Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
COLOSSIANS
Up
1 2 3 4
Toggle notes
Chapter 1
Colo Swahili 1:1  Mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na ndugu Timotheo,
Colo Swahili 1:2  tunawaandikia ninyi watu wa Mungu huko Kolosai, ndugu zetu waaminifu katika kuungana na Kristo. Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu.
Colo Swahili 1:3  Daima tunamshukuru Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, wakati tunapowaombea.
Colo Swahili 1:4  Maana tumesikia juu ya imani yenu katika Kristo Yesu na juu ya upendo wenu kwa watu wote wa Mungu.
Colo Swahili 1:5  Wakati ujumbe ule wa kweli, yaani Habari Njema, ilipowafikieni kwa mara ya kwanza, mlipata kusikia juu ya lile tumaini linalopatikana kwake. Kwa sababu hiyo imani na upendo wenu vinategemea jambo lile mnalotumainia ambalo mmewekewa salama mbinguni.
Colo Swahili 1:6  Habari Njema inazidi kuzaa matunda na kuenea ulimwenguni kote kama vile ilivyofanya kwenu ninyi tangu siku ile mliposikia juu ya neema ya Mungu na kuitambua ilivyo kweli.
Colo Swahili 1:7  Mlijifunza juu ya neema ya Mungu kutoka kwa Epafra, mtumishi mwenzetu, ambaye ni mfanyakazi mwaminifu wa Kristo kwa niaba yetu.
Colo Swahili 1:8  Yeye alitupa habari za upendo wenu mliojaliwa na Roho.
Colo Swahili 1:9  Kwa sababu hiyo tumekuwa tukiwaombeeni daima tangu tulipopata habari zenu. Tunamwomba Mungu awajazeni ujuzi kamili wa mapenzi yake, awajazeni hekima yote na elimu iletwayo na Roho wake.
Colo Swahili 1:10  Hapo mtaweza kuishi kama anavyotaka Bwana na kutenda daima yanayompendeza. Maisha yenu yatakuwa yenye matunda ya kila namna ya matendo mema na mtazidi kukua katika kumjua Mungu.
Colo Swahili 1:11  Mungu awajalieni nguvu kwa uwezo wake mtukufu ili mweze kustahimili kila kitu kwa uvumilivu.
Colo Swahili 1:12  Na kwa furaha, mshukuruni Baba aliyewawezesha ninyi kuwa na sehemu yenu katika mambo yale Mungu aliyowawekea watu wake katika utawala wa mwanga.
Colo Swahili 1:13  Yeye alituokoa katika nguvu ya giza, akatuleta salama katika ufalme wa Mwanae mpenzi,
Colo Swahili 1:14  ambaye kwa njia yake tunakombolewa, yaani dhambi zetu zinaondolewa.
Colo Swahili 1:15  Kristo ni mfano wa Mungu asiyeonekana; ni mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote.
Colo Swahili 1:16  Maana kwa njia yake vitu vyote viliumbwa duniani na mbinguni, vitu vinavyoonekana na visivyoonekana: wenye enzi, watawala, wakuu na wenye mamlaka. Vyote viliumbwa kwa njia yake na kwa ajili yake.
Colo Swahili 1:17  Kristo alikuwako kabla ya vitu vyote; kwa kuungana naye, vyote vyadumu mahali pake.
Colo Swahili 1:18  Yeye ni kichwa cha mwili wake, yaani kanisa; yeye ni chanzo cha uhai wa huo mwili. Yeye ndiye mwanzo, mzaliwa wa kwanza aliyefufuliwa kutoka wafu, ili awe na nafasi ya kwanza katika vitu vyote.
Colo Swahili 1:19  Maana Mungu alipenda utimilifu wote uwe ndani yake.
Colo Swahili 1:20  Kwa njia yake Mungu alivipatanisha naye vitu vyote naam, viumbe vyote mbinguni na duniania; alileta amani kwa damu ya Kristo msalabani.
Colo Swahili 1:21  Hapo kwanza ninyi pia mlikuwa mbali na Mungu na mlikuwa adui zake kwa sababu ya fikira zenu na matendo yenu maovu.
Colo Swahili 1:22  Lakini sasa, kwa kifo cha Mwanae aliyeishi hapa duniani, Mungu amewapatanisha naye, kusudi awalete mbele yake mkiwa watakatifu, safi na bila lawama.
Colo Swahili 1:23  Mnapaswa, lakini kuendelea kuwa imara na thabiti katika imani hiyo, na msikubali kusukumwa mbali na tumaini lile mlilopata wakati mlipoisikia Habari Njema. Mimi Paulo nimekuwa mtumishi wa hiyo Habari Njema ambayo imekwisha hubiriwa kila kiumbe duniani.
Colo Swahili 1:24  Na sasa nafurahi kuteseka kwa ajili yenu, maana kwa mateso yangu hapa duniani, nasaidia kukamilisha kile kilichopungua bado katika mateso ya Kristo kwa ajili ya mwili wake, yaani kanisa.
Colo Swahili 1:25  Nami nimefanywa kuwa mtumishi wa kanisa kufuatana na mpango wake Mungu ambao alinikabidhi kwa faida yenu. Mpango wenyewe ni kuutangaza kwa ukamilifu ujumbe wake,
Colo Swahili 1:26  ambao ni siri aliyowaficha binadamu wote tangu milele, lakini sasa amewajulisha watu wake.
Colo Swahili 1:27  Mpango wa Mungu ni kuwajulisha watu wake siri hii kuu na tukufu ambayo ni kwa ajili ya watu wote. Na, siri yenyewe ndiyo hii: Kristo yuko ndani yenu, na jambo hilo lamaanisha kwamba ninyi mtaushiriki utukufu wa Mungu.
Colo Swahili 1:28  Kwa sababu hiyo tunamhubiri Kristo kwa watu wote; tunawaonya na kuwafundisha wote kwa hekima yote, ili tuweze kumleta kila mmoja mbele ya Mungu akiwa amekomaa katika kuungana na Kristo.
Colo Swahili 1:29  Kwa madhumuni hayo mimi nafanya kazi na kujitahidi nikiitumia nguvu kuu ya Kristo ifanyayo kazi ndani yangu.
Chapter 2
Colo Swahili 2:1  Napenda mjue jinsi ninavyofanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu, kwa ajili ya watu wa Laodikea na kwa ajili ya wote ambao hawajapata kuniona kwa macho.
Colo Swahili 2:2  Nafanya hivi kusudi mioyo yao ifarijiwe na kuvutwa pamoja katika upendo, ili wajazwe uthabiti mwingi uletwao na elimu ya kweli. Hapo wataijua siri ya Mungu ambayo ni Kristo mwenyewe.
Colo Swahili 2:3  Ndani yake zimefichika hazina zote za hekima na elimu.
Colo Swahili 2:4  Basi, nawaambieni, msikubali kudanganywa na mtu yeyote kwa maneno ya uongo hata kama ni ya kuvutia sana.
Colo Swahili 2:5  Maana, ingawa mimi niko mbali nanyi kwa mwili, lakini niko pamoja nanyi kwa roho, na ninafurahi kuona uthabiti kamili mnaosimama nao pamoja katika imani yenu kwa Kristo.
Colo Swahili 2:6  Maadamu ninyi mmemkubali Kristo Yesu kuwa Bwana, basi, ishini katika muungano naye.
Colo Swahili 2:7  Mnapaswa kuwa na mizizi ndani yake, kujijenga juu yake na kuwa imara katika imani yenu kama mlivyofundishwa. Muwe na shukrani tele.
Colo Swahili 2:8  Angalieni basi, mtu asiwapotoshe kwa udanganyifu mtupu wa hekima ya kibinadamu, ambayo chanzo chake ni mafundisho ya mapokeo ya watu na ya pepo watawala, na wala si Kristo mwenyewe!
Colo Swahili 2:9  Maana, ndani yake Kristo katika ubinadamu wake, umo ukamilifu wote wa Mungu,
Colo Swahili 2:10  nanyi mmepewa uzima kamili katika kuungana naye. Yeye yuko juu ya pepo watawala wote na wakuu wote.
Colo Swahili 2:11  Katika kuungana na Kristo ninyi mlitahiriwa, lakini si kwa tohara ifanywayo na watu, bali inayofanywa na Kristo mwenyewe, na ambayo inahusikana na kukombolewa kutoka katika utu wa dhambi.
Colo Swahili 2:12  Maana, mlipobatizwa mlizikwa pamoja na Kristo, na katika ubatizo, mlifufuliwa pia pamoja naye kwa imani yenu katika nguvu ya Mungu ambaye alimfufua Kristo kutoka wafu.
Colo Swahili 2:13  Wakati mmoja nanyi mlikuwa mmekufa kwa sababu ya makosa yenu na kwa sababu ninyi mlikuwa watu wa mataifa mengine. Lakini Mungu amewapa ninyi uzima pamoja na Kristo. Mungu ametusamehe dhambi zetu zote;
Colo Swahili 2:14  alifutilia mbali ile hati ya deni iliyokuwa inatukabili na masharti yake, na kuifuta kabisa kwa kuipigilia msalabani.
Colo Swahili 2:15  Juu ya msalaba Kristo aliwapokonya nguvu zao hao pepo watawala na wakuu; aliwafanya kuwa kitu cha fedheha hadharani kwa kuwaburuta kama mateka katika msafara wa ushindi wake.
Colo Swahili 2:16  Kwa hiyo, basi, msikubali kupewa masharti na mtu yeyote kuhusu vyakula au vinywaji, siku za sherehe, sikukuu ya Mwezi mpya au Sabato.
Colo Swahili 2:17  Mambo ya aina hiyo ni kivuli tu cha yale yatakayokuja; ukweli wenyewe ndiye Kristo.
Colo Swahili 2:18  Msikubali kuhukumiwa na mtu yeyote anayejitakia kuwa wa maana kwa sababu ya maono ya pekee na ambaye anasisitiza juu ya unyenyekevu wa uongo na ibada kwa malaika. Mtu wa namna hiyo amepumbazika kwa fikira danganifu za kidunia
Colo Swahili 2:19  na amejitenga na Kristo aliye kichwa cha huo mwili. Chini ya uongozi wa Kristo, mwili wote unalishwa na kuunganishwa pamoja kwa viungo na mishipa yake, nao hukua kama atakavyo Mungu.
Colo Swahili 2:20  Ninyi mmekufa pamoja na Kristo na kukombolewa kutoka nguvu za pepo watawala wa ulimwengu. Kwa nini, basi, kuishi tena kama vile mngekuwa wa ulimwengu huu? Ya nini kuwekewa masharti:
Colo Swahili 2:21  "Msishike hiki," "Msionje kile," "Msiguse kile!"
Colo Swahili 2:22  Mambo hayo yote yanahusika na vitu vyenye kuharibika mara tu vinapotumiwa; hayo ni maagizo na mafundisho ya kibinadamu tu.
Colo Swahili 2:23  Kweli, masharti hayo yaonekana kuwa ya hekima katika namna ya ibada ya kujitakia wenyewe, unyenyekevu wa uongo na kuutendea mwili kwa ukali; lakini kwa kweli, haifai chochote kuzuia tamaa za mwili.
Chapter 3
Colo Swahili 3:1  Basi, ikiwa mmefufuka pamoja na Kristo, panieni mambo ya juu, kule Kristo aliko, ameketi upande wa kulia wa Mungu.
Colo Swahili 3:2  Muwe na hamu ya mambo ya huko juu, na siyo mambo ya hapa duniani.
Colo Swahili 3:3  Maana ninyi mmekufa na uzima wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu.
Colo Swahili 3:4  Uzima wenu halisi ni Kristo, na wakati atakapotokea ndipo nanyi pia mtakapotokea pamoja naye katika utukufu.
Colo Swahili 3:5  Basi, komesheni kabisa kila kitu kilicho ndani yenu ambacho chahusika na mambo ya kidunia: uasherati, uchafu, shauku, tamaa mbaya na uchu (ambao ni sawa na kuabudu sanamu).
Colo Swahili 3:6  Kwa sababu ya mambo hayo hasira ya Mungu huwajia wote wanaomwasi.
Colo Swahili 3:7  Wakati mmoja ninyi pia mliishi kufuatana na mambo hayo, mlipotawaliwa nayo.
Colo Swahili 3:8  Lakini sasa mnapaswa kuachana na mambo haya yote: hasira, tamaa, uovu; kufuru au maneno yasiyofaa yasitoke kamwe vinywani mwenu.
Colo Swahili 3:9  Msiambiane uongo, kwani ninyi mmekwisha vua ule utu wa kale pamoja na matendo yake yote,
Colo Swahili 3:10  mkavaa utu mpya. Huu unaendelea kurekebishwa na Mungu, Muumba wake, kadiri ya mfano wake, ili mpate kumjua Mungu kwa ukamilifu.
Colo Swahili 3:11  Katika hali hii, hakuna tena tofauti kati ya Mgiriki na Myahudi, aliyetahiriwa na asiyetahiriwa, msomi na asiye msomi, mtumwa na mtu aliye huru. Kristo ni kila kitu, na yumo katika yote.
Colo Swahili 3:12  Ninyi ni watu wake Mungu; yeye aliwapenda na kuwateua. Kwa hiyo basi, vaeni moyo wa huruma, wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu.
Colo Swahili 3:13  Vumilianeni na kusameheana iwapo mmoja wenu analo jambo lolote dhidi ya mwenzake. Mnapaswa kusameheana kama Bwana alivyowasamehe ninyi.
Colo Swahili 3:14  Zaidi ya hayo yote, zingatieni upendo kwani upendo huunganisha kila kitu katika umoja ulio kamili.
Colo Swahili 3:15  Nayo amani ya Kristo itawale mioyoni mwenu; maana kwa ajili hiyo ninyi mmeitwa katika mwili huo mmoja. Tena muwe na shukrani!
Colo Swahili 3:16  Ujumbe wa Kristo ukae ndani yenu pamoja na utajiri wake wote. Fundishaneni na kushauriana kwa hekima yote. Imbeni zaburi, nyimbo na tenzi za kiroho; mwimbieni Mungu mioyoni mwenu kwa shukrani.
Colo Swahili 3:17  Na, kila mfanyacho kwa neno au tendo, fanyeni vyote kwa jina la Bwana Yesu na kumshukuru Mungu Baba kwa njia yake.
Colo Swahili 3:18  Enyi akina mama, watiini waume zenu, kwani ndivyo apendavyo Bwana.
Colo Swahili 3:19  Nanyi waume, wapendeni wake zenu, na msiwe wakali kwao.
Colo Swahili 3:20  Enyi watoto, watiini wazazi wenu daima maana hiyo humpendeza Bwana.
Colo Swahili 3:21  Nanyi wazazi, msiwachukize watoto wenu, la sivyo watakata tamaa.
Colo Swahili 3:22  Enyi watumwa, watiini wakuu wenu wa kidunia katika mambo yote, na si tu wakati wanapowatazama kwa kuwa mnataka kujipendekeza kwao; ila fanyeni hivyo kwa moyo wote, kwa sababu ya kumcha Bwana.
Colo Swahili 3:23  Kila mfanyalo, fanyeni kwa moyo wote, kwa sababu ya Bwana na si kwa ajili ya mtu.
Colo Swahili 3:24  Kumbukeni kwamba atawapeni tuzo lile alilowawekea watu wake. Mtumikieni Kristo Bwana!
Colo Swahili 3:25  Atendaye mabaya atalipwa kufuatana na ubaya wake; Mungu hana ubaguzi.
Chapter 4
Colo Swahili 4:1  Nanyi wakuu, watendeeni watumwa wenu kwa uadilifu na haki, mkikumbuka kwamba nanyi pia mnaye Bwana mbinguni.
Colo Swahili 4:2  Dumuni katika sala, na mnaposali muwe waangalifu, mkimshukuru Mungu.
Colo Swahili 4:3  Vilevile, mtuombee sisi pia ili Mungu atupe fursa ya kuuhubiri ujumbe wake kuhusu siri ya Kristo. Kwa ajili hiyo mimi niko sasa kifungoni.
Colo Swahili 4:4  Basi, ombeni ili niweze kusema kama inavyonipasa na kwa namna itakayodhihirisha siri hiyo.
Colo Swahili 4:5  Muwe na hekima katika uhusiano wenu na watu wasioamini, mkitumia vizuri kila nafasi mliyo nayo.
Colo Swahili 4:6  Mazungumzo yenu yanapaswa kuwa daima mema na ya kuvutia, na mnapaswa kujua jinsi ya kumjibu vizuri kila mmoja.
Colo Swahili 4:7  Ndugu yetu mpenzi Tukiko, mfanyakazi mwaminifu na mtumishi mwenzetu katika kazi ya Bwana, atawapeni habari zangu zote.
Colo Swahili 4:8  Ndiyo maana namtuma, ili aichangamshe mioyo yenu kwa kuwaambieni habari zetu.
Colo Swahili 4:9  Anakuja pamoja na Onesimo, ndugu yetu mpenzi na mwaminifu, ambaye ni mwananchi mwenzenu. Watawapeni habari za mambo yote yanayofanyika hapa.
Colo Swahili 4:10  Aristarko, ambaye yuko kifungoni pamoja nami, anawasalimuni; hali kadhalika Marko, binamu yake Barnaba, (mmekwisha pata maagizo juu yake; akifika kwenu mkaribisheni).
Colo Swahili 4:11  Naye Yoshua aitwaye Yusto, anawasalimuni. Miongoni mwa Wayahudi waliokwisha pokea imani, hawa tu peke yao, ndio wanaofanya kazi pamoja nami kwa ajili ya Utawala wa Mungu; nao wamekuwa msaada mkubwa kwangu.
Colo Swahili 4:12  Epafra, mwananchi mwenzenu na mtumishi wa Kristo Yesu anawasalimuni. Daima anawaombeeni ninyi kwa bidii ili mpate kusimama imara, mkomae na kuwa thabiti kabisa katika mambo yote anayotaka Mungu.
Colo Swahili 4:13  Naweza kushuhudia kwamba anafanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu na kwa ajili ya watu wa Laodikea na Hierapoli.
Colo Swahili 4:14  Luka, daktari wetu mpenzi, na Dema, wanawasalimuni.
Colo Swahili 4:15  Salamu zetu kwa ndugu zetu wa Laodikea; msalimuni dada Nimfa pamoja na jumuiya yote ya waumini inayokutana nyumbani kwake.
Colo Swahili 4:16  Mkisha soma barua hii, hakikisheni kwamba inasomwa na Wakristo wa Laodikea; na ninyi fanyeni mpango mpate kuisoma barua waliyoipata kwao.
Colo Swahili 4:17  Mwambieni Arkipo aitekeleze vizuri ile huduma aliyokabidhiwa na Bwana.
Colo Swahili 4:18  Naandika haya kwa mkono wangu mwenyewe: Salamu kutoka kwangu, mimi Paulo. Kumbukeni kwamba niko kifungoni. Neema ya Mungu iwe nanyi.