Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
LUKE
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 13
Luke Swahili 13:1  Wakati huo watu fulani walikuja, wakamweleza Yesu juu ya watu wa Galilaya ambao Pilato alikuwa amewaua wakati walipokuwa wanachinja wanyama wao wa tambiko.
Luke Swahili 13:2  Naye Yesu akawaambia, "Mnadhani Wagalilaya hao walikuwa wahalifu zaidi kuliko Wagalilaya wengine, ati kwa sababu wameteseka hivyo?
Luke Swahili 13:3  Nawaambieni hakika sivyo; lakini nanyi, hali kadhalika, msipotubu, mtaangamia kama wao.
Luke Swahili 13:4  Au wale kumi na wanane walioangukiwa na mnara kule Siloamu wakafa; mnadhani wao walikuwa wakosefu zaidi kuliko wengine wote walioishi Yerusalemu?
Luke Swahili 13:5  Nawaambieni sivyo; lakini nanyi msipotubu, mtaangamia kama wao."
Luke Swahili 13:6  Kisha, Yesu akawaambia mfano huu: "Mtu mmoja alikuwa na mtini katika shamba lake. Mtu huyu akaenda akitaka kuchuma matunda yake, lakini akaukuta haujazaa hata tunda moja.
Luke Swahili 13:7  Basi, akamwambia mfanyakazi wake: Angalia! Kwa miaka mitatu nimekuwa nikija kuchuma matunda ya mtini huu, nami nisiambulie kitu. Ukate! Kwa nini uitumie ardhi bure?
Luke Swahili 13:8  Lakini naye akamjibu: Bwana, tuuache tena mwaka huu; nitauzungushia mtaro na kuutilia mbolea.
Luke Swahili 13:9  Kama ukizaa matunda mwaka ujao, vema; la sivyo, basi utaweza kuukata."
Luke Swahili 13:10  Yesu alikuwa akifundisha katika sunagogi moja siku ya Sabato.
Luke Swahili 13:11  Na hapo palikuwa na mwanamke mmoja aliyekuwa mgonjwa kwa miaka kumi na minane kutokana na pepo aliyekuwa amempagaa. Kwa sababu hiyo, mwili wake ulikuwa umepindika vibaya hata asiweze kusimama wima.
Luke Swahili 13:12  Yesu alipomwona, alimwita, akamwambia, "Mama, umeponywa ugonjwa wako."
Luke Swahili 13:13  Akamwekea mikono, na mara mwili wake ukawa wima tena, akawa anamtukuza Mungu.
Luke Swahili 13:14  Lakini mkuu wa sunagogi alikasirika kwa sababu Yesu alikuwa amemponya siku ya Sabato. Hivyo akawaambia wale watu walikusanyika pale, "Mnazo siku sita za kufanya kazi. Basi, fikeni siku hizo mkaponywe magonjwa yenu; lakini msije siku ya Sabato."
Luke Swahili 13:15  Hapo Bwana akamjibu, "Enyi wanafiki! Nani kati yenu hangemfungua ng'ombe au punda wake kutoka zizini ampeleke kunywa maji, hata kama siku hiyo ni ya Sabato?
Luke Swahili 13:16  Sasa, hapa yupo binti wa Abrahamu ambaye Shetani alimfanya kilema kwa muda wa miaka kumi na minane. Je, haikuwa vizuri kumfungulia vifungo vyake siku ya Sabato?"
Luke Swahili 13:17  Alipokwisha sema hayo, wapinzani wake waliona aibu lakini watu wengine wote wakajaa furaha kwa sababu ya mambo yote aliyotenda.
Luke Swahili 13:18  Yesu akauliza: "Ufalme wa Mungu unafanana na nini? Nitaulinganisha na nini?
Luke Swahili 13:19  NI kama mbegu ya haradali aliyotwaa mtu mmoja na kuipanda shambani mwake; ikaota hata ikawa mti. Ndege wa angani wakajenga viota vyao katika matawi yake."
Luke Swahili 13:20  Tena akauliza: "Nitaulinganisha Ufalme wa Mungu na nini?
Luke Swahili 13:21  Ni kama chachu aliyoitwaa mama mmoja na kuichanganya pamoja na unga debe moja kisha unga wote ukaumuka wote."
Luke Swahili 13:22  Yesu alindelea na safari yake kwenda Yerusalemu huku akipitia mijini na vijijini, akihubiri.
Luke Swahili 13:23  Mtu mmoja akamwuliza, "Je, Mwalimu, watu watakaookoka ni wachache?"
Luke Swahili 13:24  Yesu akawaambia, "Jitahidini kuingia kwa kupitia mlango mwembamba; maana nawaambieni, wengi watajaribu kuingia lakini hawataweza.
Luke Swahili 13:25  "Wakati utakuja ambapo mwenye nyumba atainuka na kufunga mlango. Ninyi mtasimama nje na kuanza kupiga hodi mkisema: Bwana, tufungulie mlango. Lakini yeye atawajibu: Sijui mmetoka wapi.
Luke Swahili 13:26  Nanyi mtaanza kumwambia: Sisi ndio wale tuliokula na kunywa pamoja nawe; na wewe ulifundisha katika vijiji vyetu.
Luke Swahili 13:27  Lakini yeye atasema: Sijui ninyi mmetoka wapi; ondokeni mbele yangu, enyi nyote watenda maovu.
Luke Swahili 13:28  Ndipo mtakuwa na kulia na kusaga meno, wakati mtakapowaona Abrahamu, Isaka na Yakobo, na manabii wote wapo katika Ufalme wa Mungu, lakini ninyi wenyewe mmetupwa nje!
Luke Swahili 13:29  Watu watakuja kutoka mashariki na magharibi, kutoka kaskazini na kusini, watakuja na kukaa kwenye karamu katika Ufalme wa Mungu.
Luke Swahili 13:30  Naam, wale walio wa mwisho watakuwa wa kwanza; na wale walio wa kwanza watakuwa wa mwisho."
Luke Swahili 13:31  Wakati huohuo, Mafarisayo na watu wengine walimwendea Yesu wakamwambia, "Ondoka hapa uende mahali pengine, kwa maana Herode anataka kukuua."
Luke Swahili 13:32  Yesu akawajibu, "Nendeni mkamwambie huyo mbweha hivi: Leo na kesho ninafukuza pepo na kuponya wagonjwa, na siku ya tatu nitakamilisha kazi yangu.
Luke Swahili 13:33  Hata hivyo, kwa leo, kesho na kesho kutwa, ni lazima niendelee na safari yangu, kwa sababu si sawa nabii auawe nje ya Yerusalemu.
Luke Swahili 13:34  "Yerusalemu! We Yerusalemu! Unawaua manabii na kuwapiga mawe wale waliotumwa kwako! Mara ngapi nimetaka kuwakusanya watoto wako pamoja kama kuku anavyokusanya vifaranga vyake chini ya mabawa yake, Lakini wewe umekataa.
Luke Swahili 13:35  Haya, utaachiwa mwenyewe nyumba yako. Naam, hakika nawaambieni, hamtaniona mpaka wakati utakapofika mseme: Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana."