Site uses cookies to provide basic functionality.

OK
JOHN
Up
1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12 13 14 15 16 17 18 19 20 21
Toggle notes
Chapter 1
John Swahili 1:1  Hapo Mwanzo, Neno alikuwako; naye alikuwa na Mungu, naye alikuwa Mungu.
John Swahili 1:3  Kwa njia yake vitu vyote viliumbwa; hakuna hata kiumbe kimoja kilichoumbwa pasipo yeye.
John Swahili 1:4  Yeye alikuwa chanzo cha uhai na uhai huo ulikuwa mwanga wa watu.
John Swahili 1:5  Na mwanga huo huangaza gizani, nalo giza halikuweza kuushinda.
John Swahili 1:7  ambaye alikuja kuwaambia watu juu ya huo mwanga. Alikuja ili kwa ujumbe wake watu wote wapate kuamini.
John Swahili 1:8  Yeye hakuwa huo mwanga, ila alikuja tu kuwaambia watu juu ya huo mwanga.
John Swahili 1:9  Huu ndio mwanga halisi, mwanga unaokuja ulimwenguni, na kuwaangazia watu wote.
John Swahili 1:10  Basi, Neno alikuwako ulimwenguni; na kwa njia yake ulimwengu uliumbwa, lakini ulimwengu haukumtambua.
John Swahili 1:11  Alikuja katika nchi yake mwenyewe, nao walio wake hawakumpokea.
John Swahili 1:12  Lakini wale wote waliompokea na kumwamini, hao aliwapa uwezo wa kuwa watoto wa Mungu.
John Swahili 1:13  Hawa wamekuwa watoto wa Mungu si kwa uwezo wa kibinadamu, wala kwa nguvu za kimwili, wala kwa mapenzi ya mtu, bali Mungu mwenyewe ndiye baba yao.
John Swahili 1:14  Naye Neno akawa mwanadamu, akakaa kwetu. Nasi tumeuona utukufu wake, utukufu wake yeye aliye Mwana wa pekee wa Baba; amejaa neema na ukweli.
John Swahili 1:15  Yohane aliwaambia watu habari zake, akasema kwa sauti, "Huyu ndiye niliyemtaja wakati niliposema: Anakuja mtu mmoja baada yangu ambaye ni mkuu kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa."
John Swahili 1:16  Kutokana na ukamilifu wake sisi tumepokea neema mfululizo.
John Swahili 1:17  Maana Mungu alitoa Sheria kwa njia ya Mose, lakini neema na kweli vimekuja kwa njia ya Kristo.
John Swahili 1:18  Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote ule. Mwana wa pekee aliye sawa na Mungu ambaye ameungana na Baba, ndiye aliyetujulisha habari za Mungu.
John Swahili 1:19  Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa wakati viongozi wa Wayahudi kule Yerusalemu walipowatuma makuhani wa Walawi kwake wamwulize: "Wewe u nani?"
John Swahili 1:20  Yohane hakukataa kujibu swali hilo, bali alisema waziwazi, "Mimi siye Kristo."
John Swahili 1:21  Hapo wakamwuliza, "Basi, wewe ni nani? Je, wewe ni Eliya?" Yohane akajibu, "La, mimi siye." Wakamwuliza, "Je, wewe ni yule nabii?" Yohane akawajibu, "La!"
John Swahili 1:22  Nao wakamwuliza, "Basi, wewe ni nani? Wasema nini juu yako mwenyewe? Tuambie, ili tuwapelekee jibu wale waliotutuma."
John Swahili 1:23  Yohane akawajibu, "Mimi ndiye yule ambaye nabii Isaya alisema habari zake: Sauti ya mtu imesikika jangwani: Nyoosheni njia ya Bwana."
John Swahili 1:25  Basi, wakamwuliza Yohane, "Kama wewe si Kristo, wala Eliya, wala yule nabii, mbona wabatiza?"
John Swahili 1:26  Yohane akawajibu, "Mimi nabatiza kwa maji, lakini yuko mmoja kati yenu, msiyemjua bado.
John Swahili 1:27  Huyo anakuja baada yangu, lakini mimi sistahili hata kumfungua kamba za viatu vyake."
John Swahili 1:28  Mambo haya yalifanyika huko Bethania, ng'ambo ya mto Yordani ambako Yohane alikuwa anabatiza.
John Swahili 1:29  Kesho yake, Yohane alimwona Yesu akimjia, akasema, "Huyu ndiye Mwana-kondoo wa Mungu aondoaye dhambi ya ulimwengu!
John Swahili 1:30  Huyu ndiye niliyesema juu yake: Baada yangu anakuja mtu mmoja aliye mkuu zaidi kuliko mimi, maana alikuwako kabla mimi sijazaliwa!
John Swahili 1:31  Mimi mwenyewe sikumfahamu, lakini nimekuja kubatiza kwa maji ili watu wa Israeli wapate kumjua."
John Swahili 1:32  Huu ndio ushahidi Yohane alioutoa: "Nilimwona Roho akishuka kama njiwa kutoka mbinguni na kutua juu yake.
John Swahili 1:33  Mimi sikumjua, lakini yule aliyenituma nikabatize watu kwa maji alikuwa ameniambia: Mtu yule utakayemwona Roho akimshukia kutoka mbinguni na kukaa juu yake, huyo ndiye anayebatiza kwa Roho Mtakatifu.
John Swahili 1:34  Mimi nimeona na ninawaambieni kwamba huyu ndiye Mwana wa Mungu."
John Swahili 1:35  Kesho yake, Yohane alikuwa tena mahali hapo pamoja na wanafunzi wake wawili.
John Swahili 1:36  Alipomwona Yesu akipita akasema, "Tazameni! Huyu ndiye Mwana-kondoo wa Mungu."
John Swahili 1:37  Hao wanafunzi walimsikia Yohane akisema maneno hayo, wakamfuata Yesu.
John Swahili 1:38  Basi, Yesu aligeuka, na alipowaona hao wanafunzi wanamfuata, akawauliza, "Mnatafuta nini?" Nao wakamjibu, "Rabi (yaani Mwalimu), unakaa wapi?"
John Swahili 1:39  Yesu akawaambia, "Njoni, nanyi mtaona." Hao wanafunzi wakamfuata, wakaona mahali alipokuwa anakaa, wakashinda naye siku hiyo. Ilikuwa yapata saa kumi jioni.
John Swahili 1:40  Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa hao wawili waliokuwa wamemsikia Yohane akisema hivyo, wakamfuata Yesu.
John Swahili 1:41  Andrea alimkuta kwanza Simoni, ndugu yake, akamwambia, "Tumemwona Masiha" (maana yake Kristo).
John Swahili 1:42  Kisha akampeleka Simoni kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama Simoni akasema, "Wewe ni Simoni mwana wa Yohane. Sasa utaitwa Kefa." (maana yake ni Petro, yaani, "Mwamba.")
John Swahili 1:43  Kesho yake Yesu aliamua kwenda Galilaya. Basi, akamkuta Filipo, akamwambia, "Nifuate."
John Swahili 1:44  Filipo alikuwa mwenyeji wa Bethsaida, mji wa akina Andrea na Petro.
John Swahili 1:45  Naye Filipo akamkuta Nathanieli, akamwambia, "Tumemwona yule ambaye Mose aliandika juu yake katika kitabu cha Sheria, na ambaye manabii waliandika habari zake, yaani Yesu Mwana wa Yosefu, kutoka Nazareti."
John Swahili 1:46  Naye Nathanieli akamwuliza Filipo, "Je, kitu chema chaweza kutoka Nazareti?" Filipo akamwambia, "Njoo uone."
John Swahili 1:47  Yesu alipomwona Nathanieli akimjia alisema juu yake, "Tazameni! Huyo ni Mwisraeli halisi: hamna hila ndani yake."
John Swahili 1:48  Naye Nathanieli akamwuliza, "Umepataje kunijua?" Yesu akamwambia, "Ulipokuwa chini ya mtini hata kabla Filipo hajakuita, nilikuona."
John Swahili 1:49  Hapo Nathanieli akamwambia, "Mwalimu, wewe ni Mwana wa Mungu. Wewe ni Mfalme wa Israeli!"
John Swahili 1:50  Yesu akamwambia, "Je, umeamini kwa kuwa nimekwambia kwamba nilikuona chini ya mtini? Utaona makubwa zaidi kuliko haya."
John Swahili 1:51  Yesu akaendelea kusema, "Nawaambieni kweli, mtaona mbingu zinafunguka na malaika wa Mungu wakipanda na kushuka juu ya Mwana wa Mtu."
Chapter 2
John Swahili 2:1  Siku ya tatu kulikuwa na arusi mjini Kana, mkoani Galilaya. Mama yake Yesu alikuwapo,
John Swahili 2:2  naye Yesu alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake.
John Swahili 2:3  Divai ilipokwisha, mama yake akamwambia, "Hawana divai!"
John Swahili 2:4  Yesu akamjibu, "Mama, usiniambie la kufanya. Saa yangu bado."
John Swahili 2:5  Hapo mama yake akawaambia watumishi, "Lolote atakalowaambieni, fanyeni."
John Swahili 2:6  Hapo palikuwa na mitungi sita ya mawe, ambayo kila mmoja uliweza kuchukua kiasi cha madebe mawili au matatu. Ilikuwa imewekwa hapo kufuatana na desturi ya Kiyahudi ya kutawadha.
John Swahili 2:7  Yesu akawaambia, "Ijazeni mitungi hiyo maji." Nao wakaijaza mpaka juu.
John Swahili 2:8  Kisha akawaambia, "Sasa choteni mkampelekee mkuu wa karamu."
John Swahili 2:9  Mkuu wa karamu alipoonja hayo maji, kumbe yalikuwa yamegeuka kuwa divai. Yeye hakujua ilikotoka, (lakini wale watumishi waliochota maji walijua). Mkuu wa karamu akamwita bwana arusi,
John Swahili 2:10  akamwambia, "Kila mtu huandaa divai nzuri kwanza hata wakisha tosheka huandaa ile hafifu. Lakini wewe umeiweka divai nzuri mpaka sasa!"
John Swahili 2:11  Yesu alifanya ishara hii ya kwanza huko Kana, Galilaya, akaonyesha utukufu wake; nao wanafunzi wake wakamwamini.
John Swahili 2:12  Baada ya hayo, Yesu alishuka pamoja na mama yake, ndugu zake na wanafunzi wake, wakaenda Kafarnaumu ambako walikaa kwa siku chache.
John Swahili 2:13  Sikukuu ya Wayahudi ya Pasaka ilikuwa imekaribia; hivyo Yesu akaenda Yerusalemu.
John Swahili 2:14  Hekaluni aliwakuta watu wakiuza ng'ombe, kondoo na njiwa, na wavunja fedha walikuwa wamekaa kwenye meza zao.
John Swahili 2:15  Akatengeneza mjeledi wa kamba, akawafukuza wote nje ya Hekalu pamoja na kondoo na ng'ombe wao, akazimwaga sarafu za wenye kuvunja fedha na kupindua meza zao.
John Swahili 2:16  Akawaambia wale waliokuwa wanauza njiwa, "Ondoeni vitu hivi hapa. Msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa soko!"
John Swahili 2:17  Wanafunzi wake wakakumbuka kwamba Maandiko yasema: "Upendo wangu kwa nyumba yako waniua."
John Swahili 2:18  Baadhi ya Wayahudi wakamwuliza Yesu, "Utafanya muujiza gani kuonyesha kwamba unayo haki kufanya mambo haya?"
John Swahili 2:19  Yesu akawaambia, "Vunjeni Hekalu hili, nami nitalijenga kwa siku tatu."
John Swahili 2:20  Hapo Wayahudi wakasema, "Hekalu hili lilijengwa kwa muda wa miaka arobaini na sita. Je, wewe utalijenga kwa siku tatu?"
John Swahili 2:21  Lakini Yesu alikuwa anaongea juu ya Hekalu ambalo ni mwili wake.
John Swahili 2:22  Basi, alipofufuliwa kutoka wafu, wanafunzi wake walikumbuka kwamba alikuwa amesema hayo, wakaamini Maandiko Matakatifu na yale maneno aliyokuwa akisema Yesu.
John Swahili 2:23  Yesu alipokuwa Yerusalemu kwa sikukuu ya Pasaka, watu wengi walimwamini walipoona ishara alizozifanya.
John Swahili 2:24  Lakini Yesu hakuwa na imani nao kwa sababu aliwajua wote.
John Swahili 2:25  Hakuhitaji kuambiwa chochote juu ya watu, maana aliyajua barabara mambo yote yaliyomo mioyoni mwao.
Chapter 3
John Swahili 3:1  Kulikuwa na kiongozi mmoja Myahudi, wa kikundi cha Mafarisayo, jina lake Nikodemo.
John Swahili 3:2  Siku moja alimwendea Yesu usiku, akamwambia, "Rabi, tunajua kwamba wewe ni mwalimu uliyetumwa na Mungu, maana hakuna mtu awezaye kufanya ishara unazozifanya Mungu asipokuwa pamoja naye."
John Swahili 3:3  Yesu akamwambia, "Kweli nakwambia, mtu asipozaliwa upya hataweza kuuona ufalme wa Mungu."
John Swahili 3:4  Nikodemo akamwuliza, "Mtu mzima awezaje kuzaliwa tena? Hawezi kuingia tumboni mwa mama yake na kuzaliwa mara ya pili!"
John Swahili 3:5  Yesu akamjibu, "Kweli nakwambia, mtu asipozaliwa kwa maji na Roho, hawezi kamwe kuingia katika ufalme wa Mungu.
John Swahili 3:6  Mtu huzaliwa kimwili kwa baba na mama, lakini huzaliwa kiroho kwa Roho.
John Swahili 3:7  Usistaajabu kwamba nimekwambia kuwa ni lazima kuzaliwa upya.
John Swahili 3:8  Upepo huvuma kuelekea upendako; waisikia sauti yake, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda. Ndivyo ilivyo kwa mtu aliyezaliwa kwa Roho."
John Swahili 3:9  Nikodemo akamwuliza, "Mambo haya yanawezekanaje?"
John Swahili 3:10  Yesu akamjibu, "Je, wewe ni mwalimu katika Israel na huyajui mambo haya?
John Swahili 3:11  Kweli nakwambia, sisi twasema tunayoyajua na kushuhudia tuliyoyaona, lakini ninyi hamkubali ujumbe wetu.
John Swahili 3:12  Ikiwa nimewaambieni mambo ya kidunia nanyi hamniamini, mtawezaje kuamini nikiwaambieni mambo ya mbinguni?
John Swahili 3:13  Hakuna mtu aliyepata kwenda juu mbinguni isipokuwa Mwana wa Mtu ambaye ameshuka kutoka mbinguni.
John Swahili 3:14  "Kama vile Mose alivyomwinua juu nyoka wa shaba kule jangwani, naye Mwana wa Mtu atainuliwa juu vivyo hivyo,
John Swahili 3:16  Maana Mungu aliupenda ulimwengu hivi hata akamtoa Mwana wake wa pekee, ili kila amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.
John Swahili 3:17  Maana Mungu hakumtuma Mwanae ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali aukomboe ulimwengu.
John Swahili 3:18  "Anayemwamini Mwana hahukumiwi; asiyemwamini amekwisha hukumiwa kwa sababu hakumwamini Mwana wa pekee wa Mungu.
John Swahili 3:19  Na hukumu yenyewe ndiyo hii: Mwanga umekuja ulimwenguni lakini watu wakapenda giza kuliko mwanga, kwani matendo yao ni maovu.
John Swahili 3:20  Kila mtu atendaye maovu anauchukia mwanga, wala haji kwenye mwanga, maana hapendi matendo yake maovu yamulikwe.
John Swahili 3:21  Lakini mwenye kuuzingatia ukweli huja kwenye mwanga, ili matendo yake yaonekane yametendwa kwa kumtii Mungu."
John Swahili 3:22  Baada ya hayo, Yesu alifika mkoani Yudea pamoja na wanafunzi wake. Alikaa huko pamoja nao kwa muda, akibatiza watu.
John Swahili 3:23  Yohane pia alikuwa akibatiza watu huko Ainoni, karibu na Salemu, maana huko kulikuwa na maji mengi. Watu walimwendea, naye akawabatiza.
John Swahili 3:24  (Wakati huo Yohane alikuwa bado hajafungwa gerezani.)
John Swahili 3:25  Ubishi ulitokea kati ya baadhi ya wanafunzi wa Yohane na Myahudi mmoja kuhusu desturi za kutawadha.
John Swahili 3:26  Basi, wanafunzi hao wakamwendea Yohane na kumwambia, "Mwalimu, yule mtu aliyekuwa pamoja nawe ng'ambo ya Yordani na ambaye wewe ulimshuhudia, sasa naye anabatiza, na watu wote wanamwendea."
John Swahili 3:27  Yohane akawaambia, "Mtu hawezi kuwa na kitu asipopewa na Mungu.
John Swahili 3:28  Nanyi wenyewe mwaweza kushuhudia kuwa nilisema: Mimi siye Kristo, lakini nimetumwa ili nimtangulie!
John Swahili 3:29  Bibiarusi ni wake bwanaarusi, lakini rafiki yake bwana arusi, anayesimama na kusikiliza, hufurahi sana anapomsikia bwana arusi akisema. Ndivyo furaha yangu ilivyokamilishwa.
John Swahili 3:30  Ni lazima yeye azidi kuwa maarufu, na mimi nipungue.
John Swahili 3:31  "Anayekuja kutoka juu ni mkuu kuliko wote; atokaye duniani ni wa dunia, na huongea mambo ya kidunia. Lakini anayekuja kutoka mbinguni ni mkuu kuliko wote.
John Swahili 3:32  Yeye husema yale aliyoyaona na kuyasikia, lakini hakuna mtu anayekubali ujumbe wake.
John Swahili 3:33  Lakini mtu yeyote anayekubali ujumbe wake anathibitisha kwamba Mungu ni kweli.
John Swahili 3:34  Yule aliyetumwa na Mungu husema maneno ya Mungu, maana Mungu humjalia mtu huyo Roho wake bila kipimo.
John Swahili 3:36  Anayemwamini Mwana anao uzima wa milele; asiyemtii Mwana hatakuwa na uzima wa milele, bali ghadhabu ya Mungu hubaki juu yake."
Chapter 4
John Swahili 4:1  Mafarisayo walisikia kwamba Yesu alikuwa anabatiza na kuwapata wanafunzi wengi kuliko Yohane.
John Swahili 4:2  (Lakini ukweli ni kwamba Yesu hakuwa anabatiza ila wanafunzi wake.)
John Swahili 4:3  Basi, Yesu aliposikia hayo, alitoka Yudea akarudi Galilaya;
John Swahili 4:5  Basi, akafika Sukari, mji mmoja wa Samaria, karibu na shamba ambalo Yakobo alikuwa amempa mwanawe, Yosefu.
John Swahili 4:6  Mahali hapo palikuwa na kisima cha Yakobo, naye Yesu, kutokana na uchovu wa safari, akaketi kando ya kisima. Ilikuwa yapata saa sita mchana.
John Swahili 4:7  Basi, mwanamke mmoja Msamaria akafika kuteka maji. Yesu akamwambia, "Nipatie maji ninywe."
John Swahili 4:8  (Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wamekwenda mjini kununua chakula.)
John Swahili 4:9  Lakini huyo mwanamke akamwambia, "Wewe ni Myahudi; mimi ni mwanamke Msamaria! Unawezaje kuniomba maji?" (Wayahudi hawakuwa na ushirikiano na Wasamaria katika matumizi ya vitu.)
John Swahili 4:10  Yesu akamjibu, "Kama tu ungalijua zawadi ya Mungu na ni nani anayekwambia: Nipatie maji ninywe, ungalikwisha mwomba, naye angekupa maji yaliyo hai."
John Swahili 4:11  Huyo mama akasema, "Mheshimiwa, wewe huna chombo cha kutekea maji, nacho kisima ni kirefu; utapata wapi maji yaliyo hai?
John Swahili 4:12  Au, labda wewe wajifanya mkuu kuliko babu yetu Yakobo? Yeye alitupa sisi kisima hiki; na yeye mwenyewe, watoto wake na mifugo yake walikunywa maji ya kisima hiki."
John Swahili 4:13  Yesu akamjibu, "Kila anayekunywa maji haya ataona kiu tena.
John Swahili 4:14  Lakini atakayekunywa maji nitakayompa mimi, hataona kiu milele. Maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji ya uzima na kumpatia uzima wa milele."
John Swahili 4:15  Huyo mwanamke akamwambia, "Mheshimiwa, nipe maji hayo ili nisione kiu tena; nisije tena mpaka hapa kuteka maji."
John Swahili 4:16  Yesu akamwambia, "Nenda ukamwite mumeo uje naye hapa."
John Swahili 4:17  Huyo mwanamke akamwambia, "Mimi sina mume." Yesu akamwambia, "Umesema kweli, kwamba huna mume.
John Swahili 4:18  Maana umekuwa na waume watano, na huyo unayeishi naye sasa si mume wako. Hapo umesema kweli."
John Swahili 4:19  Huyo Mwanamke akamwambia, "Mheshimiwa, naona ya kuwa wewe u nabii.
John Swahili 4:20  Babu zetu waliabudu juu ya mlima huu, lakini ninyi mwasema kwamba mahali pa kumwabudu Mungu ni kule Yerusalemu."
John Swahili 4:21  Yesu akamwambia, "Niamini; wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba juu ya mlima huu, wala kule Yerusalemu.
John Swahili 4:22  Ninyi Wasamaria mnamwabudu yule msiyemjua, lakini sisi tunamjua huyo tunayemwabudu, kwa maana wokovu unatoka kwa Wayahudi.
John Swahili 4:23  Lakini wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo wanaoabudu kweli, watamwabudu Baba kwa nguvu ya Roho; watu wanaomwabudu hivyo ndio Baba anaotaka.
John Swahili 4:24  Mungu ni Roho, na watu wataweza tu kumwabudu kweli kwa nguvu ya Roho wake."
John Swahili 4:25  Huyo mama akamwambia, "Najua kwamba Masiha, aitwaye Kristo, anakuja. Atakapokuja atatujulisha kila kitu."
John Swahili 4:27  Hapo wanafunzi wake wakarudi, wakastaajabu sana kuona anaongea na mwanamke. Lakini hakuna mtu aliyesema: "Unataka nini?" au, "Kwa nini unaongea na mwanamke?"
John Swahili 4:28  Huyo mama akauacha mtungi wake pale, akaenda mjini na kuwaambia watu,
John Swahili 4:29  "Njoni mkamwone mtu aliyeniambia mambo yote niliyotenda! Je, yawezekana kuwa yeye ndiye Kristo?"
John Swahili 4:31  Wakati huohuo wanafunzi wake walikuwa wanamsihi Yesu: "Mwalimu, ule chakula."
John Swahili 4:32  Lakini Yesu akawaambia, "Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi."
John Swahili 4:33  Wanafunzi wake wakaulizana, "Je, kuna mtu aliyemletea chakula?"
John Swahili 4:34  Yesu akawaambia, "Chakula changu ni kufanya anachotaka yule aliyenituma na kuitimiza kazi yake.
John Swahili 4:35  Ninyi mwasema: Bado miezi minne tu, na wakati wa mavuno utafika! Lakini mimi nawaambieni, yatazameni mashamba; mazao yako tayari kuvunwa.
John Swahili 4:36  Mvunaji anapata mshahara wake, na anakusanya mavuno kwa ajili ya uzima wa milele; hivyo mpandaji na mvunaji watafurahi pamoja.
John Swahili 4:37  Kwa sababu hiyo msemo huu ni kweli: Mmoja hupanda na mwingine huvuna.
John Swahili 4:38  Mimi nimewatuma mkavune mavuno ambayo hamkuyatolea jasho, wengine walifanya kazi, lakini ninyi mnafaidika kutokana na jasho lao."
John Swahili 4:39  Wasamaria wengi wa kijiji kile waliamini kwa sababu ya maneno aliyosema huyo mama: "Ameniambia mambo yote niliyofanya."
John Swahili 4:40  Wasamaria walimwendea Yesu wakamwomba akae nao; naye akakaa hapo siku mbili.
John Swahili 4:41  Watu wengi zaidi walimwamini kwa sababu ya ujumbe wake.
John Swahili 4:42  Wakamwambia yule mama, "Sisi hatuamini tu kwa sababu ya maneno yako; sisi wenyewe tumesikia, na tunajua kwamba huyu ndiye kweli Mwokozi wa ulimwengu."
John Swahili 4:43  Baada ya siku mbili Yesu aliondoka hapo, akaenda Galilaya.
John Swahili 4:44  Maana Yesu mwenyewe alisema waziwazi kwamba, "Nabii hapati heshima katika nchi yake."
John Swahili 4:45  Basi, alipofika Galilaya, Wagalilaya wengi walimkaribisha. Maana nao pia walikuwa kwenye sikukuu ya Pasaka, wakayaona mambo yote Yesu aliyotenda huko Yerusalemu wakati wa sikukuu hiyo.
John Swahili 4:46  Yesu alifika tena huko mjini Kana, mkoani Galilaya, mahali alipogeuza maji kuwa divai. Kulikuwa na ofisa mmoja aliyekuwa na mtoto mgonjwa huko Kafarnaumu.
John Swahili 4:47  Basi, huyo ofisa aliposikia kuwa Yesu alikuwa ametoka Yudea na kufika Galilaya, alimwendea akamwomba aende kumponya mtoto wake aliyekuwa mgonjwa mahututi.
John Swahili 4:48  Yesu akamwambia, "Msipoona ishara na maajabu hamtaamini!"
John Swahili 4:49  Huyo ofisa akamwambia, "Mheshimiwa, tafadhali twende kabla mwanangu hajafa."
John Swahili 4:50  Yesu akamwambia, "Nenda tu, mwanao yu mzima." Huyo mtu akaamini maneno ya Yesu, akaenda zake.
John Swahili 4:51  Alipokuwa bado njiani, watumishi wake walikutana naye, wakamwambia kwamba mwanawe alikuwa mzima.
John Swahili 4:52  Naye akawauliza saa mtoto alipopata nafuu; nao wakamwambia, "Jana saa saba mchana, homa ilimwacha."
John Swahili 4:53  Huyo baba akakumbuka kwamba ilikuwa ni saa ileile ambapo Yesu alimwambia: "Mwanao yu mzima." Basi, yeye akaamini pamoja na jamaa yake yote.
John Swahili 4:54  Hii ilikuwa ishara ya pili aliyoifanya Yesu alipokuwa anatoka Yudea kwenda Galilaya.
Chapter 5
John Swahili 5:1  Baada ya hayo kulikuwa na sikukuu ya Wayahudi, naye Yesu akaenda Yerusalemu.
John Swahili 5:2  Huko Yerusalemu, karibu na mlango uitwao Mlango wa Kondoo, kulikuwa na bwawa la maji liitwalo kwa Kiebrania Bethzatha, ambalo lilikuwa na baraza tano zenye matao.
John Swahili 5:3  Humo barazani mlikuwa na wagonjwa wengi wamekaa: vipofu, viwete na waliopooza. Walikuwa wakingojea maji yatibuliwe,
John Swahili 5:4  maana mara kwa mara malaika alishuka majini nyakati fulani na kuyatibua. Mtu yeyote aliyekuwa wa kwanza kuingia majini baada ya maji kutibuliwa, alipona ugonjwa wowote aliokuwa nao.
John Swahili 5:5  Basi, hapo palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa mgonjwa kwa muda wa miaka thelathini na minane.
John Swahili 5:6  Naye alipomwona huyo mtu amelala hapo, akatambua kwamba alikuwa amekaa hapo kwa muda mrefu, akamwuliza, "Je, wataka kupona?"
John Swahili 5:7  Naye akajibu, "Mheshimiwa, mimi sina mtu wa kunipeleka majini wakati yanapotibuliwa. Kila nikijaribu kuingia, mtu mwingine hunitangulia."
John Swahili 5:8  Yesu akamwambia, "Inuka, chukua mkeka wako utembee."
John Swahili 5:9  Mara huyo mtu akapona, akachukua mkeka wake, akatembea. Jambo hili lilifanyika siku ya Sabato.
John Swahili 5:10  Kwa hiyo baadhi ya Wayahudi wakamwambia huyo mtu aliyeponywa, "Leo ni Sabato, si halali kubeba mkeka wako."
John Swahili 5:11  Lakini yeye akawaambia, "Yule mtu aliyeniponya ndiye aliyeniambia: Chukua mkeka wako, tembea."
John Swahili 5:12  Nao wakamwuliza, "Huyo mtu aliyekwambia: Chukua mkeka wako, tembea, ni nani?"
John Swahili 5:13  Lakini yeye hakumjua huyo mtu aliyemponya, maana Yesu alikuwa amekwisha ondoka mahali hapo, kwani palikuwa na umati mkubwa wa watu.
John Swahili 5:14  Basi, baadaye Yesu alimkuta huyo aliyeponywa Hekaluni, akamwambia, "Sasa umepona; usitende dhambi tena, usije ukapatwa na jambo baya zaidi."
John Swahili 5:15  Huyo mtu akaenda, akawaambia viongozi wa Wayahudi kwamba Yesu ndiye aliyemponya.
John Swahili 5:16  Kwa vile Yesu alifanya jambo hilo siku ya Sabato, Wayahudi walianza kumdhulumu.
John Swahili 5:17  Basi, Yesu akawaambia, "Baba yangu anafanya kazi daima, nami pia nafanya kazi."
John Swahili 5:18  Kwa sababu ya maneno haya, viongozi wa Wayahudi walizidi kutafuta njia ya kumwua Yesu: si kwa kuwa aliivunja Sheria ya Sabato tu, bali pia kwa kuwa alisema kwamba Mungu ni Baba yake, na hivyo akajifanya sawa na Mungu.
John Swahili 5:19  Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, Mwana hawezi kufanya kitu peke yake; anaweza tu kufanya kile anachomwona Baba akikifanya. Maana kile anachofanya Baba, Mwana hukifanya vilevile.
John Swahili 5:20  Baba ampenda Mwana, na humwonyesha kila kitu anachokifanya yeye mwenyewe, tena atamwonyesha mambo makuu kuliko haya, nanyi mtastaajabu.
John Swahili 5:21  Kama vile Baba huwafufua wafu na kuwapa uzima, vivyo hivyo naye Mwana huwapa uzima wale anaopenda.
John Swahili 5:22  Baba hamhukumu mtu yeyote; shughuli yote ya hukumu amemkabidhi Mwana,
John Swahili 5:23  ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba ambaye amemtuma.
John Swahili 5:24  "Kweli nawaambieni, anayesikia neno langu, na kumwamini yule aliyenituma, anao uzima wa milele. Hatahukumiwa kamwe, bali amekwisha pita kutoka kifo na kuingia katika uzima.
John Swahili 5:25  Kweli nawaambieni, wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo wafu wataisikia sauti ya Mwana wa Mungu, nao watakaoisikia, wataishi.
John Swahili 5:26  Kama vile Baba alivyo asili ya uhai, ndivyo pia alivyomjalia Mwanawe kuwa asili ya uhai.
John Swahili 5:27  Tena amempa mamlaka ya kuhukumu kwa sababu yeye ni Mwana wa Mtu.
John Swahili 5:28  Msistaajabie jambo hili; maana wakati unakuja ambapo wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake,
John Swahili 5:29  nao watafufuka: wale waliotenda mema watafufuka na kuishi, na wale waliotenda maovu watafufuka na kuhukumiwa.
John Swahili 5:30  "Mimi siwezi kufanya kitu kwa uwezo wangu mwenyewe. Mimi nina hukumu kama ninavyosikia kutoka kwa Baba, nayo hukumu yangu ni ya haki. Nia yangu si kufanya nipendavyo mwenyewe, bali apendavyo yule aliyenituma.
John Swahili 5:31  Nikijishuhudia mimi mwenyewe, ushahidi wangu hauwezi kukubaliwa kuwa wa kweli.
John Swahili 5:32  Lakini yuko mwingine ambaye hutoa ushahidi juu yangu, nami najua kwamba yote anayosema juu yangu ni ya kweli.
John Swahili 5:33  Ninyi mlituma ujumbe kwa Yohane naye aliushuhudia ukweli.
John Swahili 5:34  Si kwamba mimi nautegemea ushahidi wa wanadamu, lakini nasema mambo haya ili mpate kuokolewa.
John Swahili 5:35  Yohane alikuwa kama taa iliyokuwa ikiwaka na kuangaza, nanyi mlikuwa tayari kufurahia mwanga huo kwa kitambo.
John Swahili 5:36  Lakini mimi nina ushahidi juu yangu ambao ni mkuu zaidi kuliko ule wa Yohane. Kwa maana kazi ninazofanya, kazi alizonipa Baba nizifanye, ndizo zinazonishuhudia kwamba Baba ndiye aliyenituma.
John Swahili 5:37  Naye Baba aliyenituma hunishuhudia. Ninyi hamjapata kamwe kusikia sauti yake, wala kuuona uso wake,
John Swahili 5:38  na ujumbe wake haukai ndani yenu maana hamkumwamini yule aliyemtuma.
John Swahili 5:39  Ninyi huyachunguza Maandiko Matakatifu mkidhani kwamba ndani yake mtapata uzima wa milele; na kumbe maandiko hayohayo yananishuhudia!
John Swahili 5:40  Hata hivyo, ninyi hamtaki kuja kwangu ili mpate uzima.
John Swahili 5:42  Lakini nawajua ninyi, najua kwamba upendo kwa Mungu haumo mioyoni mwenu.
John Swahili 5:43  Mimi nimekuja kwa mamlaka ya Baba yangu, lakini hamnipokei; bali mtu mwingine akija kwa mamlaka yake mwenyewe, mtampokea.
John Swahili 5:44  Mwawezaje kuamini, hali ninyi mnapenda kupokea sifa kutoka kwenu ninyi wenyewe, wala hamtafuti sifa kutoka kwake yeye aliye peke yake Mungu?
John Swahili 5:45  Msifikiri kwamba mimi nitawashtaki kwa Baba. Mose ambaye ninyi mmemtumainia ndiye atakayewashtaki.
John Swahili 5:46  Kama kweli mngemwamini Mose, mngeniamini na mimi pia; maana Mose aliandika juu yangu.
John Swahili 5:47  Lakini hamuyaamini yale aliyoandika, mtawezaje basi, kuamini maneno yangu?"
Chapter 6
John Swahili 6:1  Baada ya hayo, Yesu alivuka ziwa Galilaya (au Ziwa Tiberia).
John Swahili 6:2  Umati mkubwa wa watu ulimfuata kwa sababu watu hao walikuwa wameona ishara alizokuwa akifanya kwa kuwaponya wagonjwa.
John Swahili 6:3  Yesu alipanda mlimani, akaketi pamoja na wanafunzi wake.
John Swahili 6:4  Sikukuu ya Wayahudi iitwayo Pasaka ilikuwa imekaribia.
John Swahili 6:5  Basi, Yesu na alipotazama na kuona umati wa watu ukija kwake, alimwambia Filipo, "Tununue wapi mikate ili watu hawa wapate kula?"
John Swahili 6:6  (Alisema hivyo kwa kumjaribu Filipo, kwani alijua mwenyewe atakalofanya.)
John Swahili 6:7  Filipo akamjibu, "Mikate ya denari mia mbili za fedha haiwatoshi watu hawa hata kama ila mmoja atapata kipande kidogo tu!"
John Swahili 6:8  Mmoja wa wanafunzi wake aitwaye Andrea, nduguye Simoni Petro, akamwambia,
John Swahili 6:9  "Yupo hapa mtoto mmoja aliye na mikate mitano ya shayiri na samaki wawili; lakini hivi vyatosha nini kwa watu wengi kama hawa?"
John Swahili 6:10  Yesu akasema, "Waketisheni watu." Palikuwa na nyasi tele mahali hapo. Basi, watu wakaketi, jumla yapata wanaume elfu tano.
John Swahili 6:11  Yesu akaitwaa ile mikate, akamshukuru Mungu, akawagawia watu waliokuwa wameketi; akafanya vivyo hivyo na wale samaki, kila mtu akapata kadiri alivyotaka.
John Swahili 6:12  Watu waliposhiba Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Kusanyeni vipande vilivyobaki visipotee."
John Swahili 6:13  Basi, wakakusanya vipande vya mikate ya shayiri walivyobakiza wale watu waliokula, wakajaza vikapu kumi na viwili.
John Swahili 6:14  Watu walipoiona ishara hiyo aliyoifanya Yesu, wakasema, "Hakika huyu ndiye nabii anayekuja ulimwenguni."
John Swahili 6:15  Yesu akajua ya kuwa watu walitaka kumchukua wamfanye mfalme, akaondoka tena, akaenda mlimani peke yake.
John Swahili 6:16  Ilipokuwa jioni wanafunzi wake waliteremka hadi ziwani,
John Swahili 6:17  wakapanda mashua ili wavuke kwenda Kafarnaumu. Giza lilikuwa limeingia, na Yesu alikuwa hajawafikia bado.
John Swahili 6:18  Ziwa likaanza kuchafuka kwa sababu upepo mkali ulikuwa unavuma.
John Swahili 6:19  Wanafunzi walipokuwa wamekwenda umbali wa kilomita tano au sita, walimwona Yesu akitembea juu ya maji, anakaribia mashua; wakaogopa sana.
John Swahili 6:21  Walifurahi kumchukua Yesu katika mashua; na mara mashua ikawasili nchi kavu walipokuwa wanakwenda.
John Swahili 6:22  Kesho yake umati wa watu wale waliobaki upande wa pili wa ziwa walitambua kwamba kulikuwa na mashua moja tu pale, na Yesu hakuingia katika mashua pamoja na wanafunzi wake, ila wanafunzi hao walikuwa wamekwenda zao peke yao.
John Swahili 6:23  Mashua nyingine kutoka Tiberia zilifika mahali hapo watu walipokula ile mikate, Bwana alipokwisha mshukuru Mungu.
John Swahili 6:24  Basi, hao watu walipogundua kwamba Yesu na wanafunzi wake hawakuwapo mahali hapo, walipanda mashua, wakaenda Kafarnaumu wakimtafuta.
John Swahili 6:25  Wale watu walipomkuta Yesu ng'ambo ya pili wa ziwa walimwuliza, "Mwalimu, ulifika lini hapa?"
John Swahili 6:26  Yesu akawajibu, "Kweli nawaambieni, mnanitafuta si kwa kuwa mmeona ishara, bali kwa sababu mlikula ile mikate mkashiba.
John Swahili 6:27  Msikishughulikie chakula kiharibikacho; kishugulikieni chakula kidumucho kwa ajili ya uzima wa milele. Mwana wa Mtu ambaye Baba amemthibitisha atawapeni chakula hicho."
John Swahili 6:28  Wao wakamwuliza, "Tufanye nini ili tuweze kuzitenda kazi za Mungu?"
John Swahili 6:29  Yesu akawajibu, "Hii ndiyo kazi anayotaka Mungu muifanye: kumwamini yule aliyemtuma."
John Swahili 6:30  Hapo wakamwambia, "Utafanya ishara gani ili tuione tupate kukuamini? Utafanya kitu gani?
John Swahili 6:31  Wazee wetu walikula mana kule jangwani, kama yasemavyo Maandiko: Aliwalisha mkate kutoka mbinguni."
John Swahili 6:32  Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, Mose hakuwapeni mkate kutoka mbinguni; Baba yangu ndiye awapaye ninyi mkate halisi kutoka mbinguni.
John Swahili 6:33  Maana mkate wa Mungu ni yule ashukaye kutoka mbinguni na aupaye ulimwengu uzima."
John Swahili 6:34  Basi, wakamwambia, "Mheshimiwa, tupe daima mkate huo."
John Swahili 6:35  Yesu akawaambia, "Mimi ndimi mkate wa uzima. Anayekuja kwangu hataona njaa; anayeniamini hataona kiu kamwe.
John Swahili 6:36  Lakini niliwaambieni kwamba ingawa mmeniona hamniamini.
John Swahili 6:37  Wote anaonipa Baba watakuja kwangu; nami sitamtupa nje yeyote anayekuja kwangu,
John Swahili 6:38  kwani nimeshuka kutoka mbinguni si kwa ajili ya kufanya matakwa yangu, ila kutimiza matakwa ya yule aliyenituma.
John Swahili 6:39  Na matakwa ya yule aliyenituma ndiyo haya: nisimpoteze hata mmoja kati ya wale alionipa, ila niwafufue wote Siku ya mwisho.
John Swahili 6:40  Maana anachotaka Baba yangu ndicho hiki: kila amwonaye Mwana na kumwamini awe na uzima wa milele; nami nitamfufua Siku ya mwisho."
John Swahili 6:41  Basi, Wayahudi wakaanza kunung'unika kwa kuwa alisema: "Mimi ni mkate ulioshuka kutoka mbinguni."
John Swahili 6:42  Wakasema, "Je, huyu si mwana wa Yosefu? Tunawajua baba yake na mama yake! Basi, anawezaje kusema kwamba ameshuka kutoka mbinguni?"
John Swahili 6:43  Yesu akawaambia, "Acheni kunung'unika ninyi kwa ninyi.
John Swahili 6:44  Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, Baba aliyenituma asipomvuta kwangu; nami nitamfufua mtu huyo Siku ya mwisho.
John Swahili 6:45  Manabii wameandika: Watu wote watafundishwa na Mungu. Kila mtu anayemsikia Baba na kujifunza kutoka kwake, huja kwangu.
John Swahili 6:46  Hii haina maana kwamba yupo mtu aliyemwona Baba, isipokuwa yule aliyetoka kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba.
John Swahili 6:47  Kweli, nawaambieni, anayeamini anao uzima wa milele.
John Swahili 6:49  Wazee wenu walikula mana kule jangwani, lakini walikufa.
John Swahili 6:50  Huu ndio mkate kutoka mbinguni; mkate ambao anayekula hatakufa.
John Swahili 6:51  Mimi ni mkate hai ulioshuka kutoka mbinguni. Mtu yeyote akila mkate huu ataishi milele. Na mkate nitakaompa ni mwili wangu ninaoutoa kwa ajili ya uzima wa ulimwengu."
John Swahili 6:53  Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, msipokula mwili wa Mwana wa Mtu na kunywa damu yake, hamtakuwa na uzima ndani yenu.
John Swahili 6:54  Anayekula mwili wangu na kunywa damu yangu anao uzima wa milele nami nitamfufua siku ya mwisho.
John Swahili 6:55  Maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli.
John Swahili 6:56  Aulaye mwili wangu na kunywa damu yangu, akaa ndani yangu, nami nakaa ndani yake.
John Swahili 6:57  Baba aliye hai alinituma, nami naishi kwa sababu yake; vivyo hivyo anilaye mimi ataishi pia kwa sababu yangu.
John Swahili 6:58  Basi, huu ndio mkate ulioshuka kutoka mbinguni; si kama mana waliyokula babu zetu, wakafa. Aulaye mkate huu ataishi milele."
John Swahili 6:59  Yesu alisema hayo alipokuwa akifundisha katika sunagogi kule Kafarnaumu.
John Swahili 6:60  Basi, wengi wa wafuasi wake waliposikia hayo, wakasema, "Haya ni mambo magumu! Nani awezaye kuyasikiliza?"
John Swahili 6:61  Yesu alijua bila kuambiwa na mtu kwamba wanafunzi wake walikuwa wananung'unika juu ya jambo hilo, akawauliza, "Je, jambo hili linawafanya muwe na mashaka?
John Swahili 6:62  Itakuwaje basi, mtakapomwona Mwana wa Mtu akipanda kwenda kule alikokuwa kwanza?
John Swahili 6:63  Roho ndiye atiaye uzima; binadamu peke yake hawezi. Maneno niliyowaambieni ni Roho, ni uzima.
John Swahili 6:64  Hata hivyo, wako baadhi yenu wasioamini." (Yesu alisema hivyo kwani alijua tangu mwanzo ni kina nani wasioamini, na pia ni nani atakayemsaliti.)
John Swahili 6:65  Kisha akasema, "Ndiyo maana niliwaambieni kwamba hakuna awezaye kuja kwangu asipowezeshwa na Baba yangu."
John Swahili 6:66  Kutokana na hayo, wengi wa wafuasi wake walirudi nyuma wasiandamane naye tena.
John Swahili 6:67  Basi, Yesu akawauliza wale kumi na wawili, "Je, nanyi pia mwataka kwenda zenu?"
John Swahili 6:68  Simoni Petro akamjibu, "Bwana, tutakwenda kwa nani? Wewe unayo maneno yaletayo uzima wa milele.
John Swahili 6:69  Sisi tunaamini, na tunajua kwamba wewe ndiwe yule Mtakatifu wa Mungu."
John Swahili 6:70  Yesu akawaambia, "Je, sikuwachagua ninyi kumi na wawili? Hata hivyo, mmoja wenu ni Ibilisi!"
John Swahili 6:71  Yesu alisema hayo juu ya Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti; maana huyu alikuwa ndiye atakayemsaliti, ingawa alikuwa mmoja wa wale kumi na wawili.
Chapter 7
John Swahili 7:1  Baada ya hayo, Yesu alikuwa akitembea katika Galilaya. Hakutaka kutembea mkoani Yudea kwa sababu viongozi wa Wayahudi walikuwa wanataka kumwua.
John Swahili 7:2  Sikukuu ya Vibanda ya Wayahudi ilikuwa imekaribia.
John Swahili 7:3  Basi ndugu zake wakamwambia, "Ondoka hapa uende Yudea ili wanafunzi wako wazione kazi unazozifanya.
John Swahili 7:4  Mtu hafanyi mambo kwa siri kama anataka kujulikana kwa watu. Maadam unafanya mambo haya, basi, jidhihirishe kwa ulimwengu."
John Swahili 7:6  Basi, Yesu akawaambia, "Wakati wangu ufaao haujafika bado. Lakini kwenu ninyi kila wakati unafaa.
John Swahili 7:7  Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi, lakini mimi wanichukia kwa sababu mimi nauambia wazi kwamba matendo yake ni maovu.
John Swahili 7:8  Ninyi nendeni kwenye sikukuu hiyo. Mimi siendi kwenye sikukuu hiyo, maana saa yangu ifaayo haijafika."
John Swahili 7:10  Baada ya ndugu zake kwenda kwenye sikukuu, Yesu naye alikwenda, lakini hakuenda kwa hadhara bali kwa siri.
John Swahili 7:11  Viongozi wa Wayahudi walikuwa wanamtafuta kwenye sikukuu hiyo; Wakauliza: "Yuko wapi?"
John Swahili 7:12  Kulikuwa na minong'ono mingi katika umati wa watu. Baadhi yao walisema, "Ni mtu mwema." Wengine walisema, "La! Anawapotosha watu."
John Swahili 7:13  Hata hivyo hakuna mtu aliyethubutu kusema, habari zake hadharani kwa kuwaogopa viongozi wa Wayahudi.
John Swahili 7:14  Sikukuu hiyo ilipofikia katikati, Yesu naye alikwenda Hekaluni, akaanza kufundisha.
John Swahili 7:15  Basi, Wayahudi wakashangaa na kusema "Mtu huyu amepataje elimu naye hakusoma shuleni?"
John Swahili 7:16  Hapo Yesu akawajibu, "Mafundisho ninayofundisha si yangu, bali ni yake yeye aliyenituma.
John Swahili 7:17  Mtu anayependa kufanya yale anayotaka Mungu, atajua kama mafundisho yangu yametoka kwa Mungu, au mimi najisemea tu mwenyewe.
John Swahili 7:18  Yeye anayejisemea tu mwenyewe anatafuta sifa yake mwenyewe; lakini anayetafuta sifa ya yule aliyemtuma, huyo ni mwaminifu, na ndani yake hamna uovu wowote.
John Swahili 7:19  Je, Mose hakuwapeni Sheria? Hata hivyo, hakuna hata mmoja wenu anayeishika Sheria. Kwa nini mnataka kuniua?"
John Swahili 7:20  Hapo watu wakamjibu, "Una wazimu wewe! Nani anataka kukuua?"
John Swahili 7:21  Yesu akawajibu, "Kuna jambo moja nililofanya, nanyi mnalistaajabia.
John Swahili 7:22  Mose aliwapeni ile desturi ya kutahiri. (Si kwamba desturi hiyo ilitoka kwa Mose, bali ilitoka kwa mababu). Sasa ninyi humtahiri mtu hata siku ya Sabato.
John Swahili 7:23  Ikiwa basi, mtu hutahiriwa hata siku ya Sabato kusudi Sheria ya Mose isivunjwe, mbona mnanikasirikia kwa sababu nimemfanya mtu kuwa mzima kabisa siku ya Sabato?
John Swahili 7:24  Msihukumu mambo kwa nje tu; toeni hukumu ya haki."
John Swahili 7:25  Baadhi ya watu wa Yerusalemu walisema, "Je, yule mtu wanayemtafuta wamuue si huyu?
John Swahili 7:26  Tazameni sasa! Anawaonya hadharani, wala hakuna mtu anayemwambia hata neno. Je, yawezekana kuwa viongozi wametambua kweli kwamba huyu ndiye Kristo?
John Swahili 7:27  Kristo atakapokuja hakuna mtu atakayejua mahali alikotoka, lakini sisi tunajua alikotoka mtu huyu!"
John Swahili 7:28  Basi, Yesu alipokuwa anafundisha Hekaluni alipaaza sauti na kusema, "Ati mnanijua; hata nilikotoka mnakujua! Hata hivyo, sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe; ila yeye aliyenituma mimi ni wa kweli, nanyi hamumjui.
John Swahili 7:29  Lakini mimi namjua kwa sababu nimetoka kwake, naye ndiye aliyenituma."
John Swahili 7:30  Basi, watu wakataka kumtia nguvuni, lakini hakuna mtu aliyethubutu kumkamata kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado.
John Swahili 7:31  Wengi katika ule umati wa watu walimwamini, wakasema, "Je, Kristo akija atafanya ishara kubwa zaidi kuliko alizozifanya huyu?"
John Swahili 7:32  Mafarisayo waliwasikia watu wakinong'ona maneno hayo juu ya Yesu. Basi, wao pamoja na makuhani wakuu wakawatuma walinzi wamtie nguvuni.
John Swahili 7:33  Yesu akasema, "Bado niko nanyi kwa muda mfupi, kisha nitamwendea yule aliyenituma.
John Swahili 7:34  Mtanitafuta lakini hamtaniona, maana pale nitakapokuwa ninyi hamwezi kufika."
John Swahili 7:35  Viongozi wa Wayahudi wakasema wao kwa wao, "Mtu huyu atakwenda wapi ambapo hatutaweza kumpata? Atakwenda kwa Wayahudi waliotawanyika kati ya Wagiriki, na kuwafundisha Wagiriki?
John Swahili 7:36  Ana maana gani anaposema: Mtanitafuta lakini hamtanipata, na mahali nitakapokuwa ninyi hamwezi kufika?"
John Swahili 7:37  Siku ya mwisho ya sikukuu hiyo ilikuwa siku maalum. Yesu alisimama, akasema kwa sauti kubwa, "Aliye na kiu na aje kwangu anywe.
John Swahili 7:38  Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: Anayeniamini mimi, mito ya maji yenye uzima itatiririka kutoka moyoni mwake!"
John Swahili 7:39  (Alisema hayo kumhusu Roho ambaye wale waliomwamini yeye watampokea. Wakati huo Roho alikuwa hajafika kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa bado.)
John Swahili 7:40  Baadhi ya watu katika ule umati walisikia maneno hayo, wakasema, "Kweli mtu huyu ndiye yule nabii!"
John Swahili 7:41  Wengine wakasema, "Huyu ndiye Kristo!" Lakini wengine walisema, "Je, yawezekana Kristo akatoka Galilaya?
John Swahili 7:42  Maandiko Matakatifu yasemaje? Yanasema: Kristo atatoka katika ukoo wa Daudi, na atazaliwa Bethlehemu, mji wa Daudi!"
John Swahili 7:43  Basi, kukatokea mafarakano juu yake katika ule umati wa watu.
John Swahili 7:44  Baadhi ya watu walitaka kumtia nguvuni lakini hakuna aliyejaribu kumkamata.
John Swahili 7:45  Kisha wale walinzi wakarudi kwa makuhani wakuu na Mafarisayo; nao wakawauliza, "Kwa nini hamkumleta?"
John Swahili 7:46  Walinzi wakawajibu, "Hakuna mtu aliyepata kamwe kusema kama asemavyo mtu huyu!"
John Swahili 7:47  Mafarisayo wakawauliza, "Je, nanyi pia mmedanganyika?
John Swahili 7:48  Je, mmekwisha mwona hata mmoja wa viongozi wa watu, au mmoja wa Mafarisayo aliyemwamini?
John Swahili 7:49  Lakini umati huu haujui Sheria ya Mose; umelaaniwa!"
John Swahili 7:50  Mmoja wao alikuwa Nikodemo ambaye hapo awali alikuwa amemwendea Yesu. Basi, yeye akawaambia,
John Swahili 7:51  "Je, Sheria yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza na kujua anafanya nini?"
John Swahili 7:52  Nao wakamjibu, "Je, wewe pia umetoka Galilaya? Haya, kayachunguze Maandiko Matakatifu nawe utaona kwamba Galilaya hakutoki kamwe nabii!"
Chapter 8
John Swahili 8:2  Kesho yake asubuhi na mapema alikwenda tena Hekaluni. Watu wote wakamwendea, naye akaketi akawa anawafundisha.
John Swahili 8:3  Basi, walimu wa Sheria na Mafarisayo wakamletea mwanamke mmoja aliyefumaniwa katika uzinzi. Wakamsimamisha katikati yao.
John Swahili 8:4  Kisha wakamwuliza Yesu, "Mwalimu! Mwanamke huyu alifumaniwa katika uzinzi.
John Swahili 8:5  Katika Sheria yetu Mose alituamuru mwanamke kama huyu apigwe mawe. Basi, wewe wasemaje?"
John Swahili 8:6  Walisema hivyo kumjaribu, wapate kisa cha kumshtaki. Lakini Yesu akainama chini, akaandika ardhini kwa kidole.
John Swahili 8:7  Walipozidi kumwuliza, Yesu akainuka, akawaambia, "Mtu asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza kumpiga jiwe."
John Swahili 8:9  Waliposikia hivyo, wakaanza kutoweka mmojammoja, wakitanguliwa na wazee. Yesu akabaki peke yake, na yule mwanamke amesimama palepale.
John Swahili 8:10  Yesu alipoinuka akamwuliza huyo mwanamke, "Wako wapi wale watu? Je, hakuna hata mmoja aliyekuhukumu?"
John Swahili 8:11  Huyo mwanamke akamjibu, "Mheshimiwa, hakuna hata mmoja!" Naye Yesu akamwambia, "Wala mimi sikuhukumu. Nenda zako; na tangu sasa usitende dhambi tena."
John Swahili 8:12  Yesu alipozungumza nao tena, aliwaambia, "Mimi ndimi mwanga wa ulimwengu. Anayenifuata mimi hatembei kamwe gizani, bali atakuwa na mwanga wa uzima."
John Swahili 8:13  Basi, Mafarisayo wakamwambia, "Wewe unajishuhudia mwenyewe; kwa hiyo ushahidi wako si halali."
John Swahili 8:14  Yesu akawajibu, "Hata kama ninajishuhudia mwenyewe, ushahidi wangu ni wa kweli kwa sababu mimi najua nilikotoka na ninakokwenda. Lakini ninyi hamjui nilikotoka wala ninakokwenda.
John Swahili 8:15  Ninyi mnahukumu kwa fikira za kibinadamu, lakini mimi simhukumu mtu.
John Swahili 8:16  Hata nikihukumu, hukumu yangu ni ya haki kwa sababu mimi siko peke yangu; Baba aliyenituma yuko pamoja nami.
John Swahili 8:17  Imeandikwa katika Sheria yenu ya kwamba ushahidi wa watu wawili ni halali.
John Swahili 8:18  Mimi najishuhudia mwenyewe, naye Baba aliyenituma, ananishuhudia pia."
John Swahili 8:19  Hapo wakamwuliza, "Baba yako yuko wapi?" Yesu akawajibu "Ninyi hamnijui mimi wala hamumjui Baba. Kama mngenijua mimi, mngemjua na Baba yangu pia."
John Swahili 8:20  Yesu alisema maneno hayo kwenye chumba cha hazina alipokuwa anafundisha Hekaluni. Wala hakuna mtu aliyemtia nguvuni, kwa sababu saa yake ilikuwa haijafika bado.
John Swahili 8:21  Yesu akawaambia tena, "Naenda zangu nanyi mtanitafuta, lakini mtakufa katika dhambi zenu. Niendako mimi, ninyi hamwezi kufika."
John Swahili 8:22  Basi, viongozi wa Wayahudi wakasema, "Je, atajiua? Mbona anasema: Niendako ninyi hamwezi kufika?"
John Swahili 8:23  Yesu akawaambia, "Ninyi mmetoka papa hapa chini, mimi nimetoka juu; ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu.
John Swahili 8:24  Ndiyo maana niliwaambieni mtakufa katika dhambi zenu. Kama msipoamini kwamba Mimi ndimi, mtakufa katika dhambi zenu."
John Swahili 8:25  Nao wakamwuliza, "Wewe ni nani?" Yesu akawajibu, "Nimewaambieni tangu mwanzo!
John Swahili 8:26  Ninayo mengi ya kusema na kuhukumu juu yenu. Lakini yule aliyenituma ni kweli; nami nauambia ulimwengu mambo yale tu niliyoyasikia kutoka kwake."
John Swahili 8:27  Hawakuelewa kwamba Yesu alikuwa akisema nao juu ya Baba.
John Swahili 8:28  Basi, Yesu akawaambia, "Mtakapokwisha mwinua Mwana wa Mtu hapo ndipo mtakapojua kwamba Mimi ndimi, na kwamba sifanyi chochote mimi mwenyewe, ila nasema tu yale Baba aliyonifundisha.
John Swahili 8:29  Yule aliyenituma yuko pamoja nami; yeye hakuniacha peke yangu kwani nafanya daima yale yanayompendeza."
John Swahili 8:31  Basi, Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, "Kama mkiyazingatia mafundisho yangu mtakuwa kweli wanafunzi wangu.
John Swahili 8:33  Nao wakamjibu, "Sisi ni wazawa wa Abrahamu, na hatujapata kamwe kuwa watumwa wa mtu yeyote yule. Una maana gani unaposema: mtakuwa huru?"
John Swahili 8:34  Yesu akawajibu, "Kweli nawaambieni, kila mtu anayetenda dhambi ni mtumwa wa dhambi.
John Swahili 8:35  Mtumwa hana makao ya kudumu nyumbani, lakini mwana anayo makao ya kudumu.
John Swahili 8:37  Najua kwamba ninyi ni wazawa wa Abrahamu. Hata hivyo, mnataka kuniua kwa sababu hamuyakubali mafundisho yangu.
John Swahili 8:38  Mimi nasema yale aliyonionyesha Baba, lakini ninyi mwafanya yale aliyowaambieni baba yenu."
John Swahili 8:39  Wao wakamjibu, "Baba yetu ni Abrahamu!" Yesu akawaambia, "Kama ninyi mngekuwa watoto wa Abrahamu, mngefanya kama alivyofanya Abrahamu,
John Swahili 8:40  Mimi nimewaambieni ukweli niliousikia kwa Mungu; hata hivyo, ninyi mwataka kuniua. Abrahamu hakufanya hivyo!
John Swahili 8:41  Ninyi mnafanya mambo yaleyale aliyofanya babu yenu." Wao wakamwambia, "Sisi si watoto haramu! Tunaye baba mmoja tu, yaani Mungu."
John Swahili 8:42  Yesu akawaambia, "Kama Mungu angekuwa Baba yenu, mngenipenda mimi, maana mimi nilitoka kwa Mungu na sasa niko hapa. Sikuja kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila yeye alinituma.
John Swahili 8:43  Kwa nini hamwelewi hayo ninayosema? Ni kwa kuwa hamwezi kuusikiliza ujumbe wangu.
John Swahili 8:44  Ninyi ni watoto wa baba yenu Ibilisi na mnataka tu kutekeleza tamaa za baba yenu. Yeye alikuwa muuaji tangu mwanzo; hana msimamo katika ukweli, kwani ukweli haumo ndani yake. Kila asemapo uongo, husema kutokana na hali yake ya maumbile, maana yeye ni mwongo na baba wa uongo.
John Swahili 8:45  Mimi nasema ukweli, na ndiyo maana ninyi hamniamini.
John Swahili 8:46  Nani kati yenu awezaye kuthibitisha kuwa mimi nina dhambi? Ikiwa basi nasema ukweli, kwa nini hamniamini?
John Swahili 8:47  Aliye wa Mungu husikiliza maneno ya Mungu. Lakini ninyi hamsikilizi kwa sababu ninyi si (watu wa) Mungu."
John Swahili 8:48  Wayahudi wakamwambia, "Je, hatukusema kweli kwamba wewe ni Msamaria, na tena una pepo?"
John Swahili 8:49  Yesu akajibu, "Mimi sina pepo; mimi namheshimu Baba yangu, lakini ninyi hamniheshimu.
John Swahili 8:50  Mimi sijitafutii utukufu wangu mwenyewe; yuko mmoja mwenye kuutafuta utukufu huo, naye ni hakimu.
John Swahili 8:51  Kweli nawaambieni, anayeuzingatia ujumbe wangu hatakufa milele."
John Swahili 8:52  Basi, Wayahudi wakasema, "Sasa tunajua kweli kwamba wewe ni mwendawazimu! Abrahamu alikufa, na manabii pia walikufa, nawe wasema ati, Anayeuzingatia ujumbe wangu hatakufa milele!
John Swahili 8:53  Je, unajifanya mkuu zaidi kuliko baba yetu Abrahamu ambaye alikufa? Hata na manabii walikufa. Wewe unajifanya kuwa nani?"
John Swahili 8:54  Yesu akawajibu, "Nikijitukuza mwenyewe, utukufu wangu si kitu. Baba yangu ambaye ninyi mwasema ni Baba yenu, ndiye anayenitukuza.
John Swahili 8:55  Ninyi hamjapata kumjua, lakini mimi namjua. Na, nikisema simjui, nitakuwa mwongo kama ninyi. Mimi namjua na ninashika neno lake.
John Swahili 8:56  Abrahamu, baba yenu, alishangilia aione siku yangu; naye aliiona, akafurahi."
John Swahili 8:57  Basi, Wayahudi wakamwambia, "Wewe hujatimiza miaka hamsini bado, nawe umemwona Abrahamu?"
John Swahili 8:58  Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, kabla Abrahamu hajazaliwa, mimi niko."
John Swahili 8:59  Hapo wakaokota mawe ili wamtupie, lakini Yesu akajificha, akatoka Hekaluni.
Chapter 9
John Swahili 9:1  Yesu alipokuwa akipita alimwona mtu mmoja, kipofu tangu kuzaliwa.
John Swahili 9:2  Basi, wanafunzi wakamwuliza, "Mwalimu! Ni nani aliyetenda dhambi: mtu huyu, ama wazazi wake, hata akazaliwa kipofu?"
John Swahili 9:3  Yesu akajibu, "Jambo hili halikutukia kwa sababu ya dhambi zake yeye, wala dhambi za wazazi wake; ila alizaliwa kipofu ili nguvu ya Mungu ionekane ikifanya kazi ndani yake.
John Swahili 9:4  Kukiwa bado mchana yatupasa kuendelea kufanya kazi za yule aliyenituma; maana usiku unakuja ambapo mtu hawezi kufanya kazi.
John Swahili 9:5  Wakati ningali ulimwenguni, mimi ni mwanga wa ulimwengu."
John Swahili 9:6  Baada ya kusema hayo, akatema mate chini, akafanyiza tope, akampaka yule kipofu machoni,
John Swahili 9:7  akamwambia, "Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu." (maana ya jina hili ni "aliyetumwa"). Basi, huyo kipofu akaenda, akanawa, kisha akarudi akiwa anaona.
John Swahili 9:8  Basi, jirani zake na wale waliokuwa wanajua kwamba hapo awali alikuwa maskini mwombaji, wakasema, "Je, huyu siye yule maskini aliyekuwa akiketi na kuomba?"
John Swahili 9:9  Baadhi yao wakasema, "Ndiye." Wengine wakasema, "La! Ila anafanana naye." Lakini huyo aliyekuwa kipofu akasema, "Ni mimi!"
John Swahili 9:10  Basi, wakamwuliza, "Sasa, macho yako yalipataje kufumbuliwa?"
John Swahili 9:11  Naye akawajibu, "Yule mtu aitwaye Yesu alifanya tope, akanipaka machoni na kuniambia: Nenda ukanawe katika bwawa la Siloamu. Basi, mimi nikaenda, nikanawa, nikapata kuona."
John Swahili 9:12  Wakamwuliza, "Yeye yuko wapi?" Naye akawajibu, "Mimi sijui!"
John Swahili 9:13  Kisha wakampeleka huyo mtu aliyekuwa kipofu kwa Mafarisayo.
John Swahili 9:14  Siku hiyo Yesu alipofanya tope na kumfumbua macho mtu huyo, ilikuwa siku ya Sabato.
John Swahili 9:15  Basi, Mafarisayo wakamwuliza mtu huyo, "Umepataje kuona?" Naye akawaambia, "Alinipaka tope machoni, nami nikanawa na sasa naona."
John Swahili 9:16  Baadhi ya Mafarisayo wakasema, "Mtu huyu hakutoka kwa Mungu, maana hashiki sheria ya Sabato." Lakini wengine wakasema, "Mtu mwenye dhambi awezaje kufanya ishara za namna hii?" Kukawa na mafarakano kati yao.
John Swahili 9:17  Wakamwuliza tena huyo mtu aliyekuwa kipofu, "Maadam yeye amekufungua macho, wasemaje juu yake?" Naye akawaambia, "Yeye ni nabii!"
John Swahili 9:18  Viongozi wa Wayahudi hawakusadiki kwamba mtu huyo alikuwa kipofu hapo awali na sasa anaona mpaka walipowaita wazazi wake.
John Swahili 9:19  Basi, wakawauliza hao wazazi, "Je, huyu ndiye mtoto wenu ambaye ninyi mwasema alizaliwa kipofu? Sasa amepataje kuona?"
John Swahili 9:20  Wazazi wake wakajibu, "Tunajua kwamba huyu ni mtoto wetu, na kwamba alizaliwa kipofu.
John Swahili 9:21  Lakini amepataje kuona, hatujui; na wala hatumjui yule aliyemfumbua macho. Mwulizeni yeye mwenyewe; yeye ni mtu mzima, anaweza kujitetea mwenyewe."
John Swahili 9:22  Wazazi wake walisema hivyo kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Wayahudi kwani viongozi hao walikuwa wamepatana ya kwamba mtu yeyote atakayekiri kwamba Yesu ni Kristo atafukuzwa nje ya sunagogi.
John Swahili 9:23  Ndiyo maana wazazi wake walisema: "Yeye ni mtu mzima, mwulizeni."
John Swahili 9:24  Basi, wakamwita tena aliyekuwa kipofu, wakamwambia, "Sema ukweli mbele ya Mungu! Sisi tunajua kwamba mtu huyu ni mwenye dhambi."
John Swahili 9:25  Yeye akajibu, "Kama ni mwenye dhambi mimi sijui. Lakini kitu kimoja najua: Nilikuwa kipofu, na sasa naona."
John Swahili 9:26  Basi, wakamwuliza, "Alikufanyia nini? Alikufumbuaje macho yako?"
John Swahili 9:27  Huyo mtu akawajibu, "Nimekwisha waambieni, nanyi hamkusikiliza; kwa nini mwataka kusikia tena? Je, ninyi pia mnataka kuwa wafuasi wake?"
John Swahili 9:28  Lakini wao wakamtukana wakisema, "Wewe ni mfuasi wake; sisi ni wafuasi wa Mose.
John Swahili 9:29  Sisi tunajua kwamba Mungu alisema na Mose, lakini mtu huyu hatujui ametoka wapi!"
John Swahili 9:30  Naye akawajibu, "Hili ni jambo la kushangaza! Ninyi hamjui ametoka wapi, lakini amenifumbua macho yangu!
John Swahili 9:31  Tunajua kwamba Mungu hawasikilizi watu wenye dhambi, ila humsikiliza yeyote mwenye kumcha na kutimiza mapenzi yake.
John Swahili 9:32  Tangu mwanzo wa ulimwengu haijasikika kwamba mtu ameyafumbua macho ya mtu aliyezaliwa kipofu.
John Swahili 9:33  Kama mtu huyu hakutoka kwa Mungu, hangeweza kufanya chochote!"
John Swahili 9:34  Wao wakamjibu, "Wewe ulizaliwa na kulelewa katika dhambi; unawezaje kutufundisha sisi?" Basi, wakamfukuzia mbali.
John Swahili 9:35  Yesu alisikia kwamba walikuwa wamemfukuzia mbali, naye alipomkuta akamwuliza, "Je, wewe unamwamini Mwana wa Mtu?"
John Swahili 9:36  Huyo mtu akajibu, "Mheshimiwa, niambie yeye ni nani, ili nipate kumwamini."
John Swahili 9:37  Yesu akamwambia, "Umekwisha mwona, naye ndiye anayesema nawe sasa."
John Swahili 9:38  Basi, huyo mtu akasema, "Ninaamini Bwana!" Akamsujudia.
John Swahili 9:39  Yesu akasema, "Mimi nimekuja ulimwenguni kutoa hukumu, kusudi wasioona wapate kuona, na wale wanaoona wawe vipofu."
John Swahili 9:40  Baadhi ya Mafarisayo waliokuwa pamoja naye walisikia maneno hayo, wakamwuliza, "Je, sisi pia ni vipofu?"
John Swahili 9:41  Yesu akawajibu, "Kama mngekuwa vipofu, hamngekuwa na hatia; lakini sasa ninyi mwasema: Sisi tunaona, na hiyo yaonyesha kwamba mna hatia bado.
Chapter 10
John Swahili 10:1  Yesu alisema "Kweli nawaambieni, yeyote yule asiyeingia katika zizi la kondoo kwa kupitia mlangoni, bali hupenya na kuingia kwa njia nyingine, huyo ni mwizi na mnyang'anyi.
John Swahili 10:2  Lakini anayeingia kwa kupitia mlangoni, huyo ndiye mchungaji wa kondoo.
John Swahili 10:3  Mngoja mlango wa zizi humfungulia, na kondoo husikia sauti yake, naye huwaita kondoo wake kila mmoja kwa jina lake na kuwaongoza nje.
John Swahili 10:4  Akisha watoa nje huwatangulia mbele nao kondoo humfuata, kwani wanaijua sauti yake.
John Swahili 10:5  Kondoo hao hawawezi kumfuata mgeni, bali watamkimbia kwa sababu hawaijui sauti yake."
John Swahili 10:6  Yesu aliwaambia mfano huo, lakini wao hawakuelewa alichotaka kuwaambia.
John Swahili 10:7  Basi, akasema tena, "Kweli nawaambieni, mimi ni mlango wa kondoo.
John Swahili 10:8  Wale wengine wote waliokuja kabla yangu ni wezi na wanyang'anyi, nao kondoo hawakuwasikiliza.
John Swahili 10:9  Mimi ni mlango. Anayeingia kwa kupitia kwangu ataokolewa; ataingia na kutoka, na kupata malisho.
John Swahili 10:10  Mwizi huja kwa shabaha ya kuiba, kuua na kuharibu. Mimi nimekuja mpate kuwa na uzima--uzima kamili.
John Swahili 10:11  "Mimi ni mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake.
John Swahili 10:12  Mtu wa kuajiriwa ambaye si mchungaji, na wala kondoo si mali yake, anapoona mbwa mwitu anakuja, huwaacha kondoo na kukimbia. Kisha mbwa mwitu huwakamata na kuwatawanya.
John Swahili 10:13  Yeye hajali kitu juu ya kondoo kwa sababu yeye ni mtu wa mshahara tu.
John Swahili 10:14  Mimi ni mchungaji mwema. Nawajua walio wangu, nao walio wangu wananijua mimi,
John Swahili 10:15  kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Mimi nayatoa maisha yangu kwa ajili yao.
John Swahili 10:16  Tena ninao kondoo wengine ambao hawamo zizini humu. Inanibidi kuwaleta hao pia, nao wataisikia sauti yangu, na kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja.
John Swahili 10:17  "Baba ananipenda kwani nautoa uhai wangu ili nipate kuupokea tena.
John Swahili 10:18  Hakuna mtu anayeninyang'anya uhai wangu; mimi na nautoa kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa na uwezo wa kuuchukua tena. Hivi ndivyo Baba alivyoniamuru nifanye."
John Swahili 10:19  Kukawa tena na mafarakano kati ya Wayahudi kwa sababu ya maneno haya.
John Swahili 10:20  Wengi wao wakasema, "Ana pepo; tena ni mwendawazimu! Ya nini kumsikiliza?"
John Swahili 10:21  Wengine wakasema, "Haya si maneno ya mwenye pepo. Je, pepo anaweza kuyafumbua macho ya vipofu?"
John Swahili 10:22  Huko Yerusalemu kulikuwa na sikukuu ya Kutabaruku. Wakati huo ulikuwa wa baridi.
John Swahili 10:23  Naye Yesu akawa anatembea Hekaluni katika ukumbi wa Solomoni.
John Swahili 10:24  Basi, Wayahudi wakamzunguka, wakamwuliza, "Utatuacha katika mashaka mpaka lini? Kama wewe ndiye Kristo, basi, tuambie wazi."
John Swahili 10:25  Yesu akawajibu, "Nimewaambieni, lakini hamsadiki. Kazi ninazozifanya mimi kwa jina la Baba yangu zinanishuhudia.
John Swahili 10:26  Lakini ninyi hamsadiki kwa sababu ninyi si kondoo wangu.
John Swahili 10:27  Kondoo wangu huisikia sauti yangu; mimi nawajua, nao hunifuata.
John Swahili 10:28  Mimi nawapa uzima wa milele; nao hawatapotea milele, wala hakuna mtu atakayeweza kuwatoa mkononi mwangu.
John Swahili 10:29  Baba yangu ambaye ndiye aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote, wale hakuna awezaye kuwatoa mikononi mwake Baba.
John Swahili 10:32  Yesu akawaambia, "Nimewaonyesheni kazi nyingi kutoka kwa Baba. Ni ipi kati ya hizo inayowafanya mnipige mawe?"
John Swahili 10:33  Wayahudi wakamjibu, "Hatukupigi mawe kwa ajili ya tendo jema, ila kwa sababu ya kukufuru! Maana wajifanya kuwa Mungu hali wewe ni binadamu tu."
John Swahili 10:34  Yesu akawajibu, "Je, haikuandikwa katika Sheria yenu: Mimi nimesema, ninyi ni miungu?
John Swahili 10:35  Mungu aliwaita miungu wale waliopewa neno lake; nasi twajua kwamba Maandiko Matakatifu yasema ukweli daima.
John Swahili 10:36  Je, yeye ambaye Baba alimweka wakfu na kumtuma ulimwenguni, mnamwambia: Unakufuru, eti kwa sababu nilisema: Mimi ni Mwana wa Mungu?
John Swahili 10:38  Lakini ikiwa ninazifanya, hata kama hamniamini, walau ziaminini hizo kazi mpate kujua na kutambua kwamba Baba yuko ndani yangu, nami niko ndani yake."
John Swahili 10:39  Wakajaribu tena kumkamata lakini akachopoka mikononi mwao.
John Swahili 10:40  Yesu akaenda tena ng'ambo ya mto Yordani, mahali Yohane alipokuwa akibatiza, akakaa huko.
John Swahili 10:41  Watu wengi walimwendea wakasema, "Yohane hakufanya ishara yoyote. Lakini yale yote Yohane aliyosema juu ya mtu huyu ni kweli kabisa."
Chapter 11
John Swahili 11:1  Mtu mmoja aitwaye Lazaro, mwenyeji wa Bethania, alikuwa mgonjwa. (Kijiji cha Bethania kilikuwa mahali walipokaa Maria na Martha, dada yake.
John Swahili 11:2  Maria ndiye yule aliyempaka Bwana marashi na kumpangusa kwa nywele zake. Lazaro, kaka yake, ndiye aliyekuwa mgonjwa.)
John Swahili 11:3  Basi, hao dada wakatuma ujumbe huu kwa Yesu: "Bwana, rafiki yako ni mgonjwa!"
John Swahili 11:4  Yesu aliposikia hivyo akasema, "Ugonjwa huo hautaleta kifo, ila ni kwa ajili ya kumtukuza Mungu; ameugua ili kwa njia hiyo Mwana wa Mungu atukuzwe."
John Swahili 11:6  Alipopata habari kwamba Lazaro ni mgonjwa, Yesu aliendelea kukaa mahali hapo alipokuwa kwa siku mbili zaidi.
John Swahili 11:7  Kisha akawaambia wanafunzi wake, "Twendeni tena Yudea!"
John Swahili 11:8  Wanafunzi wakamwambia, "Mwalimu! Muda mfupi tu umepita tangu Wayahudi walipotaka kukuua kwa mawe, nawe unataka kwenda huko tena?"
John Swahili 11:9  Yesu akajibu, "Je, saa za mchana si kumi na mbili? Basi, mtu akitembea mchana hawezi kujikwaa kwa kuwa anauona mwanga wa ulimwengu huu.
John Swahili 11:10  Lakini mtu akitembea usiku atajikwaa kwa maana mwanga haumo ndani yake."
John Swahili 11:11  Yesu alipomaliza kusema maneno hayo, akawaambia, "Rafiki yetu Lazaro amelala, lakini mimi nitakwenda kumwamsha."
John Swahili 11:12  Wanafunzi wake wakamwambia, "Bwana, ikiwa amelala, basi atapona."
John Swahili 11:13  Wao walidhani kwamba alikuwa amesema juu ya kulala usingizi, kumbe alikuwa amesema juu ya kifo cha Lazaro.
John Swahili 11:15  Lakini nafurahi kwa ajili yenu kwamba sikuwako huko, ili mpate kuamini. Haya, twendeni kwake."
John Swahili 11:16  Thoma (aitwaye Pacha) akawaambia wanafunzi wenzake, "Twendeni nasi tukafe pamoja naye!"
John Swahili 11:17  Yesu alipofika huko alikuta Lazaro amekwisha kaa kaburini kwa siku nne.
John Swahili 11:18  Kijiji cha Bethania kilikuwa karibu na Yerusalemu umbali upatao kilomita tatu.
John Swahili 11:19  Wayahudi wengi walikuwa wamefika kwa Martha na Maria kuwafariji kwa kifo cha kaka yao.
John Swahili 11:20  Basi, Martha aliposikia kwamba Yesu alikuwa anakuja, akaenda kumlaki; lakini Maria alibaki nyumbani.
John Swahili 11:21  Martha akamwambia Yesu, "Bwana, kama ungalikuwa hapa, kaka yangu hangalikufa!
John Swahili 11:22  Lakini najua kwamba hata sasa chochote utakachomwomba Mungu, atakupa."
John Swahili 11:24  Martha akamjibu, "Najua kwamba atafufuka wakati wa ufufuo, siku ya mwisho."
John Swahili 11:25  Yesu akamwambia, "Mimi ndimi ufufuo na uzima. Anayeniamini mimi hata kama anakufa, ataishi:
John Swahili 11:26  na kila anayeishi na kuniamini, hatakufa kamwe. Je, waamini hayo?"
John Swahili 11:27  Martha akamwambia, "Ndiyo Bwana! Naamini kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu, yule ajaye ulimwenguni."
John Swahili 11:28  Baada ya kusema hayo, Martha alikwenda kumwita Maria, dada yake, akamwabia faraghani, "Mwalimu yuko hapa, anakuita."
John Swahili 11:29  Naye aliposikia hivyo, akainuka mara, akamwendea Yesu.
John Swahili 11:30  Yesu alikuwa hajaingia kijijini, ila alikuwa bado mahali palepale Martha alipomlaki.
John Swahili 11:31  Basi, Wayahudi waliokuwa nyumbani pamoja na Maria wakimfariji walipomwona ameinuka na kutoka nje ghafla, walimfuata. Walidhani alikuwa anakwenda kaburini kuomboleza.
John Swahili 11:32  Basi, Maria alipofika mahali pale Yesu alipokuwa na kumwona, alipiga magoti, akamwabia, "Bwana, kama ungalikuwa hapa, kaka yangu hangalikufa!"
John Swahili 11:33  Yesu alipomwona analia, na wale Wayahudi waliokuja pamoja naye wanalia pia, alijawa na huzuni na kufadhaika moyoni.
John Swahili 11:34  Kisha akawauliza, "Mlimweka wapi?" Wakamwambia, "Bwana, njoo uone."
John Swahili 11:36  Basi, Wayahudi wakasema, "Tazameni jinsi alivyompenda!"
John Swahili 11:37  Lakini baadhi yao wakasema, "Je, huyu aliyemfumbua macho yule kipofu, hakuweza kumfanya Lazaro asife?"
John Swahili 11:38  Basi, Yesu akiwa amehuzunika tena moyoni, akafika kaburini. Kaburi lenyewe lilikuwa pango, na lilikuwa limefunikwa kwa jiwe.
John Swahili 11:39  Yesu akasema, "Ondoeni hilo jiwe!" Martha, dada yake huyo aliyekufa, akamwambia, "Bwana, amekwishaanza kunuka; amekaa kaburini siku nne!"
John Swahili 11:40  Yesu akamwambia, "Je, sikukwambia kwamba ukiamini utaona utukufu wa Mungu?"
John Swahili 11:41  Basi, wakaliondoa lile jiwe. Yesu akatazama juu mbinguni, akasema, "Nakushukuru Baba kwa kuwa wewe wanisikiliza.
John Swahili 11:42  Najua kwamba unanisikiliza daima. Lakini nimesema hayo kwa ajili ya watu hawa waliopo hapa ili wapate kuamini kwamba wewe ndiwe uliyenituma."
John Swahili 11:43  Alipokwisha sema hayo, akaita kwa sauti kubwa: "Lazaro! Toka nje!"
John Swahili 11:44  Huyo aliyekuwa amekufa akatoka nje, huku amefungwa sanda miguu na mikono, na uso wake umefunikwa. Yesu akawaambia, "Mfungueni, mkamwache aende zake."
John Swahili 11:45  Basi, Wayahudi wengi waliokuwa wamefika kwa Maria walipoona kitendo hicho alichokifanya Yesu wakamwamini.
John Swahili 11:46  Lakini baadhi yao walikwenda kwa Mafarisayo wakatoa taarifa ya jambo hilo alilofanya Yesu.
John Swahili 11:47  kwa hiyo makuhani wakuu na Mafarisayo wakafanya kikao cha Baraza kuu, wakasema, "Tufanye nini? Mtu huyu anafanya ishara nyingi mno.
John Swahili 11:48  Tukimwacha tu watu wote watamwamini, nao Waroma watakuja kuliharibu Hekalu letu na taifa letu!"
John Swahili 11:49  Hapo, mmoja wao aitwaye Kayafa, ambaye alikuwa Kuhani Mkuu mwaka huo, akawaambia, "Ninyi hamjui kitu!
John Swahili 11:50  Je, hamwoni kwamba ni afadhali kwenu mtu mmoja afe kwa ajili ya watu, kuliko taifa zima liangamizwe?"
John Swahili 11:51  Yeye hakusema hivyo kwa hiari yake mwenyewe, bali kwa vile alikuwa Kuhani Mkuu mwaka huo, alibashiri kwamba Yesu atakufa kwa ajili ya taifa lao;
John Swahili 11:52  na wala si kwa ajili yao tu, bali pia apate kuwaleta pamoja watoto wa Mungu waliotawanyika.
John Swahili 11:53  Basi, tangu siku hiyo viongozi wa Wayahudi walifanya mipango ya kumwua Yesu.
John Swahili 11:54  Kwa hiyo, Yesu hakutembea tena hadharani kati ya Wayahudi, bali alitoka hapo, akaenda mahali karibu na jangwa, katika mji uitwao Efraimu. Akakaa huko pamoja na wanafunzi wake.
John Swahili 11:55  Sikukuu ya Wayahudi ya Pasaka ilikuwa karibu, na watu wengi walikwenda Yerusalemu ili wajitakase kabla ya sikukuu hiyo.
John Swahili 11:56  Basi, wakawa wanamtafuta Yesu; nao walipokusanyika pamoja Hekaluni wakaulizana, "Mwaonaje? Yaonekana kwamba haji kabisa kwenye sikukuu, au sivyo?"
John Swahili 11:57  Makuhani wakuu na Mafarisayo walikuwa wametoa amri kwamba mtu akijua mahali aliko Yesu awaarifu kusudi wamtie nguvuni.
Chapter 12
John Swahili 12:1  Siku sita kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu alifika Bethania alikoishi Lazaro ambaye Yesu alikuwa amemfufua kutoka wafu.
John Swahili 12:2  Huko walimwandalia chakula cha jioni, naye Martha akawa anawatumikia. Lazaro alikuwa mmoja wa wale waliokuwa mezani pamoja na Yesu.
John Swahili 12:3  Basi, Maria alichukua chupa ya marashi ya nardo safi ya thamani kubwa, akampaka Yesu miguu na kuipangusa kwa nywele zake. Nyumba yote ikajaa harufu ya marashi.
John Swahili 12:4  Basi, Yuda Iskarioti, mmoja wa wale kumi na wawili ambaye ndiye atakayemsaliti Yesu, akasema,
John Swahili 12:5  "Kwa nini marashi hayo hayakuuzwa kwa fedha dinari mia tatu, wakapewa maskini?"
John Swahili 12:6  Alisema hivyo, si kwa kuwa alijali chochote juu ya maskini, bali kwa sababu alikuwa mweka hazina, na kwa kuwa alikuwa mwizi, mara kwa mara aliiba kutoka katika hiyo hazina.
John Swahili 12:7  Lakini Yesu akasema, "Msimsumbue huyu mama! Mwacheni ayaweke kwa ajili ya siku ya mazishi yangu.
John Swahili 12:8  Maskini mtakuwa nao siku zote, lakini hamtakuwa nami siku zote."
John Swahili 12:9  Wayahudi wengi walisikia kwamba Yesu alikuwa Bethania. Basi, wakafika huko si tu kwa ajili ya kumwona Yesu, ila pia wapate kumwona Lazaro ambaye Yesu alimfufua kutoka wafu.
John Swahili 12:11  Maana kwa sababu ya Lazaro Wayahudi wengi waliwaasi viongozi wao, wakamwamini Yesu.
John Swahili 12:12  Kesho yake, kundi kubwa la watu waliokuja kwenye sikukuu walisikia kuwa Yesu alikuwa njiani kuja Yerusalemu.
John Swahili 12:13  Basi, wakachukua matawi ya mitende, wakatoka kwenda kumlaki; wakapaaza sauti wakisema: "Hosana! Abarikiwe huyo ajaye kwa jina la Bwana. Abarikiwe mfalme wa Israeli."
John Swahili 12:14  Yesu akampata mwana punda mmoja akapanda juu yake kama yasemavyo Maandiko:
John Swahili 12:15  "Usiogope mji wa Sioni! Tazama, Mfalme wako anakuja, Amepanda mwana punda."
John Swahili 12:16  Wakati huo wanafunzi wake hawakuelewa mambo hayo, lakini Yesu alipokwisha tukuzwa, ndipo walipokumbuka kwamba hayo yalikuwa yameandikwa juu yake, na kwamba watu walikuwa wamemtendea hivyo.
John Swahili 12:17  Kundi la watu wale waliokuwa pamoja naye wakati alipomwita Lazaro kutoka kaburini, akamfufua kutoka wafu, walisema yaliyotukia.
John Swahili 12:18  Kwa hiyo umati huo wa watu ulimlaki, maana wote walisikia kwamba Yesu alikuwa amefanya ishara hiyo.
John Swahili 12:19  Basi, Mafarisayo wakaambiana, "Mnaona? Hatuwezi kufanya chochote! Tazameni, ulimwengu wote unamfuata."
John Swahili 12:20  Kulikuwa na Wagiriki kadhaa miongoni mwa watu waliokuwa wamefika Yerusalemu kuabudu wakati wa sikukuu hiyo.
John Swahili 12:21  Hao walimwendea Filipo, mwenyeji wa Bethsaida katika Galilaya, wakasema, "Mheshimiwa, tunataka kumwona Yesu."
John Swahili 12:22  Filipo akaenda akamwambia Andrea, nao wawili wakaenda kumwambia Yesu.
John Swahili 12:23  Yesu akawaambia, "Saa ya kutukuzwa kwa Mwana wa Mtu imefika!
John Swahili 12:24  Kweli nawaambieni, punje ya ngano hubaki punje tu isipokuwa ikianguka katika udongo na kufa. Kama ikifa, basi huzaa matunda mengi.
John Swahili 12:25  Anayependa maisha yake, atayapoteza; anayeyachukia maisha yake katika ulimwengu huu, atayaweka kwa ajili ya uzima wa milele.
John Swahili 12:26  Anayetaka kunitumikia ni lazima anifuate, hivyo kwamba popote pale nilipo mimi ndipo na mtumishi wangu atakapokuwa. Mtu yeyote anayenitumikia Baba yangu atampa heshima.
John Swahili 12:27  "Sasa roho yangu imefadhaika, na niseme nini? Je, niseme: Baba, usiruhusu saa hii inifikie? Lakini ndiyo maana nimekuja--ili nipite katika saa hii.
John Swahili 12:28  Baba, ulitukuze jina lako." Hapo sauti ikasema kutoka mbinguni, "Nimelitukuza, na nitalitukuza tena."
John Swahili 12:29  Umati wa watu waliokuwa wamesimama hapo walisikia sauti hiyo, na baadhi yao walisema, "Malaika ameongea naye!"
John Swahili 12:30  Lakini Yesu akawaambia, "Sauti hiyo haikutokea kwa ajili yangu mimi, ila kwa ajili yenu.
John Swahili 12:31  Sasa ndio wakati wa ulimwengu huu kuhukumiwa; sasa mtawala wa ulimwengu huu atapinduliwa.
John Swahili 12:32  Nami nitakapoinuliwa juu ya nchi nitamvuta kila mmoja kwangu."
John Swahili 12:34  Basi, umati huo ukamjibu, "Sisi tunaambiwa na Sheria yetu kwamba Kristo atadumu milele. Wawezaje basi, kusema ati Mwana wa Mtu anapaswa kuinuliwa? Huyo Mwana wa Mtu ni nani?"
John Swahili 12:35  Yesu akawaambia, "Mwanga bado uko nanyi kwa muda mfupi. Tembeeni mngali mnao huo mwanga ili giza lisiwapate; maana atembeaye gizani hajui aendako.
John Swahili 12:36  Basi, wakati mnao huo mwanga uaminini ili mpate kuwa watu wa mwanga." Baada ya kusema maneno hayo, Yesu alikwenda zake na kujificha mbali nao.
John Swahili 12:37  Ingawa Yesu alifanya miujiza hii yote mbele yao, wao hawakumwamini.
John Swahili 12:38  Hivyo maneno aliyosema nabii Isaya yakatimia: "Bwana, nani aliyeuamini ujumbe wetu? Na uwezo wa Bwana umedhihirishwa kwa nani?"
John Swahili 12:39  Hivyo hawakuweza kuamini, kwani Isaya tena alisema:
John Swahili 12:40  "Mungu ameyapofusha macho yao, amezipumbaza akili zao; wasione kwa macho yao, wasielewe kwa akili zao; wala wasinigeukie, asema Bwana, ili nipate kuwaponya."
John Swahili 12:41  Isaya alisema maneno haya kwa sababu aliuona utukufu wa Yesu, akasema habari zake.
John Swahili 12:42  Hata hivyo, wengi wa viongozi wa Wayahudi walimwamini Yesu. Lakini kwa sababu ya Mafarisayo, hawakumkiri hadharani kwa kuogopa kwamba watatengwa na sunagogi.
John Swahili 12:43  Walipendelea kusifiwa na watu kuliko kusifiwa na Mungu
John Swahili 12:44  Kisha Yesu akasema kwa sauti kubwa, "Mtu aliyeniamini, haniamini mimi tu, ila anamwamini pia yule aliyenituma.
John Swahili 12:46  Mimi ni mwanga, nami nimekuja ulimwenguni ili wote wanaoniamini wasibaki gizani.
John Swahili 12:47  Anayeyasikia maneno yangu lakini hayashiki mimi sitamhukumu; maana sikuja kuhukumu ulimwengu bali kuuokoa.
John Swahili 12:48  Asiyeyashika maneno yangu anaye wa kumhukumu: neno lile nililosema ni hakimu wake siku ya mwisho.
John Swahili 12:49  Mimi sikunena kwa mamlaka yangu mwenyewe, ila Baba aliyenituma ndiye aliyeniamuru niseme nini na niongee nini.
John Swahili 12:50  Nami najua kuwa amri yake huleta uzima wa milele. Basi, mimi nasema tu yale Baba aliyoniagiza niyaseme."
Chapter 13
John Swahili 13:1  Ilikuwa kabla ya sikukuu ya Pasaka. Yesu alijua kwamba saa yake ya kuondoka ulimwenguni na kwenda kwa Baba ilikuwa imefika. Alikuwa amewapenda daima watu wake walioko duniani; naam, aliwapenda mpaka mwisho!
John Swahili 13:2  Basi, Yesu na wanafunzi wake walikuwa mezani kwa chakula cha jioni. Ibilisi alikwisha mtia Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti, nia ya kumsaliti Yesu.
John Swahili 13:3  Yesu alijua kwamba Baba alikuwa amemkabidhi kila kitu, na kwamba alikuwa ametoka kwa Mungu na anarudi kwa Mungu.
John Swahili 13:4  Basi, Yesu aliondoka mezani, akaweka kando vazi lake, akachukua kitambaa na kujifunga kiunoni.
John Swahili 13:5  Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwaosha wanafunzi wake miguu na kuipangusa kwa kile kitambaa alichojifungia.
John Swahili 13:6  Basi, akamfikia Simoni Petro; naye Petro akasema, "Bwana, wewe utaniosha miguu mimi?"
John Swahili 13:7  Yesu akamjibu, "Huelewi sasa ninachofanya lakini utaelewa baadaye."
John Swahili 13:8  Petro akamwambia, "Wewe hutaniosha miguu kamwe!" Yesu akamjibu, "Nisipokuosha hutakuwa na uhusiano nami tena."
John Swahili 13:9  Simoni Petro akamwambia, "Bwana, nioshe, si miguu tu, bali na mikono yangu na kichwa pia."
John Swahili 13:10  Yesu akamwambia, "Aliyekwisha oga hana lazima ya kunawa isipokuwa miguu, maana amekwisha takata mwili wote. Ninyi mmetakata, lakini si nyote."
John Swahili 13:11  (Yesu alimjua yule ambaye atamsaliti, ndiyo maana alisema: "Ninyi mmetakata, lakini si nyote.")
John Swahili 13:12  Alipokwisha waosha miguu na kuvaa tena vazi lake, aliketi mezani, akawaambia, "Je, mmeelewa hayo niliyowatendeeni?
John Swahili 13:13  Ninyi mwaniita Mwalimu na Bwana, nanyi mwasema vyema, kwa kuwa ndimi.
John Swahili 13:14  Basi, ikiwa mimi niliye Bwana na Mwalimu, nimewaosha ninyi miguu, nanyi pia mnapaswa kuoshana miguu.
John Swahili 13:15  Nimewapeni mfano, ili nanyi pia mfanye kama nilivyowafanyieni.
John Swahili 13:16  Kweli nawaambieni, mtumishi si mkuu zaidi kuliko bwana wake, wala mtume si mkuu zaidi kuliko yule aliyemtuma.
John Swahili 13:17  Basi, ikiwa mwayajua hayo, mtakuwa na heri mkiyatekeleza.
John Swahili 13:18  "Haya nisemayo hayawahusu ninyi nyote. Mimi nawajua wale niliowachagua. Lakini lazima yatimie Maandiko Matakatifu yasemayo: Yule aliyeshiriki chakula changu amegeuka kunishambulia.
John Swahili 13:19  Mimi nimewaambieni mambo haya sasa kabla hayajatokea, ili yatakapotokea mpate kuamini kuwa mimi ndimi.
John Swahili 13:20  Kweli nawaambieni anayempokea yule ninayemtuma anaponipokea mimi; na anayenipokea mimi, anampokea yule aliyenituma."
John Swahili 13:21  Alipokwisha sema hayo, Yesu alifadhaika sana rohoni, akasema wazi, "Kweli nawaambieni, mmoja wenu atanisaliti!"
John Swahili 13:22  Wanafunzi wakatazama wasiweze kabisa kujua anasema nani.
John Swahili 13:23  Mmoja wa wanafunzi, ambaye Yesu alikuwa anampenda sana, alikuwa ameketi karibu na Yesu.
John Swahili 13:24  Basi, Simoni Petro akamwashiria na kusema: "Mwulize anasema juu ya nani."
John Swahili 13:25  Mwanafunzi huyo akasogea karibu zaidi na Yesu, akamwuliza, "Bwana, ni nani?"
John Swahili 13:26  Yesu akajibu, "Yule nitakayempa kipande cha mkate nilichochovya katika sahani, ndiye." Basi, akatwaa kipande cha mkate, akakichovya katika sahani, akampa Yuda, mwana wa Simoni Iskarioti.
John Swahili 13:27  Yuda alipokwisha pokea kipande hicho, Shetani akamwingia. Basi Yesu akamwambia, "Unachotaka kufanya, kifanye haraka!"
John Swahili 13:28  Lakini hakuna hata mmoja wa wale waliokaa pale mezani aliyefahamu kwa nini alikuwa amemwambia hivyo.
John Swahili 13:29  Kwa kuwa Yuda alikuwa na wajibu wa kuutunza mfuko wa fedha, baadhi yao walidhani kwamba Yesu alikuwa amemwambia anunue vilivyohitajiwa kwa sikukuu, au kwamba alikuwa amemwambia akatoe chochote kwa maskini.
John Swahili 13:30  Basi, Yuda alipokwisha twaa kile kipande cha mkate, akatoka nje mara. Na ilikuwa usiku.
John Swahili 13:31  Baada ya Yuda kuondoka, Yesu akasema, "Sasa Mwana wa Mtu ametukuzwa, naye Mungu ametukuzwa ndani yake.
John Swahili 13:32  Na kama utukufu wa Mungu umefunuliwa ndani ya Mwana, basi, naye Mungu ataudhihirisha utukufu wa Mwana ndani yake mwenyewe, na atafanya hivyo mara.
John Swahili 13:33  "Watoto wangu, bado niko nanyi kwa muda mfupi tu. Mtanitafuta, lakini sasa nawaambieni yale niliyowaambia viongozi wa Wayahudi: Niendako ninyi hamwezi kwenda!
John Swahili 13:34  Nawapeni amri mpya: pendaneni; pendaneni kama nilivyowapenda ninyi.
John Swahili 13:35  Mkipendana, watu wote watajua kwamba ninyi ni wanafunzi wangu."
John Swahili 13:36  Simoni Petro akamwuliza, "Bwana, unakwenda wapi?" Yesu akajibu, "Niendako huwezi kunifuata sasa, lakini utanifuata baadaye."
John Swahili 13:37  Petro akamwambia "Bwana, kwa nini siwezi kukufuata sasa? Niko tayari kufa kwa ajili yako!"
John Swahili 13:38  Yesu akajibu, "Je, uko tayari kweli kufa kwa ajili yangu? Kweli nakwambia, kabla jogoo hajawika utanikana mara tatu!"
Chapter 14
John Swahili 14:1  Yesu aliwaambia, "Msifadhaike mioyoni mwenu. Mwaminini Mungu, niaminini na mimi pia.
John Swahili 14:2  Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi; la sivyo ningalikwisha waambieni. Sasa nakwenda kuwatayarishieni nafasi.
John Swahili 14:3  Na nikienda na kuwatayarishieni nafasi, nitarudi na kuwachukueni kwangu, ili nanyi muwe pale nilipo mimi.
John Swahili 14:5  Thoma akamwuliza, "Bwana, hatujui unakokwenda, tutawezaje basi, kuijua hiyo njia?"
John Swahili 14:6  Yesu akamjibu, "Mimi ni njia, na ukweli na uzima. Hakuna awezaye kwenda kwa Baba ila kwa kupitia kwangu.
John Swahili 14:7  Ikiwa mnanijua mimi mnamjua na Baba yangu pia. Na tangu sasa, mnamjua, tena mmekwisha mwona."
John Swahili 14:8  Filipo akamwambia, "Bwana, tuonyeshe Baba, nasi tutatosheka."
John Swahili 14:9  Yesu akamwambia, "Filipo, nimekaa nanyi muda wote huu, nawe hujanijua? Aliyekwisha niona mimi amemwona Baba. Unawezaje basi, kusema: Tuonyeshe Baba?
John Swahili 14:10  Je, huamini kwamba mimi niko ndani ya Baba, naye Baba yuko ndani yangu? Maneno ninayowaambieni nyote siyasemi kwa mamlaka yangu; Baba aliye ndani yangu anafanya kazi yake.
John Swahili 14:11  Mnapaswa kuniamini ninaposema kwamba mimi niko ndani ya Baba naye Baba yuko ndani yangu. Ama sivyo, aminini kwa sababu ya mambo ninayofanya.
John Swahili 14:12  Kweli nawaambieni, anayeniamini atafanya mambo ninayofanya mimi; naam, atafanya hata makuu zaidi, maana nakwenda kwa Baba.
John Swahili 14:13  Na chochote mtakachoomba kwa jina langu nitafanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana.
John Swahili 14:14  Mkiniomba chochote kwa jina langu, nitawafanyieni.
John Swahili 14:16  Nami nitamwomba Baba naye atawapeni Msaidizi mwingine, atakayekaa nanyi milele.
John Swahili 14:17  Yeye ni Roho wa kweli. Ulimwengu hauwezi kumpokea kwa sababu hauwezi kumwona wala kumjua. Lakini ninyi mnamjua kwa sababu anabaki nanyi na yu ndani yenu.
John Swahili 14:19  Bado kidogo nao ulimwengu hautaniona tena, lakini ninyi mtaniona; na kwa kuwa mimi ni hai, nanyi pia mtakuwa hai.
John Swahili 14:20  Siku ile itakapofika mtajua kwamba mimi niko ndani ya Baba, nanyi mko ndani yangu, nami ndani yenu.
John Swahili 14:21  Azipokeaye amri zangu na kuzishika, yeye ndiye anipendaye. Naye anipendaye mimi atapendwa na Baba yangu, nami nitampenda na kujidhihirisha kwake."
John Swahili 14:22  Yuda (si yule Iskarioti) akamwambia, "Bwana, itawezekanaje wewe kujidhihirisha kwetu na si kwa ulimwengu?"
John Swahili 14:23  Yesu akamjibu, "Mtu akinipenda atashika neno langu, na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kukaa naye.
John Swahili 14:24  Asiyenipenda hashiki maneno yangu. Na neno mlilosikia si langu, bali ni lake Baba aliyenituma.
John Swahili 14:25  "Nimewaambieni mambo haya nikiwa bado pamoja nanyi
John Swahili 14:26  lakini Msaidizi, Roho Mtakatifu, ambaye Baba atamtuma kwa jina langu, atawafundisheni kila kitu na kuwakumbusheni yote niliyowaambieni.
John Swahili 14:27  "Nawaachieni amani; nawapeni amani yangu. Siwapi ninyi kama vile ulimwengu ufanyavyo. Msiwe na wasiwasi, wala msifadhaike.
John Swahili 14:28  Mlikwisha sikia nikiwaambieni: Ninakwenda zangu, kisha nitarudi tena kwenu. Kama mngalinipenda mngalifurahi kwa sababu ninakwenda kwa Baba, maana yeye ni mkuu kuliko mimi.
John Swahili 14:29  Nimewaambieni haya sasa kabla hayajatokea, ili yatakapotokea mpate kuamini.
John Swahili 14:30  Sitasema nanyi tena mambo mengi, maana mtawala wa ulimwengu huu anakuja. Kwangu mimi hawezi kitu;
John Swahili 14:31  lakini ulimwengu unapaswa kujua kwamba nampenda Baba, na ndiyo maana nafanya kila kitu kama Baba alivyoniamuru. Simameni, tutoke hapa!"
Chapter 15
John Swahili 15:1  "Mimi ni mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima.
John Swahili 15:2  Yeye huliondoa ndani yangu kila tawi lisilozaa matunda, na kila tawi lizaalo hulisafisha lipate kuzaa zaidi.
John Swahili 15:3  Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya ule ujumbe niliowaambieni.
John Swahili 15:4  Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Tawi haliwezi peke yake kuzaa matunda lisipokaa katika mzabibu hali kadhalika nanyi hamwezi kuzaa matunda msipokaa ndani yangu.
John Swahili 15:5  "Mimi ni mzabibu, nanyi ni matawi yake. Akaaye ndani yangu, nami ndani yake, huyo atazaa matunda mengi, maana bila mimi hamwezi kufanya chochote.
John Swahili 15:6  Mtu yeyote asipokaa ndani yangu hutupwa nje kama tawi litupwalo nje hata likakauka. Watu huliokota tawi la namna hiyo na kulitupa motoni liungue.
John Swahili 15:7  Mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, basi, ombeni chochote mtakacho nanyi mtapewa.
John Swahili 15:8  Baba yangu hutukuzwa kama mkizaa matunda mengi na kuwa wanafunzi wangu.
John Swahili 15:9  Mimi nimewapenda ninyi kama vile Baba alivyonipenda mimi. Kaeni katika pendo langu.
John Swahili 15:10  Mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama vile nami nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake.
John Swahili 15:11  Nimewaambieni mambo haya ili furaha yangu ikae ndani yenu, na furaha yenu ikamilike.
John Swahili 15:12  Hii ndiyo amri yangu: pendaneni; pendaneni kama nilivyowapenda ninyi.
John Swahili 15:13  Hakuna upendo mkuu zaidi kuliko upendo wa mtu atoaye uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.
John Swahili 15:15  Ninyi siwaiti tena watumishi, maana mtumishi hajui anachofanya bwana wake. Lakini mimi nimewaita ninyi rafiki, kwa sababu nimewajulisha yote ambayo nimeyasikia kutoka kwa Baba yangu.
John Swahili 15:16  Ninyi hamkunichagua mimi; mimi niliwachagueni na kuwatuma mwende mkazae matunda, matunda yadumuyo, naye Baba apate kuwapa ninyi chochote mumwombacho kwa jina langu.
John Swahili 15:18  "Kama ulimwengu ukiwachukia ninyi, kumbukeni kwamba umenichukia mimi kabla haujawachukia ninyi.
John Swahili 15:19  Kama mngalikuwa watu wa ulimwengu, ulimwengu ungaliwapenda ninyi kama watu wake. Lakini kwa vile ninyi si wa ulimwengu, ila mimi nimewachagueni kutoka ulimwenguni, kwa sababu hiyo ulimwengu unawachukieni.
John Swahili 15:20  Kumbukeni niliyowaambieni: mtumishi si mkuu zaidi kuliko bwana wake. Ikiwa wamenitesa mimi, watawatesa na ninyi pia; kama wameshika neno langu, watalishika na lenu pia.
John Swahili 15:21  Lakini hayo yote watawatendeeni ninyi kwa sababu ya jina langu, kwani hawamjui yeye aliyenituma.
John Swahili 15:22  Kama nisingalikuja na kusema nao wasingalikuwa na hatia; lakini sasa hawawezi kujitetea kwamba hawana dhambi.
John Swahili 15:23  Anayenichukia mimi, anamchukia na Baba yangu pia.
John Swahili 15:24  Kama nisingalifanya kwao mambo ambayo hakuna mtu mwingine amekwisha yafanya wasingalikuwa na hatia; lakini sasa wameona niliyoyafanya wakinichukia mimi, wakamchukia na Baba yangu pia.
John Swahili 15:25  Na hivi ni lazima yatimie yale yaliyoandikwa katika Sheria yao: Wamenichukia bure!
John Swahili 15:26  "Atakapokuja huyo Msaidizi nitakayemtuma kwenu kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia mimi.
John Swahili 15:27  Nanyi pia mtanishuhudia kwa kuwa mmekuwa nami tangu mwanzo.
Chapter 16
John Swahili 16:2  Watu watawatenga ninyi na masunagogi yao. Tena, wakati unakuja ambapo kila atakayewaua ninyi atadhani anamhudumia Mungu.
John Swahili 16:3  Watawatendeeni mambo hayo kwa sababu hawamjui Baba, wala hawanijui mimi.
John Swahili 16:4  Basi, nimewaambieni mambo haya ili saa yake itakapofika mkumbuke kwamba niliwaambieni. "Sikuwaambieni mambo haya tangu mwanzo kwa sababu nilikuwa pamoja nanyi.
John Swahili 16:5  Lakini sasa namwendea yule aliyenituma; na hakuna hata mmoja wenu anayeniuliza: Unakwenda wapi?
John Swahili 16:6  Kwa kuwa nimewaambieni mambo hayo mmejaa huzuni mioyoni mwenu.
John Swahili 16:7  Lakini, nawaambieni ukweli: afadhali kwenu mimi niende zangu, maana nisipokwenda Msaidizi hatakuja kwenu. Lakini nikienda, basi, nitamtuma kwenu.
John Swahili 16:8  Naye atakapokuja atawathibitishia walimwengu kwamba wamekosea kuhusu dhambi, uadilifu na hukumu ya Mungu.
John Swahili 16:10  kuhusu uadilifu, kwa sababu naenda zangu kwa Baba, nanyi hamtaniona tena;
John Swahili 16:11  kuhusu hukumu kwa sababu mkuu wa ulimwengu huu amekwisha hukumiwa.
John Swahili 16:12  "Ninayo bado mengi ya kuwaambieni, ila kwa sasa hamwezi kuyastahimili.
John Swahili 16:13  Lakini atakapokuja huyo Roho wa kweli atawaongoza kwenye ukweli wote; maana hatasema kwa mamlaka yake mwenyewe, bali atawaambieni yote atakayosikia, na atasema mambo yatakayokuwa yanakuja.
John Swahili 16:14  Yeye atanitukuza mimi kwa kuwa atawaambieni yale atakayopata kutoka kwangu.
John Swahili 16:15  Vyote alivyo navyo Baba ni vyangu; ndiyo maana nimesema kwamba huyo Roho Mtakatifu atawaambieni yale atakayopata kutoka kwangu.
John Swahili 16:16  "Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona!"
John Swahili 16:17  Hapo baadhi ya wanafunzi wake wakaulizana, "Ana maana gani anapotwambia: Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona? Tena anasema: Kwa kuwa ninakwenda kwa Baba!"
John Swahili 16:18  Basi, wakawa wanaulizana, "Ana maana gani anaposema: Bado kitambo kidogo? Hatuelewi anaongelea nini."
John Swahili 16:19  Yesu alijua kwamba walitaka kumwuliza, basi akawaambia, "Je, mnaulizana juu ya yale niliyosema: Bado kitambo kidogo nanyi hamtaniona; na baada ya kitambo kidogo tena mtaniona?
John Swahili 16:20  Nawaambieni kweli, ninyi mtalia na kuomboleza, lakini ulimwengu utafurahi: mtaona huzuni lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha.
John Swahili 16:21  Wakati mama anapojifungua huona huzuni kwa sababu saa ya maumivu imefika; lakini akisha jifungua hayakumbuki tena maumivu hayo kwa sababu ya furaha kwamba mtu amezaliwa duniani.
John Swahili 16:22  Ninyi pia mna huzuni sasa; lakini nitawajieni tena, nanyi mtajaa furaha mioyoni mwenu, na furaha hiyo hakuna mtu atakayeiondoa kwenu.
John Swahili 16:23  Siku hiyo hamtaniomba chochote. Kweli nawaambieni, chochote mtakachomwomba Baba kwa jina langu, atawapeni.
John Swahili 16:24  Mpaka sasa hamjaomba chochote kwa jina langu. Ombeni nanyi mtapata ili furaha yenu ikamilike.
John Swahili 16:25  "Nimewaambieni mambo hayo kwa mafumbo. Lakini wakati utakuja ambapo sitasema tena nanyi kwa mafumbo, bali nitawaambieni waziwazi juu ya Baba.
John Swahili 16:26  Siku hiyo mtaomba kwa jina langu, na siwaambii kwamba nitamwomba Baba kwa niaba yenu;
John Swahili 16:27  maana yeye mwenyewe anawapenda ninyi, kwa sababu ninyi mmenipenda mimi na mmeamini kwamba nimetoka kwa Mungu.
John Swahili 16:28  Mimi nilitoka kwa Baba, nikaja ulimwenguni; na sasa nauacha ulimwengu na kurudi kwa Baba."
John Swahili 16:29  Basi, wanafunzi wake wakamwambia, "Ahaa! Sasa unasema waziwazi kabisa bila kutumia mafumbo.
John Swahili 16:30  Sasa tunajua kwamba wewe unajua kila kitu, na huna haja ya kuulizwa maswali na mtu yeyote; kwa hiyo tunaamini kwamba umetoka kwa Mungu."
John Swahili 16:32  Wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo ninyi nyote mtatawanyika kila mtu kwake, nami nitaachwa peke yangu. Kumbe, lakini mimi siko peke yangu, maana Baba yu pamoja nami.
John Swahili 16:33  Nimewaambieni mambo haya ili mpate kuwa na amani katika kuungana nami. Ulimwenguni mtapata masumbuko; lakini jipeni moyo! Mimi nimeushinda ulimwengu!"
Chapter 17
John Swahili 17:1  Yesu alipokwisha sema hayo, alitazama juu mbinguni, akasema, "Baba, saa imefika! Mtukuze Mwanao ili naye Mwana apate kukutukuza.
John Swahili 17:2  Maana ulimpa Mwanao mamlaka juu ya watu wote ili awape uzima wa milele wote hao uliompa.
John Swahili 17:3  Na uzima wa milele ndio huu: kukujua wewe uliye peke yako Mungu wa kweli, na kumjua Yesu Kristo uliyemtuma.
John Swahili 17:4  Mimi nimekutukuza hapa duniani; nimeikamilisha ile kazi uliyonipa nifanye.
John Swahili 17:5  Sasa, Baba, nitukuze mbele yako kwa ule utukufu niliokuwa nao kabla ya kuumbwa ulimwengu.
John Swahili 17:6  "Nimekufanya ujulikane kwa watu wale ulionipa kutoka duniani. Walikuwa watu wako, nawe ukanipa wawe wangu; nao wamelishika neno lako.
John Swahili 17:7  Sasa wanajua kwamba kila ulichonipa kimetoka kwako.
John Swahili 17:8  Mimi nimewapa ule ujumbe ulionipa nao wameupokea; wanajua kwamba kweli nimetoka kwako, na wanaamini kwamba wewe ulinituma.
John Swahili 17:9  "Nawaombea hao; siuombei ulimwengu, ila nawaombea hao ulionipa, maana ni wako.
John Swahili 17:10  Yote niliyo nayo ni yako, na yako ni yangu; na utukufu wangu umeonekana ndani yao.
John Swahili 17:11  Na sasa naja kwako; simo tena ulimwenguni, lakini wao wamo ulimwenguni. Baba Mtakatifu! Kwa nguvu ya jina lako ulilonipa, tafadhali uwaweke salama ili wawe kitu kimoja kama sisi tulivyo mmoja.
John Swahili 17:12  Nilipokuwa nao, mimi niliwaweka salama kwa nguvu ya jina lako ulilonipa. Mimi nimewalinda, wala hakuna hata mmoja wao aliyepotea, isipokuwa yule aliyelazimika kupotea ili Maandiko Matakatifu yapate kutimia.
John Swahili 17:13  Basi, sasa naja kwako, na nimesema mambo haya ulimwenguni, ili waweze kushiriki kikamilifu furaha yangu.
John Swahili 17:14  Mimi nimewapa neno lako, nao ulimwengu ukawachukia, kwa sababu wao si wa ulimwengu kama vile nami nisivyo wa ulimwengu.
John Swahili 17:15  Siombi uwatoe ulimwenguni, bali naomba uwakinge na yule Mwovu.
John Swahili 17:16  Wao si wa ulimwengu, kama vile nami nisivyo wa ulimwengu.
John Swahili 17:18  Kama vile ulivyonituma ulimwenguni, nami pia nimewatuma wao ulimwenguni;
John Swahili 17:19  na kwa ajili yao mimi mwenyewe najiweka wakfu ili nao pia wafanywe wakfu katika ukweli.
John Swahili 17:20  "Siwaombei hao tu, bali nawaombea pia wote watakaoamini kutokana na ujumbe wao.
John Swahili 17:21  Naomba ili wote wawe kitu kimoja. Baba! Naomba wawe ndani yetu kama vile wewe ulivyo ndani yangu nami ndani yako. Naomba wawe kitu kimoja kusudi ulimwengu upate kuamini kwamba wewe ulinituma.
John Swahili 17:22  Mimi nimewapa utukufu uleule ulionipa mimi, ili wawe kitu kimoja kama nasi tulivyo mmoja;
John Swahili 17:23  mimi niwe ndani yao, nawe uwe ndani yangu; naomba wakamilishwe na kuwa kitu kimoja, ili ulimwengu upate kujua kwamba wewe ulinituma, na kwamba unawapenda wao kama unavyonipenda mimi.
John Swahili 17:24  "Baba! Nataka wao ulionipa wawe pamoja nami pale nilipo, ili wauone utukufu wangu ulionipa; kwa kuwa ulinipenda kabla ya kuumbwa ulimwengu.
John Swahili 17:25  Baba Mwema! Ulimwengu haukujui, lakini mimi nakujua. Hawa nao wanajua kwamba wewe ulinituma.
John Swahili 17:26  Nimekufanya ujulikane kwao na nitaendelea kufanya hivyo, ili upendo ulio nao kwangu uwe ndani yao, nami niwe ndani yao."
Chapter 18
John Swahili 18:1  Yesu alipokwisha sema hayo, alikwenda ng'ambo ya kijito Kedroni, pamoja na wanafunzi wake. Mahali hapo palikuwa na bustani, naye Yesu akaingia humo pamoja na wanafunzi wake.
John Swahili 18:2  Yuda, aliyemsaliti Yesu, alipajua mahali hapo kwani mara nyingi Yesu alikutana na wanafunzi wake huko.
John Swahili 18:3  Basi, Yuda alichukua kikosi cha askari na walinzi kutoka kwa makuhani wakuu na Mafarisayo, akaja nao bustanini wakiwa na taa, mienge na silaha.
John Swahili 18:4  Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea, akawauliza, "Mnamtafuta nani?"
John Swahili 18:5  Nao wakamjibu, "Yesu wa Nazareti!" Yesu akawaambia, "Mimi ndiye." Msaliti Yuda alikuwa amesimama hapo pamoja nao.
John Swahili 18:6  Basi, Yesu alipowaambia: "Mimi ndiye", wakarudi nyuma, wakaanguka chini.
John Swahili 18:7  Yesu akawauliza tena, "Mnamtafuta nani?" Wakamjibu, "Yesu wa Nazareti!"
John Swahili 18:8  Yesu akawaambia, "Nimekwisha waambieni kwamba mimi ndiye. Basi, kama mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao."
John Swahili 18:9  (Alisema hayo ili yapate kutimia yale aliyosema: "Wale ulionipa sikumpoteza hata mmoja.")
John Swahili 18:10  Simoni Petro alikuwa na upanga; basi, akauchomoa, akamkata sikio la kulia mtumishi wa Kuhani Mkuu. Mtumishi huyo aliitwa Malko.
John Swahili 18:11  Basi, Yesu akamwambia Petro, "Rudisha upanga wako alani. Je, nisinywe kikombe alichonipa Baba?"
John Swahili 18:12  Kile kikosi cha askari, mkuu wake na walinzi wa Wayahudi walimkamata Yesu, wakamfunga
John Swahili 18:13  na kumpeleka kwanza kwa Anasi; Anasi alikuwa baba mkwe wa Kayafa ambaye alikuwa Kuhani Mkuu mwaka huo.
John Swahili 18:14  Huyo Kayafa ndiye aliyekuwa amewashauri Wayahudi kwamba ni afadhali mtu mmoja afe kwa ajili ya taifa.
John Swahili 18:15  Simoni Petro pamoja na mwanafunzi mwingine walimfuata Yesu. Huyo mwanafunzi mwingine alikuwa anajulikana kwa Kuhani Mkuu, hivyo aliingia pamoja na Yesu ndani ya ukumbi wa Kuhani Mkuu.
John Swahili 18:16  Lakini Petro alikuwa amesimama nje, karibu na mlango. Basi, huyo mwanafunzi mwingine aliyekuwa anajulikana kwa Kuhani Mkuu alitoka nje akasema na mjakazi, mngoja mlango, akamwingiza Petro ndani.
John Swahili 18:17  Huyo msichana mngoja mlango akamwuliza Petro, "Je, nawe pia ni mmoja wa wanafunzi wa mtu huyu?" Petro akamwambia, "Si mimi!"
John Swahili 18:18  Watumishi na walinzi walikuwa wamewasha moto kwa sababu kulikuwa na baridi, wakawa wanaota moto. Naye Petro alikuwa amesimama pamoja nao akiota moto.
John Swahili 18:19  Basi, Kuhani akamwuliza Yesu juu ya wanafunzi wake na mafundisho yake.
John Swahili 18:20  Yesu akamjibu, "Nimesema na kila mtu daima hadharani. Kila mara nimefundisha katika masunagogi na Hekaluni, mahali wakutanikiapo Wayahudi wote; na wala sijasema chochote kwa siri.
John Swahili 18:21  Kwa nini waniuliza mimi? Waulize wale waliosikia nini niliwaambia. Wao wanajua nilivyosema."
John Swahili 18:22  Alipokwisha sema hayo mlinzi mmoja aliyekuwa amesimama hapo akampiga kofi akisema, "Je, ndivyo unavyomjibu Kuhani Mkuu?"
John Swahili 18:23  Yesu akamjibu, "Kama nimesema vibaya, onyesha huo ubaya; lakini ikiwa nimesema vema, mbona wanipiga?"
John Swahili 18:24  Basi, Anasi akampeleka Yesu akiwa amefungwa, kwa Kuhani Mkuu Kayafa.
John Swahili 18:25  Petro alikuwa hapo akiota moto. Basi, wakamwuliza, "Je, nawe pia si mmoja wa wanafunzi wake?" Yeye akakana na kusema, "Si mimi!"
John Swahili 18:26  Mmoja wa watumishi wa Kuhani Mkuu, jamaa wa yule aliyekatwa sikio na Petro, akamwuliza, "Je, mimi sikukuona wewe bustanini pamoja naye?"
John Swahili 18:28  Basi, walimchukua Yesu kutoka kwa Kayafa, wakampeleka ikulu. Ilikuwa alfajiri, nao ili waweze kula Pasaka, hawakuingia ndani ya ikulu wasije wakatiwa najisi.
John Swahili 18:29  Kwa hiyo, Pilato aliwaendea nje, akasema, "Mna mashtaka gani juu ya mtu huyu?"
John Swahili 18:30  Wakamjibu, "Kama huyu hangalikuwa mwovu hatungalimleta kwako."
John Swahili 18:31  Pilato akawaambia, "Haya, mchukueni ninyi wenyewe, mkamhukumu kufuatana na Sheria yenu." Wayahudi wakamjibu, "Sisi hatuna mamlaka ya kumwua mtu yeyote."
John Swahili 18:32  (Ilifanyika hivyo yapate kutimia maneno aliyosema Yesu kuonyesha atakufa kifo gani.)
John Swahili 18:33  Pilato akaingia tena ndani ya ikulu, akamwita Yesu na kumwuliza: "Ati wewe ndiye Mfalme wa Wayahudi?"
John Swahili 18:34  Yesu akamjibu, "Je, hayo ni maneno yako au wengine wamekwambia habari zangu?"
John Swahili 18:35  Pilato akamjibu, "Je, ni Myahudi mimi? Taifa lako na makuhani wamekuleta kwangu. Umefanya nini?"
John Swahili 18:36  Yesu akamjibu, "Ufalme wangu si wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu watumishi wangu wangenipigania nisitiwe mikononi mwa Wayahudi. Lakini sasa ufalme wangu si wa hapa."
John Swahili 18:37  Hapo Pilato akamwambia, "Basi, wewe ni Mfalme?" Yesu akajibu, "Wewe umesema kwamba mimi ni Mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili hiyo; na kwa ajili hiyo nimekuja ulimwenguni kuwaambia watu juu ya ukweli. Kila mtu wa ukweli hunisikiliza."
John Swahili 18:38  Pilato akamwambia, "Ukweli ni kitu gani?" Pilato alipokwisha sema hayo, aliwaendea tena Wayahudi nje, akawaambia, "Mimi sioni hatia yoyote kwake.
John Swahili 18:39  Lakini, mnayo desturi kwamba mimi niwafungulie mfungwa mmoja wakati wa Pasaka. Basi, mwataka niwafungulieni Mfalme wa Wayahudi?"
John Swahili 18:40  Hapo wakapiga kelele: "La! Si huyu ila Baraba!" Naye Baraba alikuwa mnyang'anyi.
Chapter 19
John Swahili 19:1  Basi, Pilato akaamuru Yesu achukuliwe, apigwe viboko.
John Swahili 19:2  Nao askari wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani, wakamvika na joho la rangi ya zambarau.
John Swahili 19:3  Wakawa wanakuja mbele yake na kusema: "Shikamoo, Mfalme wa Wayahudi!" Wakampiga makofi.
John Swahili 19:4  Pilato akatoka tena nje, akawaambia, "Tazameni, namleta nje kwenu, mpate kujua kwamba mimi sikuona hatia yoyote kwake."
John Swahili 19:5  Basi, Yesu akatoka nje amevaa taji ya miiba na joho la rangi ya zambarau. Pilato akawaambia, "Tazameni! Mtu mwenyewe ni huyo."
John Swahili 19:6  Makuhani wakuu na walinzi walipomwona wakapaaza sauti: "Msulubishe! Msulubishe!" Pilato akawaambia, "Mchukueni basi, ninyi wenyewe mkamsulubishe, kwa maana mimi sikuona hatia yoyote kwake."
John Swahili 19:7  Wayahudi wakamjibu, "Sisi tunayo Sheria, na kufuatana na Sheria hiyo, ni lazima afe, kwa sababu alijifanya kuwa Mwana wa Mungu."
John Swahili 19:9  Basi, akaingia tena ndani ya ikulu, akamwuliza Yesu, "Umetoka wapi wewe?" Lakini Yesu hakumjibu neno.
John Swahili 19:10  Hivyo Pilato akamwambia, "Husemi nami? Je, hujui kwamba ninayo mamlaka ya kukufungua na mamlaka ya kukusulubisha?"
John Swahili 19:11  Yesu akamjibu, "Hungekuwa na mamlaka yoyote juu yangu kama hungepewa na Mungu. Kwa sababu hiyo, yule aliyenikabidhi kwako ana dhambi kubwa zaidi."
John Swahili 19:12  Tangu hapo, Pilato akawa anatafuta njia ya kumwachilia, lakini Wayahudi wakapiga kelele: "Ukimwachilia huyu mtu, wewe si rafiki yake Kaisari; kila mtu anayejifanya kuwa Mfalme humpinga Kaisari!"
John Swahili 19:13  Basi, Pilato aliposikia maneno hayo akamleta Yesu nje, akaketi juu ya kiti cha hukumu, mahali paitwapo: "Sakafu ya Mawe" (kwa Kiebrania, Gabatha).
John Swahili 19:14  Ilikuwa yapata saa sita mchana, siku ya maandalio ya Pasaka. Pilato akawaambia Wayahudi, "Tazameni, Mfalme wenu!"
John Swahili 19:15  Wao wakapaaza sauti: "Mwondoe! Mwondoe! Msulubishe!" Makuhani wakuu wakajibu, "Sisi hatuna Mfalme isipokuwa Kaisari!"
John Swahili 19:16  Basi, hapo Pilato akamtia Yesu mikononi mwao ili asulubiwe. Basi, wakamchukua Yesu.
John Swahili 19:17  Naye akatoka akiwa amejichukulia msalaba wake kwenda mahali paitwapo "Fuvu la Kichwa", (kwa Kiebrania Golgotha).
John Swahili 19:18  Hapo ndipo walipomsulubisha, na pamoja naye waliwasulubisha watu wengine wawili; mmoja upande wake wa kulia na mwingine upande wake wa kushoto, naye Yesu katikati.
John Swahili 19:19  Pilato aliandika ilani akaiweka juu ya msalaba. Nayo ilikuwa imeandikwa hivi: "Yesu wa Nazareti, Mfalme wa Wayahudi."
John Swahili 19:20  Wayahudi wengi waliisoma ilani hiyo, maana mahali hapo aliposulubiwa Yesu palikuwa karibu na mji. Tena ilani hiyo ilikuwa imeandikwa kwa Kiebrania, Kilatini, na Kigiriki.
John Swahili 19:21  Basi, makuhani wakuu wakamwambia Pilato, "Usiandike: Mfalme wa Wayahudi, ila Yeye alisema, Mimi ni Mfalme wa Wayahudi."
John Swahili 19:23  Askari walipokwisha msulubisha Yesu, walizichukua nguo zake, wakazigawa mafungu manne, fungu moja kwa kila askari. Walichukua pia na kanzu yake; kanzu hiyo ilikuwa imefumwa kwa kipande kimoja tu, bila mshono.
John Swahili 19:24  Basi, hao askari wakashauriana: "Tusiipasue, ila tuipigie kura itakuwa ya nani." Jambo hilo lilifanyika ili yatimie Maandiko Matakatifu yasemayo: "Waligawana mavazi yangu, na nguo yangu wakaipigia kura." Basi, ndivyo walivyofanya hao askari.
John Swahili 19:25  Karibu na msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mama yake, na dada ya mama yake, Maria mke wa Kleopa, na Maria Magdalene.
John Swahili 19:26  Yesu alipomwona mama yake, na karibu naye amesimama yule mwanafunzi aliyempenda, akamwambia mama yake: "Mama! Tazama, huyo ndiye mwanao."
John Swahili 19:27  Halafu akamwambia yule mwanafunzi: "Tazama, huyo ndiye mama yako." Na tangu saa ile huyo mwanafunzi alimchukua akae nyumbani kwake.
John Swahili 19:28  Yesu alijua kwamba yote yalikuwa yametimia; na, ili Maandiko Matakatifu yapate kutimia, akasema, "Naona kiu."
John Swahili 19:29  Hapo palikuwa na bakuli limejaa siki. Basi, wakachovya sifongo katika hiyo siki, wakaitia juu ya ufito wa husopo, wakamwekea mdomoni.
John Swahili 19:30  Yesu alipokwisha pokea hiyo siki, akasema, "Yametimia!" Kisha akainama kichwa, akatoa roho.
John Swahili 19:31  Ilikuwa Ijumaa, siku ya Maandalio. Kwa hiyo, kusudi miili isikae msalabani siku ya Sabato, maana siku hiyo ya Sabato ilikuwa siku kubwa, Wayahudi walimwomba Pilato miguu ya hao waliosulubiwa ivunjwe na miili yao iondolewe.
John Swahili 19:32  Basi, askari walikwenda, wakaivunja miguu ya yule mtu wa kwanza na yule wa pili ambao walikuwa wamesulubiwa pamoja na Yesu.
John Swahili 19:33  Lakini walipomfikia Yesu waliona kwamba alikwisha kufa, na hivyo hawakumvunja miguu.
John Swahili 19:34  Lakini askari mmoja alimtoboa ubavuni kwa mkuki, na mara ikatoka damu na maji.
John Swahili 19:35  (Naye aliyeona tukio hilo ametoa habari zake ili nanyi mpate kuamini. Na hayo aliyosema ni ukweli, tena yeye anajua kwamba anasema ukweli.)
John Swahili 19:36  Jambo hilo lilitendwa ili Maandiko Matakatifu yatimie: "Hapana hata mfupa wake mmoja utakaovunjwa."
John Swahili 19:37  Tena Maandiko mengine yanasema: "Watamtazama yule waliyemtoboa."
John Swahili 19:38  Baada ya hayo, Yosefu, mwenyeji wa Armathaya, alimwomba Pilato ruhusa ya kuuchukua mwili wa Yesu. (Yosefu alikuwa mfuasi wa Yesu, lakini kwa siri, maana aliwaogopa viongozi wa Wayahudi). Basi, Pilato akamruhusu. Hivyo Yosefu alikwenda, akauondoa mwili wa Yesu.
John Swahili 19:39  Naye Nikodemo ambaye hapo awali alikuwa amemwendea Yesu usiku, akaja akiwa amechukua mchanganyiko wa manemane na ubani kiasi cha kilo thelathini.
John Swahili 19:40  Basi, waliutwaa mwili wa Yesu, wakaufunga sanda pamoja na manukato kufuatana na desturi ya Wayahudi katika kuzika.
John Swahili 19:41  Mahali hapo aliposulubiwa Yesu palikuwa na bustani, na katika bustani hiyo kulikuwa na kaburi jipya ambalo hakutiwa bado mtu yeyote ndani yake.
John Swahili 19:42  Basi, kwa sababu ya shughuli za Wayahudi za maandalio ya Sabato, na kwa vile kaburi hilo lilikuwa karibu, wakamweka Yesu humo.
Chapter 20
John Swahili 20:1  Alfajiri na mapema Jumapili, kukiwa bado na giza, Maria Magdalene alikwenda kaburini, akaliona lile jiwe limeondolewa mlangoni pa kaburi.
John Swahili 20:2  Basi, akaenda mbio hadi kwa Petro na yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, "Wamemwondoa Bwana kaburini, na wala hatujui walikomweka."
John Swahili 20:3  Petro pamoja na yule mwanafunzi mwingine wakaenda kaburini.
John Swahili 20:4  Wote wawili walikimbia lakini yule mwanafunzi mwingine alikimbia mbio zaidi kuliko Petro, akatangulia kufika kaburini.
John Swahili 20:5  Alipoinama na kuchungulia ndani, aliona sanda, lakini hakuingia ndani.
John Swahili 20:6  Simoni Petro naye akaja akimfuata, akaingia kaburini; humo akaona sanda,
John Swahili 20:7  na kile kitambaa alichofungwa Yesu kichwani. Hicho kitambaa hakikuwekwa pamoja na hiyo sanda, bali kilikuwa kimekunjwa na kuwekwa mahali peke yake.
John Swahili 20:8  Kisha yule mwanafunzi mwingine aliyemtangulia kufika kaburini, akaingia pia ndani, akaona, akaaamini.
John Swahili 20:9  (Walikuwa bado hawajaelewa Maandiko Matakatifu yaliyosema kwamba ilikuwa lazima afufuke kutoka wafu).
John Swahili 20:11  Maria alikuwa amesimama nje ya kaburi, akilia. Huku akiwa bado analia, aliinama na kuchungulia kaburini,
John Swahili 20:12  akawaona malaika wawili waliovaa mavazi meupe, wameketi pale mwili wa Yesu ulipokuwa umelazwa, mmoja kichwani na wa pili miguuni.
John Swahili 20:13  Hao malaika wakamwuliza, "Mama, kwa nini unalia?" Naye akawaambia, "Wamemwondoa Bwana wangu, na wala sijui walikomweka!"
John Swahili 20:14  Baada ya kusema hayo, aligeuka nyuma, akamwona Yesu amesimama hapo, lakini asitambue ya kuwa ni Yesu.
John Swahili 20:15  Yesu akamwuliza, "Mama, kwa nini unalia? Unamtafuta nani?" Maria, akidhani kwamba huyo ni mtunza bustani, akamwambia, "Mheshimiwa, kama ni wewe umemwondoa, niambie ulikomweka, nami nitamchukua."
John Swahili 20:16  Yesu akamwambia, "Maria!" Naye Maria akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, "Raboni" (yaani "Mwalimu").
John Swahili 20:17  Yesu akamwambia, "Usinishike; sijakwenda bado juu kwa Baba. Lakini nenda kwa ndugu zangu uwaambie: nakwenda juu kwa Baba yangu na Baba yenu, Mungu wangu na Mungu wenu."
John Swahili 20:18  Hivyo Maria Magdalene akaenda akawapa habari wale wanafunzi kuwa amemwona Bwana, na kwamba alikuwa amemwambia hivyo.
John Swahili 20:19  Ilikuwa jioni ya siku hiyo ya Jumapili. Wanafunzi walikuwa wamekutana pamoja ndani ya nyumba, na milango ilikuwa imefungwa kwa sababu waliwaogopa viongozi wa Wayahudi. Basi, Yesu akaja, akasimama kati yao, akawaambia, "Amani kwenu!"
John Swahili 20:20  Alipokwisha sema hayo, akawaonyesha mikono yake na ubavu wake. Basi, hao wanafunzi wakafurahi mno kumwona Bwana.
John Swahili 20:21  Yesu akawaambia tena, "Amani kwenu! Kama vile Baba alivyonituma mimi, nami nawatuma ninyi."
John Swahili 20:22  Alipokwisha sema hayo, akawapulizia na kuwaambia, "Pokeeni Roho Mtakatifu.
John Swahili 20:23  Mkiwasamehe watu dhambi zao, wamesamehewa; msipowaondolea, hawasamehewi."
John Swahili 20:24  Thoma mmoja wa wale kumi na wawili (aitwaye Pacha), hakuwa pamoja nao wakati Yesu alipokuja.
John Swahili 20:25  Basi, wale wanafunzi wengine wakamwambia, "Tumemwona Bwana." Thoma akawaambia, "Nisipoona mikononi mwake alama za misumari, na kutia kidole changu katika kovu hizo, na kutia mkono wangu ubavuni mwake, sitasadiki."
John Swahili 20:26  Basi, baada ya siku nane hao wanafunzi walikuwa tena pamoja mle ndani, na Thoma alikuwa pamoja nao. Milango ilikuwa imefungwa, lakini Yesu akaja, akasimama kati yao, akasema, "Amani kwenu!"
John Swahili 20:27  Kisha akamwambia Thoma, "Lete kidole chako hapa uitazame mikono yangu; lete mkono wako ukautie ubavuni mwangu. Usiwe na mashaka, ila amini!"
John Swahili 20:29  Yesu akamwambia, "Je, unaamini kwa kuwa umeniona? Heri yao wale ambao hawajaona, lakini wameamini."
John Swahili 20:30  Yesu alifanya mbele ya wanafunzi wake ishara nyingine nyingi ambazo hazikuandikwa katika kitabu hiki.
John Swahili 20:31  Lakini hizi zimeandikwa ili mpate kuamini kwamba Yesu ni Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mpate kuwa na uzima kwa nguvu ya jina lake.
Chapter 21
John Swahili 21:1  Baada ya hayo Yesu aliwatokea tena wanafunzi wake kando ya ziwa Tiberia. Aliwatokea hivi:
John Swahili 21:2  Simoni Petro, Thoma (aitwaye Pacha), na Nathanieli mwenyeji wa Kana Galilaya, wana wawili wa Zebedayo na wanafunzi wake wengine wawili, walikuwa wote pamoja.
John Swahili 21:3  Simoni Petro aliwaambia, "Nakwenda kuvua samaki." Nao wakamwambia, "Nasi tutafuatana nawe." Basi, wakaenda, wakapanda mashua, lakini usiku huo hawakupata chochote.
John Swahili 21:4  Kulipoanza kupambazuka, Yesu alisimama kando ya ziwa, lakini wanafunzi hawakujua kwamba alikuwa yeye.
John Swahili 21:5  Basi, Yesu akawauliza, "Vijana, hamjapata samaki wowote sio?" Wao wakamjibu, "La! Hatujapata kitu."
John Swahili 21:6  Yesu akawaambia, "Tupeni wavu upande wa kulia wa mashua nanyi mtapata samaki." Basi, wakatupa wavu lakini sasa hawakuweza kuuvuta tena kwa wingi wa samaki.
John Swahili 21:7  Hapo yule mwanafunzi aliyependwa na Yesu akamwambia Petro, "Ni Bwana!" Simoni Petro aliposikia ya kuwa ni Bwana, akajifunga vazi lake (maana hakuwa amelivaa), akarukia majini.
John Swahili 21:8  Lakini wale wanafunzi wengine walikuja pwani kwa mashua huku wanauvuta wavu uliojaa samaki; hawakuwa mbali na nchi kavu, ila walikuwa yapata mita mia moja kutoka ukingoni.
John Swahili 21:9  Walipofika nchi kavu waliona moto wa makaa umewashwa na juu yake pamewekwa samaki na mkate.
John Swahili 21:10  Yesu akawaambia, "Leteni hapa baadhi ya samaki mliovua."
John Swahili 21:11  Basi, Simoni Petro akapanda mashuani, akavuta hadi nchi kavu ule wavu uliokuwa umejaa samaki wakubwa mia moja na hamsini na watatu. Na ingawa walikuwa wengi hivyo wavu haukukatika.
John Swahili 21:12  Yesu akawaambia, "Njoni mkafungue kinywa." Hakuna hata mmoja wao aliyethubutu kumwuliza: "Wewe ni nani?" Maana walijua alikuwa Bwana.
John Swahili 21:13  Yesu akaja, akatwaa mkate akawapa; akafanya vivyo hivyo na wale samaki.
John Swahili 21:14  Hii ilikuwa mara ya tatu Yesu kuwatokea wanafunzi wake baada ya kufufuka kutoka wafu.
John Swahili 21:15  Walipokwisha kula, Yesu alimwuliza Simoni Petro, "Simoni, mwana wa Yohane! Je, wanipenda mimi zaidi kuliko hawa?" Naye akajibu, "Naam, Bwana; wajua kwamba mimi nakupenda." Yesu akamwambia, "Tunza wana kondoo wangu."
John Swahili 21:16  Kisha akamwambia mara ya pili, "Simoni mwana wa Yohane! Je, wanipenda?" Petro akamjibu, "Naam, Bwana; wajua kwamba nakupenda." Yesu akamwambia, "Tunza kondoo wangu."
John Swahili 21:17  Akamwuliza mara ya tatu, "Simoni mwana wa Yohane! Je, wanipenda?" Hapo Petro akahuzunika kwa sababu alimwuliza mara ya tatu: "Wanipenda?" akamwambia, "Bwana, wewe wajua yote; wewe wajua kwamba mimi nakupenda." Yesu akamwambia, "Tunza kondoo wangu!
John Swahili 21:18  Kweli nakwambia, ulipokuwa kijana ulizoea kujifunga mshipi na kwenda kokote ulikotaka. Lakini utakapokuwa mzee utanyosha mikono yako, na mtu mwingine atakufunga na kukupeleka usikopenda kwenda."
John Swahili 21:19  (Kwa kusema hivyo, alionyesha jinsi Petro atakavyokufa na kumtukuza Mungu.) Kisha akamwambia, "Nifuate."
John Swahili 21:20  Hapo Petro akageuka, akamwona yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda, anafuata (Huyu mwanafunzi ndiye yule ambaye wakati wa chakula cha jioni, alikaa karibu sana na Yesu na kumwuliza: "Bwana ni nani atakayekusaliti?")
John Swahili 21:21  Basi, Petro alipomwona huyo akamwuliza Yesu, "Bwana, na huyu je?"
John Swahili 21:22  Yesu akamjibu, "Kama nataka abaki mpaka nitakapokuja, yakuhusu nini? Wewe nifuate mimi."
John Swahili 21:23  Basi, habari hiyo ikaenea miongoni mwa wale ndugu kwamba mwanafunzi huyo hafi. Lakini Yesu hakumwambia kwamba mwanafunzi huyo hafi, ila, "Kama nataka abaki mpaka nitakapokuja, yakuhusu nini?"
John Swahili 21:24  Huyo ndiye yule aliyeshuhudia mambo haya na kuyaandika. Nasi twajua kwamba aliyoyasema ni kweli.
John Swahili 21:25  Kuna mambo mengine mengi aliyofanya Yesu, ambayo kama yangeandikwa yote, moja baada ya lingine, nadhani hata ulimwengu wenyewe usingetosha kuviweka vitabu ambavyo vingeandikwa.