Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
LUKE
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 10
Luke Swahili 10:1  Baada ya hayo, Bwana aliwachagua wengine sabini na wawili, akawatuma wawiliwawili, wamtangulie katika kila kijiji na mahali ambapo yeye mwenyewe alitaka kwenda.
Luke Swahili 10:2  Akawaambia, "Mavuno ni mengi, lakini wavunaji ni wachache. Kwa hivyo, mwombeni mwenye shamba atume wavunaji shambani mwake.
Luke Swahili 10:3  Sasa nendeni; fahamuni kwamba ninawatuma ninyi kama kondoo wanaokwenda kati ya mbwa mwitu.
Luke Swahili 10:4  Msichukue mfuko wa fedha, mkoba, wala viatu; msimsalimu mtu yeyote njiani.
Luke Swahili 10:5  Mkiingia katika nyumba yoyote, kwanza wasalimuni hivi: Amani iwe katika nyumba hii!
Luke Swahili 10:6  Kama akiwako mwenye kupenda amani, amani yenu itakaa naye, la sivyo, itawarudieni.
Luke Swahili 10:7  Kaeni katika nyumba hiyo mkila na kunywa wanavyowapeni, maana mfanyakazi anastahili mshahara wake. Msiende mara nyumba hii mara nyumba ile.
Luke Swahili 10:8  Kama mkifika mji fulani na watu wakiwakaribisha, kuleni wanavyowapeni.
Luke Swahili 10:9  Ponyeni wagonjwa walioko huko, waambieni watu: Ufalme wa Mungu umekaribia kwenu.
Luke Swahili 10:10  Lakini mkiingia katika mji wowote, wasipowakaribisheni, tokeni; nanyi mpitapo katika barabara zao semeni:
Luke Swahili 10:11  Hata mavumbi ya mji wenu yaliyoshikamana na miguu yetu tunawakung'utieni. Lakini, jueni kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia.
Luke Swahili 10:12  Hakika nawaambieni, siku ile mji huo utapata adhabu kubwa zaidi kuliko ile ya watu wa Sodoma.
Luke Swahili 10:13  "Ole wako Korazini! Ole wako Bethsaida! Maana, kama miujiza iliyofanyika kwenu ingalifanyika kule Tiro na Sidoni, watu wake wangalikwishavaa mavazi ya gunia kitambo, na kukaa katika majivu kuonyesha kwamba wametubu.
Luke Swahili 10:14  Hata hivyo, Siku ya Hukumu ninyi mtapata adhabu kubwa zaidi kuliko ile ya watu wa Tiro na Sidoni.
Luke Swahili 10:15  Na wewe Kafarnaumu, unataka kujikweza mpaka mbinguni? La; utaporomoshwa mpaka Kuzimu."
Luke Swahili 10:16  Halafu akasema, "Anayewasikiliza ninyi, ananisikiliza mimi; na anayekataa kuwapokea ninyi, anakataa kunipokea mimi. Yeyote anayekataa kunipokea, anakataa kumpokea yule aliyenituma."
Luke Swahili 10:17  Baadaye, wale sabini na wawili walirudi wamejaa furaha, wakisema, "Bwana, hata pepo wametutii tulipolitaja jina lako."
Luke Swahili 10:18  Yeye akawaambia, "Nilimwona Shetani jinsi alivyokuwa anaporomoka kama umeme kutoka mbinguni.
Luke Swahili 10:19  Naam, nimewapeni uwezo wa kukanyaga nyoka na ng'e, na uwezo juu ya nguvu zote za yule adui; hakuna chochote kitakachowadhuru.
Luke Swahili 10:20  Hata hivyo, msifurahi kwa sababu pepo wamewatii, bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni."
Luke Swahili 10:21  Saa ileile, Yesu akafurahi kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, akasema, "Nakushukuru ee Baba, Bwana wa mbingu na dunia, kwa kuwa umewaficha wenye hekima na elimu mambo haya, ukawafumbulia wadogo. Naam, Baba, ndivyo ilivyokupendeza."
Luke Swahili 10:22  Kisha akasema, "Baba yangu ameweka yote mikononi mwangu. Hakuna amjuaye Mwana ni nani ila Baba, wala amjuaye Baba ni nani ila Mwana, na yeyote yule ambaye Mwana anataka kumfunulia hayo."
Luke Swahili 10:23  Halafu akawaelekea wafuasi wake akawaambia, "Heri wanaoona yale mnayoyaona ninyi!
Luke Swahili 10:24  Hakika, manabii na wafalme walitamani kuona yale mnayoyaona ninyi wasiyaone, na kusikia yale mnayoyasikia wasiyasikie."
Luke Swahili 10:25  Baadaye mwalimu mmoja wa Sheria alisimama akamwuliza akitaka kumtega, "Mwalimu, nifanye nini ili nipate uzima wa milele?"
Luke Swahili 10:26  Yesu akamwuliza, "Imeandikwa nini katika Sheria? Unaelewaje?"
Luke Swahili 10:27  Akamjibu, "Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yote. Na, mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe."
Luke Swahili 10:28  Yesu akawaambia, "Vema! Fanya hivyo, nawe utaishi."
Luke Swahili 10:29  Lakini yeye akitaka kujihakikishia kuwa mwema akamwuliza Yesu, "Na jirani yangu ni nani?"
Luke Swahili 10:30  Yesu akamjibu, "Mtu mmoja alikuwa anashuka kutoka Yerusalemu kwenda Yeriko. Alipokuwa njiani, alivamiwa na majambazi, wakamnyang'anya mali yake na kumpiga, wakamwacha amelala pale nusu mfu.
Luke Swahili 10:31  Kumbe, kuhani mmoja akawa anapita barabara ileile, akamwona, akapita kando.
Luke Swahili 10:32  Hali kadhalika na Mlawi mmoja, alipofika mahali akamwona, akapita kando.
Luke Swahili 10:33  Lakini Msamaria mmoja aliyekuwa anasafiri, alifika pale yule mtu alipokuwa, naye alipomwona, alimwonea huruma.
Luke Swahili 10:34  Akamwendea, akamtibu majeraha yake kwa kumtia mafuta na divai; na kuyafunga halafu akampandisha juu ya punda wake akampeleka katika nyumba moja ya wageni akamuuguza.
Luke Swahili 10:35  Kesho yake akatoa fedha dinari mbili akampa yule mwenye nyumba, akamwambia, Muuguze mtu huyu; na chochote utakachotumia zaidi, nitakulipa nitakaporudi."
Luke Swahili 10:36  Kisha Yesu akauliza, "Kati ya hao watatu, ni yupi aliyeonyesha kuwa jirani yake yule aliyevamiwa na majambazi?"
Luke Swahili 10:37  Yule mwalimu wa Sheria akamjibu, "Ni yule aliyemwonea huruma." Yesu akamwambia, "Nenda ukafanye vivyo hivyo."
Luke Swahili 10:38  Walipokuwa safarini, waliingia katika kijiji kimoja na mwanamke mmoja, aitwaye Martha, alimkaribisha nyumbani kwake.
Luke Swahili 10:39  Martha alikuwa na dada yake aitwaye Maria; huyu aliketi karibu na Yesu akisikiliza mafundisho yake.
Luke Swahili 10:40  Lakini Martha alikuwa anashughulika na mambo mengi. Basi, akamwendea Yesu, akamwambia, "Bwana, hivi hujali kwamba dada yangu ameniacha nishughulike peke yangu? Mwambie basi, anisaidie."
Luke Swahili 10:41  Lakini Bwana akamjibu, "Martha, Martha, unahangaika na kusumbuka kwa mambo mengi.
Luke Swahili 10:42  Kitu kimoja tu ni muhimu. Maria amechagua kitu bora zaidi ambacho hakuna mtu atakayemnyag'anya."