Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
LUKE
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 18
Luke Swahili 18:1  Basi, Yesu aliwasimulia mfano kuonyesha kwamba ni lazima kusali daima bila kukata tamaa.
Luke Swahili 18:2  Alisema: "Katika mji mmoja kulikuwa na hakimu ambaye hakuwa anamcha Mungu wala kumjali binadamu.
Luke Swahili 18:3  Katika mji huohuo, kulikuwa pia na mama mmoja mjane, ambaye alimwendea huyo hakimu mara nyingi akimwomba amtetee apate haki yake kutoka kwa adui yake.
Luke Swahili 18:4  Kwa muda mrefu huyo hakimu hakupenda kumtetea huyo mjane; lakini, mwishowe akajisemea: Ingawa mimi simchi Mungu wala simjali binadamu,
Luke Swahili 18:5  lakini kwa vile huyu mjane ananisumbua, nitamtetea; la sivyo ataendelea kufika hapa, na mwisho atanichosha kabisa!"
Luke Swahili 18:6  Basi, Bwana akaendelea kusema, "Sikieni jinsi alivyosema huyo hakimu mbaya.
Luke Swahili 18:7  Je, ndio kusema Mungu hatawatetea wale aliowachagua, ambao wanamlilia mchana na usiku? Je, atakawia kuwasikiliza?
Luke Swahili 18:8  Nawaambieni atawatetea upesi. Hata hivyo, je, kutakuwako na imani duniani wakati Mwana wa Mtu atakapokuja?"
Luke Swahili 18:9  Halafu Yesu aliwaambia pia mfano wa wale ambao walijiona kuwa wema na kuwadharau wengine.
Luke Swahili 18:10  "Watu wawili walipanda kwenda Hekaluni kusali: mmoja Mfarisayo, na mwingine mtoza ushuru.
Luke Swahili 18:11  Huyo Mfarisayo akasimama, akasali kimoyomoyo: Ee Mungu, nakushukuru kwa vile mimi si kama watu wengine: walafi, wadanganyifu au wazinzi. Nakushukuru kwamba mimi si kama huyu mtoza ushuru.
Luke Swahili 18:12  Nafunga mara mbili kwa juma, natoa zaka sehemu ya kumi ya pato langu.
Luke Swahili 18:13  Lakini yule mtoza ushuru, akiwa amesimama kwa mbali bila hata kuinua macho yake mbinguni, ila tu akijipiga kifua kwa huzuni, alisema: Ee Mungu, unionee huruma mimi mwenye dhambi.
Luke Swahili 18:14  Nawaambieni, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amesamehewa. Lakini yule mwingine, sivyo. Kwa maana kila anayejikweza atashushwa, na kila anayejishusha atakwezwa."
Luke Swahili 18:15  Watu walimletea Yesu watoto wadogo ili awawekee mikono yake. Wanafunzi walipowaona, wakawazuia kwa maneno makali.
Luke Swahili 18:16  Lakini Yesu akawaita kwake akisema: "Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni kwa ajili ya watu kama hawa.
Luke Swahili 18:17  Nawaambieni kweli, mtu yeyote asiyeupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hataingia katika Ufalme huo."
Luke Swahili 18:18  Kiongozi mmoja, Myahudi, alimwuliza Yesu, "Mwalimu mwema, nifanye nini ili niweze kuupata uzima wa milele?"
Luke Swahili 18:19  Yesu akamwambia, "Mbona waniita mwema? Hakuna aliye mwema ila Mungu peke yake.
Luke Swahili 18:20  Unazijua amri: Usizini; usiue; usiibe; usitoe ushahidi wa uongo; waheshimu baba yako na mama yako."
Luke Swahili 18:21  Yeye akasema, "Hayo yote nimeyazingatia tangu ujana wangu."
Luke Swahili 18:22  Yesu aliposikia hayo akamwambia, "Unatakiwa bado kufanya kitu kimoja: uza kila ulicho nacho, wagawie maskini, na hivyo utakuwa na hazina yako mbinguni; halafu njoo unifuate."
Luke Swahili 18:23  Lakini huyo mtu aliposikia hayo, alihuzunika sana kwa sababu alikuwa tajiri sana.
Luke Swahili 18:24  Yesu alipoona akihuzunika hivyo, akasema, "Jinsi gani ilivyo vigumu kwa matajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu!
Luke Swahili 18:25  Naam, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano, kuliko tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu."
Luke Swahili 18:26  Wale watu waliposikia hayo, wakasema, "Nani basi, atakayeokolewa?"
Luke Swahili 18:27  Yesu akajibu, "Yasiyowezekana kwa binadamu, yanawezekana kwa Mungu."
Luke Swahili 18:28  Naye Petro akamwuliza, "Na sisi je? Tumeacha vitu vyote tukakufuata!"
Luke Swahili 18:29  Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, mtu yeyote aliyeacha nyumba au mke au kaka au wazazi au watoto kwa ajili ya Ufalme wa Mungu,
Luke Swahili 18:30  atapokea mengi zaidi wakati huu wa sasa, na kupokea uzima wa milele wakati ujao."
Luke Swahili 18:31  Yesu aliwachukua kando wale kumi na wawili, akawaambia, "Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu na huko kila kitu kilichoandikwa na manabii kuhusu Mwana wa Mtu kitakamilishwa.
Luke Swahili 18:32  Kwa maana atakabidhiwa kwa watu wa mataifa nao watamtendea vibaya na kumtemea mate.
Luke Swahili 18:33  Watampiga mijeledi, watamuua; lakini siku ya tatu atafufuka."
Luke Swahili 18:34  Lakini wao hawakuelewa hata kidogo jambo hilo; walikuwa wamefichwa maana ya maneno hayo, na hawakutambua yaliyosemwa.
Luke Swahili 18:35  Wakati Yesu alipokaribia Yeriko, kulikuwa na mtu mmoja kipofu ameketi njiani akiomba.
Luke Swahili 18:36  Aliposikia umati wa watu ukipita aliuliza, "Kuna nini?"
Luke Swahili 18:38  Naye akapaza sauti akisema, "Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie!"
Luke Swahili 18:39  Wale watu waliotangulia wakamkemea wakimwambia anyamaze; lakini yeye akazidi kupaza sauti: "Mwana wa Daudi, nihurumie;"
Luke Swahili 18:40  Yesu alisimama, akaamuru wamlete mbele yake. Yule kipofu alipofika karibu, Yesu akamwuliza,
Luke Swahili 18:41  "Unataka nikufanyie nini?" Naye akamjibu, "Bwana, naomba nipate kuona tena."
Luke Swahili 18:43  Na mara yule aliyekuwa kipofu akapata kuona, akamfuata Yesu akimtukuza Mungu. Watu wote walipoona hayo, wakamsifu Mungu.