Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
TITUS
Up
1 2 3
Toggle notes
Chapter 1
Titu Swahili 1:1  Mimi Paulo, mtumishi wa Mungu na mtume wa Yesu Kristo naandika. Mimi nimechaguliwa kuijenga imani ya wateule wa Mungu na kuwaongoza waufahamu ukweli wa dini yetu,
Titu Swahili 1:2  ambayo msingi wake ni tumaini la kupata uzima wa milele. Mungu ambaye hasemi uongo, alituahidia uzima huo kabla ya mwanzo wa nyakati,
Titu Swahili 1:3  na wakati ufaao ulipowadia, akaudhihirisha katika ujumbe wake. Mimi nilikabidhiwa ujumbe huo nuutangaze kufuatana na amri ya Mungu, Mwokozi wetu.
Titu Swahili 1:4  Ninakuandikia wewe Tito, mwanangu wa kweli katika imani tunayoshiriki. Nakutakia neema na amani kutoka kwa Mungu Baba, na kutoka kwa Kristo Yesu, Mkombozi wetu.
Titu Swahili 1:5  Nilikuacha Krete ili urekebishe yale mambo ambayo hayakuwa yamekamilika bado, na kuwateua wazee wa kanisa katika kila mji. Kumbuka maagizo yangu:
Titu Swahili 1:6  mzee wa kanisa anapaswa kuwa mtu asiye na hatia; aliye na mke mmoja tu, na watoto wake wanapaswa kuwa waumini, wasiojulikana kuwa wakorofi au wakaidi.
Titu Swahili 1:7  Maana kwa vile kiongozi wa kanisa ni mkurugenzi wa kazi ya Mungu, anapaswa kuwa mtu asiye na hatia. Asiwe mwenye majivuno, mwepesi wa hasira, mlevi, mkorofi au mchoyo.
Titu Swahili 1:8  Anapaswa kuwa mkarimu na anayependa mambo mema. Anapaswa kuwa mtu mtaratibu, mwadilifu, mtakatifu na mwenye nidhamu.
Titu Swahili 1:9  Ni lazima ashike kikamilifu ujumbe ule wa kuaminika kama unavyofundishwa. Ndivyo atakavyoweza kuwatia wengine moyo kwa mafundisho ya kweli na kuyafichua makosa ya wale wanaoyapinga mafundisho hayo.
Titu Swahili 1:10  Maana, wako watu wengi, hasa wale walioongoka kutoka dini ya Kiyahudi, ambao ni wakaidi, wanaowapotosha wengine kwa upumbavu wao.
Titu Swahili 1:11  Lazima kukomesha maneno yao, kwani wanavuruga jumuiya nzima kwa kufundisha mambo ambayo hawapaswi kufundisha; wanafanya hivyo kwa nia mbaya ya kupata faida ya fedha.
Titu Swahili 1:12  Hata mmoja wa manabii wao, ambaye naye pia ni Mkrete, alisema: "Wakrete, husema uongo daima; ni kama wanyama wabaya, walafi na wavivu!"
Titu Swahili 1:13  Naye alitoboa ukweli kwa sababu hiyo, unapaswa kuwakaripia vikali, ili wawe na imani kamilifu.
Titu Swahili 1:14  Wasiendelee kushikilia hadithi tupu za Kiyahudi na maagizo ya kibinadamu yanayozuka kwa watu walioukataa ukweli.
Titu Swahili 1:15  Kila kitu ni safi kwa watu walio safi; lakini hakuna chochote kilicho safi kwa wale waliochafuliwa na wasioamini, maana dhamiri na akili zao zimechafuliwa.
Titu Swahili 1:16  Watu kama hao hujidai kwamba wanamjua Mungu, lakini kwa matendo yao humkana. Ni watu wa kuchukiza mno na wakaidi, hawafai kwa jambo lolote jema.
Chapter 2
Titu Swahili 2:2  Waambie wazee kwamba wanapaswa kuwa na kiasi, wawe na busara na wataratibu; wanapaswa kuwa timamu katika imani yao, upendo na uvumilivu.
Titu Swahili 2:3  Hali kadhalika waambie wanawake wazee wawe na mwenendo wa uchaji wa Mungu; wasiwe wachongezi, au watumwa wa pombe. Wanapaswa kufundisha mambo mema,
Titu Swahili 2:4  ili wawazoeze kina mama vijana kuwapenda waume zao na watoto,
Titu Swahili 2:5  wawe na kiasi na safi, waangalie vizuri mambo ya nyumbani, na wawatii waume zao, ili ujumbe wa Mungu usije ukadharauliwa.
Titu Swahili 2:7  Katika mambo yote wewe mwenyewe unapaswa kuwa mfano wa matendo mema. Uwe mnyofu na uwe na uzito katika mafundisho yako.
Titu Swahili 2:8  Maneno yako yasiwe na hitilafu yoyote ili adui zako waaibike wasipopata chochote kibaya cha kusema juu yetu.
Titu Swahili 2:9  Watumwa wanapaswa kuwatii wakuu wao na kuwapendeza katika mambo yote. Wasibishane nao,
Titu Swahili 2:10  au kuiba vitu vyao. Badala yake wanapaswa kuonyesha kwamba wao ni wema na waaminifu daima, ili, kwa matendo yao yote, wayapatie sifa njema mafundisho juu ya Mungu, Mwokozi wetu.
Titu Swahili 2:11  Maana neema ya Mungu imedhihirishwa kwa ajili ya wokovu wa watu wote.
Titu Swahili 2:12  Neema hiyo yatufunza kuachana na uovu wote na tamaa za kidunia; tuwe na kiasi, tuishi maisha adili na ya kumcha Mungu katika ulimwengu huu wa sasa,
Titu Swahili 2:13  tukiwa tunangojea siku ile ya heri tunayoitumainia, wakati utakapotokea utukufu wa Mungu Mkuu na Mwokozi wetu Yesu Kristo.
Titu Swahili 2:14  Yeye alijitoa mwenyewe kwa ajili yetu ili atukomboe kutoka katika uovu wote na kutufanya watu safi walio wake yeye mwenyewe, watu walio na hamu ya kutenda mema.
Titu Swahili 2:15  Basi, fundisha mambo hayo na tumia mamlaka yako yote ukiwahimiza na kuwaonya wasikilizaji wako. Mtu yeyote na asikudharau.
Chapter 3
Titu Swahili 3:1  Wakumbushe watu kuwastahi watawala na wenye mamlaka, kuwatii na kuwa tayari kwa kila namna kutenda mambo yote mema.
Titu Swahili 3:2  Waambie wasimtukane mtu yeyote; bali waishi kwa amani na masikizano, wawe daima wapole kwa kila mtu.
Titu Swahili 3:3  Maana, wakati mmoja sisi tulikuwa wapumbavu, wakaidi na wapotovu. Tulikuwa watumwa wa tamaa na anasa za kila aina. Tuliishi maisha ya uovu na wivu; watu walituchukia nasi tukawachukia.
Titu Swahili 3:4  Lakini wakati wema na upendo wa Mungu, Mwokozi wetu, ulipofunuliwa,
Titu Swahili 3:5  alituokoa. alituokoa si kwa sababu ya jambo lolote jema tulilotenda sisi, bali alituokoa kwa sababu ya huruma yake, kwa njia ya Roho Mtakatifu anayetujalia tuzaliwe upya na kuwa na maisha mapya kwa kutuosha kwa maji.
Titu Swahili 3:6  Mungu alitumiminia Roho Mtakatifu bila kipimo kwa njia ya Yesu Kristo, Mwokozi wetu,
Titu Swahili 3:7  ili kwa neema yake tupate kukubaliwa kuwa waadilifu na kuupokea uzima wa milele tunaoutumainia.
Titu Swahili 3:8  Jambo hili ni kweli. Ninakutaka uyatilie mkazo mambo haya, ili wale wanaomwamini Mungu, wawe na hamu ya kuutumia wakati wao katika kutenda mema, ambayo ni mambo mazuri na ya manufaa kwa watu.
Titu Swahili 3:9  Lakini jiepushe na ubishi wa kipumbavu, ugomvi na mabishano juu ya Sheria. Mambo hayo hayana faida yoyote na ni ya bure tu.
Titu Swahili 3:10  Mtu anayesababisha mafarakano mpe onyo la kwanza na la pili, kisha achana naye.
Titu Swahili 3:11  Wajua kwamba mtu wa namna hiyo amepotoka kabisa, na dhambi zake zathibitisha kwamba amekosea.
Titu Swahili 3:12  Baada ya kumtuma kwako Artema au Tukiko, fanya bidii kuja Nikopoli unione, maana nimeamua kukaa huko wakati wa majira ya baridi.
Titu Swahili 3:13  Jitahidi kumsaidia mwana sheria Zena na Apolo ili waweze kuanza ziara zao na uhakikishe kwamba wana kila kitu wanachohitaji.
Titu Swahili 3:14  Ni lazima watu wetu wajifunze kuutumia wakati wao katika kutenda mema ili wasaidie katika mahitaji ya kweli, na maisha yao yawe ya kufaa.
Titu Swahili 3:15  Watu wote walio pamoja nami wanakusalimu. Wasalimu rafiki zetu katika imani. Nawatakieni nyote neema ya Mungu.