Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
LUKE
Prev Up Next Toggle notes
Chapter 2
Luke Swahili 2:1  Siku zile, tangazo rasmi lilitolewa na Kaisari Augusto kuwataka watu wote chini ya utawala wake wajiandikishe.
Luke Swahili 2:2  Kuandikishwa huku kulikuwa mara ya kwanza, wakati Kirenio alipokuwa mkuu wa mkoa wa Siria.
Luke Swahili 2:3  Basi, wote waliohusika walikwenda kujiandikisha, kila mtu katika mji wake.
Luke Swahili 2:4  Yosefu pia alifanya safari kutoka mjini Nazareti mkoani Galilaya. Kwa kuwa alikuwa wa jamaa na ukoo wa Daudi alikwenda mjini Bethlehemu mkoani Yuda alikozaliwa Mfalme Daudi.
Luke Swahili 2:5  Alikwenda kujiandikisha pamoja na mchumba wake Maria ambaye alikuwa mja mzito.
Luke Swahili 2:6  Walipokuwa huko, siku yake ya kujifungua ikawadia,
Luke Swahili 2:7  akajifungua mtoto wake wa kwanza wa kiume, akamvika nguo za kitoto, akamlaza horini kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni.
Luke Swahili 2:8  Katika sehemu hizo, walikuwako wachungaji wakikesha usiku mbugani kulinda mifugo yao.
Luke Swahili 2:9  Malaika wa Bwana akawatokea ghafla, na utukufu wa Bwana ukawaangazia pande zote. Wakaogopa sana.
Luke Swahili 2:10  Malaika akawaambia, "Msiogope! Nimewaleteeni habari njema ya furaha kuu kwa watu wote.
Luke Swahili 2:11  Kwa maana, leo hii katika mji wa Daudi, amezaliwa Mwokozi kwa ajili yenu, ndiye Kristo Bwana.
Luke Swahili 2:12  Na hiki kitakuwa kitambulisho kwenu: mtamkuta mtoto mchanga amevikwa nguo za kitoto, amelazwa horini."
Luke Swahili 2:13  Mara kundi kubwa la jeshi la mbinguni likajiunga na huyo malaika, wakamsifu Mungu wakisema:
Luke Swahili 2:14  "Utukufu kwa Mungu juu mbinguni, na amani duniani kwa watu aliopendezwa nao!"
Luke Swahili 2:15  Baada ya hao malaika kuondoka na kurudi mbinguni, wachungaji wakaambiana: "Twendeni moja kwa moja mpaka Bethlehemu tukalione tukio hili Bwana alilotujulisha."
Luke Swahili 2:16  Basi, wakaenda mbio, wakamkuta Maria na Yosefu na yule mtoto mchanga amelazwa horini.
Luke Swahili 2:17  Hao wachungaji walipomwona mtoto huyo wakawajulisha wote habari waliyokuwa wamesikia juu yake.
Luke Swahili 2:18  Wote waliosikia hayo walishangaa juu ya habari walizoambiwa na wachungaji.
Luke Swahili 2:19  Lakini Maria aliyaweka na kuyatafakari mambo hayo yote moyoni mwake.
Luke Swahili 2:20  Wale wachungaji walirudi makwao huku wakimtukuza na kumsifu Mungu kwa yote waliyokuwa wamesikia na kuona; yote yalikuwa kama walivyokuwa wameambiwa.
Luke Swahili 2:21  Siku nane baadaye, wakati wa kumtahiri mtoto ulipofika, walimpa jina Yesu, jina ambalo alikuwa amepewa na malaika kabla hajachukuliwa mimba.
Luke Swahili 2:22  Siku zilipotimia za Yosefu na Maria kutakaswa kama walivyotakiwa na Sheria ya Mose, wazazi hao walimchukua mtoto, wakaenda naye Yerusalemu ili wamweke mbele ya Bwana.
Luke Swahili 2:23  Katika Sheria ya Bwana imeandikwa: "Kila mzaliwa wa kwanza wa kiume atawekwa wakfu kwa Bwana."
Luke Swahili 2:24  Pia walikwenda ili watoe sadaka: hua wawili au makinda wawili ya njiwa, kama ilivyotakiwa katika Sheria ya Bwana.
Luke Swahili 2:25  Wakati huo huko Yerusalemu kulikuwa na mtu mmoja, mwema na mcha Mungu, jina lake Simeoni. Yeye alikuwa akitazamia kwa hamu ukombozi wa Israeli. Roho Mtakatifu alikuwa pamoja naye.
Luke Swahili 2:26  Roho Mtakatifu alikuwa amemhakikishia kwamba hatakufa kabla ya kumwona Masiha wa Bwana.
Luke Swahili 2:27  Basi, akiongozwa na Roho Mtakatifu, Simeoni aliingia Hekaluni; na wazazi wa Yesu walipomleta Hekaluni mtoto wao ili wamfanyie kama ilivyotakiwa na Sheria,
Luke Swahili 2:28  Simeoni alimpokea mtoto Yesu mikononi mwake huku akimtukuza Mungu na kusema:
Luke Swahili 2:29  "Sasa Bwana, umetimiza ahadi yako, waweza kumruhusu mtumishi wako aende kwa amani.
Luke Swahili 2:30  Maana kwa macho yangu nimeuona wokovu utokao kwako,
Luke Swahili 2:32  Mwanga utakaowaangazia watu wa mataifa, na utukufu kwa watu wako Israeli."
Luke Swahili 2:33  Baba na mama yake Yesu walikuwa wakistaajabia maneno aliyosema Simeoni juu ya mtoto.
Luke Swahili 2:34  Simeoni akawabariki, akamwambia Maria mama yake, "Mtoto huyu atakuwa sababu ya kupotea na kuokoka kwa watu wengi katika Israeli. Naye atakuwa ishara itakayopingwa na watu;
Luke Swahili 2:35  na hivyo mawazo ya watu wengi yataonekana wazi. Nawe mwenyewe, uchungu ulio kama upanga mkali utauchoma moyo wako."
Luke Swahili 2:36  Palikuwa na nabii mmoja mwanamke, mzee sana, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila la Asheri. Alikuwa ameishi na mumewe kwa miaka saba tangu alipoolewa.
Luke Swahili 2:37  Halafu alibaki mjane hadi wakati huo akiwa mzee wa miaka themanini na minne. Wakati huo wote alikaa Hekaluni akifunga na kusali usiku na mchana.
Luke Swahili 2:38  Saa hiyohiyo alijitokeza mbele, akamshukuru Mungu, na akaeleza habari za huyo mtoto kwa watu wote waliokuwa wanatazamia ukombozi wa Yerusalemu.
Luke Swahili 2:39  Hao wazazi walipokwisha fanya yote yaliyoamriwa na Sheria ya Bwana, walirudi makwao Nazareti, mkoani Galilaya.
Luke Swahili 2:40  Mtoto akakua, akazidi kupata nguvu, akajaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa pamoja naye.
Luke Swahili 2:41  Wazazi wa Yesu walikuwa na desturi ya kwenda Yerusalemu kila mwaka wakati wa sikukuu ya Pasaka.
Luke Swahili 2:42  Mtoto alipokuwa na umri wa miaka kumi na miwili, wote walikwenda kwenye sikukuu hiyo kama ilivyokuwa desturi.
Luke Swahili 2:43  Baada ya sikukuu, walianza safari ya kurudi makwao, lakini Yesu alibaki Yerusalemu bila wazazi wake kuwa na habari.
Luke Swahili 2:44  Walidhani alikuwa pamoja na kundi la wasafiri, wakaenda mwendo wa kutwa, halafu wakaanza kumtafuta miongoni mwa jamaa na marafiki.
Luke Swahili 2:45  Kwa kuwa hawakumwona, walirudi Yerusalemu wakimtafuta.
Luke Swahili 2:46  Siku ya tatu walimkuta Hekaluni kati ya walimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali.
Luke Swahili 2:47  Wote waliosikia maneno yake walistaajabia akili yake na majibu yake ya hekima.
Luke Swahili 2:48  Wazazi wake walipomwona walishangaa. Maria, mama yake, akamwuliza, "Mwanangu, kwa nini umetutenda hivyo? Baba yako na mimi tumekuwa tukikutafuta kwa huzuni."
Luke Swahili 2:49  Yeye akawajibu, "Kwa nini mlinitafuta? Hamkujua kwamba inanipasa kuwa katika nyumba ya Baba yangu?"
Luke Swahili 2:50  Lakini wazazi wake hawakuelewa maana ya maneno aliyowaambia.
Luke Swahili 2:51  Basi, akarudi pamoja nao hadi Nazareti, akawa anawatii. Mama yake akaweka mambo hayo yote moyoni mwake.
Luke Swahili 2:52  Naye Yesu akaendelea kukua katika hekima na kimo; akazidi kupendwa na Mungu na watu.