Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
JOHN
1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 12
John Swahili 12:1  Siku sita kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu alifika Bethania alikoishi Lazaro ambaye Yesu alikuwa amemfufua kutoka wafu.
John Swahili 12:2  Huko walimwandalia chakula cha jioni, naye Martha akawa anawatumikia. Lazaro alikuwa mmoja wa wale waliokuwa mezani pamoja na Yesu.
John Swahili 12:3  Basi, Maria alichukua chupa ya marashi ya nardo safi ya thamani kubwa, akampaka Yesu miguu na kuipangusa kwa nywele zake. Nyumba yote ikajaa harufu ya marashi.
John Swahili 12:4  Basi, Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili ambaye ndiye atakayemsaliti Yesu, akasema,
John Swahili 12:5  "Kwa nini marashi hayo hayakuuzwa kwa fedha dinari mia tatu, wakapewa maskini?"
John Swahili 12:6  Alisema hivyo, si kwa kuwa alijali chochote juu ya maskini, bali kwa sababu alikuwa mweka hazina, na kwa kuwa alikuwa mwizi, mara kwa mara aliiba kutoka katika hiyo hazina.
John Swahili 12:7  Lakini Yesu akasema, "Msimsumbue huyu mama! Mwacheni ayaweke kwa ajili ya siku ya mazishi yangu.
John Swahili 12:8  Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini hamtakuwa nami siku zote."
John Swahili 12:9  Wayahudi wengi walisikia kwamba Yesu alikuwa Bethania. Basi, wakafika huko si tu kwa ajili ya kumwona Yesu, ila pia wapate kumwona Lazaro ambaye Yesu alimfufua kutoka wafu.
John Swahili 12:11  Maana kwa sababu ya Lazaro Wayahudi wengi waliwaasi viongozi wao, wakamwamini Yesu.
John Swahili 12:12  Kesho yake, kundi kubwa la watu waliokuja kwenye sikukuu walisikia kuwa Yesu alikuwa njiani kuja Yerusalemu.
John Swahili 12:13  Basi, wakachukua matawi ya mitende, wakatoka kwenda kumlaki; wakapaaza sauti wakisema: "Hosana! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana. Abarikiwe mfalme wa Israeli."
John Swahili 12:14  Yesu akampata mwana punda mmoja akapanda juu yake kama yasemavyo Maandiko:
John Swahili 12:15  "Usiogope mji wa Sioni! Tazama, Mfalme wako anakuja, Amepanda mwana punda."
John Swahili 12:16  Wakati huo wanafunzi wake hawakuelewa mambo hayo, lakini Yesu alipokwisha tukuzwa, ndipo walipokumbuka kwamba hayo yalikuwa yameandikwa juu yake, na kwamba watu walikuwa wamemtendea hivyo.
John Swahili 12:17  Kundi la watu wale waliokuwa pamoja naye wakati alipomwita Lazaro kutoka kaburini, akamfufua kutoka wafu, walisema yaliyotukia.
John Swahili 12:18  Kwa hiyo umati huo wa watu ulimlaki, maana wote walisikia kwamba Yesu alikuwa amefanya ishara hiyo.
John Swahili 12:19  Basi, Mafarisayo wakaambiana, "Mnaona? Hatuwezi kufanya chochote! Tazameni, ulimwengu wote unamfuata."
John Swahili 12:20  Kulikuwa na Wagiriki kadhaa miongoni mwa watu waliokuwa wamefika Yerusalemu kuabudu wakati wa sikukuu hiyo.
John Swahili 12:21  Hao walimwendea Filipo, mwenyeji wa Bethsaida katika Galilaya, wakasema, "Mheshimiwa, tunataka kumwona Yesu."
John Swahili 12:22  Filipo akaenda akamwambia Andrea, nao wawili wakaenda kumwambia Yesu.
John Swahili 12:23  Yesu akawaambia, "Saa ya kutukuzwa kwa Mwana wa Mtu imefika!
John Swahili 12:24  Kweli nawaambieni, punje ya ngano hubaki punje tu isipokuwa ikianguka katika udongo na kufa. Kama ikifa, basi huzaa matunda mengi.
John Swahili 12:25  Anayependa maisha yake, atayapoteza; anayeyachukia maisha yake katika ulimwengu huu, atayaweka kwa ajili ya uzima wa milele.
John Swahili 12:26  Anayetaka kunitumikia ni lazima anifuate, hivyo kwamba popote pale nilipo mimi ndipo na mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu yeyote anayenitumikia Baba yangu atampa heshima.
John Swahili 12:27  "Sasa roho yangu imefadhaika, na niseme nini? Je, niseme: Baba, usiruhusu saa hii inifikie? Lakini ndiyo maana nimekuja--ili nipite katika saa hii.
John Swahili 12:28  Baba, ulitukuze jina lako." Hapo sauti ikasema kutoka mbinguni, "Nimelitukuza, na nitalitukuza tena."
John Swahili 12:29  Umati wa watu waliokuwa wamesimama hapo walisikia sauti hiyo, na baadhi yao walisema, "Malaika ameongea naye!"
John Swahili 12:30  Lakini Yesu akawaambia, "Sauti hiyo haikutokea kwa ajili yangu mimi, ila kwa ajili yenu.
John Swahili 12:31  Sasa ndio wakati wa ulimwengu huu kuhukumiwa; sasa mtawala wa ulimwengu huu atapinduliwa.
John Swahili 12:32  Nami nitakapoinuliwa juu ya nchi nitamvuta kila mmoja kwangu."
John Swahili 12:34  Basi, umati huo ukamjibu, "Sisi tunaambiwa na Sheria yetu kwamba Kristo atadumu milele. Wawezaje basi, kusema ati Mwana wa Mtu anapaswa kuinuliwa? Huyo Mwana wa Mtu ni nani?"
John Swahili 12:35  Yesu akawaambia, "Mwanga bado uko nanyi kwa muda mfupi. Tembeeni mngali mnao huo mwanga ili giza lisiwapate; maana atembeaye gizani hajui aendako.
John Swahili 12:36  Basi, wakati mnao huo mwanga uaminini ili mpate kuwa watu wa mwanga." Baada ya kusema maneno hayo, Yesu alikwenda zake na kujificha mbali nao.
John Swahili 12:37  Ingawa Yesu alifanya miujiza hii yote mbele yao, wao hawakumwamini.
John Swahili 12:38  Hivyo maneno aliyosema nabii Isaya yakatimia: "Bwana, nani aliyeuamini ujumbe wetu? Na uwezo wa Bwana umedhihirishwa kwa nani?"
John Swahili 12:39  Hivyo hawakuweza kuamini, kwani Isaya tena alisema:
John Swahili 12:40  "Mungu ameyapofusha macho yao, amezipumbaza akili zao; wasione kwa macho yao, wasielewe kwa akili zao; wala wasinigeukie, asema Bwana, ili nipate kuwaponya."
John Swahili 12:41  Isaya alisema maneno haya kwa sababu aliuona utukufu wa Yesu, akasema habari zake.
John Swahili 12:42  Hata hivyo, wengi wa viongozi wa Wayahudi walimwamini Yesu. Lakini kwa sababu ya Mafarisayo, hawakumkiri hadharani kwa kuogopa kwamba watatengwa na sunagogi.
John Swahili 12:43  Walipendelea kusifiwa na watu kuliko kusifiwa na Mungu
John Swahili 12:44  Kisha Yesu akasema kwa sauti kubwa, "Mtu aliyeniamini, haniamini mimi tu, ila anamwamini pia yule aliyenituma.
John Swahili 12:46  Mimi ni mwanga, nami nimekuja ulimwenguni ili wote wanaoniamini wasibaki gizani.
John Swahili 12:47  Anayeyasikia maneno yangu lakini hayashiki mimi sitamhukumu; maana sikuja kuhukumu ulimwengu bali kuuokoa.
John Swahili 12:48  Asiyeyashika maneno yangu anaye wa kumhukumu: neno lile nililosema ni hakimu wake siku ya mwisho.
John Swahili 12:49  Mimi sikunena kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila Baba aliyenituma ndiye aliyeniamuru niseme nini na niongee nini.
John Swahili 12:50  Nami najua kuwa amri yake huleta uzima wa milele. Basi, mimi nasema tu yale Baba aliyoniagiza niyaseme."