo watu wataanza kuiambia milima: Tuangukieni! na vilima, Tufunikeni!
Luke Swahili 23:31  Kwa maana, kama watu wanautendea mti mbichi namna hiyo, itakuwaje kwa mti mkavu?"
Luke Swahili 23:32  Waliwachukua pia watu wengine wawili, wahalifu, wauawe pamoja naye.
Luke Swahili 23:33  Walipofika mahali paitwapo, "Fuvu la Kichwa," ndipo wakamsulubisha Yesu pamoja na wale wahalifu wawili, mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto.
Luke Swahili 23:34  Yesu akasema, "Baba, uwasamehe kwa maana hawajui wanalofanya." Kisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura.
Luke Swahili 23:35  Watu wakawa wamesimama pale wakitazama. Nao viongozi wakamdhihaki wakisema: "Amewaokoa wengine; sasa na ajiokoe mwenyewe, kama yeye ndiye Kristo, mteule wa Mungu!"
Luke Swahili 23:36  Askari nao walimdhihaki pia; walimwendea wakampa siki
Luke Swahili 23:37  wakisema: "Kama kweli wewe ni Mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe."
Luke Swahili 23:38  Vilevile maandishi haya yalikuwa yameandikwa na kuwekwa juu yake: "Huyu ndiye Mfalme wa Wayahudi."
Luke Swahili 23:39  Mmoja wa wale wahalifu waliotundikwa msalabani, alimtukana akisema: "Je, si kweli kwamba wewe ndiwe Kristo? Basi, jiokoe mwenyewe, utuokoe na sisi pia."
Luke Swahili 23:40  Lakini yule mhalifu mwingine akamkemea mwenzake akisema: "Wewe humwogopi Mungu hata kidogo? Wewe umepata adhabu hiyohiyo.
Luke Swahili 23:41  Wewe na mimi tunastahili, maana haya ni malipo ya yale tuliyotenda. Lakini mtu huyu hakufanya chochote kibaya."
Luke Swahili 23:42  Kisha akasema, "Ee Yesu! Unikumbuke wakati utakapoingia katika ufalme wako."
Luke Swahili 23:43  Yesu akamwambia, "Nakwambia kwa hakika, leo utakuwa pamoja nami peponi."
Luke Swahili 23:44  Ilikuwa yapata saa sita mchana; jua likaacha kuangaza, giza likafunika nchi yote mpaka saa tisa,
Luke Swahili 23:45  na pazia lililokuwa limetundikwa Hekaluni likapasuka vipande viwili.
Luke Swahili 23:46  Yesu akalia kwa sauti kubwa: "Baba, naiweka roho yangu mikononi mwako." Alipokwisha sema hayo, akakata roho.
Luke Swahili 23:47  Hapo, yule jemadari alipoona yaliyotukia akamsifu Mungu akisema: "Hakika huyu alikuwa mtu mwema."
Luke Swahili 23:48  Watu wale wote waliokuwa wamekusanyika hapo kwa ajili ya tukio hilo, walipoona hayo yaliyotukia, walirudi makwao wakijipiga vifua kwa huzuni.
Luke Swahili 23:49  Marafiki zake wote pamoja na wale wanawake walioandamana naye kutoka Galilaya, walisimama kwa mbali kutazama tukio hilo.
Luke Swahili 23:50  Kulikuwa na mtu mmoja jina lake Yosefu, mwenyeji wa kijiji kimoja cha Wayahudi kiitwacho Armathaya. Alikuwa mtu mwema anayeheshimika;
Luke Swahili 23:51  Alikuwa akitazamia kuja kwa Ufalme wa Mungu. Ingawa alikuwa mmoja wa Baraza kuu la Wayahudi, hakuwa amekubaliana nao katika kitendo chao.
Luke Swahili 23:52  Basi, yeye alikwenda kwa Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu.
Luke Swahili 23:53  Kisha, akaushusha mwili huo kutoka msalabani, akauzungushia sanda ya kitani, akauweka katika kaburi lililokuwa limechongwa kwenye mwamba, ambalo halikuwa limetumika.
Luke Swahili 23:54  Siku hiyo ilikuwa Ijumaa, na maandalio ya siku ya Sabato yalikuwa yanaanza.
Luke Swahili 23:55  Wale wanawake walioandamana na Yesu kutoka Galilaya walimfuata Yosefu, wakaliona lile kaburi na jinsi mwili wake Yesu ulivyowekwa
Luke Swahili 23:56  Halafu, walirudi nyumbani, wakatayarisha manukato na marashi kuyapaka mwili wa Yesu. Siku ya Sabato walipumzika kama ilivyoamriwa na sheria.