Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
MATTHEW
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 13
Matt Swahili 13:1  Siku hiyohiyo, Yesu alitoka katika ile nyumba, akaenda na kuketi kando ya ziwa.
Matt Swahili 13:2  Makundi makubwa ya watu yalimzunguka hata Yesu akapanda mashua, akaketi. Hao watu walisimama kwenye ukingo wa ziwa,
Matt Swahili 13:3  naye Yesu akawaambia mambo mengi kwa mifano. "Sikilizeni! Mpanzi alikwenda kupanda mbegu.
Matt Swahili 13:4  Alipokuwa akipanda, nyingine zilianguka njiani, ndege wakaja wakazila.
Matt Swahili 13:5  Nyingine zilianguka penye mawe pasipokuwa na udongo mwingi. Zikaota mara kwa kuwa udongo haukuwa na kina.
Matt Swahili 13:6  Jua lilipochomoza, zilichomeka; na kwa kuwa mizizi yake haikuwa na nguvu, zikanyauka.
Matt Swahili 13:7  Nyingine zilianguka kwenye miti ya miiba, nayo ikakua na kuzisonga.
Matt Swahili 13:8  Lakini nyingine zilianguka penye udongo mzuri, zikaota, zikazaa: nyingine punje mia moja, nyingine sitini na nyingine thelathini.
Matt Swahili 13:10  Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwuliza, "Kwa nini unasema na watu kwa mifano?"
Matt Swahili 13:11  Yesu akawajibu, "Ninyi mmejaliwa kuzijua siri za Ufalme wa mbinguni, lakini wao hawakujaliwa.
Matt Swahili 13:12  Maana, aliye na kitu atapewa na kuzidishiwa; lakini yule asiye na kitu, hata kile alicho nacho kitachukuliwa.
Matt Swahili 13:13  Ndiyo maana ninasema nao kwa mifano, kwa sababu wanatazama lakini hawaoni, wanasikiliza lakini hawasikii, wala hawaelewi.
Matt Swahili 13:14  Kwao yametimia yale aliyosema nabii Isaya: Kusikia mtasikia, lakini hamtaelewa; Kutazama mtatazama, lakini hamtaona.
Matt Swahili 13:15  Maana akili za watu hawa zimepumbaa, wameyaziba masikio yao, wameyafumba macho yao. La sivyo, wangeona kwa macho yao. wangesikia kwa masikio yao, wangeelewa kwa akili zao, na kunigeukia, asema Bwana, nami ningewaponya.
Matt Swahili 13:16  "Lakini heri yenu ninyi, maana macho yenu yanaona na masikio yenu yanasikia.
Matt Swahili 13:17  Kweli nawaambieni, manabii na watu wengi wema walitamani kuyaona yale mnayoyaona, wasiyaone, na kuyasikia yale mnayoyasikia, wasiyasikie.
Matt Swahili 13:18  "Basi, ninyi sikilizeni maana ya mfano huo wa mpanzi.
Matt Swahili 13:19  Yeyote asikiaye ujumbe wa ufalme bila kuuelewa, ni kama zile mbegu zilizoanguka njiani; yule Mwovu huja na kunyakua kile kilichopandwa moyoni mwake.
Matt Swahili 13:20  Ile mbegu iliyopandwa penye mawe ni mfano wa mtu asikiaye ujumbe huo na mara akaupokea kwa furaha.
Matt Swahili 13:21  Lakini haumwingii na kuwa na mizizi ndani yake; huendelea kuuzingatia ujumbe huo kwa kitambo tu, na wakati taabu au udhalimu vinapotokea kwa sababu ya ujumbe huo, anakata tamaa mara.
Matt Swahili 13:22  Ile mbegu iliyoanguka kati ya miti ya miiba, ni mfano wa mtu asikiaye huo ujumbe, lakini wasiwasi wa ulimwengu huu na anasa za mali huusonga ujumbe huo, naye hazai matunda.
Matt Swahili 13:23  Ile mbegu iliyopandwa katika udongo mzuri ni mfano wa mtu ausikiaye ujumbe huo na kuuelewa, naye huzaa matunda; mmoja mia, mwingine sitini na mwingine thelathini."
Matt Swahili 13:24  Yesu akawaambia watu mfano mwingine: "Ufalme wa mbinguni unafanana na mtu aliyepanda mbegu nzuri katika shamba lake.
Matt Swahili 13:25  Lakini watu wakiwa wamelala, adui yake akaja akapanda magugu kati ya ngano, akaenda zake.
Matt Swahili 13:26  Basi, mimea ilipoota na kuanza kuchanua, magugu pia yakaanza kuonekana.
Matt Swahili 13:27  Watumishi wa yule mwenye shamba wakamwendea, wakamwambia, Mheshimiwa, bila shaka ulipanda mbegu nzuri katika shamba lako. Sasa magugu yametoka wapi?
Matt Swahili 13:28  Yeye akawajibu, Adui ndiye aliyefanya hivyo. Basi, watumishi wake wakamwuliza, Je, unataka twende tukayang'oe
Matt Swahili 13:29  Naye akawajibu, La, msije labda mnapokusanya magugu, mkang'oa na ngano pia.
Matt Swahili 13:30  Acheni vikue pamoja mpaka wakati wa mavuno. Wakati huo nitawaambia wavunaji: kusanyeni kwanza magugu mkayafunge mafungumafungu ya kuchomwa. Lakini ngano ikusanyeni mkaiweke ghalani mwangu."
Matt Swahili 13:31  Yesu akawaambia watu mfano mwingine: "Ufalme wa mbinguni unafanana na mbegu ya haradali aliyotwaa mtu mmoja, akaipanda katika shamba lake.
Matt Swahili 13:32  Yenyewe ni ndogo kuliko mbegu zote, lakini ikishaota huwa kubwa kuliko mimea yote. Hukua ikawa mti, na ndege wa angani huja na kujenga viota katika matawi yake."
Matt Swahili 13:33  Yesu akawaambia mfano mwingine: "Ufalme wa mbinguni umefanana na chachu aliyotwaa mama mmoja, akaichanganya na unga pishi tatu, hata unga wote ukaumuka."
Matt Swahili 13:34  Yesu aliwaambia watu hayo yote kwa mifano. Hakuwaambia chochote bila kutumia mifano,
Matt Swahili 13:35  ili jambo lililonenwa na nabii litimie: "Nitasema kwa mifano; nitawaambia mambo yaliyofichika tangu kuumbwa ulimwengu."
Matt Swahili 13:36  Kisha Yesu aliwaaga wale watu, akaingia nyumbani. Wanafunzi wake wakamwendea, wakamwambia, "Tufafanulie ule mfano wa magugu shambani."
Matt Swahili 13:37  Yesu akawaambia, "Mpanzi wa zile mbegu nzuri ni Mwana wa Mtu.
Matt Swahili 13:38  Lile shamba ni ulimwengu. Zile mbegu nzuri ni watu wale ambao Ufalme ni wao. Lakini yale magugu ni wale watu wa yule Mwovu.
Matt Swahili 13:39  Adui aliyepanda yale magugu ni Ibilisi. Mavuno ni mwisho wa nyakati na wavunaji ni malaika.
Matt Swahili 13:40  Kama vile magugu yanavyokusanywa kuchomwa moto, ndivyo itakavyokuwa mwishoni mwa nyakati;
Matt Swahili 13:41  Mwana wa Mtu atawatuma malaika wake wawakusanye kutoka katika Ufalme wake wale wote wenye kusababisha dhambi, na wote wenye kutenda maovu,
Matt Swahili 13:42  na kuwatupa katika tanuru ya moto, na huko watalia na kusaga meno.
Matt Swahili 13:43  Kisha, wale wema watang'ara kama jua katika Ufalme wa Baba yao. Sikieni basi, kama mna masikio!
Matt Swahili 13:44  "Ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyofichika shambani. Mtu mmoja aliigundua, akaificha tena. Alifurahi sana hata akaenda kuuza yote aliyokuwa nayo, akalinunua shamba lile.
Matt Swahili 13:45  "Tena, Ufalme wa mbinguni umefanana na mfanyabiashara mmoja mwenye kutafuta lulu nzuri.
Matt Swahili 13:46  Alipopata lulu moja ya thamani kubwa, alienda akauza yote aliyokuwa nayo, akainunua lulu ile.
Matt Swahili 13:47  "Tena, Ufalme wa mbinguni unafanana na wavu uliotupwa baharini, ukanasa samaki wa kila aina.
Matt Swahili 13:48  Ulipojaa, watu waliuvuta pwani, wakaketi, wakachagua samaki wazuri wakawaweka ndani ya vikapu vyao, na wabaya wakawatupa.
Matt Swahili 13:49  Ndivyo itakavyokuwa mwishoni mwa nyakati: malaika watatokea, watawatenganisha watu wabaya na watu wema,
Matt Swahili 13:50  na kuwatupa hao wabaya katika tanuru ya moto. Huko watalia na kusaga meno."
Matt Swahili 13:51  Yesu akawauliza, "Je, mmeelewa mambo haya yote?" Wakamjibu, "Naam."
Matt Swahili 13:52  Naye akawaambia, "Hivyo basi, kila mwalimu wa Sheria aliye mwanafunzi wa Ufalme wa mbinguni anafanana na mwenye nyumba atoaye katika hazina yake vitu vipya na vya kale."
Matt Swahili 13:53  Yesu alipomaliza kusema mifano hiyo alitoka mahali hapo,
Matt Swahili 13:54  akaenda kijijini kwake. Huko akawa anawafundisha watu katika sunagogi hata wakashangaa, wakasema, "Huyu amepata wapi hekima hii na maajabu?
Matt Swahili 13:55  Je, huyu si yule mwana wa seremala? Je, mama yake si anaitwa Maria, na ndugu zake si kina Yakobo, Yosefu, Simoni na Yuda?
Matt Swahili 13:56  Na dada zake je, si wote wako hapa pamoja nasi? Basi amepata wapi haya yote?"
Matt Swahili 13:57  Basi, wakawa na mashaka naye. Lakini Yesu akawaambia, "Nabii hakosi kuheshimiwa, isipokuwa katika nchi yake na nyumbani mwake!"
Matt Swahili 13:58  Kwa hiyo, hakutenda miujiza mingi pale kwa sababu ya kutoamini kwao.